Kundi la G55 walioidai Tanganyika mwaka 1993...

Kundi la G55 walioidai Tanganyika mwaka 1993...

Gerald Gachocha
Phares Kashemeza Kabuye
Sebastian Rukiza Kinyondo
John Elikana Byeitima

Yes mkuu wangu hawa walikua ni wabunge wa Mkoa wa Kagera. Gachocha mbunge wa Ngara, Phares Kashemeza Kabuye wa Biharamulo, Sebastian Rukiza Kinyondo wa Bkb vijijini,John Elikana Byeitima wa Karagwe! Wenzao wengine kutoka Kagera waliokua ktk G55 ni Samwel Ntambala Luangisa wa Bkb mjini na Jenerali Ulimwengu mbunge wa Taifa!
 
Bila kusahau jembe la wakati huo Tuntemeke sanga {makete}
 
  1. Njelu Kasaka
  2. Philip Marmo
  3. Saidi Nakua
  4. Azim Premji
  5. Patrick Qorro
  6. Mateo Qares
  7. William Mpiluka
  8. Tumtemeke Sanga
  9. Pascal Degera
  10. John Malecela
  11. Sebastian Kinyondo
  12. Arcado Ntagazwa
  13. Dr Deogratius Mwita
  14. Jenerali Ulimwengu
  15. John Mhina
  16. Musa Nkangaa
  17. Guntram Itatiro
  18. Charles Kagonji
  19. Ismail Ivata
  20. Alipiki Kasyupa
  21. Ombel Mwamfupe
  22. Polile Ombee
  23. Maria Kham
  24. Tabitha Siwale
  25. Edith Mnuo
  26. Evarist Mwanansao
  27. Pascal Mabiti
Well done!
 
hawa walikua wanaume washoka kwelikweli, wazo la saa ya ukombozi wwa Tanganyika walilitekeleza kwa vitendo....nafikiria je wangefanikiwa ingekuwaje? je JK angekua rais katika Jamuhuri ya watu wa Tanganyika?

Mkuu,Jk na yeye alikuwamo katika hilo kundi
 
Mkuu,Jk na yeye alikuwamo katika hilo kundi

JK na Tuntemeke Sanga hawakuwemo ktk orodha ya G55. Kumbuka JK alitolewa Newala na Mwinyi akamteua kuwa mbunge na akamteua kuwa naibu waziri. Na kama sijakasoe ktk kipindi hicho cha 1993 atakua aidha alikua waziri Nishati ama Fedha!

Unaweza soma majina zaidi ktk ukurasa wa 6 wa thread hii nimeongezea kwa mkuu Bello! Ni jukumu la wote waliochaguliwa kuingia ktk Bunge la Katiba kutanguliza maslahi ya taifa ili historia iwakumbuke kama hawa G55. Watakumbukwa kama watapitisha rasmu yenye maoni ya wananchi na siyo vyama vyao!
 
Naomba uwaondoe.
01. John Malecela
02. Tuntemeke Sanga
03. Premji.
Hawakuwemo ktk G55. Ongeza wafuatao;

24. Phares Kabuye
25. Edward Ayila
26. Ramadhan Kombo
27. Dr. Ndembelwa Ngunangwa
28. Guntram Itatiro
29. Othman Mpakani
30. Gerald Gachocha
31. John Byeitima
32. Edson Halinga
33. Dr. Ole Kipuyo
34. Adam Karumbeta
35. Halimeshi Mayonga
36. Dr. John Katunzi
37. Tobi Kimweri
38. Aidan Livigha
39. Erasto Losioki
40. Nassoro Malocho
41. Venance Ngula
42. Benedict Losurutia
43. Pines Nnko
44. Chedil Mgonja
45. Shempemba
46. Nighula
47. Fundikira
48. Kinuno
49. Samwel Luangisa
50. Japhet Sichona
51 Abel Mwanga
52. Pro. Aaron Masawe
53. Shashu Lugeye
54. Kisyeri Chambiri
55. Mathias Kihaule

Naomba mkuu kitambiheshima asome post yangu na aunganishe na orodha ya mkuu bello ili apate majibu wabunge waliokua ktk G55 ni akina nani!
 
Wakuu nimeutafuta uzi huu baada ya kusoma uzi mmoja hapa ambao umehamishiwa Jukwaa la Katiba Mpya ukimtuhumu mzee Warioba mambo mengi ya uwongo mojawapo eti alikua ktk G55!
 
