Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,733
- 40,846
NB: kichwa cha habari nilichopendekeza kutoka kwenye gazeti ndiyo hicho lakini naona waliamua kubadili kwa discretion yao. Hii ni hoja yangu ya leo.
KABLA hamjanijia juu, niseme mapema kuwa si mimi niliyeuita uamuzi wa kufuta haki ya mtu kuchaguliwa kwa vile hataki kujiunga na chama cha siasa kuwa ni wa kipumbavu.
Nimerudia tu maneno aliyoyasema Baba wa Taifa mbele ya watawala wetu kwenye sherehe za Mei Mosi mwaka 1995, katika Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya. Mwalimu hakuwa amewatukana au kuwatusi reja reja bali aliweza kuona kitu ambacho mtu yeyote mwenye akili timamu na ambaye haogopi kufikiri anaweza kukiona bila kutumia darubini au kurunzi kuwa kumkataza mtu kuchaguliwa kwa sababu hataki kuwa UDP, TLP, CCM au chama kingine chochote cha kisiasa ni kufanya uamuzi wa kipumbavu. Nakubaliana na Mwalimu.
Ule mchezo wa kuigiza wa mgombea binafsi naona unaendelea bila kukoma. Baada ya Mahakama kuthibitisha maamuzi ya awali yaliyoona kuwa sheria inayomtaka mtu kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa ili achaguliwe ni kinyume cha katiba, watawala wetu wameanza tena kuandaa rufaa nyingine ili hatimaye uamuzi wa mwisho uwe wa Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo yenye uamuzi wa mwisho nchini.
Binafsi nimechoka na danadana hii ya serikali kwani haihitaji mtu uwe msomi wa chuo kikuu au kuwa ni mtaalamu wa anga za juu kuweza kuona kuwa serikali haina hoja hata ikijitahidi vipi kuhalalisha msimamo wake wa kupinga mgombea binafsi.
Na kwa kadiri wanavyozidi kuchelewesha kufanyia mabadiliko katiba na sheria ya uchaguzi, ndivyo wanavyozidi kuthibitisha kuwa bado hawajajijengea utaratibu wa kuheshimu maamuzi ya mahakama kama zilivyo nchi nyingine za kidemokrasia. Ninasema hivyo kwa sababu kesi hii ya mgombea binafsi imeanza tangu mwaka 1993 baada ya Mchungaji Christopher Mtikila kufungua kesi hiyo kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambako alishinda kesi hiyo lakini serikali ilikwepa kutekeleza hukumu ya mahakama.
Hiyo ilisababisha Mtikila kufungua kesi ya kikatiba ambayo nayo alishinda na serikali wakakata rufaa tena, na kwa mara nyingine hoja ya mgombea binafsi imeshinda tena. Hata hivyo, kama habari zilizoripotiwa na gazeti moja ni za ukweli, basi serikali bado haioni upumbavu wa uamuzi huo na badala yake wanataka kwenda mahakama ya rufaa kuona kama itauthibitisha au la. Miaka 15 baadaye bado wanajaribu kuonyesha kuwa wana hoja. Sidhani kama atateremka malaika kutoka mbinguni kuwapigia parapanda ya mwisho kuwa mmeshindwa! Nilipokaa chini kuyasikiliza tena maneno ya Baba wa Taifa hasa alipoelezea kwanini alikwenda kinyume na chama chake, tena hadharani kwenye maelfu ya watu, nilitambua jambo moja kuwa hoja ya kukataza mgombea binafsi ni hoja ya kibaguzi, ya hatari, na ambayo asili yake ni woga wa mtu kukimbia kivuli chake yeye mwenyewe.
Nikiwa mwanafunzi mzuri wa Mwalimu, nikajiuliza ni kitu gani kweli kilimfanya Mwalimu aipinge hoja hiyo kwa nguvu namna hiyo? Hatimaye nimepata majibu na ninaomba mpendwa msomaji ufuatane nami ili uweze nawe kuona kuwa uamuzi wa kuwanyima wagombea binafsi nafasi ya kuchaguliwa kwa hakika na pasipo shaka ni uamuzi wa kipumbavu.
Vipo vipengele vikubwa viwili ndani ya katiba ambavyo ndiyo chanzo cha mgogoro huu wa mgombea binafsi. Kwanza ni kifungu cha 67: 2 kinachosema: Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo (b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; na kifungu cha 39 (1) ambacho nacho kinasema kuwa mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama..(c) ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
Mahakama Kuu ilikuwa sahihi
Mahakama Kuu ilipopitisha uamuzi wake wa kukubaliana na hoja za mawakili wa Mchungaji Mtikila walifafanua kwa kina kwanini serikali haina hoja hasa kwa mtu anayeangalia katiba kama sheria mama na kiini cha sheria nyingine zote nchini. Kilichofanyika ni kitendo ambacho hakina budi kuwatia aibu wanasheria walioshiriki kukifanya.
Baada ya serikali kushindwa katika ile kesi ya awali ya Mtikila, ilitaka kukata rufaa lakini kwa namna ambayo wanajua wao wakaamua kuachana na rufaa hiyo na badala yake kwenda bungeni kutunga sheria iliyopinga amri ya mahakama na hivyo kuingiza kwenye katiba vipengele hivyo hapo juu.
Sheria hiyo ya mwaka 1994 ndiyo iliyomfanya Baba wa Taifa kuita uamuzi wa serikali kufuta haki ya raia ni wa kipumbavu na kuwaambia kuwa kati ya nguvu nyingi ambazo serikali inafikiri inazo, haina nguvu ya kufuta haki ya mtu.
Kitendo cha Bunge kuingilia kesi iliyokuwa mahakamani na kupitisha sheria iliyokuwa na lengo la kuwahi maamuzi ya mahakama hakikupokewa vizuri na Mahakama Kuu.
Majaji wakiongozwa na aliyekuwa Jaji Kiongozi Manento, walisema hivi kuhusu kitendo hicho cha wabunge kuwa: Sheria namba 34 ya mwaka 1994 ambayo kama ilivyosemwa awali, ilipitishwa na Bunge tarehe 16/10/94 wakati uamuzi wa Jaji Lugakingira (kama alivyokuwa wakati huo) ulitolewa tarehe 24/10/94, kwa vile bado shauri lilikuwa mahakamani, Bunge lilipopitisha sheria. Kwa kuzingatia utaratibu, ni lazima, kwa mara moja tulaani kitendo hiki. Lakini wao hawakusikiliza wakaendelea na utaratibu wao. Ni kwa sababu hiyo basi nichambue kwanini serikali haina hoja na ni kwanini mahakama ilitupilia mbali hoja zao na ni kwanini Baba wa Taifa aliita uamuzi huo wa kufuta haki ya mtu kuwa ni wa kipumbavu.
Katiba inataja masharti ya mpiga kura
Ibara ya 5 vipengele vya 1 na 2 vya katiba yetu vinasema hivi kuhusu haki ya raia ya kupiga kura, Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofaywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya katiba hii na ya sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi (2).
Bunge laweza kutunga sheria na kuweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura kutokana na yoyote kati ya sababu zifuatazo, yaani raia huyo: (a) kuwa na uraia wa nchi nyingine; (b) kuwa na ugonjwa wa akili; (c) kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai; (d) kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura, mbali na sababu hizo hakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura.
Swali ambalo linanikabili mimi ninaposoma ibara hiyo ni kuwa, kama mtu ana haki ya kupiga kura baada ya kutimiza masharti hayo machache bila kumlazimisha awe mwanachama wa kisiasa, kwanini yule anayechaguliwa (ambaye anaweza pia kuwa ni yeye) alazimishwe kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa? Kama wabunge wa CCM hawakuona umuhimu wa kumtaka kila mpiga kura awe mwanachama wa chama cha kisiasa, kwanini walikubali kuandika sheria ambayo inamtaka kila anayechaguliwa kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa?
Kwanini masharti ya mpiga kura yasiwe sawasawa na yale ya mpigiwa kura na hivyo kuoanisha mambo mawili ambayo yanahusiana?
Katiba inakataza sheria za kibaguzi
Kifungu kingine cha katiba yetu kinasema hivi kuhusu kutungwa kwa sheria yoyote ya kibaguzi na chombo chochote (kwanza kabisa ni Bunge).
Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake. Ibara ya 13 (2). Kwa maneno mengine kwa kuwataka wale wanaotaka kugombea nafasi ya uchaguzi kuwa wawe wanachama na wapendekezwe na chama cha kisiasa ni kuwabagua endapo wanatimiza masharti mengine yote. Ndiyo maana sheria iliyotungwa kuakisi mabadiliko hayo ya kikatiba kimsingi ni sheria ya kibaguzi japo si wa moja kwa moja, lakini ni wa taathira yake.
Katiba inakataza mtu kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa.
Ibara ya 20 ya Katiba yetu kipengele cha 4 kinasema hivi: Bila ya kuathiri sheria za nchi zinazohusika ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote au shirika lolote, au kwa chama chochote au cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa. Sasa kipengele hicho kinapingana kabisa na vile vipengele vyetu viwili vya hapo juu ambavyo vinamtaka mgombea wa ubunge au urais lazima awe mwanachama wa chama cha kisiasa.
Kwa kuandika sheria inayomtaka mtu anayetaka kuitumikia nchi yake na raia wenzake kuwa lazima awe mwanachama wa chama cha kisiasa inamfanya mtu huyo kwanza kujiunga na chama cha kisiasa hata kama hakubaliani nacho na pili kumlazimisha aanzishe chama ambacho kitakidhi mahitaji yake. Tatizo la kwanza si kubwa sana lakini la pili ndilo lenye matatizo. Haiwezekani kila anayetaka kugombea nafasi ya uongozi katika nchi yake na hakubaliani na sera za chama chochote kile na yeye aanzishe chama chake! Kwanini tusimpe nafasi mtu huyo kuuza sera zake na ilani yake yeye mwenyewe na kuelezea jinsi gani ataitekeleza na tukikubali tunamchagua, tukiona hana mpango tunamkataa? Kwanini mtu ambaye hapendi ukiritimba na nidhamu ya vyama vya kisiasa alazimishwe kujiunga navyo wakati anaamini na kutambua kuwa sera zake zinaweza kukubalika?
Haki ya kuchaguliwa ni haki ya binadamu
Katiba hiyo hiyo katika kipengele cha pili kinachohusu haki zetu za msingi kinatambua kwamba kila binadamu ana haki ya kuthaminiwa na kutambuliwa utu wake.
Kwa kusema kuwa anayeweza kuongoza katika Tanzania ni yule mwenye kadi ya chama cha siasa ambaye amepitishwa na chama hicho, hatuoni kuwa kwa taathira yake tunawafanya wale wasio katika vyama vya siasa kuwa duni na kuwatweza?
Je, fisadi mwanachama wa chama cha siasa anayetuongoza ni bora zaidi kuliko mwadilifu asiye na chama na ambaye ananyimwa kuongoza?
Kwanini mwanachama wa chama cha siasa awe na ujiko huu wa kuweza kugombea nafasi ya uongozi wakati raia mwingine ambaye naye ana uwezo wa kuongoza anyimwe? Kama raia ana haki ya kuchagua basi na yeye ana haki ya kuchaguliwa vile vile.
Si hivyo tu, kama vile hukumu ya kina Jaji Manento ilivyosema kuwa sheria hiyo ya 1994 iliyosababisha kufutwa kwa haki ya mtu kugombea bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa marekebisho hayo yamekiuka katiba na pia yamekiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Kwanini serikali inaogopa wagombea huru/binafsi?
Hata hivyo kutoangalia sababu za serikali kuruhusu wagombea huru ni kutowatendea haki. Hebu tuangalie kwa haraka sababu wanazotoa, kwanini serikali haiko tayari kuruhusu wagombea binafsi.
Wazo la wagombea binafsi/huru ni la kigeni
Hoja hii hutolewa ili kuonyesha kuwa katika Tanzania mambo ya kuwa na wagombea huru ni ya kigeni na hivyo Watanzania hawajazoea mtindo kama huo. Kimsingi hoja hii inawafanya Watanzania kama watoto wadogo. Mwalimu katika ile hotuba yake aliiponda na kuisagasaga hoja hii pale alipotolea mfano jinsi Mbulu ilivyoweza kumsimamisha Chifu Sarwat ambaye alikuwa anakubalika huko kuliko mgombea wa TANU ambaye Nyerere mwenyewe alimpigia kampeni.
