......
SEHEMU YA 01
Tarehe 09 disemba, Dar es salaam Tanzania hali ilirudi kuwa ya Mzizima Tanganyika. Shangwe za sikukuu ya uhuru zilizimwa kwa vilio na majonzi. Furaha zilisalimu amri na huzuni kutwaa utawala . Nafsi za waja zilifunikwa ukiwa kwa gubiko la simanzi. Si kwa raia tu na viongozi wa dini bali hadi kwa wakuu wa nchi na wapinzani. Kila mtu aliguswa kwa namna yake kwa kilichotokea. Haikuwa rahisi kuamini lakini ukweli ulichukua hatamu yake. Kijana mashuhuri aliyevuma na kutikisa nchi na mipaka yake hatimaye ameenda jumla. Pumzi zake zimekatika wala si wa kujitingisha tena. Amelala katika usingizi wa wafu usio uamsho hadi siku ya mwisho. Ingawa kifo ni haki ya kila kiumbe lakini kwake kiligeuka dhuluma machoni mwa waja.
Kifo cha yatima wa fukara aliyeingia kwenye historia ya dunia akiwa si kiongozi wa dini, mwanasiasa ama mfanya biashara mkubwa. Vilevile hakuwa mtoto wa tajiri wala hakuwa mtoto wa kiongozi yeyote wa nchi. Hakuwa msanii, mwanahabari wala hakuwa mtoto wa mtu maarufu. Na ajabu hata jina lake halisi tu walilijua watu wachache.
Alizaliwa na kupokewa kama mwana mtumwa kwenye nchi yake lakini leo hii amekufa na kuagwa kama mwana mfalme wa dunia.
Umati uliojitokeza kumuaga toka ndani na nje ya nchi ulitosha kutafsiri kiasi gani alikuwa nyota adhimu ya shani iliyopamba uso wa dunia. Wengi walisikika wakilaumu kwa masikitiko kwanini Mungu amemchukua mapema vile! miaka ishirini tu?
"Ametutoka akiwa bado mdogo kipindi taifa na dunia ikimuhitaji sana."
Maneno ya mkuu wa nchi yalitosha kuwaliza wengi na kuonesha kiasi gani mtajwa alikuwa ndani ya mboni ya nchi na dunia kwa manufaa makubwa ya baadae.
'GERMAN MACHINE'
ama kweli maneno huumba.....!
Nikiwa nimesimama kwenye mstari miongoni mwa watanzania wengi waliojitokeza siku hiyo kumuaga kijana mwenzetu aliyetangulia mbele za haki. Nilishindwa kuzuia machozi kila nilipoutazama umati uliofurika wakiongozwa na mkuu wa nchi kumuaga rafiki yangu kipenzi. Rafiki tangia shule utoto. Mtu wangu wa karibu ambaye niliyajua mengi ya moyo wake. Siri yake siri yangu na ya kwangu siri yake. Ingawa wengi walilia na kusikitika kuwa amekufa kabla hajatimiza ndoto zake, lakini mimi pekee nilikiri na kuamini kuwa ndoto zake zilitimia. Niliyasikia maneno yake yakijirudia kichwani mwangu na kunithibitishia kwa kile nilichokuwa nakiona.
"HAKIKA NI KWELI UTABAKI KUWA GERMAN MACHINE"
Niliipaza sauti mara msafara wa magari ulipoingia kulisindikiza gari iliyobeba mwili wake swahiba. Gari ambayo mbele ilikuwa na bendera mbili ya Tanzania na Ujerumani zikipepea kwa pamoja kama ambavyo watu wengi walikuwa wameshika wakipepeesha bendera hizo mikononi katika moja ya heshima na kumuenzi marehemu. Heshima ambayo niliikumbuka miaka ya nyuma ilionekana kiburi, dharau na utovu mkuu wa nidhamu tangia namjua mara ya kwanza.
Kumbukumbu zangu zilinirudisha nyuma nikiwa katikati ya tukio lile zito la kihistoria.
* * * *
||MIAKA 12 NYUMA||
"German Machine.......! German Machinee..! Nani huyu anayechafua daftari la somo langu kwa kuandika majina ya ajabu ajabu eeeh! Nani huyu German Machine?"