Sasa kumbe kweli Sam Six haaminiki. Kumbe alikuwa kundi la G55 na leo anasema atawashughulikia wanaodai serikali 3? Sasa nimekubali kuwa Old age is not an investment. Huyu jamaa siwezi tena kumwamini kamwe. Tatizo lake kubwa ni kwamba yeye tu ndo mwenye akili na bila yeye hakuna mafanikio. Asipoangalia atavuna aibu nyingine ndipo atajua kuwa wako watu wenye akili na busara kumzidi.
 
Inabidi Watanganyika tutafute njia ya kuwaenzi/kuwakumbuka G55, Pamoja na wengine wote waliopigania kwa VITENDO kurudi kwa serikali ya Tangayika including Wajumbe wa tume ya Judge Francis Nyalali, wajumbe wa Tume ya Judge Robert Kisanga, bila kumsahau Mch. Christopher Mtikila.
 
Najaribu kukumbumbuka hawa jamaa waliomletea headache mwalimu mwaka ule 1993.

Naweza kupata orodha yao na pengine wako wapi sasa? Naweza kuwakumbuka Philip Marmo na Njelu Kasaka tu.

Naomba msaada

Mkuu umepewa majibu vipande vipande itakusumbua sana wewe na wengine kuelewa. Wanataja majina bila kumalizia hawanoneshi hata majimbo yao hao mashujaa wapigania Tanganyika. Jibu kamili na pointi nyingine za kukusaidia jimwage hapa!


[h=1]G55 WALIODAI TANGANYIKA MIAKA 21 ILIYOPITA[/h]Na Daniel Mbega

ILIKUWA ni Jumapili, Aprili 26, 1964, saa 4.00 asubuhi wakati Mwenyekiti wa TANU Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mwenyekiti wa Afro-Shiraz Party (ASP) Sheikh Abeid Amani Karume walipokutana mjini Dar es Salaam na kusaini hati ya makubaliano ya kuziunganisha nchi zao.


Muungano huo ulifikiriwa kwa takribani miezi mitatu na siku 24 tu tangu yalipofanyika mapinduzi ya kuung’oa utawala dhalimu wa Kisultani visiwani Zanzibar Januari 12, 1964. Kabla ya kutiwa saini, wakuu hao wa nchi mbili walikuwa wamefanya mazungumzo mara kadhaa mjini Dar es Salaam na Unguja na ndipo wakafikia muafaka wa kuziunganisha nchi hizo.

Wapo walioupinga (na wanaendelea kuupinga) kwamba haukufuata misingi inayotakiwa katika muungano halisi kama inavyotakiwa, lakini pia wapo walioufurahia na wanaendelea kuufurahia kwa kuwa umeleta udugu na kujenga umoja na mshikamano.

Kwa miaka yote 49 na sasa tunaelekea katika miaka 50, muungano huo umewaunganisha vyema Watanganyika na Wazanzibari na hivyo kuijenga Tanzania yenye nia, umoja, amani, upendo na mshikamano.


Hata hivyo, muungano huo umepitia katika vipindi vigumu na kuna nyakati ambapo umetiwa msukosuko kiasi cha kutishia hatma yake. Hilo, kwa kiasi kikubwa, limetokana na baadhi ya watu kutoa mapendekezo anuani yanayoashiria kwamba muungano huo ama unaweza kuendelea kudumu au kuvunjika kabisa. Kipindi hiki wakati Bunge Maalum la Katiba likiendelea na mjadala mjini Dodoma, ni kigumu zaidi pengine kuliko vipindi vingine.


Hali hiyo imezidi kuwaweka njiapanda Watanzania, na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameazimia kuulinda kwa hali na mali.


Katika hotuba yake ya kwanza aliyoitoa mjini Dodoma baada ya kuapishwa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliweka bayana kwamba suala la muungano litashughulikiwa kikamilifu ili kuunusuru, na kwa kuthibitisha hilo akaunda wizara mpya inayoshughulikia masuala ya Muungano.


Rais Kikwete akaenda mbali zaidi baada ya kukubali mchakato wa Mabadiliko ya Katiba wakati alipoteua Tume Maalum ambayo tangu mwaka 2012 imetumia mabilioni ya shilingi kukusanya maoni na hatimaye kupitisha rasimu ya Katiba, ambayo leo hii imezua mjadala mkubwa Bungeni na kila pembe.


