Kupinga wagombea huru, ni uamuzi wa "Kipumbavu"

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,991
NB: kichwa cha habari nilichopendekeza kutoka kwenye gazeti ndiyo hicho lakini naona waliamua kubadili kwa discretion yao. Hii ni hoja yangu ya leo.

KABLA hamjanijia juu, niseme mapema kuwa si mimi niliyeuita uamuzi wa kufuta haki ya mtu kuchaguliwa kwa vile hataki kujiunga na chama cha siasa kuwa ni wa kipumbavu.

Nimerudia tu maneno aliyoyasema Baba wa Taifa mbele ya watawala wetu kwenye sherehe za Mei Mosi mwaka 1995, katika Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya. Mwalimu hakuwa amewatukana au kuwatusi reja reja bali aliweza kuona kitu ambacho mtu yeyote mwenye akili timamu na ambaye haogopi kufikiri anaweza kukiona bila kutumia darubini au kurunzi kuwa kumkataza mtu kuchaguliwa kwa sababu hataki kuwa UDP, TLP, CCM au chama kingine chochote cha kisiasa ni kufanya uamuzi wa kipumbavu. Nakubaliana na Mwalimu.

Ule mchezo wa kuigiza wa ‘mgombea binafsi’ naona unaendelea bila kukoma. Baada ya Mahakama kuthibitisha maamuzi ya awali yaliyoona kuwa sheria inayomtaka mtu kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa ili achaguliwe ni kinyume cha katiba, watawala wetu wameanza tena kuandaa rufaa nyingine ili hatimaye uamuzi wa mwisho uwe wa Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo yenye uamuzi wa mwisho nchini.

Binafsi nimechoka na danadana hii ya serikali kwani haihitaji mtu uwe msomi wa chuo kikuu au kuwa ni mtaalamu wa anga za juu kuweza kuona kuwa serikali haina hoja hata ikijitahidi vipi kuhalalisha msimamo wake wa kupinga mgombea binafsi.

Na kwa kadiri wanavyozidi kuchelewesha kufanyia mabadiliko katiba na sheria ya uchaguzi, ndivyo wanavyozidi kuthibitisha kuwa bado hawajajijengea utaratibu wa kuheshimu maamuzi ya mahakama kama zilivyo nchi nyingine za kidemokrasia. Ninasema hivyo kwa sababu kesi hii ya mgombea binafsi imeanza tangu mwaka 1993 baada ya Mchungaji Christopher Mtikila kufungua kesi hiyo kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambako alishinda kesi hiyo lakini serikali ilikwepa kutekeleza hukumu ya mahakama.

Hiyo ilisababisha Mtikila kufungua kesi ya kikatiba ambayo nayo alishinda na serikali wakakata rufaa tena, na kwa mara nyingine hoja ya mgombea binafsi imeshinda tena. Hata hivyo, kama habari zilizoripotiwa na gazeti moja ni za ukweli, basi serikali bado haioni upumbavu wa uamuzi huo na badala yake wanataka kwenda mahakama ya rufaa kuona kama itauthibitisha au la. Miaka 15 baadaye bado wanajaribu kuonyesha kuwa wana hoja. Sidhani kama atateremka malaika kutoka mbinguni kuwapigia parapanda ya mwisho kuwa ‘mmeshindwa’! Nilipokaa chini kuyasikiliza tena maneno ya Baba wa Taifa hasa alipoelezea kwanini alikwenda kinyume na chama chake, tena hadharani kwenye maelfu ya watu, nilitambua jambo moja kuwa hoja ya kukataza mgombea binafsi ni hoja ya kibaguzi, ya hatari, na ambayo asili yake ni woga wa mtu kukimbia kivuli chake yeye mwenyewe.

Nikiwa mwanafunzi mzuri wa Mwalimu, nikajiuliza ni kitu gani kweli kilimfanya Mwalimu aipinge hoja hiyo kwa nguvu namna hiyo? Hatimaye nimepata majibu na ninaomba mpendwa msomaji ufuatane nami ili uweze nawe kuona kuwa uamuzi wa kuwanyima wagombea binafsi nafasi ya kuchaguliwa kwa hakika na pasipo shaka ni uamuzi wa ‘kipumbavu’.

Vipo vipengele vikubwa viwili ndani ya katiba ambavyo ndiyo chanzo cha mgogoro huu wa mgombea binafsi. Kwanza ni kifungu cha 67: 2 kinachosema: “Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo…(b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; na kifungu cha 39 (1) ambacho nacho kinasema kuwa mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kama..(c) ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.”

Mahakama Kuu ilikuwa sahihi

Mahakama Kuu ilipopitisha uamuzi wake wa kukubaliana na hoja za mawakili wa Mchungaji Mtikila walifafanua kwa kina kwanini serikali haina hoja hasa kwa mtu anayeangalia katiba kama sheria mama na kiini cha sheria nyingine zote nchini. Kilichofanyika ni kitendo ambacho hakina budi kuwatia aibu wanasheria walioshiriki kukifanya.

Baada ya serikali kushindwa katika ile kesi ya awali ya Mtikila, ilitaka kukata rufaa lakini kwa namna ambayo wanajua wao wakaamua kuachana na rufaa hiyo na badala yake kwenda bungeni kutunga sheria iliyopinga amri ya mahakama na hivyo kuingiza kwenye katiba vipengele hivyo hapo juu.

Sheria hiyo ya mwaka 1994 ndiyo iliyomfanya Baba wa Taifa kuita uamuzi wa serikali kufuta haki ya raia ni wa kipumbavu na kuwaambia kuwa kati ya nguvu nyingi ambazo serikali inafikiri inazo, haina nguvu ya kufuta haki ya mtu.

Kitendo cha Bunge kuingilia kesi iliyokuwa mahakamani na kupitisha sheria iliyokuwa na lengo la ‘kuwahi’ maamuzi ya mahakama hakikupokewa vizuri na Mahakama Kuu.

