SoC03 Maadili na uwajibikaji ukokotezwe katika utamaduni wa Mtanzania kustaarabisha mifumo ya kisiasa na kijamii nchini

Stories of Change - 2023 Competition

Librarian 105

JF-Expert Member
May 6, 2023
239
325
UTANGULIZI
Ukarimu ni mfano mmojawapo wa kete wanayotumia wanasiasa na viongozi wa serikali kusisitiza Watanzania kuuenzi utamaduni wa Mtanzania. Kimsingi ni malengo yetu sote tuufikie ustaarabu wa kijamii ambao binafsi siuoni ukikidhi kikamilifu vipengele vya utamaduni huo. Isitoshe una kasoro za kimfumo na kiutendaji kuitwa wa kitaifa mbali na changamoto zake za maadili na uwajibikaji pamoja na za kifalsafa kuchochea ustawi wa kisiasa na kiuchumi nchini.

Mapungufu Yake Kimfumo na Kiutendaji:

Ukiondoa lugha ya Taifa pekee. Vipengele vyake vilivyosalia vinakosa mfumo na dhana ya Utaifa kutokana na kujikita kiutendaji kuenzi tamaduni za makabila hususan mila na desturi, sanaa zake kama vile ngoma za asili,mavazi,vyakula na kadhalika. Ushahidi wa hili tunaupata kwa jinsi tunavyoteseka kupata vazi la taifa sambamba na watanzania wengi kuupa kipaumbele utamaduni wa kimagharibi katika kuendea njia zao za maisha ya kila siku.

Mapendekezo Yangu: Itifaki Ya Utamaduni Wa Mtanzania Iratibiwe.

Wakati sahihi uliopaswa kuratibiwa itifaki ya utamaduni wa taifa ilikuwa punde tu baada ya uhuru. Lau ingelikuwepo mapema tusingelijeruhiwa kisiasa na kiuchumi kufuatia ufutwaji wa Azimio La Arusha, kupisha siasa za vyama vingi na uchumi wa soko huria ulioambatana na sera za ubinafsishaji, ukiachilia kashfa za ufisadi na rushwa sasa hivi tunashuhudia vuta nikuvute ya katiba mpya kulinda maslahi ya kisiasa badala ya kukhitilafiana kimtazamo wa namna ya kuijenga nchi yetu kwa misingi ya kidemokrasia na utawala bora.

Kwanini? Tunaendea maisha yetu binafsi na ya kitaifa bila mafungamano ya kimaadili na kiuwajibikaji kuanzia ngazi ya familia hadi taifa. Kwa hiyo uratibu wa Itifaki ya Utamaduni wa Mtanzania inapata umuhimu kuanzia hapa. Na hakika yafaa kuwa tanzu ya Tunu za Taifa ili kuhuhisha zaidi maono ya ; utu, umoja, uzalendo, uadilifu, uwajibikaji, uwazi na lugha ya taifa ; kusawiri barabara vipengele vya itifaki hiyo vya maadili, falsafa, fasihi, sanaa na usanifu. Kwa sababu sheria zinazosimamia maisha ya kijamii uzoefu unaonyesha kuwa hudhibiti kwa njia ya kutawala tu.

Wakati utamaduni unahimiza uchungaji wa maadili na uwajibikaji na pia mtazamo wa kiakili kuendea udhibiti wa kijamii na mazingira yake.

Kwa muktadha huu hakika tunahitaji itifaki ya utamaduni nchini. Ili kuimarisha uwajibikaji kuchagiza ustaarabu na maendeleo ya kisiasa na kiuchumi. Halikadhalika kuwa kama azimio la kupambana na mmomonyoko wa maadili kijamii na kisiasa.

Maudhui Yake Ya Kifalsafa Na Kimaadili:

Itifaki ya utamaduni husika haina budi kuidhinishwa na kubanwa na katiba ya nchi kuipa kinga kisheria na uwezo wa kudhibiti maendeleo ya pamoja na shirikishi. Kwa kufunda raia wote maadili na uwajibikaji kuandaa jamii yenye kuwajibika kwaajili ya maslahi ya umma.

