Waungwana
Hapa suala la kuuliza sio kwamba mitihani imevuja au la, ila, kwa sababu gani imevuja? Huo ndio mjadala endelevu ambao tukiujadili kwa kirefu tutajua sababu zinazochangia (mwaka hadi mwaka) mitihani kuvuja, na nini kifanyike kuzujia uvujaji huo.
Kama mnavyokumbuka, taarifa zilitolewa na Serikali Kuu kwamba mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa utata huu umeanzishwa, hata hivyo, mpaka sasa, Serikali Kuu haijatamka ni nini kimefanyika, na mpaka sasa ni hatua gani zilizokwisha tekelezwa.
Kwa mtazamo wangu, mitihani inavuja na itaendelea kuvuja mpaka siku ambayo tutaacha kumwonea aibu Nyani Jiladi (au ni Giladi)! Wanasema, ukitaka kumchinja nyani usimtazame usoni. Sisi tunataka kumchinja, lakini tunamtazama, aibu inatuingia, tunamwonea huruma, anasepa! Huo ndio ukweli!
Ujinga ulioje!
Mitihani inavuja kwa kuwa hakuna nyenzo za kudhibiti isivuje. Tatizo la uvujaji wake ni kwamba (i) mitihani inaandaliwa na watu, (ii) mitihani inasimamiwa/inalindwa, (iii) watu wanaosimamia/kulinda mitihani hiyo "wana njaa", lakini (iv) hata kama "njaa" yao ikipatiwa ufumbuzi, bado wataendelea KUIBA, kwa kuwa wana tamaa, na kwamba kipato chao za ziada bado ni muhimu kwao, kwa kuwa ni KIKUBWA!
Kuna msemo kwamba wafanyakazi wa Baraza la Mitihani huwa wanasheherekea mitihani ya kitaifa inapoanza, kwani, wengine wanajua kwamba (i) watamalizia nyumba zao na za "nyumba ndogo" zao, (ii) watawapeleka wake zao shopping Ulaya, (iii) watafanya ufisadi wowote mwingine waupendao, kwa kuwa, HAWAJADHIBITIWA ipasavyo, wasiweze kuiba mitihani hiyo.
Sasa, kwa kuwa tunatambua kwamba tatizo la uvujaji wa mitihani ni WATU, basi, tuangalie ni namna gani ambapo tutaweza kutumia TEKNOLOJIA ili kuhakikisha kwamba WATU hawapati nafasi ya kuiona, kuigusa wala kuishuhudia mitihani hiyo, pasi na ruksa maalum. Na kwamba, watakaokasimu madaraka ya usimamizi wa mitihani hiyo watakuwa ni watu ambao WAMEKULA KIAPO ili mitihani hiyo ikivuja tutaweza kuwaadhibu na kuwawajibisha. Kumbukeni, jambo muhimu hapa ni ADHABU na KUWAJIBISHWA!
Yapo mengine mengi ambayo nitayazungumia hapo baadaye, lakini nawaachine uwanja, nanyi mchangie. Nimebuni mfumo ambao tunaweza kuutengeneza, sisi wenyewe, Watanzania, kwa kutumia teknolojia rahisi, kuweza kudhibiti jambo hili. Nitaupeleka mfumo huu, fursa itakapowadia, muda si mrefu ujao, kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Education and Vocational Education) ili wahusika waweze kuangalia fursa zitakazotokea ili tuanze mchakato wa KIZALENDO wa kudhibiti hali hii isitokee tena.
Suala ni, je, kuna WAZALENDO kwenye Wizara hii, ambao wako tayari kujiunga nami?
./Mwana wa Haki
P.S. Wizi wa Mitihani ya Kitaifa ni UFISADI! Hakuna jina lingine! Tusimwonee haya Nyani Giladi!