Majaji wakiongozwa na aliyekuwa Jaji Kiongozi Manento, walisema hivi kuhusu kitendo hicho cha wabunge kuwa: “Sheria namba 34 ya mwaka 1994 ambayo kama ilivyosemwa awali, ilipitishwa na Bunge tarehe 16/10/94 wakati uamuzi wa Jaji Lugakingira (kama alivyokuwa wakati huo) ulitolewa tarehe 24/10/94, kwa vile bado shauri lilikuwa mahakamani, Bunge lilipopitisha sheria. Kwa kuzingatia utaratibu, ni lazima, kwa mara moja tulaani kitendo hiki.” Lakini wao hawakusikiliza wakaendelea na utaratibu wao. Ni kwa sababu hiyo basi nichambue kwanini serikali haina hoja na ni kwanini mahakama ilitupilia mbali hoja zao na ni kwanini Baba wa Taifa aliita uamuzi huo wa kufuta haki ya mtu kuwa ni wa kipumbavu.

Katiba inataja masharti ya mpiga kura

Ibara ya 5 vipengele vya 1 na 2 vya katiba yetu vinasema hivi kuhusu haki ya raia ya kupiga kura, “Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofaywa Tanzania na wananchi. Na haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya katiba hii na ya sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi (2).

Bunge laweza kutunga sheria na kuweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura kutokana na yoyote kati ya sababu zifuatazo, yaani raia huyo: (a) kuwa na uraia wa nchi nyingine; (b) kuwa na ugonjwa wa akili; (c) kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai; (d) kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura, mbali na sababu hizo hakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura.”

Swali ambalo linanikabili mimi ninaposoma ibara hiyo ni kuwa, kama mtu ana haki ya kupiga kura baada ya kutimiza masharti hayo machache bila kumlazimisha awe mwanachama wa kisiasa, kwanini yule anayechaguliwa (ambaye anaweza pia kuwa ni yeye) alazimishwe kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa? Kama wabunge wa CCM hawakuona umuhimu wa kumtaka kila mpiga kura awe mwanachama wa chama cha kisiasa, kwanini walikubali kuandika sheria ambayo inamtaka kila anayechaguliwa kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa?

Kwanini masharti ya mpiga kura yasiwe sawasawa na yale ya mpigiwa kura na hivyo kuoanisha mambo mawili ambayo yanahusiana?

Katiba inakataza sheria za kibaguzi

Kifungu kingine cha katiba yetu kinasema hivi kuhusu kutungwa kwa sheria yoyote ya kibaguzi na chombo chochote (kwanza kabisa ni Bunge).

“Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.” Ibara ya 13 (2). Kwa maneno mengine kwa kuwataka wale wanaotaka kugombea nafasi ya uchaguzi kuwa wawe wanachama na wapendekezwe na chama cha kisiasa ni kuwabagua endapo wanatimiza masharti mengine yote. Ndiyo maana sheria iliyotungwa kuakisi mabadiliko hayo ya kikatiba kimsingi ni sheria ya kibaguzi japo si wa moja kwa moja, lakini ni wa taathira yake.

Katiba inakataza mtu kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa.

Ibara ya 20 ya Katiba yetu kipengele cha 4 kinasema hivi: “Bila ya kuathiri sheria za nchi zinazohusika ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote au shirika lolote, au kwa chama chochote au cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa.” Sasa kipengele hicho kinapingana kabisa na vile vipengele vyetu viwili vya hapo juu ambavyo vinamtaka mgombea wa ubunge au urais lazima awe mwanachama wa chama cha kisiasa.

Kwa kuandika sheria inayomtaka mtu anayetaka kuitumikia nchi yake na raia wenzake kuwa lazima awe mwanachama wa chama cha kisiasa inamfanya mtu huyo kwanza kujiunga na chama cha kisiasa hata kama hakubaliani nacho na pili kumlazimisha aanzishe chama ambacho kitakidhi mahitaji yake. Tatizo la kwanza si kubwa sana lakini la pili ndilo lenye matatizo. Haiwezekani kila anayetaka kugombea nafasi ya uongozi katika nchi yake na hakubaliani na sera za chama chochote kile na yeye aanzishe chama chake! Kwanini tusimpe nafasi mtu huyo kuuza sera zake na ilani yake yeye mwenyewe na kuelezea jinsi gani ataitekeleza na tukikubali tunamchagua, tukiona hana mpango tunamkataa? Kwanini mtu ambaye hapendi ukiritimba na nidhamu ya vyama vya kisiasa alazimishwe kujiunga navyo wakati anaamini na kutambua kuwa sera zake zinaweza kukubalika?

Haki ya kuchaguliwa ni haki ya binadamu

Katiba hiyo hiyo katika kipengele cha pili kinachohusu haki zetu za msingi kinatambua kwamba “kila binadamu ana haki ya kuthaminiwa na kutambuliwa utu wake”.

Kwa kusema kuwa anayeweza kuongoza katika Tanzania ni yule mwenye kadi ya chama cha siasa ambaye amepitishwa na chama hicho, hatuoni kuwa kwa taathira yake tunawafanya wale wasio katika vyama vya siasa kuwa duni na kuwatweza?

Je, fisadi mwanachama wa chama cha siasa anayetuongoza ni bora zaidi kuliko mwadilifu asiye na chama na ambaye ananyimwa kuongoza?

Kwanini mwanachama wa chama cha siasa awe na ujiko huu wa kuweza kugombea nafasi ya uongozi wakati raia mwingine ambaye naye ana uwezo wa kuongoza anyimwe? Kama raia ana haki ya kuchagua basi na yeye ana haki ya kuchaguliwa vile vile.

Si hivyo tu, kama vile hukumu ya kina Jaji Manento ilivyosema kuwa sheria hiyo ya 1994 iliyosababisha kufutwa kwa haki ya mtu kugombea bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa “marekebisho hayo yamekiuka katiba na pia yamekiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.”

Kwanini serikali inaogopa wagombea huru/binafsi?

Hata hivyo kutoangalia sababu za serikali kuruhusu wagombea huru ni kutowatendea haki. Hebu tuangalie kwa haraka sababu wanazotoa, kwanini serikali haiko tayari kuruhusu wagombea binafsi.

