Makapuku Forum

Makapuku Forum

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 19
ILIPOISHIA:
Kuna wakati hofu ilinizidi na kutaka nigeuze nilikotoka lakini kitu ndani ya moyo wangu kikaniambia nizidi kusonga mbele. Kadiri nilivyokuwa nazidi kusonga mbele ndivyo zile sauti zilivyokuwa zinazidi kuongezeka, nikazidi kutetemeka kwa hofu huku nikiwa sijui nini itakuwa hatma yangu.
SASA ENDELEA...

Sauti zilizidi kuongezeka, nikawa nasikia sauti nyingine zikiugulia maumivu makali mno, nilitamani nione nini kilichokuwa kinaendelea lakini sikuweza kutokana na lile giza. Ilifika mahali ikabidi niwe natembea kwa uangalifu sana kwani nilihisi nilikuwa nikipita jirani kabisa na wale watu waliokuwa wakilia kwa maumivu makali.
Kiasili mimi ni mwoga sana kiasi kwamba nikiwa nyumbani kwangu, hata panya akipita darini kwa kasi, lazima nitashtuka sana lakini nashangaa siku hiyo kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo hofu ilivyokuwa inazidi kupungua.
Haikuwa rahisi kupita sehemu ambayo unasikia kabisa wenzako wanalia kwa kusaga meno kwa maumivu makali kama ile. Ukiachilia mbali sauti hizo za watu, kulikuwa pia na sauti za watoto wachanga waliokuwa wamepamba moto kulia, ungeweza kudhani wamelazwa kwenye siafu.
Nilizidi kutembea kusonga mbele kufuata ile sauti iliyokuwa ikiliita jina langu, zile sauti za watu zikaanza kupungua kidogo kuonesha kwamba tayari nilishapita eneo walilokuwepo, zikawa zinasikika za wale watoto wachanga huku pia sauti za wanyama wakali nazo zikianza kuongezeka.
Nikiwa naendelea kutembea, nilishtukia sauti ya kutisha ya ndege mkubwa ikija kwa kasi pale nilipokuwepo, kufumba na kufumbua nilijikuta nikipigwa kikumbo na ndege yule mkubwa ambaye hata sikuweza kujua ni ndege gani kutokana na jinsi alivyokuwa mkubwa.
Kucha zake kali zikaniparua upande wa shavu langu la kushoto na kunifanya nijihisi maumivu makali sana. Hata hivyo, nilijikaza na kuendelea kusonga mbele. Lile dege ambalo baada ya kunipiga kikumbo lilipotelea mbali, nililisikia likianza kurudi tena, safari hii likipiga kelele kwa sauti kubwa kuliko mwanzo.
Sikumbuki kama katika maisha yangu ya kawaida nimewahi kusikia mlio wa namna hiyo wa ndege. Ilibidi niwe makini lisije kuniumiza tena, nikainua mikono na kujiziba upande wa usoni, likaja kwa kasi na kunipita, nikasikia upepo ukinipuliza kisha likatokomea kule ile sauti iliyokuwa ikiniita ilikokuwa inatokea.
Nilipojigeuza pale lilipokuwa limeniparua, niligundua kwamba vitu vya majimaji vilikuwa vikinitoka. Niliamini kwamba ni damu kwa sababu binadamu anapoumia, kinachotoka ni damu ingawa kutokana na giza lile, sikuweza kuthibitisha hilo zaidi ya kuendelea kujiaminisha mwenyewe.
Nikiwa nazidi kuelekea kule ile sauti ilikotokea, kwa mbali nilianza kuona kama mwanga hafifu ukionekana mita nyingi kutoka pale nilipokuwa nimefika. Nilishusha pumzi ndefu kwa sababu niliamini mwanga ni dalili ya uhai, nikajua lazima naweza kupata msaada nikifika pale kwani mpaka muda huo, sikuwa naelewa nini itakuwa hatima yangu.
