Tafasiri Unavyoweza: Kosa Kusiasisha Elimu
Maendeleo katika jamii ya kidemokrasia yanahusiana sana na utashi wa kisiasa. siasa kama sayansi ya nani anapata nini wakati gani ni mfumo unaolenga kujenga jamii yenye kuheshimu na kukubaliana kutokubaliana katika mambo yanayolisukuma taifa mbele. Utashi wa kisiasa unapolenga maslahi ya binafsi na kujipendelea basi wengi wataumia. Utashi sahihi wa kisiasa kwenye elimu unafanya elimu kuwa bora kwa wote. Tunachokiona kwenye taifa letu kwa sasa ni tofauti, utashi wa kisiasa unaua elimu ya watoto wetu. Tafasiri unavyoweza.
Hivi karibuni kumekuwa na picha mbalimbali zinasambaa kweye makundi ya WhatsApp na mitandaoni kuhusu vitabu vya shule ya msingi vilivyokosewa na kujaa upotoshi mkubwa na mbaya zaidi vitabu hivi vipo mashuleni. Nikiwa kama mtu ambaye amewahi kushika chaki (sijawahi kusomea ualimu) na kujaribu kuondoa ujinga kwa wanafunzi, natambua kabisa mika ya nyuma mwalimu anatoka chuoni anajua anafundisha nini, ana kitabu cha kufundishia na kitabu cha mwongozo (kitabu cha majibu).
Bodi ya vifaa vya kielimu (EMAC) iliundwa na kupitisha vitabu vya kufundishia, lakini wabunge wetu wakaiua na kufanya soko holela na sasa tunaona vitabu wanavyopelekewa watoto wetu mashuleni havina ubora na vimejaa upotoshaji mkubwa. Hii ni hatari kwa afya ya taifa la leo, kesho na keshokutwa. Wabunge wengi hawajui wanafanya nini wanapoamua kuchezea elimu yetu, walipoharibu kwa azimio lao la mwaka 2013 (kuiua Emac kwa kuleta OAS-Open-ended Approval System) wakaanza kupiga kelele baada ya kuambiwa mnakosea na wakaja na TIE na bado tunaona tatizo kwenye vitabu. Elimu holela haisaidii taifa, wabunge tumieni akili na nafasi yenu kuifanya elimu yetu iwe bora na shindani kwenye dunia ya sasa.