Wananchi wa Tanzania wanazijua faida na hasara za muungano huo kwa kipindi chote hicho na ni wazi kwamba wako katika nafasi nzuri ya kuchangia na kurekebisha kasoro zilizojitokeza ama mapungufu yaliyopo ili kuuimarisha zaidi.
Hoja ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume ya kuanzisha Muungano haikuwa mbaya asilani, lakini katika kipindi cha karibuni kila upande wa Muungano umekuwa ukiona kama unakandamizwa na upande mwingine.


Wakati Wazanzibari wanasema Muungano umeumeza utaifa wao, baadhi ya Watanganyika nao wamekuwa wakisema rasilimali nyingi za Tanzania Bara zimekuwa zikitoweka kuwanufaisha Wazanzibari katika kile kinachoonekana kama kujipendekeza kwa serikali ya CCM kulinda kwa nguvu zote ili usivunjike.


Wazanzibari, kwa upande wao wanaendelea kusema kwamba kwa kipindi chote hicho wameshindwa kufanya jambo lolote kwa maendeleo yao kutokana na kivuli cha muungano na kwamba kila wanalotaka kulifanya lazima serikali ya Muungano itahoji.


SUALA LA UTAIFA…
Yapo mengi ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imekuwa ikitaka kufanya baadhi ya mambo bila kupitia kwenye Muungano na mojawapo ni uamuzi wake wa kutaka kujiunga na Shirikisho la Nchi za Kiislamu Duniani (Organisation of Islamic Conference – OIC) mwaka 1992. Hapo ndipo hasa ‘chunusi’ wa Muungano alipoingia.

Lengo kubwa la SMZ kwa wakati ule, chini ya ‘Komandoo’ Dk. Salmin Amour Juma, lilikuwa kuifanya Zanzibar kuwa nchi au taifa la Kiislamu, wakati inafahamu fika kwamba suala kama hilo lilipaswa kujadiliwa kabla ya kuchukua maamuzi mazito kama alikuwa amechukua Dk. Salmin.


Uamuzi huo ukazua mjadala mrefu sana ndani ya Chama cha Mapinduzi (wakati huo serikali ilikuwa bado ya chama kimoja) na hata bungeni, ambako wabunge na wana-CCM wa Bara waliona wamesalitiwa na kiongozi huyo wa Zanzibar ambaye pia kikatiba, ndiye Makamu Mwenyekiti wa CCM upande wa Zanzibar na pia wakati huo alikuwa ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano!


Lakini Zanzibar haikujiondoa OIC kama tulivyoelezwa na viongozi wetu, bali kilichotokea ni kwamba, OIC ilichunguza na kukuta kwamba Zanzibar siyo Taifa linalojitegemea, yaani Sovereignty State, na kwa mujibu wa masharti yao, haikustahili kuwa mwanachama, hivyo wakaiondoa, siyo kwamba yenyewe ilijitoa baada ya shinikizo.


Pamoja na kuondolewa huko, Zanzibar iliendelea kulalamika kwa kuingiliwa katika mambo yake ya ndani kwa kisingizio cha muungano, ambao kwa kizazi cha sasa wanaiona hali hiyo kana kwamba imewadumaza.


Kujiunga kwa Zanzibar katika OIC kuliwazindua wabunge wa Tanzania Bara, ambao waliona kwamba kuwepo kwa serikali mbili ndani ya Muungano kulikuwa ni kama kuwapa kiburi Wazanzibari, kiasi cha kufanya lolote wanalotaka bila kusubiri baraka za upande mwingine.


Ndipo katika kikao cha Bunge la Bajeti cha mwaka 1993, aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Mheshimiwa Njelu Kasaka akawasilisha hoja binafsi bungeni na kudai Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano ili kutoa uwiano sawa.
Kwa bahati nzuri, hoja hiyo ilipata baraka za Waziri Mkuu wa wakati huo, John Samwel Malecela ‘Cigwiyemisi’ na kupitishwa na Spika wa Bunge wa wakati huo, marehemu Chifu Adam Sapi Mkwawa ili ijadiliwe ingawa alizuia mjadala usiwe mrefu sana.


Ni katika mjadala huo ambapo kulionekana kuna mchanganyiko; wengine wakiunga mkono na wengine wakipinga mabadiliko ya Katiba ya Muungano kufanya ziwepo serikali tatu.