Milio ya wanyama wa kutisha ilizidi kusikika kutoka kila upande lakini sikukata tamaa, nilizidi kusonga mbele huku giza bado likiwa nene vilevile, akili zangu zote zikiwa ni kwenye ule mwanga niliokuwa nauona. Cha ajabu, licha ya kutembea sana, bado ule mwanga uliendelea kuonekana ukiwa umbali uleule, jambo ambalo lilinishangaza sana.
Nilijaribu kuongeza urefu wa hatua lakini ilikuwa sawa na kazi bure, miungurumo ya wanyama wakali ikawa inazidi kuongezeka huku kwa mbali nikisikia sauti kama za yule ndege mkubwa aliyenijeruhi zikija tena lakini tofauti na awali, safari hii ilionesha kwamba walikuwa zaidi ya mmoja kutokana na ukubwa wa sauti zao.
“Mungu wangu, nimekwisha,” nilijikuta nikijisemea moyoni lakini jambo la ajabu tena, wakati mimi nikiamini maneno hayo niliyasemea moyoni, yalisikika kwa sauti kubwa utafikiri nimezungumza kwa kufumbua mdomo.
“Jamal mbona hufiki? Fanya haraka,” ile sauti iliyoniita ilisikika tena kutokea umbali ambao siwezi kuukadiria, nikataka nifumbue mdomo na kumuuliza yule mtu aliyekuwa ananiita ni nani, pale ni wapi na nilipelekwa pale kufanya nini lakini nilipofumbua mdomo, nilishangaa sauti ikiwa haitoki.
“Leo ndiyo mwisho wa maisha yangu,” nilijisemea moyoni baada ya kuona nimeshindwa kuwasiliana na yule mtu lakini cha ajabu tena, sauti ilisikika kwa nguvu. Nilishangaa sana, yaani nikifumbua mdomo na kuzungumza, sauti haisikiki lakini nikizungumza kimoyomoyo ndiyo sauti inasikika, nilibaki nimepigwa na butwaa.
Niliamua kujaribu kitu, kuzungumza kimoyomoyo kumuuliza yule mtu yale niliyotaka kumuuliza. Cha ajabu sasa, sauti yangu ndiyo ilisikika kwa nguvu na naamini yule mtu aliyekuwa ananipa maelekezo alinisikia.
“Wewe ni nani? Hapa ni wapi na kwa nini nimeletwa huku?”
“Mh! Hutakiwi kuuliza swali lolote,” ilisikika sauti ile kwa mwangwi mkubwa kama ilivyokuwa mwanzo.
“Mbona natembea lakini sifiki?” nilijisemea tena moyoni lakini sauti ikasikika vizuri kabisa.
“Geuka ulikotoka,” ilisikika ile sauti, safari hii milio ya wale ndege wakubwa ilikuwa imekaribia kabisa na kwa jinsi walivyokuwa wanakuja kwa kasi, nilijua lazima watanijeruhi tena.
Nilijaribu kugeuka kwa kutumia upande wa kulia lakini nikashangaa mwili wangu ukiwa mzito mno, nikajaribu upande wa kushoto, nikageuka bila tatizo lolote, nikawa natazama kule nilikotokea ambako nako kulikuwa na giza totoro kama kule nilikokuwa naelekea, tofauti yake ni kwamba huku nilikogeukia hakukuwa na mwanga unaoonekana kwa mbali.
“Haya tembea kinyumenyume,” ilisikika ile sauti, kweli nilipojaribu kupiga hatua moja tu, nilijikuta mwili ukiwa mwepesi sana, nikawa naenda bila kikwazo chochote, huku nyuma sauti za wale ndege zikawa zinazidi kufifia. Ndani ya muda mfupi tu, tayari nilikuwa nimefika pale ule mwanga ulipokuwa unatokea, niliisikia ile sauti ikiniamuru kugeuka, nikafanya hivyo, macho yangu yakatua kwenye jiwe la ukubwa wa wastani lililokuwa likiwaka bila kuteketea.