Sauti ya mwalimu wa kike ilisikika ikifoka kwa ukali ndani ya darasa. Moyo wangu ulipasuka na kushangaa kusikia mtu ameandika jina kama hilo kwenye daftari la shule. Wanafunzi walibaki wakitazamana kujua nani huyo mwenye jina hilo alilouliza mwalimu. Mwalimu alizidi kukunja ndita baada ya kuona hakuna aliyejitokeza huku macho yake akiyaelekeza zaidi nyuma ya darasa mahali nilipokuwa nimekaa na kunifanya moyo uzidi kwenda mbio kwa kuhisi mimi ndiye mshukiwa namba moja.
"Ina maana hayupo eeeh! nanyi mmeamua kumficha si ndio? sasa adhabu itapita darasa zima mpaka mumtaje huyu German Machine ni nani" Mwalimu aliwaka zaidi huku akilipiga piga kwa fimbo daftari aliloshika na kuanza kupiga hatua kuelekea upande ule wa nyuma nilipokuwa nimeketi dawatini. Nilitazama kushoto pembeni ya dawati ndipo niligundua mwenzangu tuliyekaa dawati moja kuwa muda wote alikuwa amelala kwa kuegesha kichwa kwenye meza ya dawati.
"Weweee! hebu amka." Alifoka mwalimu alipofika huku akimtikisa yule jirani yangu na kumstua kwenye usingizi mzito uliompitia pale darasani.
"Ina maana kwenu hulali eeeh! kwa adhabu yako naanza na wewe japo mgeni...! Unamjua mwenye hili daftari?" Aliongea mwalimu yule wa kike ambae wanafunzi wengi walimuogopa kwa ubabe na ukali wake wa kutopenda masihara wala utani. Alimkazia macho huku akimuonesha lile daftari lililoandikwa nje maneno kwa herufi kubwa zilizopambwa vizuri yakisomeka GERMAN MACHINE.
Ajabu katika hali si ya kawaida hakustuka yule mwanafunzi alipoliona daftari zaidi alinyoosha mkono kulipokea huku akijibu kwa kujiamini.
"La kwangu mwalimu."
"La kwako...?!" Alishangaa mwalimu huku akimtazama kwa macho ya staajabu akimpandisha na kumshusha mara mbilimbili. Hapo ndipo darasa zima walipoangua vicheko ingawa mimi nilibaki kimya nikimshangaa yule mwanafunzi ambae pia alikuwa mgeni amehamia hata wiki bado. Kwa picha iliyokuwa inaendelea ilikuwa kama kituko. Mwalimu alimshangaa mwanafunzi huku mwanafunzi naye akimshangaa mwalimu.
"Nyie la sita keleleni kabla sijawabadilikia sasa hivi." Mwalimu alitoa amri kama mwanajeshi, darasa likatulia tuli na ndipo alipomgeukia yule mwanafunzi na kumuuliza kwa ukali.
"wewe! wee unaitwa nani?"
"GERMAN MACHINE."
Alijibu yule mwanafunzi mvulana ambapo kimuonekano tu alikuwa miongoni mwa wanafunzi watoto wadogo wa darasa la sita. Jibu lake lilitushangaza sote na kumkera zaidi mwalimu. Tulibaki tumeachama midomo kwa kumuhurumia tukiamini hamjui yule mwalimu kuwa hafanani na walimu aliowazoea huko alipokuwa anasoma awali.
'PWAAP' Sauti ya kofi kali ilisikika baada ya mwalimu kumzaba yule mwanafunzi kabla hajamshika kola ya shati na kumnyanyua msobemsobe pale kwenye dawati alipokuwa na kumburuza mpaka mbele ya darasa.
"Piga magoti hapa mpuuzi wee samaki mdogo kabisa unanijibu kidharau hivyo? Unaleta uhuni wa kuazima eeeh! Nakuuliza unaitwa nani unazidi kunitajia ujinga wako ulioandika humu? Mmccchhxx" Povu lilimtoka mwalimu na kutoka darasani kwa hasira. Zogo lilianza upya darasani baada ya mwalimu kutoka. Nilishangaa na kumtazama mwanafunzi mwenzangu ambae mimi nilikuwa jirani yake baada ya kuletwa darasani na mwalimu wa darasa aliyempanga kwangu na kutwambia kuwa ni mwenzetu. Sikuwahi kumuuliza jina wala kujenga mazoea naye siku chache tulizokuwa darasani na kwa mara ya kwanza siku hiyo darasa tulimjua na kumshangaa kwanini ameandika jina la utani kwenye daftari la shule. Dakika chache mara jopo la walimu lilivamia darasani. Walimu zaidi ya sita huku wakiwa na bakora mikononi.