Wabunge 55 waliofahamika kama G55, wakiongozwa na mtoa hoja, Njelu Kasaka, waliiunga mkono hoja hiyo. Baadaye wakaongezeka wengine kumi na kuifanya idadi yao kuwa 65 hadi kufikia Julai 22, 1994.

Wabunge wengine waliounga mkono na majimbo yao ya wakati huo yakiwa kwenye mabano ni; Mateo Tluway Qaresi (Babati), Jenerali Twaha Khalfani Ulimwengu (Taifa/Jumuiya ya Vijana), Mbwete Polile Hombee (Mbeya Vijijini), marehemu John Byeitima (Karagwe), Chediel Yohane Mgonja (same), Japhet Sichona (Mbozi), Benedict Losurutia (Kiteto – bado yuko bungeni), Dk. Mganga Kipuyo (Arumeru Magharibi), Stanley Kinuno (Nyang’hwale), Dk. Aaron Chiduo (Gairo), Edward Oyombe Ayila (Rorya) na Shashu Lugeye (Solwa).



Wengine walikuwa John Mwanga (Moshi Mjini), Dk. Deogratius Mwita (Serengeti), Abel Mwanga (Musoma Mjini), Juma Jamaldin Akukweti (Tunduru), Patrick Silvanus Qorro (Karatu), Steven Mwaduma (Iringa Mashariki), Dk. Ndembwela Ngunangwa (Njombe Kusini), Richard Koillah (Ngorongoro), Ahmed A. Mpakani (Iringa Magharibi), Paschal K. Mabiti (Mwanza), Luteni Lepilal Ole Moloimet (Monduli), Lumuli Alipipi Kasyupa (Kyela), Profesa Aaron Masawe (Hai) na Arcado Ntagazwa (Kibondo).



Katika kundi hilo walikuwemo pia Phineas Nnko (Arumeru Mashariki), Paschal Degera (Kondoa Kusini), Mussa Nkhangaa (Singida Mjini), Halimenshi Kahema Mayonga (Kigoma Kaskazini), Said Abdallah Nakuwa (Lindi Mjini), na Mosi Tambwe (Taifa/Wanawake).



Wengine ni Luteni Kanali John Mhina (Muheza), Charles Kagonji (Mlalo), Kisyeri Werema Chambiri (Tarime), Tobi Tajiri Mweri (Pangani), William H. Mpiluka (Mufindi), Aidan Livigha (Ruangwa), Philip Sanka Marmo (Mbulu), Erasto K. Lossioki (Simanjiro), Shamim Khan (Morogoro Mjini), Raphael Shempemba (Lushoto), Phares Kabuye (Biharamulo – alihamia CUF), marehemu Evarist Mwanansao (Nkasi), Mussa Masomo (Handeni), Jared Ghachocha (Ngara), na Mariam Kamm (Taifa/Wanawake).


MAMBO WALIYOYATAKA…
Walitaka Muungano wa Tanzania, uliozaliwa bila kupata baraka za wananchi wengine na hivyo kuwa na mapungufu, utazamwe upya. Walifikiria kwamba kwa wakati huo ulizaliwa kwa makubaliano tu kati ya TANU na Afro-Shiraz Party (ASP), lakini bila ridhaa ya wananchi.


Wakaeleza kwamba kwa wakati huo ilikuwa lazima Muungano huo ufanywe haraka haraka ili kulinda mapinduzi ya kumwaga damu ya ndugu zatu wa Zanzibar; Unguja na Pemba, ambavyo ni visiwa vidogo sana, kwa hiyo Sultan Jamshid angeweza kurejea tena kwa msaada kutoka kokote kule duniani na inasemekana tayari alikuwa ameandaa majeshi ili arudi kuivamia Zanzibar.


Lakini baada ya kusikia Zanzibar na Tanganyika zimeungana hata yeye kule alikokimbilia na wafadhili wake walikata tamaa kabisa kurejesha tena utawala wa kibwanyenye (Usultani) visiwani humo.
Kwa maana nyingine, tunaweza kusema nchi hizo ziliungana kwa sababu za ki-ulinzi au kiudugu zaidi na kwa uzalendo wa Kiafrika, Muungano ambao haukupata baraka za wananchi kama walivyokuwa wakipigania uhuru wao. Lakini sasa hakuna tena tishio kama hilo (dhidi ya ndugu zetu wa Visiwani).


