Rais wangu Kikwete, kabla ya kuanguka wananchi watajibu
Paschally Mayega
RAIS wangu, Piyo (Matamshi ya Mwalimu Nyerere kwa Pius) amemgeukia baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutangaza hadharani rasmi kuunga mkono kwake hoja ya mgombea binafsi. Huyu ni Makamu Mwenyekiti Bara wa chama kinachotawala.
Mwenyekiti wake ndiye mkuu wa nchi. Mungu bwana, ana mipango ambayo mwanadamu hawezi kuijua. Husema na watu wake kwa njia tofauti tofauti. Kwa hili Piyo abarikiwe sana. Kama amesema hivyo baada ya kupata baraka kutoka kwa mwenyekiti wake, basi na wewe baba ubarikiwe sana.
Rais wangu, mzee wetu maskini mchapakazi baada ya kusikia uamuzi wa mahakama aliniambia: Sasa sisi ndiyo tumekwisha. Nilimjibu: Siyo nyinyi CCM tu, bali vyama vyote vilivyofifisha demokrasia. Vyama ambavyo vimegeuka na kuwa vya viongozi badala ya wanachama sasa vimekwisha. Huu ndiyo mwisho wa wagombea wabovu waliokuwa wanabebwa na vyama vyao.
Mgombea binafsi anakuja kurejesha matumizi ya haki za Watanzania wote. Haki hii aliyopewa Mtanzania na katiba ya nchi yake, kwa muda mrefu imekuwa imehodhiwa na vyama vya siasa. Mahakama imesema huko ni kuvunja katiba ya nchi. Zamani tuliambiwa kuwa kuvunja katiba ya nchi ni uhaini.
Rais wangu, nilipomsikia Mathias Chikawe, Waziri wetu wa Sheria na Katiba anasema serikali itakata rufaa sikumwelewa. Angekuwa mbumbumbu wa sheria kama mimi ningemwelewa kuwa hajui asemalo. Kuna jamaa kaniambia huyu kasoma sheria hasa.
Ina maana lugha iliyotamkwa na mahakama kuwa kuendelea na sheria hii ni kuendelea kuvunja katiba anaelewa inasema nini. Anapotetea kuvunja katiba haiingii akilini.
Ndugu Rais, hawa jamaa huwa wanaapa nini? Wanaelewa wanachokiapa? Au wanafanya kiapo kama ni utaratibu wa mtu kuwa waziri tu na hakina maana yoyote! Huyu alishika Biblia takatifu.
Kwa imani yangu nilidhani anamwapia Mwenyezi Mungu kuwa atailinda na kuitetea katiba ya nchi yetu. Mtu akisema alikuwa anafanya dhihaka au alikuwa anamdanganya tu rais wetu mimi sitamkatalia. Tuangalie upya viapo vya viongozi wetu kama vina maana yoyote tena! Hawa wote ambao kwa lugha ya kisasa wanaitwa mafisadi au majasiri waliapa. Sizungumzii watu wasio na dini hapa.
Rais wangu, wewe uliapa pale Uwanja wa Taifa. Nilikuona ulishika kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu. Wahakikishie wananchi wako kuwa ulipokuwa unaapa ulikuwa unamwapia Mwenyezi Mungu kuwa utailinda na kuitetea katiba ya nchi yetu kwa ajili ya amani na ustawi wa waja wake. Madhehebu yenu ni tofauti, lakini Mwenyezi Mungu ni mmoja. Waziri wako amekiuka kiapo chake.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaposhupalia kukata rufaa ili kudhulumu haki za raia mimi namwelewa vizuri. Kwanza mimi mwenyewe sijui ipi ni dhambi kubwa kuliko nyingine kati ya kudhulumu haki za raia na kushiriki kuleta maafa kwa raia kwa kuikubali Richmond, kuisafisha na baadaye kuihalalisha Dowans. Najua zote ni dhambi za mauti.
Kwa jinsi ofisi yake ilivyochafuka kwa sasa, na yeye mwenyewe kutakiwa ajiuzulu mwacheni aishupalie hoja hii. Hivi kuna raha gani kufanya kazi ambayo kila upitapo watu wanaonyeshana fulani mwenyewe ndiye yule! Huku Mahakama ya Rufaa ikisema mawakili wa serikali waliwasilisha hoja dhaifu. Wengine wanasema udhaifu hufanywa na mtu dhaifu.
Rais wangu, Mungu ni wa ajabu kabisa. Hebu tazama alivyowachanganya wale wanasheria wasomi wa serikali hata wasijue kuwa tarehe ni muhimu. Wanatukumbusha wale wajenzi wa Mnara wa Babeli. Aliyegundua tarehe hakuwa mjinga. Mimi si mwanasheria, lakini tarehe ningeandika.