Wazo la wagombea binafsi/huru ni la kigeni

Hoja hii hutolewa ili kuonyesha kuwa katika Tanzania mambo ya kuwa na wagombea huru ni ya kigeni na hivyo Watanzania hawajazoea mtindo kama huo. Kimsingi hoja hii inawafanya Watanzania kama watoto wadogo. Mwalimu katika ile hotuba yake aliiponda na kuisagasaga hoja hii pale alipotolea mfano jinsi Mbulu ilivyoweza kumsimamisha Chifu Sarwat ambaye alikuwa anakubalika huko kuliko mgombea wa TANU ambaye Nyerere mwenyewe alimpigia kampeni.

Chifu Sarwat alichaguliwa na watu wa Mbulu kama mgombea huru na mgombea wa chama cha siasa (TANU) alishindwa na serikali ikaheshimu uamuzi wa watu wa Mbulu. Hivyo hii si hoja ya msingi.

Hivyo tunaporudisha wagombea huru hatuigi mambo ya kigeni au hatuigi alimradi tunaiga tu.

Ukweli ni kuwa wazo zima la vyama vya kisiasa ni la kigeni, wazo la kuwa na katiba ni la kigeni na hata mambo ya kuandika sheria vitabuni nk, nayo pia ni ya kigeni. Hata hivyo si kila kitu kigeni au utaratibu wa kigeni ni mbaya na usio na manufaa. Mimi sioni ulazima wa kuiga alimradi tu kuiga ili kufanana, hapana, tuige pale tunapoona kuwa kwa kufanya hivyo tunajipa nafasi ya kufanikiwa.

Wazo zima la kuruhusu wagombea huru siyo kwa sababu tutapata viongozi bora huko, hapana, bali kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo na nafasi ya kutaka kuwa kiongozi, basi anapewa nafasi hiyo na si kulazimishwa kutumia chombo fulani. La maana ni kuwa, kiongozi yeyote yule (wa chama au huru) anapatikana kwa kupigiwa kura.

Chama kitakachopoteza sana ni CCM

Ukweli rahisi hapa ni kuwa endapo wagombea huru watarudishwa tena, chama ambacho kitapata athari kubwa sana ni CCM, ambacho ni chama tawala.

Kwa sasa hivi nguvu kubwa ya CCM dhidi ya wanachama wake ni kuwa kama wanataka kufanikiwa kweli ni lazima wapendekezwe nacho, vinginevyo unaweza kushinda kwenye kura ya maoni lakini ukatemwa na wakubwa wa chama, kama yalivyomkuta Njelu Kasaka, miaka michache iliyopita.

Ni kutokana na sheria hiyo mbovu ndiyo Njelu akajibandika uanachama wa chama kimoja cha upinzani ili agombee kule Chunya.

Kama sheria hiyo isingekuwepo, Njelu angeweza kusimama kama mgombea huru na kuwapa wananchi wa Chunya nafasi ya kumkubali tena kama mbunge wao au kumkataa.

Kwa kuwanyima watu haki hiyo, CCM inawanyima watu haki ya kumchagua mtu wamtakaye.

Kama wagombea huru watakubaliwa tena, ina maana CCM haitakuwa tena na ule ubabe wa kuwaambia wanachama wake kuwa wasipojipanga mstari wa nidhamu basi hawana nafasi huko mbeleni.

Si kwa nafasi ya ubunge tu, hata urais. Hebu fikiria kama mwaka 2005 tungekuwa na wagombea huru na jukwaa la wagombea huru wangekuwemo kina Dk. Kigoda, Mzee Malecela au Dk. Salim.

Kwa kulazimisha mgombea mmoja wa CCM na kuwakatalia wengine kushiriki nafasi hiyo, CCM inajilinda kutokana na fedhea inayoweza kupata kama ilivyotokea kule Mbulu, ambapo mgombea wa CCM angeangushwa na mgombea binafsi.

CCM isiendelee na sheria hizi za woga kwani faida ya kurudisha wagombea huru inazidi sana hasara zake. Kabla ya kuangalia faida hizo niseme kuwa hasara kubwa ya kuwa na wagombea huru ni uwezekano wa watu wenye utajiri au uwezo mkubwa wa mali na rasilimali watu mkubwa kuweza kujiingiza katika kinyang’anyiro cha uchaguzi. Wafanyabiashara au wanasiasa matajiri wanaweza kutumia hazina zao kufadhili kampeni zao na hakuna utaratibu mzuri wa kuwasimamia.

Jibu langu kwa hilo ni kuwa ni jukumu la serikali na wadau wengine kukaa chini na kujifunza kutoka nchi nyingine ni jinsi gani tunaweza kuwarudisha wagombea binafsi bila kuanza kutengeneza mamluki wa kisiasa au kuwanyima watu haki zao za msingi za kuchagua na kuchaguliwa.

Faida za wagombea binafsi

Ukiangalia kwa undani hata kwenye nchi zilizoruhusu wagombea binafasi hakuna wagombea binafsi wengi ambao wameweza kushika nafasi za uongozi wa juu.

Ross Perot, licha ya mapesa yake yote hakufua dafu dhidi ya wagombea wa Democratic Party na Republican kule Marekani, ingawa alianza kwa vishindo.

Ni vigumu sana kwa wagombea binafsi kushika nafasi za juu za uongozi. Hata hivyo, uzuri wa kuwa na wagombea huru ni kwanza: Wanawakilisha mawazo ambayo yako nje ya vyama vikuu. Kwa sababu hiyo wanaweza kuzungumzia nje ya taratibu za chama bila hofu ya kulazimishwa kutimiza nidhamu ya chama au kujiweka chini ya mfumo wa mikutano na vikao vya chama.

Pili, inawapa uhuru Watanzania kujaribu kushika nafasi ya uongozi bila kulazimishwa kufungamana na chama au kuanzisha chama kingine. Kwa mfano, watu kama kina Mtikila, Mrema etc wasingelazimika kutafuta nafasi za uongozi kwa kuamua kuanzisha chama cha siasa. Ingependeza kuona Mrema anagombea ubunge wa jimbo fulani bila kutumia chama fulani ila mawazo yake tu.

Ni mambo haya ya kulazimisha vyama yaliyomnyima nafasi Njelu Kasaka mwaka uliopita kwani bila ya chama hakuwa na jinsi ya kugombea ingawa kama angepewa nafasi nina uhakika angeshinda kule Chunya.