Nukta za kifalsafa na kimaadili zinazopaswa kuidhinishwa na kubanwa kikatiba chini ya ibara ya Tunu za Taifa ni kama ifuatavyo:
  • unyoofu wa uzalendo.
  • Ujasiri
  • uwajibikaji (wa kibinafsi na kijamii)
  • ufahamu wa utatuzi wa matatizo; kuona mbali na kutathmini.
  • Tabia njema, uaminifu na ukweli.
  • Nguvu ya ushawishi na kujitafakari.
  • Uthabiti.
  • Upambanuzi wa haki na wajibu.
  • Uchungaji wa amana na uongozi.
  • Stadi za maisha.
  • Elimu ya uraia na misingi ya kidemokrasia.
  • Kuchukia rushwa, ufisadi na ubinafsi.
  • Utii na kuegemea nguvu ya ushauri na maamuzi ya mashauriano.
  • Udadisi na ubunifu.
  • Ukarimu.
  • Mengineyo.
Urasimishaji Wa Itifaki Hii:

i / KIJAMII
Inafahamika ya kuwa jamii inastaarabishwa kwa njia ya kupatiwa elimu bora. Ni vema itifaki ya utamaduni huu ikaingizwa kwenye mitaala ya elimu na taaluma ya fani mbalimbali nchini ili kufunda raia maadili na uwajibikaji tangu wangali mashuleni na vyuoni. Kulingana na mipango ya muda mfupi na ile ya muda mrefu. Bila kusahau kwenye tansia ya burudani na sanaa kama vile filamu za mithiolojia na vichekesho vya watoto kuonya na kufunza athari ya maadili na uwajibikaji kama nyenzo za ukuaji na au anguko la jamii.

ii / KISIASA
Nashauri pia itifaki hii ya kiutamaduni kuwekewa mazingira ya kisheria kuwa chimbuko la katiba za vyama vya kisiasa nchini. Muradi wake ukiwa kuja kutupatia jukwaa la siasa za ushindani lenye kusimamia mzani wa uhuru wa kujieleza pamoja na misingi ya utawala bora. Ilhali ukichunga mihimili ya dola na taasisi zake kuongozwa kwa manufaa ya utumishi kwa umma na siyo kutanguliza maslahi ya chama kwanza. Huku kanuni na maadili ya utumishi wa umma na miiko ya uongozi ikaendelea kusisitiza uwajibikaji na uwazi.

Hitimisho:
Nimesimamia umuhimu wa kuratibu na kurasimisha itifaki ya utamaduni wa mtanzania hapa nchini. Kutokana na kutathmini madhara ya ukosekanaji wake unavyochochea mmomonyoko wa maadili na uwajibikaji, kwa namna unavyoendelea kuathiri utendaji wa mihimili ya dola na taasisi zake na hadi maisha ya raia mmoja mmoja kijamii na kiuchumi, umeweka uhusiano wa jamii katika nadharia ya "kila mtu afe na msalaba wake" au ya kitabu cha " Shamba la Wanyama".

Leo hii unakuta kiongozi anahamasisha ukarimu ndio nguzo ya amani na utulivu wa nchi, ila yeye binafsi hana uadilifu wala ukarimu huo katika utumishi wake kulinda maslahi ya taifa. Au raia anakemea vitendo vya rushwa na ufisadi hali ya kuwa naye siyo muaminifu na mkweli katika eneo lake la kujipatia kipato ama kifamilia.

Kwa ujumla ukosefu wa maadili na uwajibikaji nchini umefisidi umma kuanzia ngazi ya taifa hadi katika maeneo madogo mno ya kiraia kama vile utendaji kazi wa mafundi na vibarua mitaani. Wizi, rushwa na ufisadi umekithiri. Tena maovu haya yamepewa majina mazuri na kautamaduni kasicho rasmi cha " marupurupu yakoje?"

Kwa mantiki hii, na baada ya kuchunguza kiini cha ukosefu wa maadili na uwajibikaji kisiasa na kijamii, nimepata majibu ya kwamba usemwao kuwa "utamaduni wa mtanzania" ndio kiini cha matatizo na tiba vilevile ya matokeo ya matatizo hayo. Kwa vile viongozi au raia ni matokeo ya utamaduni wa jamii yake. Hunavuna walichopanda.

Mwisho, wakati huu wa kupigania katiba mpya, ni vyema pia wadau wake na watanzania wote kwa ujumla kujitafakari kisha kuishauri serikali kuratibu itifaki ya utamaduni wa taifa.

Ambayo kwayo itakokoteza na kusimamia maadili na uwajibikaji kijamii na kisiasa kuendana na falsafa ya nchi na mipango ya maendeleo. Ili kufikia ustaarabu na kuchagiza maendeleo ya viwanda pamoja na sayansi na teknolojia.
 
Back
Top Bottom