"Enhee! mwalimu Kisayo kumbe kitoto chenyewe ndio hiki kilichohamishiwa hapa juzi?"
"Ndio mwalimu. Wewe ndiye mwalimu wake wa darasa je unalijua hilo?"
"Hee! haya maajabu yaani tumepokea mwanafunzi taahira hivi hivi."
Walimu walizidi kuleta nongwa huku darasa zima tukiwa tumetulia tukimtazama mwenzetu kwa huruma akiwa amepiga magoti pale mbele mikono juu. Walimu watatu kati yao nao walikuwa wameshika daftari kila mmoja. Nakumbuka alikuwa mwalimu wa English, Kiswahili na wa Sayansi ambao madaftari yetu toka tuandike na kukusanywa walikuwa hawajasahisha kuturudishia siku hiyo. Wote walionekana kukunja ndita na walichoongea ndipo tulishangaa darasa zima.
"Mmeyaona haya madaftari yalivyochorwa?"
"ndiooooo"
Mwalimu aliuliza na wanafunzi kujibu huku tukiyatazama yale madaftari ambapo kama ilivyokuwa lile la mwalimu Kisayo nayo yalikuwa hayajaandikwa majina yoyote zaidi ya lile jina 'German Machine' sambamba na somo husika tu.
"Twaha?" mwalimu wa darasa aliniita kwa ukali na kuyapandisha mapigo ya moyo huku nikiitika kwa sauti ya hofu.
"Naam, mwalim."
"Njoo mbele pamoja na begi la hiki kimashine cha ujerumani." Aliniamuru nami nilitii agizo kama alivyotaka. Nilichukua mfuko wa rambo mweusi uliokuwa na madaftari machache ndani ambao ndio ulikuwa begi la German Machine na kuwafikishia walimu pale mbele.
"Haya nawe piga magoti hapa." Mwalimu alitoa agizo na kunishangaza. Yaani na mimi napaswa kuadhibiwa? kwa kosa gani haswa? Nilijiuliza moyoni huku nikitii amri na kuungana na mwenzangu pale mbele. Darasa lilizidi kuwa tuli. Mwalimu yule aliupindua ule mfuko wa madaftari na kuyamwaga yote pale chini. Walipoyatazama na yale yote yalikuwa yameandikwa vilevile 'German Machine'. Kitu chengine kilichoonekana kwenye ule mfuko ni kitabu cha kamusi ya kijerumani kwa kiingereza, kamusi ambayo sidhani kama shule nzima ilikuwapo mara baada ya kuwashangaza hata walimu na kumtazama mara mbilimbili.
"Twaha shika chini. Jamani walimu kila mmoja amchape bakora mbili za nguvu huyu kwa kosa la kutomkaribisha vizuri jirani yake na kumwambia taratibu za nidhamu ya shule yetu." Sauti ya mwalimu wa darasa iliamuru na ndipo hapo makalio yangu yalipoanza kupata shuruba ya bakora zaidi ya kumi kutoka kwa walimu wote sita walikuwa darasani muda huo. Niliumia sana na kuchukia kupewa adhabu ambayo sikustahili.
"Wewe nyanyuka twende ofisini." Aliamrishwa mwenzangu na walimu kutoka darasani. Nilimtazama kwa uchungu na hasira kwa kuniponza huku yeye akinitazama kwa upole na tabasamu. Alitolewa mkuku na walimu kama mtuhumiwa mikononi mwa polisi, lakini hakusita kugeuka na kusema.
"Unisamehe bure Twaha kwa kukuponza. Ila ukweli nitabaki kuwa German Machine hata nikifukuzwa na hapa." Alisema maneno yaliyomfanya mwalimu wa nyuma amtie konzi la kichwa na kuwafanya wanafunzi wote wakimbilie madirishani kumtazama kwa nje alivyokuwa anapelekwa ofisini msobe msobe.
Nilistaajabu kwa ujasiri aliouonesha kutetea jina lile hadharani pasipo kuogopa.
Hapo ndipo nilipoijenga shauku na hamu ya kumjua kiundani mwanafunzi huyu ni nani haswa na kwanini anajiita hivyo hata awe radhi kufukuzwa shule lakini si kubadili jina? Ilikuwa ni tukio la ajabu la kwanza kuliona kwake.
Aaaah! German Machine...! ama kweli maneno huumba.
.......