Nilishangaa sana kuona jiwe likiwaka, tena moto mkali unaoweza hata kuchemsha maji ndani ya muda mfupi. Hata hivyo, licha ya kwamba jiwe hilo lilikuwa likiwaka, mwanga wake haukuweza kunisaidia kuona chochote, nikawa naangaza macho huku na kule nikitarajia naweza kumuona yule mtu aliyekuwa ananipa maelekezo lakini haikuwa hivyo.
Kufumba na kufumbua, lile jiwe lilianza kutetemeka kama kuna tetemeko la ardhi kisha likaanza kubingirika kuelekea upande wa kushoto kutoka pale lilipokuwepo. Nilishtuka mno, nikawa natetemeka kwa hofu kubwa. Likaendelea kubingirika kwa kasi huku ikionesha kwamba kule lilikokuwa likiendelea kulikuwa na mteremko.
Sijui akili gani ilinituma kuanza kulifuata lile jiwe kwani hakika huo haukuwa uamuzi sahihi. Nilipopiga tu hatua moja, nilijikuta nikianza kuserereka kuelekea kule lile jiwe lilikokuwa linaelekea.
Nilijaribu kufunga breki lakini ilikuwa sawa na kazi bure, niliendelea kuserereka na kila nilipojaribu kujishikiza sehemu, sikuona chochote cha kunisapoti, ikafika mahali na mimi nikawa nabingirika kulifuata lile jiwe huku mteremko ukizidi kuwa mkali kadiri nilivyokuwa nasonga mbele.
Kwa mbali nilianza kuhisi joto kali huku lile giza nene likianza kupungua na kumezwa na mwanga mwekundu ambao hata bila kuuliza, nilijua kuwa ni wa moto mkubwa uliokuwa unawaka. Zile sauti za watu waliokuwa wakilia kwa maumivu makali, nilianza kuzisikia tena lakini tofauti na awali, safari hii zilikuwa kubwa zaidi huku ikionesha kwamba zilikuwa zikitoka kwa kundi kubwa la watu.
Nilizidi kuserereka kwa kasi kubwa kuelekea kule chini huku joto nalo likizidi kuongezeka. Nikiwa mdogo nimewahi kusikia kwamba Jehanum kuna moto mkali unaowaka muda wote, ambao ni maalum kwa ajili ya kuwateketeza watu wanaofanya dhambi duniani.
Nilianza kuhisi kwamba huenda kule nilikokuwa nikisererekea ni kwenye moto wa Jehanum na zile sauti za watu waliokuwa wakilia kwa kusaga meno walikuwa ni watu wenye dhambi, nikajikuta nikitetemeka kuliko kawaida.
Mpaka muda huo nilikuwa nimeshindwa kabisa kujizuia nisiendelee kuporomokea kule chini, kwa mbali nikaanza kuliona shimo kubwa ambalo ukubwa wake hata sijui nifananishe na nini lakini kwa kifupi lilikuwa kubwa mno, lisilo na mwisho, moto mkali ukiwa unawaka ndani yake. Kibaya zaidi, na mimi nilikuwa nikiendelea kuporomoka kuelekea ndani ya shimo hilo, nikajua huo ndiyo mwisho wangu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue
 
Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 20
ILIPOSHIA:
Mpaka muda huo nilikuwa nimeshindwa kabisa kujizuia nisiendelee kuporomokea kule chini, kwa mbali nikaanza kuliona shimo kubwa ambalo ukubwa wake hata sijui nifananishe na nini lakini kwa kifupi lilikuwa kubwa mno, lisilo na mwisho, moto mkali ukiwa unawaka ndani yake. Kibaya zaidi, na mimi nilikuwa nikiendelea kuporomoka kuelekea ndani ya shimo hilo, nikajua huo ndiyo mwisho wangu.
SASA ENDELEA...
“Jamal! Jamal! Don’t go my love, come back to me! Come back Jamal,” (Jamal! Jamal! Usiende mpenzi wangu, rudi kwangu! Rudi kwangu Jamal) wakati nikiendelea kuporomokea kule kwenye lile shimo kubwa lililokuwa na moto mkali ambao siwezi kuuelezea, nilisikia sauti ikiniita.
