Hoja hii si amefundishwa na Mwanakijji?nakumbuka makala ya mwanakijiji aliyoitoa kesho yake kuelezea suala la Lowasssa kuanguka mara ya Pili.alkiongelea suala la Lowasaa kutohojiwa ..ila MZee Mwanakijiji naomba umhoji this week akuelezee ni nani anahusika na dili la RDC kama yeye hakuhusika ,na lazima awe anajua sababu aliishauri kamati iwastose kwa sababu ni kampuni Tapeli.
Mie nadhani Lowassa ni kioo cha Mtu Mpole wa kucheka cheka
Mkuu Gembe kuna makala ya jana ya Ansbert Ngurumo inayoelekea huko , na naibadika hapa chini. I salute Ngurumo, he can real call a spade a spade.
YALIYOTOKEA yametokea, lakini baadhi yetu bado tunapata shida kutenganisha majina haya mawili Jakaya Kikwete na Edward Lowassa.
Na kama tungeweza kuhoji, labda kifalsafa kidogo, tungependa kujua Kikwete na Lowassa watakuwa watu wa namna gani miaka 2000 ijayo!
Ni wazi, kama mimi na wewe, watakuwa wametoweka katika uso wa dunia, lakini kazi zao na majina yao vitabaki kuwatangaza kwa mema au mabaya waliyowatendea Watanzania.
Nataka kuamini kwamba, kwa vyovyote watakavyokuwa wanafahamika, hawatakuwa wametenganishwa litakapokuwa linajadiliwa suala la historia ya uongozi na utawala wa Tanzania.
Zipo sababu zaidi ya 1,000. Hadi sasa, chache tu ndizo zinajadiliwa. Na hatutaacha kuwajadili hadi hapo tutakapohakikisha kuwa historia imeandikwa kikamilifu, bila kupotoshwa, kuhusu athari za umoja, urafiki, uswahiba na usanii wa Kikwete na Lowassa.
Kwa baadhi yetu tunaowafahamu kiasi wawili hawa, si makosa makubwa kusema kwamba, kisiasa, Lowassa ni kioo cha Kikwete.
Ni vigumu kumshangilia au kumzomea Lowassa ukamuacha Kikwete. Ndivyo walivyojiunda, ndivyo walivyokuwa na ndivyo wanavyoishi.
Mojawapo ya mambo ambayo yamesemwa sana kuhusu maswahiba hawa, ni jinsi Lowassa alivyopandikiza wazo la urais kichwani na moyoni mwa Kikwete kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.
Labda hatutakubaliana wote kuhusu hili, lakini sehemu ya ukweli ni kwamba, ndoto ya urais ilianzia kwa Lowassa. Akamwendea rafiki yake na wakawa na mjadala unaofanana hivi:
EL: Jakaya, nataka kuweka jina kugombea urais kipindi hiki. Na wewe weka jina tujaribu.
JK: Tutaweza lakini? Mbona mimi bado ni mchanga kisiasa?
EL: Si tuweke tu majina? Kwani hata tukikosa tuna hasara gani? Uchanga maana yake nini? Kwani urais unasomewa?...
Wanaokumbuka mchakato wa kugombea urais mwaka 1995, mwishoni mwa awamu ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, watakubaliana nami kwamba baada ya Augustine Mrema, jina la Lowassa lilikuwa linavuma kama lilivyokuwa la John Magufuli katika awamu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Lowassa alikuwa na mtandao wa makada vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomuunga mkono nchi nzima. Alikuwa akiungwa mkono na baadhi ya wanahabari mahiri waliokuwa wakijua anachofanya.
Tulimsikia na kumsoma sana Lowassa katika vyombo vya habari; akizuia hili, akiruhusu lile, akivunja hili na kujenga lile, alipokuwa Waziri wa Nyumba na Makazi.
Hapana shaka kwamba Lowassa ndiye muasisi halisi wa dhana ya mtandao wa Kikwete tunaozungumzia leo; na ndiye amekuwa baba na mratibu mkuu wa mtandao huo.
Yawezekana pale alipomwendea Kikwete na kumshauri waweke majina, moyoni mwake aliamini kwamba Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Fedha - angekuwa msindikizaji tu. Kumbe yeye ndiye alikuwa anaanza safari ya kumsindikiza Kikwete!
Ghafla wakakubaliana, wakachukua fomu kusindikizana. Wakala yamini; kwamba atakayedondoka amuunge mkono mwenzake. Na atakayefanikiwa kuwa rais, amteue mwingine kuwa waziri mkuu.
