Kushamiri kwa makampuni ya usambazaji yanayomilikiwa na watanzania kwaonesha maendeleo makubwa ya ushirikiano wa kibiashara kati ya China na Tanzania

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111443383818.jpg


VCG111443386635.jpg


Kwenye maonesho ya 3 ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika yaliyofanyika mjini Changsha, mkoani Hunan China kati ya Juni 29 na Julai mbili, makampuni ya usambazaji yalijitokeza kwa wingi yakijitangaza kwa wafanyabiashara wanaotaka kusafirisha bidhaa zao kwenda barani Afrika, na hata kwa wale wanaotaka kuagiza bidhaa kutoka barani Afrika. Kujitokeza kwa wingi kwa makampuni haya, sio tu kunaonesha kuwa sekta ya usafirishaji kati ya China na Afrika imefufuka kikamilifu baada ya janga la COVID-19, bali pia biashara kati ya China na Afrika inazidi kuimarika.

Mmoja kati ya wageni walioalikwa kwenye maonesho ya 3 ya uchumi na biashara kati ya China na Afrika ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, ambaye kabla ya kuelekea mjini Changsha kushiriki kwenye mkutano wa uwekezaji kati ya China na Afrika, alipitia mjini Guangzhou ambako alifungua rasmi kampuni moja ya Silent Ocean ya Tanzania, inayofanya kazi ya kusafirisha mizigo kutoka China kwenda katika nchi mbalimbali za Afrika na hata mashariki ya kati. Alipofika mjini Changsha kwenye jumba kuu la maonyesho kujionea banda la Tanzania, aliona makampuni kadhaa ya usafirishaji wa mizigo kati ya China na Tanzania.

Zamani kulikuwa na kampuni moja tu iliyohodhi soko la usafirishaji wa bidhaa kutoka China kwenda Tanzania na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, lakini sasa eneo hilo limekuwa na ushindani mkubwa kutokana na kuwepo kwa makampuni mengi. Mameneja wa makampuni hayo waliokuwepo kwenye banda la Tanzania, wamesema tangu Rais Samia Suluhu wa Tanzania alipotangaza kufungua zaidi milango ya uchumi na biashara, kumekuwa na mahitaji makubwa ya huduma ya usafirishaji wa mizigo. Mbali na kusafirisha bidhaa kwenda Tanzania, kumekuwa na mahitaji ya usafirishaji wa bidhaa za kilimo kutoka kwenye nchi mbalimbali za Afrika, kwa makampuni hayo hiyo pia ni fursa nzuri ya biashara.

Kwenye maonyesho hayo kulikuwa na mazao mbalimbali ya kilimo kama vile korosho, kahawa, ufuta, soya, chai, ambayo wajasiriliamali wengi kutoka nchi za Afrika walikuwa wakiyatangaza kwenye soko la China. Vilevile kulikuwa na bidhaa nyingi za sanaa ya mikono kama vile vikapu, vinyago, na waonyeshaji wote wa bidhaa hizo walieleza kuwa kuna mahitaji makubwa ya huduma nafuu ya kusafirisha bidhaa zao kutoka Afrika na kuzileta kwenye soko la China.

Shirika la ndege la Tanzania ATCL pia limeshiriki kwenye maonesho hayo. Mbali na kutangaza huduma yake ya usafirishaji wa abiria mara tatu kwa wiki, mwakilishi wa ATCL nchini China Bw. Josephat Kagirwa amesema kuongezeka kwa biashara kati ya China na Tanzania imekuwa ni fursa kubwa kwa ATCL. Kwa sasa wafanyabiashara wa Tanzania na wa nchi jirani, hawafikirii tena watasafirisha vipi bidhaa zao kati ya nchi zao na China, bali wanafikiria watasafirisha kwa kasi kiasi gani. Kwa sasa ATCL imekuwa ni shirika linalosafirisha mizigo kwa muda wa saa 10 tu kati ya China na Tanzania. Bw. Kagirwa amesema wafanyabiashara kutoka nchi jirani na Tanzania pia wanachagua kutumia ndege hiyo kwa kuwa ni rahisi kufikisha mizigo katika nchi zao kwa kutumia ndege hizo.
 
Back
Top Bottom