Kilimanjaro ilivyonusurika kuwa nchini Kenya.

idawa

JF-Expert Member
Jan 20, 2012
25,284
38,314
Kilimanjaro ilivyonusurika kuwa nchini Kenya, Mombasa kuangukia TanzaniaJUN 15, 2017by JOSEPH MIHANGWAin MAKALA

JE, umewahi kujiuliza swali hili: “Kwa nini mpaka [wote] kati ya Tanzania na Kenya, upande wa kaskazini mashariki, kuanzia Bahari ya Hindi kuelekea kaskazini magharibi hadi ncha ya Ziwa Victoria (Shirati), umenyooka mithili ya mstari uliochorwa kwa msaada wa penseli na rula kwa madhumuni maalumu?”

Tena, kwa nini mstari huo umenyooka hivyo kisha unapinda na kupaa kidogo kaskazini zaidi unapokaribia safu (range) ya Mlima Kilimanjaro kuingiza ndani ya Tanzania safu ya mlima huo, kabla ya kunyooka tena kuelekea kaskazini magharibi, bila hivyo mlima huo na Mikoa ya Kilimanjaro na Mara (Musoma) ingekuwa nchini Kenya? Nani alichora mpaka huo na kwa madhumuni gani hata kunusuru kwa ajili ya Tanzania, zawadi ya mlima huo? Fuatana nami katika makala haya kuweza kupata majibu sahihi.

Miaka ya 1800 inafahamika kama kipindi cha ubeberu wa mataifa ya Ulaya kugombania maeneo, kuvamia na kuchora mipaka barani Afrika (Scramble and Partition of Africa) kwa maslahi ya kibiashara na kiuchumi ya mataifa hayo. Hatua hii ni matokeo ya taarifa za kijasusi za “Wavumbuzi” waliotumwa na mataifa hayo kabla ya hapo, kwenda ndani ya Afrika kuonauwezekano wa kupora kilichokuwa cha manufaa kwao.

Kwa Pwani ya Afrika Magharibi na Misri; Ufaransa na Uingereza ziliumana kugombea haki ya ukuu wa maeneo. Naye Mfalme Leopold waII wa Ubelgiji, yeye alijimilikishaeneo la Kongo kamanchi yake binafsi (The Congo Free State) bila kuwa sehemu ya Ufalme wa Ubelgiji hadi mwaka 1908. Kufikia mwaka 1880, Ujerumani ambayo mwanzoni haikuwa nakiu ya makoloni, nayo ilianza kujitutumua kuwa moja ya mataifa hayo.

Kwa Afrika Mashariki, mwaka 1884, Mfalme wa Ujerumani alitambua na kuridhia kazi ya kijasusi iliyofanywa na watu wake (kwa kificho cha Umisionari), na kufuatiwa na utiaji saini mikataba ya kilaghai na watawala wa jadi wa Uzigua, Ukaguru na Usagara, wakatoa ardhi yenye eneo la ukubwa wa kilometa140,000za mraba kwa Kampuni la biashara la Kijerumani – “The German East African Company” [GEAC] kuendeshea shughuli zake.

Kwa hofu ya kuvurugwa na mataifa mengine na “maasi” ya wenyeji pia, Februari 1885, GEAC iliomba na kupatiwa Hati ya Ulinzi [Imperial Letter of Protection] na dola ya Ujerumani kwenye maeneo hayo na mengine; na kuanzia hapo eneo la nchi yetu likafahamika kama Afrika Mashariki ya Kidachi [Deusch Ostafrika], wakati eneo la Kenya likijulikana kama Afrika Mashariki ya Waingereza [British East Africa].

Lakini biashara kwa GEAC bila bandari kupitishia bidhaa na mali ingekuwa kazi bure.Kwa hiyo, GEAC ilitaka kupata bandari pwani kwa udi na uvumba bila kutozwa kodi. Wakati huo, Pwani yote ya Bahari ya Hindi, kutoka Somalia upande wa Kaskazini hadi Rasi ya Delgado [Msumbiji] upande wa Kusini pamoja na eneo lote la bara [mrima] ilimopitakimisafara [Caravans] ya biashara hadi Maziwa Makuu, lilikuwa chini ya himaya ya Sultani wa Zanzibar.Ndoto hiyo ya GEAC ya kujipatia bandari Pwani ya bahari ya Hindi ilikuwa tusi kwa Sultani yenye kuweza kuzua mtafaruku na Sultani huyo ambaye tayari alikuwa amechukizwa na mikataba ya “majasusi” wa Kijerumani na watawala wa jadi.

