Mkoa wa Tabora unaongoza Mikoa ya Kanda ya Kati kwa Tanzania Bara kwa uwiano mkubwa kati ya Wakazi wa Mkoa huo na laini za simu zilizosajiliwa, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za mawasiliano nchini, hadi Juni 2022 laini 3,000,849 za simu zilikuwa zimesajiliwa Mkoa wa Tabora, wenye Wakazi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya Milioni mbili.
Takwimu hizo za kila robo mwaka, zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonyesha kwamba Singida ni ya pili kwa wingi wa laini zilizosajiliwa, kwa Kanda ya Kati ikiwa na laini 1,397,359, aidha takwimu hizo zinaonesha kwamba jumla ya laini 56,153,097 zilikuwa zimesajiliwa hadi Juni 2022 kwa nchi nzima; huku mikoa 10 ikisajili zaidi ya laini milioni mbili kila mmoja.
Baadhi ya Idadi ya laini zilizosajiliwa kwenye mikoa hiyo, ni Tabora 3,000,849, Kigoma 1,257,318, Singida 1,397,359, Mbeya 2,961,516, Morogoro 2,945,790, Dodoma 2,864,302, Kilimanjaro 2,211,867, Tanga 2,098,929, na Geita 2,050,124.
Hata hivyo, ifahamike kwamba idadi ya laini zilizosajiliwa hailingani na idadi ya Watumiaji, ambao ni wachache zaidi kwakuwa kuna Watu wenye laini zaidi ya moja, kanuni zinaruhusu Mtu kusajili hadi laini tano (5) kwa matumizi mbalimbali, kwa mfano intaneti.
Vilevile, kuna sababu nyingi zinazofanya Watu kuwa na zaidi ya laini moja; zikiwemo kutokupatikana huduma za mtandao husika eneo fulani au utaratibu wa baadhi ya ofisi ambamo Watumishi wanapewa namba za kazini na wanakuwa na za binafsi.