Tatu, hata kama wagombea huru hawapati nafasi ya kushika uongozi lakini mara nyingi kama hoja wanazojenga zina nafasi, basi vyama vikubwa vinaweza kuzidandia hoja hizo ama sivyo wapinzani wanaweza kuzitumia na kupata ushindi.

Nne, kama mgombea huru anashinda katika nafasi ya uongozi na hivyo kuwa katika nafasi ya ubunge, basi anakuwa ni mtu mwenye kura ya turufu hasa pale ambapo Bunge au halmashauri imegawanyika karibu nusu kwa nusu na hivyo kufanya maamuzi na kura kuwa ngumu. Kwa mfano, kama Bunge lina viti 100 na wagombea wa chama tawala wana kura 50 na wa vyama vya upinzani wana kura 40 na wagombea huru wana 10 na kama hoja inapitishwa kwa theluthi mbili basi utaona umuhimu wa wagombea huru! Tano, zaidi ya yote, kwenye vyama ambavyo vinafanya kura za maoni na kuwaengua baadhi ya wanachama wake, kuwa na wagombea huru kunawapa watu nafasi ya kumpigia kura wanayemtaka na si yule ambaye chama kinamtaka. Hivyo, wale walioenguliwa kutokana na wivu, kisasi au husuda ya aina yoyote wanaweza kugombea katika majimbo yale yale na kushinda.

Ukiangalia faida hizo, utaona ni kwanini Chama Cha Mapinduzi hakiko tayari kuruhusu wagombea huru!

Mwisho


Ni kwa sababu hiyo basi nitoe wito kwa serikali na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuwa itupilie mbali wazo lake na mpango wake wa kukata rufaa kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu (kwa mara nyingine) kwani haina maana, haiingii akilini na kwa hakika kama alivyosema Mwalimu Nyeyre kuanzia mwanzo uamuzi wa kufuta haki ya wagombea huru uamuzi huo ni ‘kipumbavu’.

Si maneno yangu, ni ya Nyerere na kwa vile mnamuenzi basi nawasihi mkubali tu yaishe. Na msiote hata ndoto ya kwenda bungeni kutunga sheria nyingine ya kupinga mahakama; wabunge wetu hawaburuzwi tena.
 
Mwaka 2003 kuna Mkutano ulifanyika Afrika kusini Ukijumuisha Tume za uchaguzi za nchi za SADC na taasisi ya uchaguzi Kusini mwa Afrika,na hoja kubwa ilikuwa ni kuongolea misingi ya udhibiti,Ufuatiliaji na Uangalizi katika eneo la SADC ambapo kuna washiriki kutoka ZEC(ZANZIBARI-Jaji Agustino Ramadhani na Tume ya TAIFA ya uchaguzi( Jaji Lewis makame) walikuwepo.
Moja wapo ya kitu kilichozungumziwa ni hiki
"Kwamba usivunje misingi ya haki za msingi za binadamu na za uhuru (kwa mfano, vifungu maalum vya
kuheshimu haki za binadamu kama vile uhuru wa kujumuika na uhuru wa kujieleza), uhuru ambao
unapaswa kuingiza haki ya kuunda na kuwa mwanachama wa vyama vya siasa na kuwa Mgombea
binafsi"
.Na hivi ndivyo katiba yetu inavyosema.
Mbona Zimbabwe kulikuwa na Mgombea binafsi mwaka huu?
Hivi hii katiba wanavoapa kuilinda ni kwa matumbo ya watu?Another Vanity under the sun!!!
 
hawa watu ni waoga....wanaogpa wakiweka wagombea binafsi watu watakamata majimbo na hivyo kushindwa kupitisha mamuzi yao ya kipumbavu ya kila siku..na lingine wameanza kuogopa baada ya kuona hawa wabunge wa ccm nao wameanza kuwabadilikia hivyo kuruhusu wagombea binafsi utawakutawakina....mengi na wengine wasiotaka upuuzi wa kipumbavu wa ccm na natuamini 2010 wataona sauti ya watu sauti ya mungu...
 
! WANAOGOPA MADONGO KAMA HAYA WAONE SASA
HAWAKUJUA WATU WAMEBADILIKA BADALA YA KUSOMA NYAKATI...HAWANA ADABU....BABA MTIKILA TUKO NYUMA YAKO..

""CCM kukata rufani kesi dhidi ya Dk. Slaa""

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha kimetangaza kusudio la kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na Jaji Robert Makaramba wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu kesi ya matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Karatu.

Akitangaza kusudio la kukata rufaa ya hukumu hiyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mohamed Mbonde alisema uamuzi wa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo umefikiwa na Kamati ya Siasa ya Mkoa katika kikao chake kilichofanyika Mei 17 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katibu huyo kusudio hilo la kukata rufaa litawasilishwa mahakamani wiki hii kabla rufaa yenyewe mwezi ujao.

“Katika kikao hicho Kamati ya Siasa ilijadili kwa kina hukumu hiyo na kukubaliana kuwa hukumu ya Jaji Makaramba haikuwatendea haki wana CCM,” alisema Mbonde jana ofisini kwake.

Alisema kati ya vipengele ambavyo wanaona havijawatendea haki kile cha idadi ya kura zilizokosewa kutangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Solanus Nyimbi.

“Lakini hapa tunaomba Watanzania watuelewe kuwa CCM inachotafuta ni haki yake na tutatumia taratibu za kisheria kuwa haki hiyo inapatikana,” alisema Mbonde.

Alisema Kamati hiyo ya siasa katika kikao chake imeamua mlalamikaji katika kesi hiyo ya rufaa atatangazwa baadaye pamoja na mawakili watakaowatumia.

Hukumu ya kesi hiyo liyofunguliwa na wanachama watatu wa CCM wakiongozwa na Joseph Haymu kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 yaliyompa ushindi mgombea wa Chadema Dk.Wilbrod Slaa dhidi ya Patrick Tsere wa CCM, ilitolewa Mei 15 mwaka huu.