Kwanza hata wale ambao wangefanya hivyo, sasa nao wamekata tamaa kabisa. Pili, kikubwa zaidi ni kwamba hata serikali vyenyewe ya Mapinduzi Zanzibar sasa ina uhusiano mzuri tu hata na watawala wake wa zamani.
Ni suala la u-taifa tu kwa sababu chini ya mwavuli wa Muungano, Mtanganyika amepoteza kabisa utaifa wake (National Identity). Hakuna popote katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano panapotaja kitu kinachoitwa ‘Tanganyika’ au u-Tanganyika. Badala yake sehemu kama hiyo imemezwa na neon Tanzania. Lakini Zanzibar ina serikali yake yenyewe, SMZ.

Ndiyo maana hata serikali ya CCM ilipoagiza hoja hiyo iondolewe Bungeni mwaka 1994 na kuamua kuendelea na mfumo wa serikali mbili ndani ya Muungano huku ikifanya mikakati kuunda serikali moja, Wazanzibari waligoma kabisa kuafiki muundo huo wa serikali moja.


Wazanziibari, wakiongozwa na Rais wao wa wakati ule Dk. Salmin Amour Juma, walisema katu SMZ haiwezi kufa na kwamba hawaafiki serikali moja. Wengine wakaendelea kusema kwamba Muungano haujainufaisha Zanzibar kwa lolote, hivyo kumaanisha kwamba hawana haja nao.


CCM iliamua kuendesha kura za maoni kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla ili kuona walikuwa na mtazamo gani kuhusu suala la Muungano. Waliokuwa wakitetea Muungano ilionekana waliutetea kwa lugha kali ya hasira, ghadhabu na hata vitisho vya kuwafukuza wenzao kwenye Chama. Waliodai Utanganyika nao walidai kwa lugha hiyo hiyo ya ukali, wakijibu mapigo.


Kitu kilichopaswa ama kinachopaswa kutazamwa hapa ni mambo machache kama yafuatayo; Kwanza kabisa, kudai Utanganyika siyo kosa la uhaini wala la jinai.
Pili, Chama cha Mapinduzi siyo wananchi kwa sababu wananchi wako milioni 35, lakini wanachama wa CCM hadi kufikia mwaka 1994 walikuwa 3,506,355 tu. Pengine kutokana na kuwepo kwa vyama vingi vya siasa idadi hiyo imepungua kwa sasa.

Tatu, walioulizwa maoni hayo kuhusu Muungano mwaka 1994 ni wanachama wa CCM peke yao, tena wapatao 1,349,501. Hesabu hiyo ilikuwa sawa na asilimia 33.49 tu ya wanachama wote nchi nzima. Asilimia 61.75 ya asilimia 33.49 walipendekea serikali mbili, asilimia 29.21 walipendekeza serikali moja, na asilimia 8.27 walitaka serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Kura za maoni zilizoharibika zilikuwa asilimia 0.67.


Jambo la kujiuliza, kura hizo zilihesabiwa na nani? Waliopiga kura ni wana CCM na waliozihesabu ni hao hao wanachama wa CCM pamoja na viongozi wao, ambao walikuwa wakipinga hoja hiyo. Unategemea wangetoa majibu gani? Walichosahau ni kwamba, suala hili ni nyeti na linawagusa wote, wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao, bila kujali itikadi zao za siasa.


Nakumbuka Mkuu wa Mkoa wa Mara wa wakati huo, Bwana Josph Butiku, alitoa kauli kali kwamba msimamo uliokuwa umefikiwa na CCM ni kuwa na serikali mbili katika Muungano kuelekea serikali moja na kwamba kama Rais wa Zanzibar, Dk. Salman Amour Juma, alikuwa anapinga shauri yake.


Bwana Butiku aliyasema hayo Jumanne, Agosti 23, 1994 kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati akishiriki mjadala wa hoja ya serikali ya kufuta Azimio la Bunge la mwaka 1993 la kuanzisha kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Nanukuu maneno yake: “Wananiuliza, umemsikia Rais wa Zanzibar? Aah mimi nasema Rais wa Zanzibar ni kiongozi wetu… tunamheshimu … lakini kakosea … Huu ndio msimamo wa Chama; serikali mbili kuelekea serikali moja na kama Waziri Mkuu hataki, shauri yake, kama Rais wa Zanzibar hataki, shauri yake, maana Chama cha Mapinduzi kina utaratibu wa kuliongoza taifa hili…” mwisho wa kunukuu.


