na Asha Bani
UAMUZI wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Winfred Lwakatare, kujiuzulu nyadhifa zote na tetesi za kukihama, zimezidi kukichanganya chama hicho.
Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amemsihi asikivuruge chama hicho baada ya kuwapo tetesi kuwa kuna baadhi ya viongozi wa CUF wanataka kukihama.
Akifungua kongamano la siku moja la vijana lenye lengo la kushinikiza serikali kuunda tume huru ya uchaguzi na kudai mabadiliko ya Katiba ya Tanzania, lililofanyika katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni, jijini Dar es Salaam, Lipumba alisema wanaheshimu uamuzi wowote akatakaochukua Lwakatare.
Alisema hatashangazwa kama atasikia Lwakatare kaihama CUF kwa kuwa ni kawaida ya viongozi wa Tanzania Bara waliomo ndani ya vyama vya upinzani kuhama chama mara yanapotokea mabadiliko ya uongozi.
Lipumba alisema tabia hiyo ya kuhama inaonekana kuanza kuwa sugu, lakini ni vema wanaohama wakajenga utamaduni wa kutambua na kukubali mabadiliko yanayofanyika ndani ya vyama vyao.
Lwakatare ana haki na uhuru wa kuhama CUF, lakini asivuruge amani ndani ya chama, alisema Lipumba.
Lipumba aliwataja baadhi ya viongozi waliokihama chama hicho baada ya kutokea mabadiliko ya uongozi kuwa ni Shaibu Akwilombe, aliyehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Tambwe Hizza, aliyehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema si busara kwa viongozi waliopo madarakani kufikiri kuwa watakaa madarakani milele katika CUF, kwa kuwa ni chama cha wananchi, kinachoendeshwa kama taasisi.
Alibainisha kuwa hata yeye muda wake ukiwadia ataondoka ndani ya chama hicho, kwa vile atakuwa anaheshimu uamuzi wa wanachama wake na kukubali matokeo.
Hakuna mtu ambaye atakaa katika nafasi ya uongozi ndani ya CUF muda wote, ni lazima kuwe na mabadiliko. Mimi (Lipumba), Maalim Seif Shariff Hamad (Katibu Mkuu) na Juma Duni, muda wetu ukifika hatutangangania madaraka, alisema Profesa Lipumba.
Aidha, pia Lipumba alibainisha kuwa wakati wote wa uongozi wake Lwakatare, hakuwa na matatizo ya kiutendaji, kwani alishiriki kikamilifu katika masuala ya chama.
Alisema hata mkutano mkuu uliofanyika mapema mwaka huu, alishiriki na kutumia nafasi hiyo kukabidhi barua ya kujiuzulu.
Alisema Lwakatare hakuteuliwa kushika wadhifa wake wa Naibu Katibu Mkuu, si kwa sababu ya ugomvi au lengo la kumuudhi, bali yalikuwa ni mabadiliko ya kawaida.
Nilimweleza kuwa lengo la CUF hivi sasa ni kujiimarisha, hasa Bukoba Mjini ambako tunakubalika zaidi, nilimsihi tusikivuruge chama, alisema Profesa Lipumba.
Wakati Lipumba akisema hayo, mwishoni mwa wiki hii, Lwakatare aliiambia Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Bukoba kuwa hajajivua uanachama wa CUF, bali alichokifanya ni kujivua uongozi.
Mpaka sasa mimi bado ni mwanachama hai wa CUF, ingawa wapiga kura wangu wameniomba nikihame chama hiki, nimewaambia ombi lao nimelipokea kwa mikono miwili, nimewaomba wanipe muda nikashauriane na familia yangu, na baada ya muda nitatoa uamuzi wangu wa mwisho, alisema Lwakatare.
Aidha, Lipumba alitumia mkutano huo kuwasihi wanachama wake kutokatishwa tamaa na matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Busanda, ambapo CUF ilifanya vibaya, tofauti na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Alisema kutokana na chama kufanya vibaya kwenye uchaguzi huo, tayari viongozi kadhaa wamefukuzwa ndani ya chama hicho.
Aliwataka vijana kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu, kwa kuchagua viongozi bora na kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Naye Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Juma Duni Haji, alisema ili kuwapo uchaguzi huru ni lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwe huru, ili kuepuka vitendo vya wizi wa kura. Alisema katika chaguzi zote ndogo za Tanzania Bara na Zanzibar kuna ubadhirifu mkubwa wa wizi wa kura unaofanywa na CCM.
Tanzania Daima.