Katika hukumu yake Jaji Makaramba alisema kuwa Mahakama imeridhika kuwa Dk. Slaa alikuwa mshindi halali wa uchaguzi huo na kura zilizokosewa kuhesabiwa ziliwaathiri wagombea wote wawili lakini hayakuathiri matokeo ya uchaguzi huo.
 
Hivi nani anasomaga haya maandiko ya Mwanakijiji.....nani anamuda wa kusoma haya?
 
Tunawezaje kuwafikishia bandiko hilo wale wanaotaka kukata rufaa. Maana wanaweza kupata shule nzuri sana na nafikiri hawatakuwa na mawazo hayo tena.

"Hoja Hujibiwa kwa Hoja!._ MMKJ" wakiweza kupeleka mahakamani hoja zao zikajibu hoja hii waende.

Lakini kama wao ni kama kichwa cha habari hii basi pia wanaweza kwenda.

Nina uhakika kwa sababu serikali Ipo kwa ajili ya maendeleo ya taifa hawatarudia tena kutaka kwenda mahakamani
 
Nina uhakika kwa sababu serikali Ipo kwa ajili ya maendeleo ya taifa hawatarudia tena kutaka kwenda mahakamani

Ingekuwa vizuri sana kama hii ingekuwa kweli, kwa jinsi mambo yanavyoenda kila siku inayopita nazidi kushawishika kwamba hii siyo kweli.

Na kama siyo kweli, tutaandika tunavyotaka lakini it will take action kuwatoa hawa watu.

Tukifikiri kuwa wana "moral sensitivity" ya kusoma, kuelewa na kuchomwa na articles kama hizi tutakuwa naive indeed.
 
Kama Demokrasia ya Sasa ni 'Upumbavu,' ya Nyerere ilikuwa 'Upunguani'


Mwanakijiji, unapoanza Makala na ‘Nyerere kasema…’ haisaidii kunikaribisha, ili upate nafasi ya kuwasilisha unacho taka kunishawishi, kwa sababu sio wote tunakubaliana na Nyerere alivyo sema.

Usiendelee kunisoma zaidi ya mwisho wa sentensi hii kama umewaandikia wenzako tu, wanaoamini hivyo tayari, kama ambavyo Mchungaji wa Kanisa anavyo fanya misa katikati ya wiki. Kwa sababu Wakristo wengi huwa wana swali Jumapili, misa za ziada za Jumatano zinakosa waumini wa kutosha, halafu Mchungaji anaishia kukihubiria kikundi cha Kwaya. Ili kujiunga na kikundi cha kuimba Kanisani mara nyingi unakuwa tayari umesha yapokea jumla jumla yoyote atakayo sema Mchungaji kabla hata hajafungua kinywa chake. Ukiihubiria Kwaya hupati mwenye dhambi mpya. Sasa jaribu kunishawishi mimi niliyeko nje ya Kwaya, ili upate wafuasi wapya.

Yangekuwa ni mawazo yako, nisinge mgusa Mwalimu Nyerere. Lakini kwa sababu umejenga na kutetea hoja yako kwa sababu Nyerere kasema, basi ngoja nilenge moja kwa moja huko yaliko toka. Wazungu wanasema ‘tukatishe mbio.’

Mwalimu Nyerere alipokuwa ameshika hatamu, wakati ana nguvu ya kuonyesha kujitoa kwake katika Demokrasia ya uchaguzi, alifanya mabaya zaidi ya aliyo yaita upumbavu baada ya kuondoka madarakani. Tukiwa ndani ya Meli ambayo yeye alikuwa ameshika hatamu yake, sio tu ulilazimika kuwa katika CCM kugombea Urais, bali haikuruhusiwa kuwepo ‘CCM nyingine.’ Ghafla Mwalimu akagundua dini, karuka nje ya meli inayo enda mrama Kidemokrasia akaanza kubeza mawazo yale yale aliyo yalinda kwa ‘mkono mzito.’ Ni vigumu kuamini nia ya mtu kama huyo. Kama kulazimisha mgombea awe katika moja ya vyama ni upumbavu, basi kushurutisha kuwe na CCM moja -tena ndani ya CCM moja unachagua kiboxi cha Nyerere au kiboxi tupu - ni vibaya zaidi. Kwa Kiswahili changu finyu, sikupata neno baya kuliko ‘upumbavu’ zaidi ya ‘upunguani.’

Angefanya mabadiliko akiwa bado ndani, wakati meli inazama kabla hajajirusha nje kutafuta usalama wake, na kuanza kutuambia aliotuacha ndani ya jahazi la CCM bila msaada wa Demokrasia ya kweli, oooh, meli yenu inaendeshwa kipumbavu, inazama. Sawa, tuache tujiokoe tunavyo jua wenyewe. Alitaka kurudi kushika hatamu halafu sasa ututose sisi nje ya meli kama ulivyo tutelekeza mara ya kwanza?

Hakuruhisiwa kushauri lolote Kiongozi mstaafu ambaye hakufanya anayo yahubiri baada ya kutoka madarakani.

Moja ya namna ya kurekebisha Demokrasia yetu bila kutegemea vigezo vya Nyerere ambae haaminiki katika Demokrasia ni kubadili Katiba. Lakini kwanza tusubiri uamuzi wa mwisho wa Mahakama.

Pia umesema Sheria inayopingwa na CCM inawanufaisha CCM. Kwa hiyo tunategemea, tena nahakika wana haki, waende Mahakamani kutetea maslahi yao. Ukikubali hilo, basi inabidi pia ukubali haki yao ya kumaliza options zao zote, ikiwa ni pamoja na kukata rufaa mpaka ngazi za juu kabisa za Mahakama.

Mahakama ikitengua uamuzi wa awali na kuenda kama Serikali ya CCM inavyotaka yabidi tuangalie mpango wa kubadili Katiba.

Tukiiweka Katiba sawasawa basi hii haki ya mgombea huru itakuwa haitegemei upepo geugeu unavyo mpuliza mwanasiasa fulani na siasa alizo turithisha za chama chake.
 
Kama Demokrasia ya Sasa ni 'Upumbavu,' ya Nyerere ilikuwa 'Upunguani'

Hakuna mahali popote niliposema kuwa "demokrasia ya sasa ni 'upumbavu' kwa hiyo kwanza umeingia na assumption which totally unfounded and immaterial.


