Tai
Ndege huyu ana kila aina ya sifa ambazo hujitokeza kwa ndege wenzie, pia ni ndege ambaye jina lake linajitokeza hata katika vitabu vya dini, kwa asili ni ndege mkorofi sana, si kwa wanyama wengine anaopenda kuwabughuzi kwa kuwaparua kwa makucha yake, bali hata ndege wenzie huionja shubiri yake, achilia mbali mchezo wake wa kunyang'anya chakula kwa binadamu, ni ndege mwenye nguvu sana kiasi cha kufanya baadhi ya Mataifa makubwa kumtumia kama mnyama wa Taifa, kwa Afrika Egypt wamempa heshima hiyo, na Taifa la marekani wanafanya hivyo pia.
Pamoja na sifa hiyo pia Tai ni ndege mwenye mbio sana, ukimtoa ndege kozi ni yeye ambaye hufuata kwa kukimbia, zipo aina nyingi sana za Tai na kila mmoja wao hubeba sifa yake ya upekee, wapo ambao hukimbia sana, wapo ambao ni wakatili sana, wapo wapole na wengine wengi wenye sifa kem kem.
Unapomuona jicho lake huwa na rangi nyeusi iliyotawala sana, mdomo wake umechongoka, miguu yenye nguvu na kucha kali, mbawa zake ni kubwa sana na ndio humfanya aonekane na kimo kikubwa zaidi pamoja kwamba mwili wake si mkubwa sana, uzito wake hucheza kati ya kg 4 mpaka 8, miaka yake ya kuishi huwa ni zaidi ya 25, na chakula chake kikuu ni nyama, huweza kula mizoga, nyoka wakubwa, wanyama wadogo nk.