Wakazi wa mtaa wa Bugando jijini Mwanza wamevamia nyumba ya mwenyekiti wa mtaa huo wakishinikiza awasilishe Sh1.2 milioni walizochangishwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na ofisi ya mtaa.
Akizungumza na Mwananchi Digital mkazi wa mtaa huo, Matiko Mwiteki amesema walikuwa wakichangishwa Sh1,000 kila Jumamosi kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa mita 300 kwa kiwango cha changarawe.
"Tunahofu kwamba fedha tulizochanga zimeliwa kwa sababu mwenyekiti kila tukimwambia atoe fedha hizo ili tununue vifaa vya kujengea barabara anatupiga chenga wakati mwingine anatumia lugha ya ubabe kutushinikiza tusifuatilie," amesema Mwiteki.
Jeni Yusuph amesema kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa na mlima mrefu, wakazi wa eneo hilo wanalazimika kubeba wagonjwa mgongoni au kwa kutumia machela kuwapeleka hospitali.
"Hapa ni karibu na hospitali ya Bugando lakini wajawazito wanapozidiwa tunalazimika kuwabeba mgongoni ili tuwapeleke hospitali kwa sababu huku magari hayafiki wala pikipiki," amesema Jeni.
Akijibu tuhuma hizo mwenyekiti huyo, Jumah Masanja amekana kutumia fedha hizo akiahidi kwamba fedha hizo hazitatolewa kama utaratibu wa kutoa fedha benki hautazingatiwa.