Serikali imeeleza kuwa inakusudia kuanzisha vituo vya kulea vipaji katika shule mbalimbali na katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, ili kuhakikisha vipaji vya Watoto havipotei.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ametoa kauli hiyo leo katika uzinduzi wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) inayofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara huku Mgeni rasmi akiwa ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Bashungwa amesema mashindano hayo ni msingi wa kuvumbua vipaji maana ili kufanya vizuri katika michezo ni lazima uimara uanzie chini, mashindano yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya TAMISEMI.
Bashungwa amesema ili kukuza vipaji zaidi katika uzinduzi huu wamealikwa wavumbua vipaji kutoka vilabu mbalimbali nchini, Taasisi ya Mbwana Samatta na mawakala kutoka nchini Sweden.