Tofauti na sauti za kutishatisha nilizokuwa nikizisikia, hii ilionesha dhahiri kwamba siyo ngeni masikioni mwangu. Ilikuwa ni sauti ambayo niliitambua kuwa ni ya Raya, msichana aliyetokea kunipenda kwa moyo wake wote.
Raya alikuwa akipaza sauti huku akilia, maneno aliyokuwa akiniambia yalinichoma sana moyoni mwangu.
Katika hali ambayo sijui niielezeeje, nilijikuta nikipata nguvu kubwa kutoka ndani, nikajipindua kwa nguvu na kujikuta ile kasi ya kuporomokea kule chini inapungua, nikazidi kufurukuta kupambana na ile nguvu kubwa iliyokuwa inanivuta na hatimaye nikajikuta nikiangukia sehemu nyingine tofauti kabisa na kule nilikokuwa nikielekea.
Pale nilipoangukia, palikuwa na unyevunyevu mkubwa chini utafikiri nimekanyaga matope lakini giza lilikuwa nene pengine hata kule nilikotoka, nikawa naangaza macho huku na kule lakini sikuweza kuona chochote. Ukimya wa ajabu ukatanda kiasi cha kunifanya nianze kuyasikia mapigo ya moyo wangu yalivyokuwa yakinidunda.
Kufumba na kufumbua, nilijikuta nimerudi pale nilipokuwepo mwanzoni kabisa, kwenye kona ya ile wodi niliyolazwa. Kama ilivyokuwa mwanzo, nilikuwa nauona mwili wangu ukiwa umelazwa pale kitandani lakini tofauti na awali, safari hii nilikuta ubize mle ndani ya wodi ukiwa umeongezeka sana.
Madaktari walikuwa wakipigana vikumbo, kila nesi alikuwa bize kuhakikisha anaokoa maisha yangu. Sikuelewa nini kimetokea mpaka ubize uongezeke kiasi kile lakini niliwasikia baadhi ya madaktari wakijadiliana kwamba kilichonitokea kilikuwa kitu adimu sana.
“His heartbeats almost stopped but now they are stabilizing, ooh my God he was dead!” (Mapigo ya moyo wake yalisimama kabisa lakini sasa naona yameanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida, ooh Mungu wangu, alikuwa tayari amekufa).
“It’s my eleventh year in this career and I have never witnessed something like this,” (Huu ni mwaka wangu wa kumi na moja nafanya kazi hii, sijawahi kushuhudia tukio kama hili) alisema daktari mmoja, kila mtu akawa anaendelea kuzungumza lake.
Bado niliendelea kujiuliza maswali mengi bila majibu lakini kwa jinsi mazungumzo hayo yalivyokuwa yakiendelea, inaonesha nilikuwa nimetokewa na jambo baya sana. Nikiwa bado palepale kwenye kona ya ile wodi, nikiangalia kila kilichokuwa kinaendelea mle ndani, niliisikia tena ile sauti niliyoisikia muda mfupi uliopita, tena ikizungumza maneno yaleyale.
“Jamal! Jamal! Don’t go my love, come back to me! Come back Jamal,” (Jamal! Jamal! Usiende mpenzi wangu, rudi kwangu! Rudi kwangu Jamal).
Ilikuwa ni sauti ya Raya na ilionesha ikitokea nje ya ile wodi. Nilijikuta nikiwa na shauku ya kutaka kumuona Raya, ile kuwaza tu kwamba nataka kumuona, nilijikuta tayari namtazama lakini katika mazingira ambayo yalionesha kwamba yeye pamoja na watu wengine wote waliokuwa wamemzunguka, hawakuwa na taarifa juu ya uwepo wangu mahali pale.
“Jamal is dead! (Jamal amekufa) Nitakuwa mgeni wa nani mimii? Eeeh Mungu, kwa nini mimi? Why?”
“Raya ukilia sana unakufuru. Wewe unajua jinsi Jamal alivyo rafiki yangu kipenzi lakini mwenzio bado sitaki kuamini kama ni kweli ametangulia mbele za haki. Hebu jikaze, tunaweza kuwa tunamchulia akafa kweli.”
