Je, huwa unasikiliza sera za wagombea na vyama usivyoviunga mkono?

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
Inaeleweka kuwa kuna baadhi ya wafuasi wa vyama au wagombea fulani hawana utayari wa kusikiliza wagombea au sera za vyama wasioviunga mkono. Hii ni kwakuwa, kwa namna fulani, ‘wamefunga ndoa’ na sera zile wanazozijua tu na hawajawaza umuhimu wa kufungua akili na kuruhusu mitazamo mipya kutoka kwa wengine.

Hata hivyo, kufungua masikio na akili zetu kwa sera tofauti ni namna bora ya kupokea taarifa mpya na kubadili au kuboresha mitazamo yetu. Kupata taarifa zote za muhimu kwa kadiri inavyowezekana kipindi cha uchaguzi kunaweza kutufungua kwa hoja mpya au bora zaidi ya tunazozijua, maoni na mitazamo ambayo hatukuwahi kuizingatia awali lakini kwa namna moja au nyingine inaweza kuwa na manufaa kwetu.

Kusikiliza wanasiasa na wagombea kutoka vyama tofauti kunaweza kutusaidia kuelewa kwa undani zaidi masuala yanayotukabili kama jamii, na hivyo kutusaidia kufanya maamuzi ya busara. Hivyo, ni vyema endapo kila mmoja, pasi kujali chama au mgombea anayemuunga mkono, akawa tayari kusikiliza hoja na mawazo ya wengine na kuweka ushabiki pembeni. Kwa kufanya hivi mtu anaweza kupiga kura akiwa na taarifa za kutosha na hivyo kumsaidia kufanya maamuzi sahihi bila upendeleo au ushabiki.

Kila chama na mgombea anapenda kuona watu wengi wakihudhuria kwenye mikutano yao. Hi ni kwakuwa wanahitaji watu kuzisikia sera zao. Huu ndiyo wakati sahihi wa mwananchi kusikiliza na kujua yale ambayo mgombea au chama fulani kinayaamini na kinatazamia kuyatekeleza. Huu ni wakati muhimu wa kupata taarifa muhimu ambazo zitamsaidia mwananchi kupiga kura akiwa anajua anachokitaka.

Kusikiliza upande mmoja tu wa watu au taasisi zinazowania nafasi zinazogusa maisha yako moja kwa moja ni kujinyima taarifa za msingi. Ni vyema kujiridhisha na kila upande ili ujue ni upande gani unalinda maslahi yako na kisha kufanya maamuzi yanayotokana na kuwa na taarifa za msingi na si kwa kufuata mkumbo au kwa ushabiki tu.

Lakini pia, kuwa na utayari wa kusikiliza na kuchambua mitazamo tofauti kisha kufanya maamuzi tunayoridhia kunahakikisha kuwa tunachangia katika ujenzi wa demokrasia yenye nguvu. Kufanya maamuzi ya kura kwa msingi wa ufahamu na uelewa, tunakuwa sehemu ya mchakato wa kisiasa unaotegemea taarifa na hoja badala ya upendeleo wa kibinafsi au ‘ubabe wa kisiasa’, ambapo watu wanapiga kura kutokana na umaarufu wa chama au mgombea.

Kwa hivyo basi, ni vyema kusisitizana kuwa linapokuja suala la kufanya maamuzi ya kupiga kura, ni muhimu kufungua macho na masikio yetu. Tusiwe wapiga kura wenye kukosoa bila kusikiliza au kuunga mkono bila kuhoji na kujiridhisha. Tunapaswa kuwa wachambuzi wa sera na mipango ya wagombea ili tuchangie katika ujenzi wa jamii bora na demokrasia yenye nguvu.

Swali ninalokuacha nalo ni: Je, huwa unasikiliza sera za wagombea na vyama usivyoviunga mkono? Kwanini unadhani ni muhimu kusikiliza au kutosikiliza?
 
Sijawahi kupanga muda wa kusikiliza uongo wa wanasiasa, lakini inapo tokea sera zao zimenikuta nilipo basi pengine naweza nikajikuta nasikiliza.
 
Back
Top Bottom