Enyi wasomi wa elimu dunia tuliisha waambia kuwa kudhulumu haki za waja wa Mwenyezi Mungu ni kumdhulumu Mungu mwenyewe. Siku zote Mungu hukaa upande wa wanaodhulumiwa. Endeleeni tuone nani zaidi kati yenu na yule aliye juu. Naye anasema: Adui zenu ni marafiki wenu. Waombeeni mema wale wanaowadhulumu. Mwacheni bwana apambane nao. Hivi nyinyi wanasheria wa serikali mnaotetea hili, hamna dini? Dini zote zinahubiri haki.
Dini zote zinakataza dhuluma. Anayewatuma mahakamani anatenda dhambi, lakini nyinyi mnaofanikisha dhuluma hiyo mahakamani mnatenda dhambi kubwa zaidi.
Rais wangu, hebu tuambie hizi fedha mnazotumia kukatia rufaa zaidi ya mara tatu, mnashindwa halafu mnalipa gharama, mnazitoa wapi? Usituambie kuwa ni kodi ya wale wale mnaotaka kuwadhulumu haki yao! Kama ni kodi yao nawaambieni hamtaikwepa hukumu maana kwa hili Mungu atawalipia.
Tunamchinja raia wa nchi hii kwa kutumia kisu chake mwenyewe. Hakuna dhuluma inayoendelea milele. Hii ya mgombea binafsi imefika mwisho. Wananchi sasa ni waelewa. Sasa wataanza kuja mahakamani kusikiliza kesi yao. Na huko mitaani watawasubiri hao mawakili wa serikali kuwashangilia. Wakishindwa kuwatia mikononi watawazomea. Nani alaumiwe? Tulipokuwa wadogo watu waliokuwa wanazomewa ni wachawi na vikojozi. Wenye akili wataelewa. Wanaotaka kupima mafuta ya moto kwa kichwa waachwe waendelee.
Rais wangu, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu naye kaja na ya kwake. Anasema watu wasiangalie upande mmoja tu, serikali nayo ina upande na haki yake. Ina haki ya kukata rufaa. Sijui kama alikuwa na maana kuwa serikali ya watu inaweza ikawa na msimamo tofauti na watu wale wale walioiweka madarakani, hicho kitu ndio akakiita haki ya serikali, sijui! Nilikuwa najua kuwa serikali ya watu, huchaguliwa na watu ili iendeshe nchi ya watu kulingana na matakwa ya watu wenyewe.
Ndiyo kusema serikali ya watu siku zote itakuwa upande wa watu maana ni sehemu ya watu hao. Kusigana kokote kati ya watu na serikali yao ndiyo kufanana na usaliti. Mahakamani ni mahali pa kutafuta haki iliyopotea au iliyopokonywa. Ni haki ipi hiyo ambayo serikali inaona imedhulumiwa na watu wake? Ni haki ya serikali kuvunja katiba! Tusije tukamwonea Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, labda tuangalie upande wa pili. Yawezekana alitaka kusema kuwa pamoja na kwamba wewe ndiye mwenye mbwa, lakini mbwa naye ana haki zake. Sawa, mbwa apatiwe chakula atunzwe, atibiwe, lakini si haki ya mbwa kumpangia mwenye mbwa namna ya kuishi au kuendesha maisha yake.
Rais wangu, mahakama imeishatamka kuwa kumzuia mtu kuchaguliwa na wenzake kwa kumwekea sharti la kuwa mwanachama wa chama cha siasa ni kuvuja katiba, serikali yako inakata rufaa. Rufaa ilivyotafsiriwa na kamusi ya Kiswahili sanifu ya Oxford ni maombi yanayopelekwa kwenye baraza au mahakama yenye mamlaka zaidi ili kukataa uamuzi uliokwishafanywa. Serikali yako inayakataa maamuzi ya mahakama kuwa kumnyima raia haki yake ni kuvunja katiba. Inataka na mahakama ya juu ikatae hivyo hivyo. Usaliti maana yake ni nini? Rais wangu, hebu tuangalie muasisi wa taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anasemaje kuhusu haki ya mtu kuwa mgombea binafsi. Katika kitabu chake cha Tumetoka wapi, Tuko wapi, Tunakwenda wapi ukurasa wa 32-35 Mwalimu Nyerere anasema:
Tulipokubali tuwe na vyama vingi vya siasa tulisema hivi vyama vingi vina migogoro. Mnaweza mkawa na chama cha dini, kabila, mkoa kinaitwa chama cha Mbeya ama katika nchi kikaitwa cha Wazanzibar au cha Watanganyika tu.