Mwanakijiji, unapoanza Makala na ‘Nyerere kasema…’ haisaidii kunikaribisha, ili upate nafasi ya kuwasilisha unacho taka kunishawishi, kwa sababu sio wote tunakubaliana na Nyerere alivyo sema.

Kila mtu anavyoandika anaandika apendavyo na siwezi kuanza kuandika vile mtu mwingine anataka. Kama Nyerere alisema kitu fulani ukweli unabakia kuwa alikisema na kama ni kweli; kitabakia kuwa kweli. Kuogopa kunukuu alichosema Nyerere kwa sababu Kuhani Mkuu atakwazika ni woga ambao sina, siwezi kuwa nao, na sitokuwa nao. You should've figured that out by now.


Usiendelee kunisoma zaidi ya mwisho wa sentensi hii kama umewaandikia wenzako tu, wanaoamini hivyo tayari, kama ambavyo Mchungaji wa Kanisa anavyo fanya misa katikati ya wiki. Kwa sababu Wakristo wengi huwa wana swali Jumapili, misa za ziada za Jumatano zinakosa waumini wa kutosha, halafu Mchungaji anaishia kukihubiria kikundi cha Kwaya. Ili kujiunga na kikundi cha kuimba Kanisani mara nyingi unakuwa tayari umesha yapokea jumla jumla yoyote atakayo sema Mchungaji kabla hata hajafungua kinywa chake. Ukiihubiria Kwaya hupati mwenye dhambi mpya. Sasa jaribu kunishawishi mimi niliyeko nje ya Kwaya, ili upate wafuasi wapya.

Sikuwa na kujaribu kukushawishi wewe au mtu yeyote mwingine ambaye anakubaliana na hoja hizo. Nilikuwa najenga hoja nyepesi na ya moja kwa moja kuwa uamuzi wa kuzuia wagombea binafsi/huru ni uamuzi wa kipumbavu. Simlengi mtu yeyote zaidi ya hoja ya "wagombea binafsi".


Yangekuwa ni mawazo yako, nisinge mgusa Mwalimu Nyerere. Lakini kwa sababu umejenga na kutetea hoja yako kwa sababu Nyerere kasema, basi ngoja nilenge moja kwa moja huko yaliko toka. Wazungu wanasema ‘tukatishe mbio.’

Ni mawazo yangu na yangu mwenyewe ambayo yanathibitisha na kuungwa mkono pia na mawazo ya watu wengine wengi miongoni mwao ni Nyerere. Mtu anaweza kuwa na mawazo yake lakini mawazo hayo yanakolezwa na kutiwa chumvi na mawazo ya mtu mwingine au yanamulikwa vizuri kama kwa kurunzi na kauli au manano ya mtu mwingine. Hivyo ondoa shaka, Nyerere hakusema yote niliyoyasema mimi hapo.


Mwalimu Nyerere alipokuwa ameshika hatamu, wakati ana nguvu ya kuonyesha kujitoa kwake katika Demokrasia ya uchaguzi, alifanya mabaya zaidi ya aliyo yaita upumbavu baada ya kuondoka madarakani. Tukiwa ndani ya Meli ambayo yeye alikuwa ameshika hatamu yake, sio tu ulilazimika kuwa katika CCM kugombea Urais, bali haikuruhusiwa kuwepo ‘CCM nyingine.’ Ghafla Mwalimu akagundua dini, karuka nje ya meli inayo enda mrama Kidemokrasia akaanza kubeza mawazo yale yale aliyo yalinda kwa ‘mkono mzito.’ Ni vigumu kuamini nia ya mtu kama huyo. Kama kulazimisha mgombea awe katika moja ya vyama ni upumbavu, basi kushurutisha kuwe na CCM moja -tena ndani ya CCM moja unachagua kiboxi cha Nyerere au kiboxi tupu -

Absurd, unnecessary and completely immaterial. Sikuwa na mjadili Nyerere, sikuwa najadili demokrasia wakati wa Nyerere, sikuwa najadili uchaguzi wakati wa Nyerere, sikujaribu kujadili suala la dini or whatever other think you might have thought I was discussing.

Nitarudia tena pole pole ili usipotee njia; Mjadala wangu ni kuwa uamuzi wa serikali ya sasa na iliyotangulia ya kupinga wagombea huru ni uamuzi usio wahaki, hauna msingi wa Kikatiba na kwa hakika kama Mwalimu alivyosema ni wa "kipumbavu".

Jukumu lako kama mkosoaji wa hoja yangu ni kunishawishi mimi kwanini uamuzi huu si wa kipumbavu, unakubaliana na Katiba na haki za raia na kwanini serikali iko sahihi na mahakama imekosea. Hapo ndipo Hoja hujibiwa kwa hoja inapokuja. Mengine yote unaweza kuyaanzishia mada au yameshajadiliwa. Unakubaliana na serikali kupinga wagombea huru/binafsi na kwanini? iti izi veri veri simpo!

ni vibaya zaidi. Kwa Kiswahili changu finyu, sikupata neno baya kuliko ‘upumbavu’ zaidi ya ‘upunguani.’

Yawezekana kwa vile tunazungumzia vitu viwili tofauti. Ila kama ungekuwa nilichokuwa nazungumzia ungejaribu kusema "uamuzi wa kutaka wagombea binafsi/huru ni uamuzi wa busara na wa kisomi" halafu unajenga hoja. Halafu ungeweza kuuita msimamo wa Mwalimu wa kutetea wagombea huru kuwa ni wa "kipunguani" na kuonesha kwa hoja upunguani huo. Kwa vile umeona jina la "nyerere" basi umeshindwa kutulia na kuangalia kilichoandikwa na umekuwa 'turned off" due to your own prejudice, bias and unreasonable fear of the name Nyerere.

Angefanya mabadiliko akiwa bado ndani, wakati meli inazama kabla hajajirusha nje kutafuta usalama wake, na kuanza kutuambia aliotuacha ndani ya jahazi la CCM bila msaada wa Demokrasia ya kweli, oooh, meli yenu inaendeshwa kipumbavu, inazama. Sawa, tuache tujiokoe tunavyo jua wenyewe. Alitaka kurudi kushika hatamu halafu sasa ututose sisi nje ya meli kama ulivyo tutelekeza mara ya kwanza?