Sultani alipogomea matakwa ya GEAC, merikebu za kivita za Mjerumani zilitia nanga hima kwenye bandari ya Zanzibar,na kuelekeza mitutu ya mizinga kwenye Kasri lake; naye akanywea. Kuanzia hapo, ikaundwa Tume ya ukomo wa mipaka [Delimitation Commission] yenye Wajumbe kutoka mataifa mawili – Ujerumani na Uingereza, kwa lengo la kuangalia upya mipaka na haki za Sultani. Mipaka iliyokusudiwa kwa suluhisho ili kuepuka “vita” kutokea ni ile ya Afrika Mashariki ya Wadachi; Afrika Mashariki ya Waingereza na ile ya himaya ya Sultani wa Zanzibar.

Sultani [Barghash bin Said] alifadhaika kwa kuhisi matata kwamba huenda angepokonywa maeneo hayo na ya Kilimanjaro na Uchagani ambako hata hivyo alikuwa na ushawishi mdogo sana. Na ili kupata ushahidi wa uhalali wa kudhibiti maeneo hayo tarehe 30 Mei 1885, alituma kikosi cha Askari 200 kwenda Uchagani chini ya Kamanda wa Kiingereza, Jenerali Mathews, kushinikiza Machifu wa eneo hilo kutia sahihi Mkataba [treaty] kutambua himaya ya Sultani katika “nchi” zao kwa kiapo kisemacho: “….Sisi Masultani [Machifu] wa Uchagga na Kilimanjaro tunatambua na kukiri kwamba tu raia wa Mtukufu Sultani wa Zanzibar, na kwamba tunapeperusha bendera yake katika nchi yetu kuthibitisha utiifu kwake….”.

Machifu 25 waliotia sahihi kiapo hicho ni pamoja na Chifu Mandara wa Moshi; Kitungeti wa Kiruwa; Marealle wa Marangu; Mitanuvi wa Mamba, Fumba wa Kilema na Machifu wa Machame, Rombo, Taveta na wengine.

Wakati kikosi cha Sultani kikirejea Zanzibar, kilikumbana uso kwa uso na kikosi cha Wajerumani karibu na Taveta, wakiwepo pia wafanyabiashara wa Kiingereza; vita ikazuka kidogo kabla ya amri kutoka juu [Ujerumani] kusitisha mapigano kutolewa.

Haya yakitokea, wiki mbili baadaye, Chifu Mandara aliruka kihunzi kwa kubadili nia na kuingia Mkataba mwingine wa ulinzi [kulindwa] na Kampuni la Kijerumani – GEAC kwa kutoa “haki zote kwa Kampuni hilo za kutumia ardhi na kutoza kodi na ushuru; kuanzisha utawala wa Kijerumani na mfumo wa Kimahakama; kuvuna Mlima Kilimanjaro, mito, maziwa na misitu”. Mandara akahakikishiwa pia usalama na cheo chake pamoja na elimu ya kutosha kwa watoto wake.

Kuhusu utata wa kuingia Mkataba na Sultani wa Zanzibar, Chifu Mandara alidai kuwa yeye alikuwa Sultani huru kama alivyokuwa Sultani tu wa Zanzibar, na kwamba alitia sahihi makaratasi hayo na kupeperusha bendera ya sultani wa Zanzibar kuonesha tu kwamba alikuwa rafiki yake. Akawatuliza Wajerumani kwa kusema: “Nawapenda Wajerumani kuliko mataifa yote; zaidi kuliko hata Waingereza na ni kwenu tu ninyi Wajerumani nitatoa ardhi yangu”.

Kufikia hapo, mtanziko wa kimataifa kwa kusababishwa na Chifu Mandara, ulikuwa dhahiri juu ya umiliki wa eneo la Kilimanjaro kati ya Sultani wa Zanzibar, Wajerumani na Waingereza na ambao ulihitaji utatuzi makini kuepusha vita.

Kwa upande wao, Wajerumani hawakutaka kuingia mgogoro na wafanyabiashara wa Kiingereza kuhusu Kilimanjaro, wakawaza: “Kama tutaelewana na Uingereza ikawa upande wetu, madai ya Sultani yatakuwa mepesi”. Na ilipokuwa hivyo, Sultani hakushirikishwa katika tume ya kushughulikia mipaka; akajadiliwa bila kuwapo wala uwakilishi kwenye majadiliano ya Tume Mjini London, mwezi Agosti 1886.