Mwasisi wa Muungano huo, Hayati Nyerere, aliamua kuingilia kati hoja ya Tanganyika na kusema kwamba, kuundwa kwa serikali hiyo kungemaanisha kifo cha Muungano. Hivyo, akasema kwamba, asingekuwa tayari kuona Muungano unakufa hali yeye akiwa hai!


Ndipo akaamua kutunga kitabu cha ‘Uongozi wetu na hatma ya Tanzania’ kilichokuwa kinaponda utaratibu uliotumiwa na viongozi wa Muungano wakati huo kuipitisha hoja ya Tanganyika ijadiliwe bungeni bila kupata baraka za CCM.
Pengine kwa kuwa sasa amekufa ndiyo maana baadhi ya watu wanatumia mwanya huo kutaka kuua Muungano kama walivyoshiriki kuua ‘mtoto mwingine’ wa Mwalimu, Azimio la Arusha lililosisitiza Ujamaa na Kujitegemea.


Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, wale wabunge walioonekana kuipigia kelele sana hoja hiyo walipewa vyeo enzi zile za Rais Ally Hassan Mwinyi; wengine walikuwa mawaziri, na wengine manaibu mawaziri, wakuu wa mikoa na nyadhifa nyingine. Sisi akina yakhe ambao tulitegemea kwamba tungeona mabadiliko, tulitafsiri kitendo hicho kama kuwaziba midomo wabunge hao, maana baada ya kupata vyeo hivyo wakakaa kimya, wengine mpaka sasa hawataki kabisa kuisikia hiyo. Ya nini? Mbona wanakula na kusaza? Hakika inatia uchungu sana.


SERIKALI ILIKUWEPO…
Wazanzibari wanaendelea kupinga muundo wa muungano wa serikali moja, pengine ndiyo maana mpaka sasa (miaka 12 baadaye) CCM haijasema lolote kuhusu muundo wa serikali kwenye muungano, iwe ni serikali mbili kama ilivyo sasa, moja au tatu.


Sababu kubwa inayowafanya Wazanzibari wakatae muundo huo ni kwamba wanadai Zanzibar ilikuwa na serikali yake kamili wakati Muungano ulipofanyika Aprili 26, 1964! Ni kweli kabisa, tangu Januari hadi Aprili 1964 Zanzibar ilikuwa nchi huru (Sovereign State) ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Mnamo Aprili 6, 1964 Zanzibar ilikuwa imefungua Balozi tatu; London, Uingereza alikuwepo Othman Shariff; Cairo, Misri alikuwepo Salim Ahmed Salim, na New York, Marekani alikuwepo Hasnu Makame. Waziri wa Mambo ya Nje alikuwa Profesa Abdulrahman Mohammed Babu.


Pia nchi 17 zilikwishaitambua Zanzibar hadi kufikia Aprili 26, 1964. Nchi hizo ni Ghana (28/1/1964), Cameroon (30/1/1964), German Democratic Republic – GDR (30/1/1964), Poland (30/1/1964), Israel (1/2/1964), Misri (4/2/1964), Urusi (4/2/1964), China (6/2/1964), Czechoslovakia (18/2/1964), Algeria (18/2/1964), India (22/2/1964), Uingereza (24/2/1964), Marekani (24/2/1964), Mali (26/2/1964), Congo-Brazzaville (26/2/1964), Ceylon (26/2/1964) na Liberia (29/2/1964).


Aidha, nchi tisa zilikwishafungua Balozi zao huko Zanzibar kabla ya Muungano. Nchi hizo ni Ghana, GDR, Israel, Urusi, China, Uingereza, Vietnam, Marekani na Ufaransa.


Zanzibar pia tayari ilikuwa mjumbe katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN), mnamo Aprili 6,1964, na ilikuwa inashirikishwa UNESCO, ADB na mashirika mengine ya kimataifa.
Hata hivyo, hiyo siyo hoja ya msingi kwao kukataa serikali moja eti kwa vile wakati huo ilikuwa na serikali yake. Ikumbukwe pia kwamba Tanganyika nayo ilikuwa na serikali yake kamili kabla ya Muungano.