Once again, hakusema "meli yenu inaendeshwa kipumbavu, inazama", alisema serikali haina haki ya kufuta haki ya raia ya kuchaguliwa ati kwa sababu mtu hataki kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa. Hayo mengine unajaza kisanduku kisicho sahihi kwenye mtihani.


Hakuruhisiwa kushauri lolote Kiongozi mstaafu ambaye hakufanya anayo yahubiri baada ya kutoka madarakani.

Inahusu wagombea binafsi. Vidole vyangu vinauma kukurudisha kwenye mada.

Moja ya namna ya kurekebisha Demokrasia yetu bila kutegemea vigezo vya Nyerere ambae haaminiki katika Demokrasia ni kubadili Katiba. Lakini kwanza tusubiri uamuzi wa mwisho wa Mahakama.

Demokrasia inatengenezwa na watu na ukiniuliza mimi yawezekana tulikuwa na demokrasia kubwa katika maeneo wakati wa Nyerere kuliko ilivyo sasa. Kama Nyerere alikubali na kuheshimu matokeo ya Mbulu ambako mgombea huru wa TANU aliyesimama yeye mwenyewe baada ya Kamati ya Tanu kupitisha mtu mwingine kwanini usikubali kuwa hiyo ni Demokrasia? Si wangemuacha Njelu agombee kama mwanaCCM huru? Yaani ya Njelu ni Demokrasia na ya Chifu Swarat siyo?
Pia umesema Sheria inayopingwa na CCM inawanufaisha CCM. Kwa hiyo tunategemea, tena nahakika wana haki, waende Mahakamani kutetea maslahi yao. Ukikubali hilo, basi inabidi pia ukubali haki yao ya kumaliza options zao zote, ikiwa ni pamoja na kukata rufaa mpaka ngazi za juu kabisa za Mahakama.

Ukisoma makala nzima utaona kuwa hakuna mahali ambapo nimesema kuwa CCM au mtu yeyote hana haki ya kwenda Mahakamani kukata rufaa. Kwa vile umeona jina "Nyerere" na mawazo yako yameenda mbali zaidi basi umesoma kuwa nimesema CCM hawana haki ya kwenda mahakamani.

Hoja yangu ni ile ile, uamuzi wa kupinga wagombea huru/binafsi Tanzania ni uamuzi wa kipumbavu, hauna msingi katika Katiba n.k Na mahakama zimeshaamua hivyo kwa karibu miaka 15 sasa! Waende Mahakama ya Rufaa au wafanye uhuni waliofanya mwanzo wa kwenda kubadili sheria wakati kesi iko mahakamani.

Mahakama ikitengua uamuzi wa awali na kuenda kama Serikali ya CCM inavyotaka yabidi tuangalie mpango wa kubadili Katiba.

Tukiiweka Katiba sawasawa basi hii haki ya mgombea huru itakuwa haitegemei upepo geugeu unavyo mpuliza mwanasiasa fulani na siasa alizo turithisha za chama chake.


Ukiiweka katiba sawa wewe na nani? Kama CCM ingetaka kuwa inatii mahakama ingeshatii zamani sana. Walibadili sheria baada ya kushtakiwa katika kesi ya Chavda ili kufanya serikali iwe vigumu kudaiwa, na walibadili sheria walipotakiwa kuruhusu wagombea huru. CCM hawatobadili Katiba ili watu wengine wanufaike.
 
Jaribu kuwa open minded. Just because nimekupinga huwezi kusema sikutaka kukushawishi wewe. Hizo lugha za mipasho. Si umemwandikia kila mtu? Mwandishi anatafuta as big an audience as one can get.

Huwezi kususa.

Halafu, hakuna sehemu nime quote Nyerere. Lugha ya Meli, na kuzama jahazi ni 'metaphor,' au 'figurative.' Kila siku unakosea hapo. Kama ulivyo sema nime nukuu sheria vibaya. Wewe ni mwandishi kwa nini huelewi metaphors?
 
Jaribu kuwa open minded. Just because nimekupinga huwezi kusema sikutaka kukushawishi wewe. Hizo lugha za mipasho. Si umemwandikia kila mtu? Mwandishi anatafuta as big an audience as one can get.

Huwezi kususa.

Halafu, hakuna sehemu nime quote Nyerere. Lugha ya Meli, na kuzama jahazi ni 'metaphor,' au 'figurative.' Kila siku unakosea hapo. Kama ulivyo sema nime nukuu sheria vibaya. Wewe ni mwandishi kwa nini huelewi metaphors?

Wewe Kuwadi Mkuu, nakusihi uache mara moja kubishana na Mwanakijiji kuhusu Nyerere......utaishia kulamba sakafu bure....oohooooo
 
Ni kweli,

Serikali inasahau kabisa kuwa chama cha siasa ni kikundi cha watu wenye itikadi moja. Kutokukubaliana na itikadi za vyama vyote vilivyosajiriwa hakumnyimi raia haki yake ya kuchagua viongozi na vile vile kwa yeye kuchaguliwa kuwa kiongozi. Haki hiyo ni ya msingi kwa raia wote wa nchi hii bila kujali rangi, itikadi, jinsia, itikadi zao. In fact kipengele cha kusema kuwa mgombea uraisi au ubunge lazima awe na elimu fulani nacho kinakiuka haki za raia hasa kwa vile inajulikana kuwa kwa Tanzania, elimu ya chuo kikuu bado ni anasa; ni wachache sana wanaoipata.
 
......acha hasira na ma-emotions wewe!! kama ni mawazo yako na yako mwenyewe basi si ungebaki nayo mwenyewe?? nani alikuomba uyalete hapa??
kila mara unapoingiza Nyerere kwenye mazungumzo basi kwa taarifa yako ua una-compromise sana credibility yako!!! si amini kama wewe si mwana sisiemu.....huwezi kuipinga SISIEMU wakati unakumbatia Nyerere. Kama hiyo inawezekana basi haupo smart enuff kufanya hivyo na ndicho kisa hasa Bongo upinzani ni Ziro!!!.