Baadaye kidogo wawili hao wakaitwa Boyz II Men, wakachukua na kurejesha fomu kwa mbwembwe. Kwa bahati mbaya yao (wakati huo), ndoto yao ilizimwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwanza alimzuia Lowassa kugombea - kwa sababu alizojua. Lakini Lowassa ndiye alikuwa na wafuasi wengi walioandaliwa (mtandao). Katika kujitoa, Lowassa akawaomba wafuasi wake wamuunge mkono Kikwete.
Ndivyo Kikwete alivyopata nguvu ya ghafla na ya ajabu hadi akawa miongoni mwa Tatu Bora Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Cleopa Msuya. Ndivyo alivyochomoza na kudiriki kuwashinda wenzake.
Mwalimu Nyerere, kama alivyofanya kwa Lowassa, akamzuia pia Kikwete, kwa staili ya kiungwana zaidi.
Baada ya yote tunayoshuhudia chini ya uongozi wa Kikwete sasa, napata shida kuelewa Kikwete aliyegombea ghafla mwaka 1995 angeongozaje nchi hii! Kama baada ya maandalizi ya miaka 10, mambo yenyewe ndiyo haya tunayoshuhudia leo, nadiriki kusema kwamba katika hili, Mwalimu Nyerere alikuwa sahihi sana kuweka vizuizi vyake.
Maana tukizingatia Tanzania ya Mzee Mwinyi ilipoishia, na Mzee Mkapa alipoitoa na kuifikisha kwa miaka 10; tukipalinganisha na ujanja ujanja na usanii unaofanyika sasa katika miaka miwili tu ya utawala wa Kikwete, baadhi yetu tunachelea kusema kwamba Watanzania tulifanya makosa kukifungua kile ambacho kilifungwa na Mwalimu Nyerere.
Na hapa ndipo ulipo ushindi wa Lowassa dhidi ya Nyerere. Mtandao wa Lowassa haukufa. Ukageuka na kuwa mtandao wa Kikwete.
Siku alipokataliwa na Nyerere, ndiyo siku mtandao huo ulianza upya kazi ya kumsimika Kikwete kwa wananchi. Wapambe walitumia mbinu nyingi, hata kutuongopea eti Mwalimu Nyerere alimwambia Kikwete asubiri hadi Mkapa amalize ngwe yake, ili akue kidogo na apate uzoefu.
Baada ya miaka 10 mfululizo, Kikwete akajipenyeza kwa kila kada ya Watanzania wanasiasa wenzake, vijana wa itikadi zote, viongozi wa dini, wanahabari, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wasanii wa fani zote, kina mama na hata watoto. Bahati mbaya, wote hawa hawakumjua vizuri. Lakini walimpenda na kumshabikia, hata kabla yeye hajajitokeza rasmi hadharani kutangaza nia yake ya kuutaka urais.
Ni jambo lililo wazi kwamba kazi ya kueneza mtandao huu haikufanywa na Kikwete mwenyewe. Nguzo zake kuu zimekuwa mbili - Rostam Aziz (Mbunge wa Igunga) na Edward Lowassa. Wengine wote waliunganishwa na hawa.
Lowassa ni mmoja wa mawaziri wa Mkapa aliyezunguka sana nchi nzima, akifanya kazi ya kujenga mtandao huo sambamba na kazi za wizara aliyosimamia ya Maji na Mifugo (bila Rais Mkapa kujua)! Baadaye, nguvu hiyo hiyo ndiyo ilitumika kumngoa Pius Msekwa katika uspika wa Bunge na kumweka Samwel Sitta.
Katika muda wote huo, Rostam amebaki kuwa mwanamkakati mkuu, mfadhili na mtafutaji wa pesa za kampeni kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi. Lowassa ndiye alikuwa kamanda mkuu, akisaidiwa na vijana wenye nafasi na ushawishi ndani ya CCM, waliohangaika mchana na usiku kuongeza nguvu na kukamilisha kazi ya kumuuza Kikwete kwa wana CCM na Watanzania, hadi akawa rais.
Kikwete mwenyewe hakuonekana kuhangaika. Hata hivyo, yeye alikuwa na mbinu yake moja (kuu) aliyoitumia kuonekana mwenzetu, mtu wa watu. Haitatajwa katika makala hii, kwani si mahali pake.
Na bila kujua, Rais Mkapa akamweka Kikwete katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10 mfululizo; akawa mbali na umma. Akamweka mbali na migogoro na misiguano ya moja kwa moja na wananchi. Akamweka mbali na kashfa za kila siku zilizowagusa mawaziri wengine. Watu wasiofuatilia wakadhani Kikwete ni dhahabu!