Cha msingi kuzungumzia ili kuunusuru Muungano ni kuangalia maeneo gani muhimu yanayotakiwa kurekebishwa na muundoa gani wa serikali unaoweza kuwa muafaka, maana pamoja na hoja hiyo kuzimwa miaka 1iliyopita, hivi sasa imeibuka tena na inazidi kufukuta kama moto wa volvano, matokeo yake yatakuwa mabaya zaidi hasa katika kipindi hiki cha siasa ya vyama vingi.

…KUJIPENDEKEZA
Tayari Serikali ya Muungano imeonyesha kuwapa nafasi kubwa pia Wazanzibari kwa kuwapa nyadhifa nyingi kwenye Muungano, baada ya Wazanzibari kulalamika kwamba wanabaguliwa.


Hata hivyo, uamuzi huo umetafsiriwa na wengi kama kujipendekeza kwa serikali ya CCM ili kuhakikisha Muungano hauvunjiki. Wengine wanahoji, kama hakuna haja ya serikali ya Tanganyika, iweje basi Wabara nao wasipewe nafasi kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au kushiriki kwenye Baraza la Wawakilishi?


Linaweza kuwa kama suala la kuchimbana, lakini wachunguzi wengi wa siasa wanahoji hata uhalali wa baadhi ya Wizara ambazo si za Muungano kusimamiwa na mawaziri kutoka Zanzibar, wakati huo SMZ nayo ina wizara kama hizo.
Chukulia mfano kwa Wizara ya Ujenzi kupewa Mzanzibari kuiongoza, kwa mtazamo wangu, sidhani kama inawezekana kabisa akatilia maanani ujenzi wa barabara huko Mpanda, Rukwa au Kibakwe kule Dodoma, ambako tangu azaliwe hajawahi kufika na hajui adha wanazozipata wakazi wa huko!


Lakini kama nilivyosema hapo juu, hoja ya msingi hapa ni hii, wanaodai serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano wasichukuliwe kama wahaini, wanafanya hivyo kwa mujibu wa Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama, na viongozi wa CCM wanaposherehekea miaka 43 ya Muungano, hawapaswi kupuuza maoni ya walio wengi na badala yake wanatakiwa kuketi na kuutazama upya muundo wa Muungano huo, siyo kwa sababu waasisi wake hatunao.
Katiba ya Tanzania siyo Msahafu, yaani siyo Biblia wala Qur’an, ambayo haiwezi kukosolewa. Hii imetungwa na wananchi kwa manufaa yao wenyewe, na wanapoona kwamba kuna ulazima wa kufanya matengenezo (marekebisho) basi wanaweza kwa kufuata taratibu.


Kwa maana hiyo, mjadala wa Bunge Maalum la Katiba unapaswa kuwa huru na haki na usiendeshwe kwa shinikizo la yeyote.
 
Mag3,

..Mwalimu aligeuza kibao na kudai serikali 3 siyo sera ya CCM na anayepingana na hilo ajitoe.

..wale G-55 hawakuwa tayari kutoka CCM na kuipigania Tanganyika.

..utekelezaji wa azimio la bunge ulisitishwa, na hoja ya Tanganyika ikarudishwa kwa wanachama wa CCM kupigiwa kura ya maoni.

..kilichoendelea ndani ya CCM hakijulikani mpaka leo, kitu ambacho nadhani at best ni ubabashaji.

..nadhani kilichofanyika ni kuahirisha tatizo tu, lakini tunaelekea kulekule kwenye serikali ya Tanganyika, this time kwa shinikizo la wa-Zanzibari.

Nionavyo mimi, haya mambo ya kudai serikali tatu yataendelea kujirudia rudia nia kama namba inayojirudia, yaani hata ikiganyika vp itaibuliwa upya tu. Reference sasa zitakuwa ni nyingi yaani katiba ya Zanzibar 1985, Katiba ya Zanzibar 2010, UKAWA,G55, hati za Muungano, kwani kwa bahati mbaya historia ni vigumu kufutika. Hibyo hata kama italazimika kuendelea kwa serikali2 kwa wakati huu kwa mfano, lakini suala hili litajirudia tu!
 
Ha ha ha! unanikumbusha mbali sana!!

Kakosea bana ni BILLIONS OF BILIOUS BLUE BLISTERING BARNACLES by this chap.......Watoto wetu hata hawajui TINTIN ni nini!

haddock.jpg

 
Back
Top Bottom