Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Mgeni wake Rais wa Rwanda Paul Kagame wameongea na Waandishi wa Habari leo baada ya kufanya mazungumzo yao, Ikulu, Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine Rais Kagame amesema Tanzania ni Mshirika mkubwa wa Rwanda.
Rais Kagame amenukuliwa akisema “Asante Dada yangu Samia Suluhu Hassan kwa kuniwezesha kufika kwa ajili ya ziara hii ambayo ni fupi, mambo muhimu umeyasema Mimi nitazungumza kwa ufupi sana, naomba uniruhusu nitumie Kiingereza, ingawa najitahidi kuzungumza Kiswahili kizuri ningependa kuzungumza Kiswahili kizuri kama chako lakini bado kazi inahitajika"
"Mimi na Rais Samia tulikuwa na mazungumzo na tumekubaliana kudumisha uhusiano zaidi wa kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kihistoria, Tanzania na Rwanda zina mzizi mzuri wa ushirikiano wa muda mrefu"
"Tanzania ni Mshirika mkubwa wa Rwanda hususani kwenye upande wa biashara, tunaheshimu kitendo cha Tanzania kukubali kudumisha zaidi ushirikiano huu kwa faida za Mataifa yote mawili ili kuruhusu Watu wetu kupata maendeleo ya haraka na Kampuni zetu kushindana vizuri kwenye Masoko ya Kimataifa"
"Mwisho Mh.Rais Samia nakushukuru kwa Uongozi wako katika kutafuta suluhisho la kudumu kwenye mgogoro ambao upo kwenye Kanda yetu ya Afrika Mashariki hususani mgogoro tunaoshughulika nao Mashariki ya Congo, ukishirikiana na Viongozi wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki"
"Kujenga amani ya kudumu na usalama kwenye Ukanda wetu tunahitaji kujitoa na kuwa na msimamo imara kwetu sote ikiwemo wale ambao wameathirika moja kwa moja na mgogoro huu, amani na utulivu ni hitaji muhimu sana kwa ajili ya maendeleo na umoja wa Afrika, Mh.Rais kwa mara nyingine tena nakushukuru kwa mapokezi mazuri yanayotufanya tujisikie tuko nyumbani, asanteni sana