Chifu Sarwat alichaguliwa na watu wa Mbulu kama mgombea huru na mgombea wa chama cha siasa (TANU) alishindwa na serikali ikaheshimu uamuzi wa watu wa Mbulu. Hivyo hii si hoja ya msingi.
Hivyo tunaporudisha wagombea huru hatuigi mambo ya kigeni au hatuigi alimradi tunaiga tu.
Ukweli ni kuwa wazo zima la vyama vya kisiasa ni la kigeni, wazo la kuwa na katiba ni la kigeni na hata mambo ya kuandika sheria vitabuni nk, nayo pia ni ya kigeni. Hata hivyo si kila kitu kigeni au utaratibu wa kigeni ni mbaya na usio na manufaa. Mimi sioni ulazima wa kuiga alimradi tu kuiga ili kufanana, hapana, tuige pale tunapoona kuwa kwa kufanya hivyo tunajipa nafasi ya kufanikiwa.
Wazo zima la kuruhusu wagombea huru siyo kwa sababu tutapata viongozi bora huko, hapana, bali kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo na nafasi ya kutaka kuwa kiongozi, basi anapewa nafasi hiyo na si kulazimishwa kutumia chombo fulani. La maana ni kuwa, kiongozi yeyote yule (wa chama au huru) anapatikana kwa kupigiwa kura.
Chama kitakachopoteza sana ni CCM
Ukweli rahisi hapa ni kuwa endapo wagombea huru watarudishwa tena, chama ambacho kitapata athari kubwa sana ni CCM, ambacho ni chama tawala.
Kwa sasa hivi nguvu kubwa ya CCM dhidi ya wanachama wake ni kuwa kama wanataka kufanikiwa kweli ni lazima wapendekezwe nacho, vinginevyo unaweza kushinda kwenye kura ya maoni lakini ukatemwa na wakubwa wa chama, kama yalivyomkuta Njelu Kasaka, miaka michache iliyopita.
Ni kutokana na sheria hiyo mbovu ndiyo Njelu akajibandika uanachama wa chama kimoja cha upinzani ili agombee kule Chunya.
Kama sheria hiyo isingekuwepo, Njelu angeweza kusimama kama mgombea huru na kuwapa wananchi wa Chunya nafasi ya kumkubali tena kama mbunge wao au kumkataa.
Kwa kuwanyima watu haki hiyo, CCM inawanyima watu haki ya kumchagua mtu wamtakaye.
Kama wagombea huru watakubaliwa tena, ina maana CCM haitakuwa tena na ule ubabe wa kuwaambia wanachama wake kuwa wasipojipanga mstari wa nidhamu basi hawana nafasi huko mbeleni.
Si kwa nafasi ya ubunge tu, hata urais. Hebu fikiria kama mwaka 2005 tungekuwa na wagombea huru na jukwaa la wagombea huru wangekuwemo kina Dk. Kigoda, Mzee Malecela au Dk. Salim.
Kwa kulazimisha mgombea mmoja wa CCM na kuwakatalia wengine kushiriki nafasi hiyo, CCM inajilinda kutokana na fedhea inayoweza kupata kama ilivyotokea kule Mbulu, ambapo mgombea wa CCM angeangushwa na mgombea binafsi.
CCM isiendelee na sheria hizi za woga kwani faida ya kurudisha wagombea huru inazidi sana hasara zake. Kabla ya kuangalia faida hizo niseme kuwa hasara kubwa ya kuwa na wagombea huru ni uwezekano wa watu wenye utajiri au uwezo mkubwa wa mali na rasilimali watu mkubwa kuweza kujiingiza katika kinyanganyiro cha uchaguzi. Wafanyabiashara au wanasiasa matajiri wanaweza kutumia hazina zao kufadhili kampeni zao na hakuna utaratibu mzuri wa kuwasimamia.