Sasa na wewe haya si maoni/ mawazo yako? Nani kakuomba uyalete hapa? Kwa nini hukubaki nayo mwenyewe?
 
acha upambe wewe.....kila siku ua ana shindwa hizi battle za nyerere this nyerere that!!! hoja nzima ya mada hii ipo fraud kwa kosa lake la kum-qoute nyerere kiushabiki na upofu wa hali ya juu, bila jaribio lolote la kuzingatia historia ya utawala wa huyo nyerere na issue husika ya wagombea binafsi na vyama vingi vya siasa!!! shame....

Tatizo lako wewe una hasira tokea babu yako anyang'anywe ng'ombe wake na Nyerere....kwa hiyo nakuelewa...
 
Wewe Kuwadi Mkuu, nakusihi uache mara moja kubishana na Mwanakijiji kuhusu Nyerere......utaishia kulamba sakafu bure....oohooooo

Mwanakijiji anaeona 'N word' ni sawa likitumika willy nilly humu kwenye forum ni mtu wa kumuogopa kwenye hoja huyo jamani? (angalia tundiko lake la mwisho kwenye ishu ya Ballal)

Mtu anaesema, oooh sikukuandia wewe, sikutaka kukushawishi wewe. Huyo ni wa kuogopa kweli huyo au yeye ndio anasusa?

Duuh, sijaona unayo yasema bado. Halafu hata angekuwa ni hivyo mimi nisinge mpaka mafuta ya baraka kama wewe. Napenda ka uhuru kangu kidogo, na sipendi kupelekeshwa na mtu yeyote kama hivyo.
 
Jaribu kuwa open minded. Just because nimekupinga huwezi kusema sikutaka kukushawishi wewe. Hizo lugha za mipasho. Si umemwandikia kila mtu? Mwandishi anatafuta as big an audience as one can get.

Kuhani hiki ndicho ulichosema, if you allow me refresh your recent memory:

Mwanakijiji, unapoanza Makala na ‘Nyerere kasema…’ haisaidii kunikaribisha, ili upate nafasi ya kuwasilisha unacho taka kunishawishi, kwa sababu sio wote tunakubaliana na Nyerere alivyo sema.

Ungejaribu kusema "haisaidii kunikaribisha mtu kama mimi.... au unachotaka kushawishi mtu "kama mimi". Lakini ulivyoandika ni kana kwamba ningekaa chini na kufikiri jinsi gani nitamshawishi Kuhani Mkuu. I never think like that... Na kuhusu audience lengo ni kupata audience yoyote ile na wewe ni ushahidi kuwa nimefanikiwa.

Huwezi kususa.

Now where did you get that idea? Kuna wakati usifikiri zaidi ya kile kilichosemwa ndio maana wakati mwingine mtu anaambiwa "unamchumai mtu dhambi" hivi hivi.

[/quote]Halafu, hakuna sehemu nime quote Nyerere. Lugha ya Meli, na kuzama jahazi ni 'metaphor,' au 'figurative.' Kila siku unakosea hapo. Kama ulivyo sema nime nukuu sheria vibaya. Wewe ni mwandishi kwa nini huelewi metaphors?[/QUOTE]

Metaphor ni kufananisha vitu ambavyo kiasili havifanani lakini kuvifanya vifanane. Unaposema "nchi yetu kwa kweli ni kama meli inayowekwenda kombo" unatumia simile (metaphors). Tatizo ni kuwa unatumia vibaya na mimi kama mwandishi na mjuzi mzuri tu wa istihali ya lugha yetu basi lazima nijaribu kukuonesha hivyo. Hebu nikukumbushe ulivyotumia simile nje ya mada hii.

Angefanya mabadiliko akiwa bado ndani, wakati meli inazama kabla hajajirusha nje kutafuta usalama wake, na kuanza kutuambia aliotuacha ndani ya jahazi la CCM bila msaada wa Demokrasia ya kweli, oooh, meli yenu inaendeshwa kipumbavu, inazama.

Ni wewe uliyeashiria kuwa Mwalimu alisema something even remotely close to "meli yenu inaendeshwa kipumbavu, inazama". Mimi katika kukuonesha kuwa uko nje ya mada na ulichokisema hakihusiani na hoja iliyoko mbele yetu sikubeza simile yako nilichosema na hiki kama ulichukua muda kusoma:

Once again, hakusema "meli yenu inaendeshwa kipumbavu, inazama", alisema serikali haina haki ya kufuta haki ya raia ya kuchaguliwa ati kwa sababu mtu hataki kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa. Hayo mengine unajaza kisanduku kisicho sahihi kwenye mtihani.

Sasa kwa vile kuna tatizo hapa niseme kuwa, mimi nimesema kuwa Nyerere alizungumzia "uamuzi" kuwa ni wa kipumbavu. Hakuzungumzia jinsi meli inavyokwenda au kuwa "inazama". NI wewe ndiyo umechukulia maneno hayo kama hukumu ya Nyerere juu ya mwelekeo wa Meli. Sasa unapotumia simile hakikisha hupotei njiani.
 
CCM wanaogopa mgombea binafsi kwa sababu wanafahamu kutokana na madudu yao atajitokeza Mwanakijiji kutoka kijijini na kushinda uchaguzi kilaini bila wao kujua nani kawafunga goli. Njia muhimu kwa CCN ni kuwakamata MAFISADI wote na kuwaweka rumande na kuacha kutapanya pesa ya walipa kodi huyo mgombea binafsi hataweza kupata kura.

Lakini kwa mwendo huu mgombea binafsi atachukua madaraka 2010.
 
acha upambe wewe.....kila siku ua ana shindwa hizi battle za nyerere this nyerere that!!! hoja nzima ya mada hii ipo fraud kwa kosa lake la kum-qoute nyerere kiushabiki na upofu wa hali ya juu, bila jaribio lolote la kuzingatia historia ya utawala wa huyo nyerere na issue husika ya wagombea binafsi na vyama vingi vya siasa!!! shame....

Hata mimi siamini Nyani Ngabu is riding on Mwnkjj's cocktails. He sounds tough some times. Siamini.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom