Niliona tu kwamba jamaa alikuwa anaandaa njia ya kuondoka CUF. Viongozi kama hawa ndio wanataka wakabidhiwe nchi?
Lwakatare: CUF imepoteza mwelekeo
*Asema hakuingia kwenye siasa kutafuta umaarufu
Na Theonestina Juma
HARAKATI za kambi ya upinzani kupata kura za kutosha ili kuwa na idadi kubwa ya uwakilishi Bungeni, sio jambo lahisi bali linahitaji mpango kabambe, tutaendelea kuomba makanisani na misikitini lakini hatuwezi kupata mafanikio
Kauli hiyo nzito, ilitolewa hivi karibuni na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), kuanzia mwaka 2000 mpaka 2005, Bw. Wilfred Lwakatare, alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye Uwanja wa Mashujaa, Mjini Bukoba, mkoani Kagera.
Haikuwa rahisi kwa wafuasi wake, kuamini uamuzi aliochukuliwa Bw. Lwakatare ambaye mwaka 2005, alishindwa kutetea kiti hicho kwenye Uchaguzi Mkuu. Mpaka anatangaza kujivua rasmi uanachama wa CUF, Bw. Lwakatare alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.
Bw. Lwakatare aliwaeleza wananchi hao kuwa, hakuingia kwenye siasa kwa lengo la kutafuta umaarufu kwenye vyama visivyokuwa na mwelekeo wa kuwasaidia wananchi.
Nilipokuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, nilijaribu kuwa karibu kuwa na watu wa rika zote kwa sababun ya tabia yangu ya kusema ukweli, lakini inapofikia hatua ya kuwepo kwa majungu na fitina ambazo hazijengi, kazi ya ziada inahitajika kuondokana na tatizo hili, alifafanua Bw. Lwakatare.
Bw. Lwakatare ambaye ametangaza rasmi kuondoka CUF, aliwataka wananchi hao, wasimuhukumu kwa maneno wanayoyasikia pembeni, bali wamuhuku kwa yale atakayosema mwenyewe akisisitiza kuwa, utamaduni alionao ni kuweka mambo mezani ili yajadiliwe na kushindna kwa hoja.
Anasema kwa mujibu wa utaratibu na kanuni za nchi, katika uchaguzi wa mwaka 2010 atagombea Ubunge katika Jimbo la Bukoba Mjini. Alifafanua kuwa, uvumi uliopo kwamba yupo mbioni kuhamia kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ni hoja iliyopandikiwa na viongozi wa CUF, kwa makusudi.
Anafafanua kuwa, pamoja na vyombo vya habari nchini kumtafa awaeleze sababu za kuchukua uamuzi huo, hakuwa tayari kuwaeleza mabapo kusudio lake ni kutaka kuelezea sababu hiyo kwa wananchi ambao ndio mtaji wake kisiasa na kufanya ajulikane.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuondoka CUF, kamwe hawezi kuhamia CCM kama inavyodhaniwa na wananchi wengi. Sera ya CCM, sio kutengeneza maisha bora kwa wananchi bali ni inatengeneza maisha magumu kwa ari, nguvu na kasi mpya, hivyo hana sababu ya kujiunga na chama hicho.
Anasema mfumo wa vyama vingi vya siasa ni msukumo mzuri kimsingi unaofanya kazi ya kuwasaidia Watanzania ili chama kinachopo madaraka kisijisahau kutimiza malengo ya kuwasaidia wananchi.
Naomba niwaambie ndugu zangu, katika vyama vya siasa wamo baadhi ya viongozi ambao wameanza kuvibadilisha kama vichaka vya kufanyia ubinafsi, ufisadi na kuendeleza mambo mengine yasiofaa.
Ikifikia hatua ya chama kupata ruzuku, viongozi wengine wanaona wamefika mwisho wa reli Kigoma, bila kujua kwamba bado tunaendelea kutafuta maisha bora, lakini ikishafikia hapo vyama vya siasa vinajisahu kwa hilo, anasema.
Anasema kwa hali ilivyo sasa ndani ya CUF, hali si shwari baada ya kupoteza mwelekeo na kushika kisiasa na matokeo juu ya hilo, ni kushindwa katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika majimbo mbalimbali.
Aliongeza kuwa, alikipenda CUF kwa sababu ya uwazi na ukweli uliokuwepo awali tofauti na sasa ambapo matatizo mengi hayawekwi hadharani na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka
Anasema licha ya badhi ya wananchi kumtaka aende CHADEMA, atakaa na familia yake na kujadili suala hilo kwa makini na kutoa jibu badae.
Katika moja ya vitabu alivyotunga Bw. Lwakatare ameelezea jinsi asivyoridhishwa na mafao yake ndani ya CUF, licha ya wajumbe kumwona nadhifu akiendesha VX ambalo anadai kuwa, alilipata kutokana na kura za wana Bukoba mwaka 2000.
Sula lingine aliloandika kwenye kitabu hicho ni jinsi CUF ilivyo na utaratibu mbovu wa kutowatambua waasisi wa chama hicho. Anasema kwa upande wa Tanzania Bara maendeleo ya chama hicho ni hafifu na hayatii matumaini hali inayoonesha dahihiri kuwa, CUF ipo kwa ajili ya kusindikiza vyama vingine kutokana na chama hicho kutokuwa na mwakilishi hata mmoja bungeni kama ilivyo kwa vyama vingine.
Pia kitabu hicho, kinaelezea mpango ulioandaliwa kumuondoa katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Taifa, na kuonesha namna ambavyo aliweza kutulizwa na Makamu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Bw. Yusuph Machano ya kumtaka asibweteke kutokana na mabadiliko yaliofanywa na chama.
Ni kweli nilipata mshtuko wa mabadiloiko hayo, baada ya kujitathimini mara mbili zaidi juu ya uwezo wangu kiutendaji kwa kuzingatia kuwa wenzangu kwa upande wa Zanzibar, Bw. Juma Duni Haji, jina lake lilirudi na kufanikiwa kutetea kiti chake na jina langu likaachwa, anasema.
Bw. Lwakatare ni miongoni mwa waasisi wa CUF, kama kiongozi mwandamizi na mwenye uwezo mkubwa wa kupanga mikakati na mipango mbalimbali ya kukijenga chama pamoja na kuhakikisha kinapata ushindi katika chaguzi zake mbalimbali.