Siku za hivi karibuni imekuwa ni fahari au kawaida kwa watu wengi kuishi pamoja na mbwa au paka ndani ya nyumba zao.
Tunaweza kusema ni usasa, kwani wakati mwingine, mbwa hao wamekuwa wakibebwa na kubembelezwa mithili ya binadamu, wakati mwingine hata kulala kitandani katika viti na wengine kupewa mahitaji yote ya kibinadamu.
Hapa nchini hili limeonekana kufanywa zaidi na mstaa wa tasnia ya burudani.
Baadhi wamekuwa wakiambatana na mbwa hao kila sehemu wanayokwenda, kuwabeba mikononi na kuwabusu pale wanapoona inastahili.
Kituo cha Udhibiti wa magonjwa nchini Marekani ‘Center for Disease Control (CDC)’ kinaonyesha kuwa uwepo kwa mbwa hao katika nyumba husaidia kuwaondolea watu msongo wa mawazo, lakini pia kinatahadharisha uwezekano wa wamiliki kupata magonjwa kutoka kwa mbwa hao.
Hiyo ni kwa sababu mbwa hao wakati mwingine hubeba vijidudu au bakteria ambao husababisha maradhi. Magonjwa hayo wakati mwingine huwa madogo madogo na mengine makubwa.
Kwa mujibu wa CDC, yapo magonjwa, bakteria, minyoo, kupe na viroboti kwa ujumla wake takribani 17 anavyoweza kuambukizwa binadamu kutoka kwa mbwa.
Baadhi ya magonjwa ni kichaa cha mbwa ambacho hutokea mhusika anapong’atwa, lakini bakteria, minyoo na wadudu wengine humuathiri mtu bila kung’atwa.
Yapo magonjwa mengine ambayo binadamu huweza kuyapata kwa kumgusa au kumshika mbwa aliyeathiriwa na ugonjwa huo.
View attachment 1962569