Kwenye Tume, Ujerumani iliwasilisha hoja tano nzito kutetea maslahi yake na ya wafanyabiashara wake wa GEAC. Kwanza, kwamba ilihitaji kutumia bandari ya Dar es Salaam [iliyokuwa chini ya himaya ya Sultani] bila kutozwa kodi wala ushuru. Pili, ilitaka Sultani apunguziwe eneo la Pwani alilolimiliki kubakia upana wa maili kumi tu toka bahari. Tatu, kwamba Sultani apatiwe ulinzi na usalama wa Kijerumani kwa eneo la Witu, kaskazini mwa mji wa Mombasa.

Nne, kuhusu eneo la Mlima Kilimanjaro lililogombewa na pande zote tatu, Ujerumani ikaungana na GEAC kwamba eneo hilo lilikuwa muhimu kwake kuliko taifa lolote, ikizingatiwa pia kwamba wamisionari na wafanyabiashara wake walitia sahihi mikataba na machifu wa maeneo karibu na hilo [Usagara, Ukaguru na Uzigua], pia na Chifu Mandara wa Kilimanjaro mapema tangu 1884/85; na kwamba, mkataba kati ya sultani na machifu haukuwa na nguvu wala uhalali kisheria kwa sababu ulifikiwa kwa ujanja ujanja na vitisho vya kijeshi chini ya Jenerali Mathews.

Wakati huo, mwakilishi wa Uingereza, Sir Percy Anderson, alisikiliza kwa makini huku akitafuta suluhisho mbadala ili kutoiudhi Ujerumani. Kisha akaja na pendekezo: kwamba mlima Kilimamjaro ukatwe katikati ili nusu ya Kusini wapewe Wajerumani, na nusu ya pili ya Kaskazini, iende kwa Waingereza. Kutoka hapo Mmpaka unyoke moja kwa moja hadi Ziwa Victoria Nyanza, ncha ya “Speke Gulf” [sasa Kamanga Ferry]

Hoja hiyo ikapingwa na mwakilishi wa Ujerumani; kwamba ilikuwa vigumu kugawa hivyo eneo lenye milima kama hilo. Pili, kwamba Uingereza haikustahili ardhi hiyo kwasababu haikuwekeza kwa njia ya Mikataba isipokuwa eneo dogo tu kuzunguka Taveta. Percy Anderson akasalimu amri, lakini bila kukata tamaa.

Kisha Anderson akarukia suala la Bandari ya Mombasa, mali ya Sultani iliyokuwa ikiwaniwa na wote – Waingereza na Wajerumani; akasema, Waingereza waliitaka kwa matumizi ya ghala kuu, karakana na kituo cha Jeshi la wanamaji na kuongeza kwamba, nchi yake haikuwa tayari kuachia Mombasa,ima faima, miji yake midogo midogo na miundombinu ya kibiashara, Vituo vya Wamisionari na kambi ya Askari “kurutsa”, kuwa mikononi mwa Taifa lolote shindani.Pili, Uingereza ilitaka kuwa na barabara yake huru kutoka Mombasa hadi Ziwa Victoria “kule mto Nile unakoanzia na ambako njia ya kuifikia Sudani ya Chini ungeweza kupatikana”.

Kufikia hapo, mtanziko mwingine kati ya mataifa haya mawili yenye nguvu sawa ulikuwa dhahiri. Hapa kulikuwa na Ujerumani ikitaka kumiliki eneo lote la Kilimanjaro na bandari ya Mombasa kwa pamoja kama bandari karibu na eneo la Kilimanjaro. Kwa upande wa pili kulikuwa na Uingereza iliyotaka kumiliki Mombasa ambako nayo ilidai kuwekeza mengi kama tulivyoona hapo juu.Lakini pia kulikuwa na sultani aliyedai kumiliki maeneo yote hayo japo alitupwa nje ya mazungumzo kusubiri tu hatima ya maridhiano ya “wakubwa” hao wawili. Suala lilikuwa ni nani apate vyote alivyotaka na nani apoteze kipi? Hapo, kwa Kiswahili cha mitaani, “ngoma ikawa droo”.

Anderson akakubali kuachia Mlima Kilimanjaro ili abakie na Mombasa. Akapendekeza Mmpaka upya kwa kuchora mstari ulionyooka kuanzia Pwani Kusini mwa Mombasa kuelekea kaskazini magharibi kupitia Taveta hadi Himo na kupinda juu kaskazini kukwepa Mlima Kilimanjaro [uwe ndani ya Tanganyika] na kunyooka tena kaskazini magharibi hadi ncha ya mashariki ya Ziwa Victoria Nyanza eneo la Ghuba ya Speke [Speke Gulf] ilipo Kamanga Ferry kwa kutupa nje kuwa ndani ya Kenya, sehemu ya kaskazini ya Mkoa wa sasa wa Arusha na Mkoa wote wa Mara.

Bado pendekezo hili halikumridhisha mwakilishi wa Wajerumani aliyetaka Bandari ya Mombasa kwa udi na uvumba, huku akiwa makini pia kutoitibua Uingereza kwa ubishi. Hata hivyo, lakini mwakilishi huyo alilegea tu baada ya kubaini kwamba Uingereza haikuwa tayari kwa mazungumzo zaidi kuhusu Mombasa. Akakubali kuachia hoja hiyo kwa sharti kwamba Sultani wa Zanzibar adhibitiwe kwa kupunguziwa eneo la Pwani kubakia upana wa kilomita kumi tu na aruhusu Ujerumani kutumia bandari ya Dar es Salaam bila masharti.

Pili, kwamba pendekezo la Mmpaka la Uingereza kutoka Pwani ya Bahari ya Hindi hadi Speke Gulf lirekebishwe, badala yake uanzie Pwani Kusini mwa Mombasa kwenda Kaskazini Magharibi kupita Taveta, na kupinda juu Mashariki unapofika Himo kunusuru safu ya kaskazini ya Mlima Kilimanjaro [iwe Tanganyika] kabla ya kunyooka tena kaskazini magharibi hadi ncha ya Mashariki ya Ziwa Victoria Nyanza, juu kidogo ya mji wa Shirati, kabla ya kukata kona kali magharibi na kupasua Ziwa katikati hadi Ziwa Magharibi. Lengo la Ujerumani la kupendekeza hivyo lilikuwa ni “fidia” kwa kupoteza Mombasa ilikujipatia ardhi ya Mikoa ya sasa ya Arusha, Mara na nusu ya Ziwa Victoria.

Makubaliano ya mpaka wa Tanzania na Kenya ambayo Ujerumani na Uingereza ziliridhia na kubadilishana Hati, Novemba 1, 1886 sasa yalisomeka hivi: “Mstari wa Mmpaka unaanzia kwenye mdomo wa Mto Wanga au Umbe; unapanda juu moja kwa moja hadi Ziwa Jipe, unapita upande wa mashariki kuzunguka upande wa kaskazini wa Ziwa na kuvuka Mto Lumi; kisha unapita katikati ya ardhi ya Taveta na Uchagga; unaruka kitako cha kaskazini cha safu ya Mlima Kilimanjaro na kutoka hapo unanyooka hadi kituo upande wa mashariki wa Ziwa Victoria Nyanza unaokatishwa na nyuzi ya kwanza ya mstari wa “latitudo” Kusini.

Kwa makubaliano hayo pia, himaya ya Sultani Pwani ya Bahari ya Hindi na Mrima [Bara], ilipunguzwa na kudhibitiwa kubakia upana wa maili 10 tu,eneo ambalo hata hivyo, mwaka 1888 alilazimika kulisalimisha kwa Wajerumani kwa mtutu wa mizinga ya Manowari.Oktoba 6, 1889, bendera ya Ujerumani ilisimikwa na kupepea kileleni mwa Mlima Kilimanjaro na Mjerumani Hans Meyer, akiwa mzungu wa kwanza kufika kileleni mwa mlima huo. Na ni hapo hapo Desemba 9, 1961, bendera ya Tanzania huru iliposimikwa na kupepea kuanzia siku hiyo.

Kama pendekezo la Uingereza juu ya mpaka lingepita, Mwalimu Nyerere angezaliwa Kenya badala ya Tanganyika.Ingetokea kuwa hivyo, ni nani angekuwa Baba wa Taifa letu?
 
Ingekuwaje kama Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na Msoma ingekuwa Kenya halafu Mombasa iwe Tanzania.?
 
Mkuu asante sana kwa madini adhimu sana kama haya.Nimejifunza mengi sana hapa.Asante
 
Ingekuwaje kama Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na Msoma ingekuwa Kenya halafu Mombasa iwe Tanzania.?
Tungekua tumepata hasara, sasa tuna bandari, part of lake Victoria, Kilimanjaro na hiyo mikoa.. Oh bila kumsahau Baba wa Taifa Nyerere
 
Ata tupewe Congo DRC yote ile na rasilimali zao bado sana .....
Mnafikiri ni mjinga yule aliyesema ELIMU ELIMU ELIMU .......
 
Mada nzuri, kwa mtizamo wangu Tanzania ingekua ipo juu sana.. Bandari zake zingetegemewa na nchi zote za ukanda huu. Ila Hapo kwa wachaga kua Kenya sijui
 
Back
Top Bottom