Jibu langu kwa hilo ni kuwa ni jukumu la serikali na wadau wengine kukaa chini na kujifunza kutoka nchi nyingine ni jinsi gani tunaweza kuwarudisha wagombea binafsi bila kuanza kutengeneza mamluki wa kisiasa au kuwanyima watu haki zao za msingi za kuchagua na kuchaguliwa.
Faida za wagombea binafsi
Ukiangalia kwa undani hata kwenye nchi zilizoruhusu wagombea binafasi hakuna wagombea binafsi wengi ambao wameweza kushika nafasi za uongozi wa juu.
Ross Perot, licha ya mapesa yake yote hakufua dafu dhidi ya wagombea wa Democratic Party na Republican kule Marekani, ingawa alianza kwa vishindo.
Ni vigumu sana kwa wagombea binafsi kushika nafasi za juu za uongozi. Hata hivyo, uzuri wa kuwa na wagombea huru ni kwanza: Wanawakilisha mawazo ambayo yako nje ya vyama vikuu. Kwa sababu hiyo wanaweza kuzungumzia nje ya taratibu za chama bila hofu ya kulazimishwa kutimiza nidhamu ya chama au kujiweka chini ya mfumo wa mikutano na vikao vya chama.
Pili, inawapa uhuru Watanzania kujaribu kushika nafasi ya uongozi bila kulazimishwa kufungamana na chama au kuanzisha chama kingine. Kwa mfano, watu kama kina Mtikila, Mrema etc wasingelazimika kutafuta nafasi za uongozi kwa kuamua kuanzisha chama cha siasa. Ingependeza kuona Mrema anagombea ubunge wa jimbo fulani bila kutumia chama fulani ila mawazo yake tu.
Ni mambo haya ya kulazimisha vyama yaliyomnyima nafasi Njelu Kasaka mwaka uliopita kwani bila ya chama hakuwa na jinsi ya kugombea ingawa kama angepewa nafasi nina uhakika angeshinda kule Chunya.
Tatu, hata kama wagombea huru hawapati nafasi ya kushika uongozi lakini mara nyingi kama hoja wanazojenga zina nafasi, basi vyama vikubwa vinaweza kuzidandia hoja hizo ama sivyo wapinzani wanaweza kuzitumia na kupata ushindi.
Nne, kama mgombea huru anashinda katika nafasi ya uongozi na hivyo kuwa katika nafasi ya ubunge, basi anakuwa ni mtu mwenye kura ya turufu hasa pale ambapo Bunge au halmashauri imegawanyika karibu nusu kwa nusu na hivyo kufanya maamuzi na kura kuwa ngumu. Kwa mfano, kama Bunge lina viti 100 na wagombea wa chama tawala wana kura 50 na wa vyama vya upinzani wana kura 40 na wagombea huru wana 10 na kama hoja inapitishwa kwa theluthi mbili basi utaona umuhimu wa wagombea huru! Tano, zaidi ya yote, kwenye vyama ambavyo vinafanya kura za maoni na kuwaengua baadhi ya wanachama wake, kuwa na wagombea huru kunawapa watu nafasi ya kumpigia kura wanayemtaka na si yule ambaye chama kinamtaka. Hivyo, wale walioenguliwa kutokana na wivu, kisasi au husuda ya aina yoyote wanaweza kugombea katika majimbo yale yale na kushinda.
Ukiangalia faida hizo, utaona ni kwanini Chama Cha Mapinduzi hakiko tayari kuruhusu wagombea huru!
Mwisho
Ni kwa sababu hiyo basi nitoe wito kwa serikali na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuwa itupilie mbali wazo lake na mpango wake wa kukata rufaa kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu (kwa mara nyingine) kwani haina maana, haiingii akilini na kwa hakika kama alivyosema Mwalimu Nyeyre kuanzia mwanzo uamuzi wa kufuta haki ya wagombea huru uamuzi huo ni kipumbavu.
Si maneno yangu, ni ya Nyerere na kwa vile mnamuenzi basi nawasihi mkubali tu yaishe. Na msiote hata ndoto ya kwenda bungeni kutunga sheria nyingine ya kupinga mahakama; wabunge wetu hawaburuzwi tena.