Si lengo langu kusimulia kila hatua iliyochukuliwa na wanamtandao kumpatia Kikwete urais. Mengi yanajulikana, na mengine yatajulikana baadaye.
Lakini napenda kusisitiza kwamba, inawezekana sana kwamba bila jitihada binafsi za Lowassa na wenzake, Kikwete asingeupata urais. Na ndiyo maana hata alipokwishaupata, licha ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya wakongwe ndani ya CCM kwamba asimteue Lowassa kuwa waziri mkuu, Kikwete alikaidi, akamteua.
Alikuwa anajua anachofanya. Alikuwa na sababu za msingi na za muda mrefu. Alimwamini sana. Ndoto yao iliyozimwa na Nyerere, ilikuwa imetimia baada ya miaka 11 hivi ya maandalizi.
Sina shaka kwamba katika miaka miwili iliyopita, Kikwete na Lowassa wamekuwa wakikumbushana ndoto yao hiyo na jitihada zilizowafikisha hapo walipo. Bila shaka, Kikwete hakutarajia kwamba Lowassa angejiuzulu kirahisi hivyo, tena wakati huu.
Wala hakuwa na nia ya kumfukuza kazi kwa sababu yoyote. Kikwete huyu huyu anayeogopa kumuengua Andrew Chenge (licha ya kashfa zote za wazi zinazomwandama), asingeweza kupata ujasiri wa kumuondoa Lowassa. Hakuwa nao.
Ndiyo maana hata Chenge mwenyewe alipohojiwa na wanahabari kuhusu kurudishwa kwake katika baraza, aliwaambia waandishi: Kamuulize rais, ndiye anajua kwanini ameniteua!
Kwa maneno mengine, Chenge anasema rais anajua makosa yangu, lakini ni mimi ninayeweza kuyasimamia ili serikali isianguke.
Ndiyo maana pia katika mojawapo ya makala zangu, wiki mbili zilizopita, nilisema aliyevunja Baraza la Mawaziri si Kikwete bali Lowassa, ingawa kimantiki na kikatiba ni kazi ya rais kuvunja baraza.
Licha ya sifa alizopewa wakati anagombea nafasi hiyo, Kikwete ni mzito na mgumu wa kuchukua hatua kali na ngumu. Watu wengine wanamuita rais mwoga, mpenda sifa. Mifano miwili inaweza kutusaidia kusisitiza hili.
Alisubiri Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali ajiuzulu ndipo akatangaza kuwa amemfukuza kazi. Amesubiri Waziri Mkuu Edward Lowassa ajizulu ndipo akatangaza kuvunja Baraza la Mawaziri.
Anaogopa kukosea na kulaumiwa. Na hata akikosea, anataka wengine ndio waonekane wakosaji, walaumiwe. Wao wawajibike, mwenyewe asifiwe! Ndiyo maana mwanablogu na mwanahabari mwenzangu, Reginald Simon Miruko, wiki hii amediriki kusema wazi:
Niaminivyo ni kwamba JK hawezi kuchinja hata kuku! Akichinja, anataka damu iwamwagikie wengine.
Tukilitazama sakata la Richmond, tunaweza kukubaliana na Reginald, kwani ndivyo Kikwete alivyomfanyia Lowassa. Wafuatiliaji wa mambo wanajua, kama nilivyodokeza katika makala zangu wiki mbili zilizopita, kwamba huwezi kuzungumzia kashfa ya Richmond bila kuwataja Kikwete, Rostam na Lowassa. Kila mmoja alihusika katika hatua kadhaa.
Tutakubaliana na Reginald kwamba ingawa taifa zima linamtazama Lowassa kama fisadi mkuu katika mradi huo, ukweli ni kwamba yeye alitumwa kazi akaitekeleza.
Yawezekana Kamati ya Bunge iliuona mkono wa rais katika Richmond, ikaogopa kwenda mbele zaidi. Lakini ilijua ni rahisi kumtikisa waziri mkuu kuliko rais. Ikaamua iishie kwa waziri mkuu.
Yawezekana ndiyo maana haikumuhoji Lowassa. Maana kama Lowassa angehojiwa, angesema anachokijua walau nje ya kiapo kwamba baada ya uamuzi wa kikao rasmi cha Baraza la Mawaziri, rais alipata ndoto mpya kuhusu Richmond, na akaagiza mchakato uende kwa kasi mpya; na akampa kazi ya kufanya: Hakikisha unasimamia hili hadi linafanikiwa. Sitaki visingizio.
Katika nchi zetu zenye katiba legelege, zinazotawaliwa na maagizo ya rais na utii wa wadogo kwa wakubwa, ambapo viongozi wanaona bora kumtii rais kuliko kuitii jamhuri, jambo hili linawezekana sana. Ndivyo mawaziri wetu wanavyotenda kazi zao; na ndiyo maana tunakwama.
Na hili ndilo kosa kuu la Lowassa. Ndiyo! Alikuwa anatii amri na maagizo ya mkubwa wake. Lakini je, hakuona kuwa yamepinda?
Akiwa mshauri wake mkuu, alimweleza hatari zinazoweza kutokea kutokana na shinikizo hilo? Kama Kikwete alishauriwa akakataa, akangangana lazima Richmond ipate tenda hiyo, kwa nini Lowassa hakujiuzulu pale pale?
Yawezekana wote wawili walidhani mambo haya yangepita tu kwa sababu Watanzania ni wapole, watiifu, wapenda amani na hawafuatilii mambo. Hata wakifuatilia hawahoji! Hata wakihoji, hawachukui hatua.
Walidhani yataibuka baada ya miaka 10 ya utawala wao, kama ilivyokuwa ya Mkapa na wenzake, wao wakishastaafu na kulindwa! Walikosea.
Najua jinsi Lowassa anavyofadhaika sasa kwa suala hili. Anajutia kosa lake na la mkubwa wake. Anaona ametoswa. Anabebeshwa udhaifu na ufisadi wote wa Kikwete, Rostam na wengine waliohusika na Richmond.
Nafika mahali namwonea huruma Lowassa; maana tofauti na kauli ya Reginald, zamu hii Kikwete alijaribu kuchinja kuku (Richmond), lakini damu yake imemmwagikia Lowassa.
Na bahati mbaya ni kwamba, sasa Watanzania hawamtazami mchinjaji, bali yule mwenye damu! Sijui kwanini Kikwete hakukubali kubeba lawama za uamuzi wake mwenyewe.
Ndiyo! Akubali, atuombe radhi; kuliko kuendelea kuishi katika uongo unaoviringishwa kwenye ufisadi wa Lowassa.
Lowassa alikwishajiuzulu, wala asingemrejesha. Lakini wanaojua mwenendo wa sakata hili, walitarajia kwamba hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa Dar es Salaam, wiki iliyopita, ingekuwa ya maungamo yake kwa taifa.
Hiyo ndiyo ilikuwa fursa ya rais kutuambia ushiriki wake na ukweli anaoujua. Tulitarajia akiri makosa (kwani naye ni binadamu), na aahidi kujisahihisha yeye na serikali yake. Tungemsamehe. Na tungeelewa maana ya kauli yake kuhusu ajali ya kisiasa iliyomkumba Lowassa.
Kama nilivyosema wiki iliyopita, si sahihi kwa Kikwete kusema tu kwamba Lowassa alifanya kazi kwa uzalendo, uadilifu na umakini mkubwa sana, huku akijua kwamba wananchi wanamzomea mtu huyo huyo na kumuita fisadi.
Ni wazi, wanaofahamu mchakato mzima na mwenendo wa uongozi chini ya Kikwete na Lowassa, wanajua fika kwamba unapomuita Lowassa fisadi, unamzungumzia Kikwete pia.
Sababu ni moja. Kama ilivyosemwa huko nyuma, Lowassa ndiye amekuwa mkono wa kulia wa Kikwete kwa muda mrefu. Sasa kama mkono umekatwa, mwenye kilema ni mwenye mkono.
Kwa maoni yangu, suala la Richmond halijaisha. Na haliwezi kuisha na Lowassa, hasa kama rais mwenyewe anajaribu, lakini anaogopa kulizungumzia.
Na kama anataka kumtetea na kumlilia Lowassa, na kuonekana muungwana, aseme ukweli kwamba ndiye alimtuma kuibeba Richmond.
Tayari Lowassa amechafuka, amejichafua na amechafuliwa. Mtu pekee anayeweza kumsafisha ni yule yule aliyeshiriki kumchafua - swahiba aliyembeba kwa zaidi ya miaka 10 Kikwete!
Sisi wengine tukimtazama Lowassa katika hali aliyomo leo, tunamuona Kikwete halisi. Naamini hata Kikwete mwenyewe hahitaji kioo kujitazama sura na haiba yake halisi. Amtazame Lowassa!
Source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2008/2/24/makala4.php