Muhtasari wa Mkutano wa Waandishi wa Habari wa Arne Slot Kabla ya Mechi ya Ngao ya Jamii (FA Community Shield)
Kuhusu msiba wa Diogo Jota na heshima zilizotolewa tangu wakati huo...
Slot alisema kuwa msiba huo uliwaathiri sana, lakini zaidi aliwahurumia mke wa Jota, watoto wake na wazazi wake. Aligusia heshima na sala zilizotolewa Asia na Preston kuwa za kugusa moyo na za kipekee.
Kuhusu washambuliaji alionao na uwezekano wa mabadiliko kabla ya dirisha la usajili kufungwa...
Slot alikwepa kuzungumzia wachezaji ambao hawajasajiliwa na Liverpool lakini alimsifu Hugo Ekitike aliyejiunga hivi karibuni. Alisema anafurahishwa na kikosi chake licha ya baadhi ya wachezaji kuondoka. Alikiri kuwa kuna uwezekano Darwin Núñez akaondoka, lakini bado hakuna kilichosainiwa.
Kuhusu hitaji la beki mwingine wa kati...
Alitaja kuwa Gravenberch, Robertson na Endo wanaweza kucheza nafasi hiyo, pia Joe Gomez ambaye kwa sasa ana majeraha madogo lakini anarudi hivi karibuni. Kwa ujumla alisema ameridhika na chaguzi alizonazo kwa sasa.
Kuhusu fursa ya kutwaa taji la kwanza msimu huu...
Slot alisema ni jambo zuri kuanza msimu ukiwa na nafasi ya kushinda taji, jambo ambalo kawaida huchukua muda mrefu. Alionya kuwa Crystal Palace ni wapinzani wagumu, wakikumbusha sare ya 1-1 mwishoni mwa msimu uliopita.
Kuhusu maendeleo ya Rio Ngumoha na kushughulikia umaarufu baada ya mabao yake ya maandalizi ya msimu...
Slot alisema ni vigumu kutabiri jinsi vijana wanavyokabiliana na umaarufu, akimlinganisha Rio na Trey Nyoni. Alisema wana nafasi nzuri ya kujifunza kutoka kwa mastaa kama Salah na Van Dijk. Lakini alisisitiza kuwa wanapaswa kulindwa kutokana na kiwango kikubwa cha mazoezi na mechi.
Kuhusu wingi wa washambuliaji kikosini...
Slot alihoji tafsiri ya neno "wachezaji wakubwa" na kusisitiza kuwa hata vijana kama Rio wanaweza kuwa na mchango mkubwa. Alitaja kuwa ana washambuliaji wengi wenye uwezo: Gakpo, Chiesa, Ekitike, Salah, Frimpong (anaweza cheza kama winger), na Florian Wirtz.
Kuhusu maandalizi dhidi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON)...
Slot alithibitisha kuwa wamezingatia hilo. Alisema Mo Salah anaweza kuukosa hadi mechi sita, na usajili wa Jeremie Frimpong ni sehemu ya maandalizi hayo, kwani anaweza kucheza kama beki wa kulia au winga wa kulia, kumrithi Mo Salah.