"Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya."