Tafasiri Unavyoweza: Usile Mbegu, Kesho Ina Mtondogoo
Hali ya utu uzima ina mengi na wala haihusiani na kuwa na umri mkubwa peke yake. Utu uzima unahusisha zaidi ya miaka mingi, well, kwa wengi inajulikana umri wa utu uzima unaanzia miaka 30, unaweza kuwa na maoni yako juu ya umri huu lakini safu hii inaitwa tafasiri unavyoweza, kwa hiyo kama utatafasiri vinginevyo basi utakuwa umeitendea haki kona hii. Kikubwa hapa ni kutambua kuwa utu uzima unaendana na majukumu mbalimbali, kuanzia ya kifamilia, kisiasa na kijamii kwa ujumla.
Mtu mzima timamu, aliyekamilika anasifa moja kubwa ambayo tunaweza kuiita mwendelezo (generativity), hii ni hulka ya kutaka kuleta mabadiliko si kwako binafsi bali kwa jamii nzima. Ndiyo maana tunajitahidi kujifamilisha, kufanya kazi na shughuli zozote za maendeleo ambazo nazo tunajitahidi ziache alama (legacy). Pamoja na hali hii ya kuwiwa kuchangia katika jamii kuna utu uzima mwingine ambao umetawaliwa na kukata tamaa (stagnation) na kujiona kuwa huwezi kuchangia chochote kwenye jamii. Haya yalielezwa vizuri na msomi wa mambo ya saikolojia, jina lake Erik erickson unaweza kumsoma kwa muda wako.
Hapa leo ni kutaa kukumbushana tu kuwa utu uzima maana yake ni majukumu, majukumu ambayo yanaifanya leo iwe nzuri na kesho iwe bora zaidi. Utu uzima uzalishe kutokana na mtaji ulionao na ukumbuke kuwa kuna kesho na kesho kutwa hivyo hakuna haja ya kuwa mroho, mbinafsi na kujikuta unakula hadi mbegu. Matokeo yake unashindwa kuacha chata (making your mark).
Wengi tulio humu tuko kwenye utu uzima na ni muhimu kutimiza wajibu wetu utakaotufanya tukumbukwe kwa sisi kuwepo hapa kabla hatujayajaza makaburi. Kama ni kulea familia basi tuilee kwenye misingi inayohimiza uwajibikaji na kujitegemea, hii itatusaidia leo na ni mbegu nzuri ya kesho. Kukata tamaa ni sumu inayokuua wewe na jamii nzima. usiwe mbinafsi, kuwa mwendelevu na si mkata tamaa hata kama milima ni mingi