“Usinipe moyo Justice, wote tumeshuhudia mashine ya kusoma mapigo yake ya moyo ikishuka mpaka mwisho kuonesha kwamba mapigo yake ya moyo yamesimama, madaktari wamefanya kila kitu na kujiridhisha kwamba amekufa, ina maana huamini tu?”
“Angekuwa ameshakufa angezungushiwa shuka la kijani pale kitandani kwake na madaktari wote ungeona wameshatoka chumba cha wagonjwa mahututi, mimi naamini bado yupo hai,” Justice na Raya walikuwa wakizungumza pale nje, Raya akilia kwa uchungu huku wafanyakazi wenzao kadhaa pamoja na watu wengine, wakisaidiana kumtuliza msichana huyo.
Pembeni kulikuwa na kundi lingine la watu ambao siwafahamu vizuri, lakini nao walionesha kufika pale kwa sababu yangu, muda mwingi wakawa wanajadiliana huku wakiwatazama akina Raya.
Niliwaona pia waandishi wawili wa habari, mmoja nadhani alikuwa anatoka kwenye kituo cha runinga na mwingine wa magazeti. Niliwatambua hivyo kutokana na jinsi walivyokuwa wamevaa na zana za kazi ambazo kila mmoja alikuwa amebeba. Nilijaribu kuangaza huku na kule kuangalia kama nitamuona Shenaiza lakini hakuwepo eneo hilo.
Nilitamani sana kujua ukweli wa mambo yote ambayo Shenaiza alikuwa akinificha lakini sikujua nitaanzia wapi. Yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha matatizo yote yaliyonitokea lakini cha ajabu ni kwamba hata mimi, muathirika namba moja wa mambo yote yale yaliyokuwa yakiendelea kutokea, nilikuwa sielewi hasa nini kilichojificha nyuma ya pazia.
Kwa tafsiri nyepesi nyepesi, kama Mungu angeamua kunichukua moja kwa moja, ningeacha maswali mengi sana ambayo hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuyajibu, zaidi ya Shenaiza mwenyewe. Hali ilikuwa ya simanzi kubwa pale nje ya hospitali, niliwaona watu wengine wakizungumza na simu, kila mmoja akilitaja jina langu.
Maneno mengi yalikuwa yakiendelea kumtoka Raya, akiendelea kulia kwa uchungu kiasi cha kufikia hatua ya kukufuru. Kwa juujuu tu, kupitia maelezo yake pamoja na yale niliyoyasikia kule ndani kwa madaktari, nilielewa kilichokuwa kimetokea.
Ilionesha kwamba, kuna muda mapigo ya moyo wangu yalisimama, kwa tafsiri nyepesi, kuna muda nilikufa! Lilikuwa ni jambo la ajabu ambalo lilinitisha sana. Sikuelewa ni muda gani nilikuwa nimekufa kwa sababu muda wote nilikuwa timamu na nilikuwa naelewa kila kilichokuwa kinaendelea.
Sikukumbuka muda ambao pengine nilipoteza fahamu au sikuwa naelewa kinachoendelea! Nasisitiza tena, muda wote nilikuwa na akili zangu timamu. Nilijisikia uchungu sana kwa jinsi Raya alivyokuwa akilia, ukichanganya na hofu kubwa niliyokuwa nayo, nilijikuta nikianza kutokwa na machozi. Ajabu ni kwamba, wakati mimi nikiendelea kulia, wale madaktari pale kitandani walishtuka baada ya kuona mwili wangu nao ukitokwa na machozi, wakawa wanatazamana. Nikiwa naendelea kulia, nilipaliwa na mate, hali iliyofanya nikohoe mfululizo, ajabu zaidi, na ule mwili wangu pale kitandani ukakohoa, madaktari wakazidi kupigwa na butwaa, wakawa wanatazamana wakiwa ni kama hawaamini kilichokuwa kinatokea.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom