Kuhusu vituo vya kulelea watoto: samaki mmoja akioza si wote wameoza!

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Apr 29, 2023
4,695
6,398
Nimeamua kuuleta huu uzi kutokana na mada kadhaa nilizoziona humu JF zinazoongelea vituo vya watoto yatima kwa mtazamo hasi. Baadhi ya watu wametamani hata hivyo vituo visipewe misaada au vifutwe kabisa.

Uzi ulionichochea hasa ni wa Bexb alioutoa 04/10/2023 wenye kichwa, NIFAHAMISHE KITUO CHA WATOTO YATIMA CHENYE UHITAJI MKUBWA SANA.

Ingawa mleta mada alionekana kuwa na shauku ya kutaka kuhakikisha kuwa msaada husika utaelekezwa mahali sahihi, kuna baadhi ya wachangiaji waliomkejeli na wengine kuonesha hali ya kutokuwa na imani na vituo vya kulelea watoto, maarufu kama vituo vya watoto yatima.

Kwa kuwa kuna ninayoyafahamu yaliyo mazuri yanayotendwa na vituo vya watoto, nimeona niyashirikishe humu jukwaani kwa lengo la kuwatia moyo Watanzania wenzangu , na watu wengine pia, wasione tashwishwi kuvisaidia vituo hivyo kulingana na uwezo waliojaliwa na Mungu.

Ni kweli kuwa kuna baadhi ya vituo vinavyotenda isivyo sahihi, lakini si sababu ya msingi kuhukumu kuwa vituo vyote vya kulelea watoto ni vya kimagumashi.

Na hata vinavyotumika vibaya, kuvifungia au kukataa kuvisaidia si suluhisho. Kufanya hivyo ni kuwatesa zaidi watoto wanaolelewa humo. Watoto wanaweza kuumia zaidi kuliko wamiliki wa hivyo vituo. Ni kuwahukumu (watoto) kwa kosa lisilowahusu.

Ikitokea ikabainika kuna vituo vinatumika ndivyo sivyo, badala ya kuchukua maamuzi yatakayowaumiza watoto, ni bora wahusika wachukuliwe hatua stahiki, ikilazimu, wanyang'anywe hivyo vituo, na kukabidhiwa kwa watu watakaoweza kuviendesha kwa kuzingatia sheria za nchi na maslahi ya watoto.

Huu ni utangulizi. Nitakuja na sehemu ya kwanza, ya pili, ya tatu, n.k. kwa kadiri nikakavyokuwa nikipata muda.

Lakini narudia kutazamisha, kuwa pamoja na kuweko kwa vituo vya "kimchongo" vya kulelea watoto, kuna vingine vingi tu vinavyofanya kazi nzuri sana ya kuwahudumia watoto "wetu" kwa moyo wa upendo.

Ndiyo, ni watoto wetu kwa sababu ama wamezaliwa na Watanzania, au basi wamezaliwa nchini mwetu, Tanzania. Ni sahihi kusema, ni watoto wetu, ni ndugu zetu, ni wenzetu! Tuwasaidie kwa hali na mali, kwa kadiri ya uwezo wetu.

Tukutane tena baadaye kidogo!

Asante.

NB: Niyaelezayo ni ushuhuda binafsi uliotokana na uzoefu wa kufanya kazi kwa miaka kadhaa (katika ngazi ya utawala) kwenye kituo cha kulelea watoto. Hata hivyo , isichukukliwe kuwa vituo vyote vipo hivyo. Ukweli utaendelea kubaki kuwa kuna vitu vinavyotoa huduma kwa uaminifu na kuna vya kimagumashi.

Sitataja jina la kituo wala mkoa isije ikaleta mtazamo kuwa pengine ninawapigia kampeni.
 
SEHEMU YA KWANZA: USHUHUDA ULIONINYENYEKESHA
Baada ya kufunga Chuo, nikiwa mwaka wa kwanza, tulifanya ziara na wenzangu kutembelea Mkoa fulani kutoa huduma za kijamii. Mojawapo ya eneo tulilolitembelea, ni kituo cha watoto, japo ilikuwa kama tunapita tu.

Nikiwa mwaka wa pili, baada ya kufunga Chuo, Meneja wa hiyo taasisi aliniomba nikautumie sehemu ya muda wangu wa likizo kwenye kituo chao, ombi ambalo hatimaye nililikubali, japo mwanzoni nilitaka kughairi. Ni kipindi hicho ndiyo mitazamo yangu ilianza kubadilika kuhusu watoto yatima na wa mitaani wanaolelewa kwenye makao ya watoto. Nilifahamu mambo ambayo yalikuwa tofauti na nilivyokuwa nikifikiria.

Nilipokaribia kuondoka kituoni hapo, Mkurugenzi wa hicho kituo alinialika kwake kwa chakula. Mazingira niliyoyashuhudia, hasa jinsi alivyokuwa akiishi na familia yake, yalinifurahisha sana. Nilijisemea kimoyomoyo, kama kuna mfano wa familia bora, basi ni ya hao watu.

Nilifurahia, jinsi wakati mwingine alivyokuwa akitaniana na mmoja wa watoto wake waliokuwa wakisoma shule ya Msingi kipindi hicho. Nilifurahia jinsi watoto walivyokuwa huru kwa mama yao. Niliondoka nikiwa nimeipata taswira nzuri ya ndoa bora.

Kesho yake, mmoja wa wafanyakazi wa hicho kituo aliniuliza kama ninafahamu chochote kuhusiana na watoto wa huyo Mkurugenzi na mkewe, na niliposema hapana, aliniambia mtoto fulani na fulani si watoto wao wa damu. Waliwaasili wakiwa wachanga, kupitia ustawi wa Jamii. Walienda kuwachukua hospitalini. Na mpaka wakati huo, hao watoto walikuwa hawaujui huo ukweli. Waliamua kuwaficha hadi watakapofikia umri wa kustahimili kuambiwa hayo.

Nilipokumbuka jinsi hao watoto walivyokuwa wanaonekana kuwafurahia wazazi wao, nilipokumbuka jinsi ilivyo shida kwa watu wengi kuishi na watoto wa ndugu zao, nilipotafakari jinsi ilivyo changamoto kwa watu wengi kuishi na watoto wa wenzi wao ambao hawajawazaa, na nikalinganisha na kilichokuwa kimefanywa na hao watu, hakika, "niliwavulia" kofia.

Tokea kipindi hicho, mpaka leo na hata "kesho" nimewaheshimu sana. Si ajabu, baada ya kuhitimu Chuo, nilikubali kwenda kufanya nao kazi kwa miaka kadhaa. Nilitaka nifanye kwa miezi kama sita, lakini ilikuwa kila nikifikiria kuondoka, najihisi kama mchango wangu ulikuwa bado unahitajika. Namshukuru Mungu, pamoja na kuwa kiuchumi mambo yangu yalikuwa "tight" sana kipindi nikiwa nafanya kazi hapo (lakini kamwe sikuwahi kulalamika wala kunung'unika), nafurahi siku hizi ninapopata ushuhuda wa mafanikio ya watoto/ vijana waliokuwa wakisaidiwa na hicho kituo, hasa wale ambao nilishiriki kuwalea/kuwahudumia.

Ikitokea, kwa mfano, mtu akamtuhumu huyo mtu kuwa anakula hela ya watoto, ningekuwa miongoni mwa watu ambao wangejitokeza kupotosha huo uongo. Nakumbuka jinsi mambo ya kifedha wakati mwingine yalivyokuwa "tight" kwa namna ambayo, wakati mwingine, ilalazimu kufunga na kuomba Mungu afanye mwujiza, na kweli miujiza ilikuwa ikitendeka. Si mara moja wala si mara mbili. Kama sikuwa nimewahi kushuhudia miujiza, basi mahali hapo niliona hayo yakitendeka, tena, wakati mwingine, kupitia maombi ya watoto wadogo.

Nitoe mfano mmoja, japo wenyewe ulitokea kabla ya mimi kwenda pale.

Kuna wakati waliishiwa chakula, na uongozi, pamoja na kujitahidi kutafuta suluhisho, hawakufanikiwa. Hawakuwa na wafadhili wa kudumu, wala vyanzo vya uhakika vya kipato

Uongozi, wakishirikiana na watoto wote wanaowalea kituoni hapo, waliamua kufunga na kuomba kwa siku tatu mfululizo kumwomba Mungu awapatie chakula. Mpaka siku ya tatu inatimia, siku ya kuhitimisha maombi, hakukuweko na jibu lolote dhahiri la maombi yao. Lakini, siyo kwamba maombi hayakuwa yamejibiwa, jibu lilikuwa njiani.

Wakahitimisha maombi, bila kuwa hata na unga wa kufungulia mfungo. Kumbuka hawakuwa wamekula kwa siku tatu.

Lakini muda mfupi baadaye, baada ya kuhitimisha maombi, mfanyabiashara mmoja maarufu alimpigia simu Meneja wa hicho kituo kuwa wakutane mahali fulani mjini.

Baada ya masaa machache, alirejea na kile ambacho kila mmoja aliamini ni majibu ya maombi yao: gari la mizigo likiwa limesheheni vitu mablimbali kama unga, sukari, mchelale, maharage, sabuni, n.k.

Hata walipoamua wajenge shule yao, hawakuwa na fedha. Lakini kwa kuamini kuwa Mungu atawasaidia, walichukua hatua ya Imani na kuanza kuchimba msingi, bila kujua zitakakotoka "material".

Kila siku walikuwa wakiomba Mungu awapelekee vifaa vya ujenzi, ambapo watoto wengine walikuwa wakiomba wakiwa wamelala kwenye msingi uliokuwa umechimbwa kusubiria material. Haukuchukua muda mrefu, material yalianza kupelekwa kituoni hapo. Kuna watu waliojitoea, tena bila kuombwa, kupeleka mchanga, mawe, n.k., hatimaye majengo ya primary yakakamilika.

Hata Sekondari, walijenga kwa staili iyo hiyo. Nilishuhudia hilo kwa sababu nilikiwa nimeshaanza kazi mahali hapo kipindi ujenzi wa Sekondari unafanyika.

Naomba niwahakikishie, kabisa, kuwa kuna watu wanaofanya hiyo huduma si kwa sababu ya maslahi yao binafsi, bali upendo pekee.

Mkurugenzi wa hicho kituo aliishi kwa muda mrefu kwenye nyumba ya kupanga, ingawa siyo kwamba alipenda kufanya hivyo. Alitamani kuwa na nyumba yake binafsi, lakini hakuwa na fedha za kufanyia hilo. Fedha zilizokuwa zikipatikana si zake bali za watoto, hivyo zikiwnda kwenye shughuli za Kituo.

Kuna watu waliguswa na moyo wake wa kujituma kuwahudumia watoto na vijana wanaoishi kwenye mazingira magumu, wakaamua kumchangia hela ya kujengea nyumba yake binafsi. Lakini mara zote, alikuwa akiishia kuzitumia kwenye mahitaji ya hao watoto.

Mtu kama huyo, unaanzaje kumtilia mashaka juu ya huduma anayoitoa? Mimi sitathubutu kwa kweli! Kuna watu wanajitoa sana kwa ajili ya watoto"wetu". Uovu wa wachache usiwachafue na walio wema.

Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake apewe. Wanaowahudumia watoto "wetu" kwa upendo waheshimiwe!
 
SEHEMU YA PILI: WATOTO WENYE WAZAZI WANAOISHI KWENYE VITUO VYA WATOTO
Ni kweli kuwa kuna watoto wenye wazazi wanaoishi kwenye vituo vya watoto. Lakini ukiona Ustawi wa Jamii wameliridhia hilo, ujue watakuwa wameshajiridhisha kuwa kituoni kutakuwa ni mahali salama zaidi kwa mtoto husika kuliko kwingineko. Kwa kawaida, kabla mtoto hajasajiliwa kituoni, taarifa hutolewa kwanza Ustawi wa Jamii (labda kama utaratibu umebadilika siku hizi).

Tena, wakati mwingine, ni Ustawi wa Jamii ndiyo unaowapeleka vituoni hao watoto. Unafikiri wenyewe wangefanyeje, kwa mfano, wakienda kubwagiwa mtoto kutokana na wazazi wa mtoto kuwa na mgogoro, unafikiri watampeleka wapi? Nina mifano mingi wa matukio yanayofanana na hayo.

Wakati fulani, mtu mmoja alimtelekeza mtoto mmoja getini mwa kituo cha watoto. Uongozi ulipobaini, ulitoa taarifa Ustawi wa Jamii na kisha msako ukaanza wa kumsaka mtu aliyelifanya hilo.

Wakati huo, mtoto aliyetelekezwa alikuwa akiendelea kulelewa kituoni, baada ya Ustawi wa Jamii kuomba akae kwenye hicho kituo kwa muda wakati jitihada zikifanyika za kumtafuta mhusika. Alipopatikana na kupelekwa Polisi, Ustawi waliomba huyo mtoto asirejeshwe kwa ndugu zake, badala yake aendelee kulelewa na hicho kituo. Hivi hata kama ni wewe, ungekubali mtu kama huyo, aliyeenda kumtelekeza mtoto getini, aachiwe mtoto amlee?

Kama kusingekuwepo na vituo kama hivyo, watoto wa sampuli hiyo wangepelekwa wapi?

Yapo matukio mengi ninayoyajua ambayo kwangu mimi ni uthibitisho kuwa uwepo wa vituo vya kulelea watoto una umuhimu mkubwa sana.

Kuna watoto waliokuwa wakiishi mitaani baada ya wazazi wao kutengana, lakini kwa jitihada za vituo vya watoto, waliweza kupata msaada na hatimaye kuweza kutimiza ndoto zao zikiwemo za kielimu.

Kuna watoto waliokuwa wakiishi mitaani na kutumia madawa ya kulevya baada ya kukataliwa na baba zao kwa madai kuwa si wao waliowazaa, lakini kwa jitihada za vituo vya watoto, waliweza kupata msaada na kugundua kuwa japo alikataliwa na "Jamii" yake, kuna watu wengine wanaoweza kuwapenda na kuwathamini kama watoto wao.

Naendelea kusisitiza! Kwa sababu tu baadhi ya watu wamevitumia vibaya vituo vya watoto, kwa kuvitumia kwa manufaa yao binafsi, bado hakuondoi umuhimu wa kuwepo kwa hivyo vituo. Serikali inafahamu jinsi vilivyo vya muhimu. Kama unataka kuthibitisha hilo, kaliulize Jeshi la Polisi na Ustawi wa Jamii. Watakueleza vizuri.
 
SEHEMU YA TATU: KUHOFIA MISAADA KUTOKUWAFIKIA WALENGWA
Kuna wenye mashaka kuwa huenda misaada inayotolewa haiwafikii walengwa.

Hapa ninaweza nikasema mambo kadhaa.

Kwanza, ni kweli kuwa kuna watu wenye tabia ya kujimilikisha vitu vinavyotolewa kwa ajili ya wahitaji, iwe ni watoto yatima, wajane, watu maskini, n.k. Watu wa aina hiyo wapo karibia kila mahali: makanisani, misikitini, serikalini, na hata kwenye vituo vya watoto. Kwani hujawahi kusikia kashfa ya watu kuiba sadaka maeneo ya ibada?

Lakini ikiwa uongozi wa mahala husika utakuwa makini katika kusimamia utendaji watumishi wake, watu wa aina hiyo huweza kuthibitiwa.

Pili, kuna taasisi zingine viongozi wao wa juu si waaminifu. Na ikiwa mtu kama Mkurugenzi, mfano, wa taasisi si mwamimifu, ni sahihi kusema kuwa hicho kituo ni kibovu.

Inapotokea kina tatizo kama hilo, ni bora busara itumike ili mhailfu ashughulikiwe bila kuathiri maslahi ya watoto.

Kama unataka kutoa msaada kituo fulani lakini una mashaka na jinsi utakvyotumiwa, unaweza ukafanya upelelezi wako kwanza kujiridhisha.

Kama ni kituo cha watoto wadogo sana, angalia afya zao. Mwonekano wao unaweza ukakujulisha kama wanapata huduma sahihi au la.

Kama ni kituo chenye watoto/vijana wanaoweza kujieleza, patembelee mara kadhaa ili utengeneze urafiki na baadhi yao utakaoweza kuwahoji juu ya huduma za hapo.

Lakini kama huwezi kufanya hayo yote, basi upeleke vitu ambavyo utaruhusiwa kuwagawia wewe mwenyewe ukiwa hapo kituoni. Unaweza ukawapekea biskuti, juisi, n.k.

Kamwe, usiyaruhusu mashaka yako kukuzuia kuwatendea wengine mema, hasa wahitaji, wakiwemo watoto wanaolelewa vituoni.
 
Ophanage centers asilimia 99 ni utapeli
Kuna diwani wangu wa ccm yule ni jambazi kabisa, yeye aliwahi kuwa na wafadhili wazungu zaidi ya 100 walimkimbia, anapewa pesa anakula tu.

Akiletewa chakula cha watoto, usiku anawapelekea watu wa maduka kuwauzia.
 
Kuna diwani wangu wa ccm yule ni jambazi kabisa, yeye aliwahi kuwa na wafadhili wazungu zaidi ya 100 walimkimbia, anapewa pesa anakula tu.

Akiletewa chakula cha watoto, usiku anawapelekea watu wa maduka kuwauzia.
Huyo alikuwa mwizi kama wezi wengine, lakini najua kuna watu wanaofanya hizo huduma kwa uaminifu kabisa.

Na inasikitisha sana kwa jinsi Watanzania wengine wasivyokuwa na huruma kwa Watanzania wenzao.

Misaada ya watoto yatima wanaila.

Misaada inayotolewa kwa ajili ya wajane wanajimilikisha.

Misaada ya kuwasaidia maskini wanaitafuna.

Hivi watu wengine wameleogwa na nani?

Lakini, pamoja na kuwepo kwa watu wenye hizo tabia, na waaminifu pia wapo.
 
Huyo alikuwa mwizi kama wezi wengine, lakini najua kuna watu wanaofanya hizo huduma kwa uaminifu kabisa.

Na inasikitisha sana kwa jinsi Watanzania wengine wasivyokuwa na huruma kwa Watanzania wenzao.

Misaada ya watoto yatima wanaila.

Misaada inayotolewa kwa ajili ya wajane wanajimilikisha.

Misaada ya kuwasaidia maskini wanaitafuna.

Hivi watu wengine wameleogwa na nani?

Lakini, pamoja na kuwepo kwa watu wenye hizo tabia, na waaminifu pia wapo.
Mimi ninaishi maeneo ambayo wazungu wanazagaa mitaani kufadhili hivi vituo...mtaani tu vipo zaidi ya 7 jirani kabisa na ninapoishi, wote wezi tu mkuu

Hawana vyanzo vyovyote vya mapato lkn cha kwanza wakioewa misaada wananunua magari na usiku wanakesha clubs.

Niambie wanatoa wapi pesa?
 
Mimi ninaishi maeneo ambayo wazungu wanazagaa mitaani kufadhili hivi vituo...mtaani tu vipo zaidi ya 7 jirani kabisa na ninapoishi, wote wezi tu mkuu

Hawana vyanzo vyovyote vya mapato lkn cha kwanza wakioewa misaada wananunua magari na usiku wanakesha clubs.

Niambie wanatoa wapi pesa?
Mkuu, labda ungefafanua kidogo. Wezi ni wepi hasa, hao wafadhili au wasimamizi wa kituo?

Vipi hali ya hao watoto, wana unafuu wowote tofauti na kabla ya kuketwa kwenye hicho kituo?

Kwa mtazamo wako, endapo hicho kituo kitafungwa, hao watoto wanaweza kupata hasara yoyote?

Samahani kwa kuuliza maswali mengi 🙏
 
SEHEMU YA NNE: KAMA INGELIKUWA NI WEWE UNGEFANYEJE?
Huu ni ushuhuda unaoonesha umuhimu wa hivyo vituo, ambao watu wengine wanaweza wasiwe wanauona. Japo na mimi nilisimuliwa, naamini ni sahihi kwa sababu aliyenieleza si mtu mwenye tabia ya kusema uongo.

Mtu mmoja alianzisha kituo cha kulelea watoto wenye tatizo la akili.

Katika kujitahidi kuhakikisha kuwa kunakuwepo na chanzo cha uhakika cha fedha kwa ajili ya kukiendeshea kituo, alipambana hadi akapata gari aliamua kulitumia kama gari la abiria.

Kutokana na uchakavu wa hilo gari, ilikuwa ni kawaida kukamtwa mara kwa mara na kupigwa faini. Kujitetea kwake, kuwa anatafuta hela ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum anaowalea hakukusaidia.

Siku moja, baada ya kuandikiwa faini, aliamua kuwa siku hiyo liwalo na liwe. Kwa hasiria, alirejea kituoni kwake na hilo gari na kuwapakiza watoto kwenye hilo gari na kwenda kulipaki kwenye ofisi ya RPC. Aliwaacha watoto pamoja na hilo gari, kwamba Serikali na yenyewe iwalee, na kwamba kawapatia na kianzio, gari kuukuu.

Alikuwa yupo tayari kwa lolote, hata kufungwa, lakini ujumbe wake uzifikie mamlaka husika.

Inasemekana vitisho na ushawishi wa maofisa wa ngazi za chini haukumfanya abadilishe msimamo. Ni RPC pekee ndiye aliyekuja kifanikiwa kumshawishi kuwarejesha hao watoto kituoni, kwa ahadi ya kuishughulikia kero yake.

Hivi ingelikuwa ni wewe ndiye RPC, na jambo hilo likafanyika maeneo ya ofisi yako, ungefanyeje?

Vituo vya watoto vipo vingi. Kwa kuwa baadhi, na hata vingi, vimeharibu, visikufanye uamini kuwa vyote vipo hivyo. Hutakuwa umewatendea haki wale ambao wanajitahidi kufanya kazi nzuri ya kuwahudumia kwa upendo watoto wahitaji.
 
SEHEMU YA TANO: SHUHUDA ZA JINSI BAADHI YA VITUO VYA WATOTO VIMEWEZA KUWASAIDIA WALENGWA.
Hizi ni shuhuda nilizo na uhakika nazo, toka kituo ambacho nimeamua kukiita MAFANIKIO (siyo jina lake halisi). Nitatumia pia majina yasiyo halisi lakini ya watu halisi.

TAJIRI
Alifukuzwa na baba yake saa nane za Usiku, kufuatia ugomvi uliozuka baina ya mama yake na baba yake, babaye akituhumu kuwa TAJIRI si mwanawe. Fikiri mvulana mdogo kiasi hicho kufukuzwa Usiku wa maneno bila huruma.

Tajiri alitafuta pa kujibanza hadi Asubuhi, akaelekea mjini alikoenda kujiunga na "machokoraa" wengine. Akiwa huko, alijifunza tabia mablimbali zikiwemo za uvutaji bangi, uvutaji gundi, udokozi na hata ujambazi.

Kutokana na kuonekana mchangamfu na "mjanja", wakaka wakubwa waliamua kumuingiza kwenye kundi lao la ujambazi wa kutumia silaha. Kwa bahati yake nzuri, hakufanikiwa kushiriki kwenye tukio la ujambazi wa silaha za moto, kwani siku ambayo tukio lilikuwa likafanyike mahali, yeye alipendekezwa asiende siku hiyo. Ilikuwa kama vile ni Mungu Ndiyo aliyemwepusha na janga lilikokuwa mbele ya hilo kundi, kwani walipoenda kwenye tukio, walibainika na Polisi na kusababisha majibizano ya risasi na kupeleka majambazi(sikumbuki kama ni wote au baadhi) kuuwawa.

Tukio hilo lilimtafakarisha sana. Pamoja na kuwa alikuwa bado mvulana mdogo, alijua kuwa kama naye angeshiriki kwenye hilo tukio, huenda naye angepoteza maisha.

Aliendelea kukaa mitaani, mpaka siku moja mtu mmoja alipokutana naye, na baada ya kumhoji, aliamua kumsaidia kwa kumtafutia mahali atakakoweza kupata msaada wa kusomeshwa.

Hivyo ndivyo Tajiri alivyofika kituo cha kulelea watoto kiitwacho MAFANIKIO.

Hapo kituoni, maofisa husika walijitahidi kumpa ushauri nasaha hadi akafanikiwa kuacha bangi na madawa mengine ya kulevya, pamoja na kuwasamehe wazazi wake. Kituo pia kilifanikiwa kumkutanisha tena na "baba" yake, ingawa hakuwa tayari kumpokea kwake, lakini hilo halikuwa tatizo kwa kuwa MAFANIKIO palikuwa pakimfadhili kwa mahitaji yake yote, kuanzia chakula, malazi, malezi, Elimu, n.k.

Tajiri aliweza kusoma kuanzia shule ya Msingi hadi kidato cha Sita na hatimaye Elimu ya juu.

Kwa sasa Tajiri ni "bosi" katika taasisi fulani kubwa, na ni miongoni mwa watu ambao wakati mwingine wanapeleka misaada kwenye kituo cha MAFANIKIO.

Japo kwa sasa ana mafanikio mazuri na anaishi kwake na familia yake, bado anapachukulia MAFANIKIO kuwa ni nyumbani kwao.
 
SEHEMU UA SITA: SHUHUDA ZA JINSI BAADHI YA VITUO VYA WATOTO VIMEWEZA KUWASAIDIA WALENGWA

Wise na Smart
Hao niliowapa hayo majina, ni watoto wawili ndugu. Waliletwa katika kituo nilichokuwa nikifanyia kazi, ikiwa ni mimi ndiye niliyekuwa na jukumu la kuwapokea watoto wapya kituoni wakati huo

Ilikuwaje? Siku moja, mmoja wa vijana waliokuwa wakiasiaidwa na kituo chetu, yeye kipindi hicho akiwa Sekondari, alikutana na wavulana wawili wakiwa wanaokota makopo muda ambao walipaswa kuwa shuleni. Kijana wetu, acha nimwite Sanguine, alivutiwa kuwahoji na kujua sababu inayowafanya kuwepo mitaani muda wa masomo. Walimweleza kuwa hawasomi kwa sababu wao ndiyo wanaomsaidia baba yao, baada ya mama yao kutengana na baba yao na hatimaye kuolewa kwingineko. Baba yao alikuwa mgonjwa, kwa hiyo ilikuwa inawalazimu watafute chakula watakachokula na baba yao.

Huyo kijana, kwa kujua kuwa kuna watoto si wakweli, aliwashawishi wampeleke kwao, nao wakafanya hivyo.

Mazingira aliyoyaona na ya baba yao hao watoto, yalimwaminisha kuwa hao watoto ni wakweli, isipokuwa tu hawakuwa waeeleza changamoto zote wanazokutana nazo.

Mahali walipokuwa wakipaita nyumbani, kulikuwa hakuna tofauti kubwa sana na kulala nje.

Ilikuwa inawalazimu wakatafute vyuma chakavu na makopo, kisha huyauza na kununulia chakula cha kwenda kula na baba yao.

Wakati mwingine, walikuwa wanaenda majalalani kutafuta chochote watakachoona kitawafaa ama kutumia kama chakula au kukiuza wapate hela ya chakula.

Hali yao ilimkumbusha Sanguine jinsi alivyoanza kuishi mitaani baada ya ndoa ya wazazi wake kuvunjika, kabla ya kupata msaada uliomfikisha kituo cha kulelea watoto kiitwacho MAFANIKIO. Japo hakuwa na uhakika, alihisi kuwa kama uongozi wa kituo utapata taarifa za hao watoto, huenda wakakubalika kupokelewa. Alichukua jukumu la kuja nao kituoni.

Uamuzi wake ulitushangaza, lakini hatukuupuuzia. Tuliamua kumtuma mmoja wa staff kwenda kufanya uchunguzi kwenye familia husika. Matokeo aliyorudi nayo yalitusmshawishi kukubali kuwapokea kituoni, na kisha wakaanza kusoma kama watoto wengine. Walianzia chekechea, hatimaye, wakaendelea na darasa la kwanza, na sasa mmoja, yule mkubwa , yupo Sekondari.

Halafu sasa, darasni wapo vizuri sana.

Sawa, hao walikuwa na wazazi wao, lakini bado walikuwa wakikosa mahitaji ya msingi.

Ingelikuwa ni wewe ungefanyeje? Kituo kilikosea kuwapa hiyo fursa, kwa vile wazazi wao walikuwa hai lakini hawakuwa wakiwasaidia?
 
Back
Top Bottom