Tulisema sisi hapana ni taifa changa
Basi, sheria hiyo ndivyo ilivyotungwa na ndivyo ilivyo
Hata hivyo, mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi
Hili jambo limekosewa ni la msingi
Linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura. Hii ni haki ya uraia. Madhali wewe ni raia wa Tanzania (huna kichaa, huko gerezani, umetimiza umri unaotakiwa wa miaka kumi na minane) una haki ya kupiga kura. Ni haki yako ya uraia. Iko mfukoni mwako! Hii haki ya kuomba upigiwe kura pia ni haki ya uraia; huwezi kunyimwa. Maadamu wewe ni raia wa Tanzania kisiasa una haki ya kuomba uwe rais. Ukiwa katika chama ama haupo katika chama.
Aidha, raia wa Tanzania hawezi akanyanganywa haki hii ya kuomba uongozi wa nchi yake tangu ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya taifa
Sina hakika kama vimechukua Watanzania wote. Watanzania wengine hawamo CCM, hawapo wapi na hawana chama chochote. Hata hivyo nikikataa kuingia katika chama isiwe sababu ya kuninyanganya haki yangu ya kupiga au kupigiwa kura
Sasa sheria inawanyima raia wa Tanzania haki hiyo. Mtu mmoja akaenda mahakamani kudai haki hiyo akasema: Sheria hii si haki. Jaji mmoja akahukumu akasema naam si haki. Mimi nakubaliana na maamuzi yale ya jaji kabisa. Jaji alikuwa sahihi
kwa sababu haki hii iko katika katiba. Ingekuwa haiko katika katiba, ungekuwapo ubishi, lakini imo ndani ya katiba
Sasa serikali wakafanyaje? Badala ya kukubali uamuzi wa jaji, kwa kweli walichokifanya kwa kweli ni kuifuta. Ndiyo, hamwezi kufuta haki za raia. Hamna uwezo wa kufuta haki za raia. Ndugu waziri, hamna uwezo wa kufuta haki za raia. Hamwezi kweli kabisa kabisa
Sasa mimi nina ugomvi huo na ni ugomvi wa kasoro kubwa, si kasoro ndogo
Hatuwezi kumyima raia haki yake.
Rais wangu, hamwezi kufuta haki za raia. Hamna uwezo wa kufuta haki za raia. Ndugu Mathias Chikawe, hamna uwezo wa kufuta haki za raia. Hamwezi kweli kabisa kabisa. Kama hamtamsikiliza Baba wa Taifa, hapa duniani mtamsikiliza nani? Wengine Mbeya Mei 1, 1995 mlikuwapo. Mlimwona Mwalimu Nyerere alivyokuwa akiitetea haki hii ya watu wake kutoka serikali ya awamu ya pili. Utadhani alikuwa anadai uhuru kutoka kwa wakoloni. Rais wangu, nchi yako imefikia hapa, tulikuomba uwaondoe wote wanaodhulumu haki za raia kwa kutumia jina la serikali yako. Tukasema, kutwa mchungaji peke yake anahangaika mahakamani kutetea haki ya raia ya kuchaguliwa na wenzake yeye binafsi. Mahakama imetenda haki. Serikali ya watu inakata rufaa dhidi ya watu wake.
Aisee! Nilikuwa sijawahi kusikia Jaji Mkuu na majaji wote wenye uwezo wa kuisikiliza rufaa hii wameteuliwa na rais. Serikali ya rais wao (Mwajiri) inawataka waitengue hukumu hii. Sisemi haki haitatendeka, lakini ni ngumu kama ngamia kupita katika tundu la sindano.
Ni kwa mapenzi ya Mungu tu maana kwake hakuna kinachoshindikana. Wananchi wameinua macho yao juu wakiitizama milima. Msaada wao utatoka wapi? Wanapiga mbiu ganjoni watasikiwa na nani? Matumaini ya wananchi sasa ni kwa mchungaji badala ya wabunge na serikali yao. Hivi usaliti ni kitu gani?
Rais wangu, kwa nini watu wako wamlilie Nyerere na wewe upo? Nyerere hakuzikwa na haki zao. Simama na useme watu wako wafarijike. Ukiwa kimya watu wako watajuaje kuwa upo pamoja nao katika kuhangaika kwao? Baki nao hata siku zako zitakapokwisha, ukifika mbele ya haki uweze kumwambia Muumba wako: Baba katika wote ulionipa sikumpoteza hata mmoja ila mwana mpotevu.
Msomaji wangu, mhariri wangu amesema nifupishe maongezi haya, naomba tuonane wiki ijayo, nitakapomfunulia moyo wangu wote rais wangu.
Tel: 0713-334239
Email:
gowe2006@yahoo.com