KIFO CHA HAWARA (mkono wa jini)
SEHEMU YA THELATHINI NA SITA
MTUNZI:
Mbogo EDGAR
ILIPOISHIA SEHEMU YA THELATHINI NA TANO: “vipi umesha toka nje, mimi natembea kwa miguu nakuja kwenu” nilimueleza Jessenia kwa sauti kavu isiyo ya kimapenzi wala kubembeleza” “nimetoka kwaajili yako, lakini natafuta matatizo kwa mjomba, maana nimetoka bila taarifa, nipo njia ya kueleka njia panda, ila ungeniambia kwanza kuna nini” alisema Jessenia kwa sauti ya kubembeleza, “mimi natokea huku sheri, chake chake, ni vyema kama ungekuja upande huu” nilimueleza Jessenia kwa sauti ile ile, na yeye akakubaliana na mimi……ENDELEA…..
Dakika kumi baadae tayari nilikuwa nimesha kutana na Jessenia, ambae ilibakia kidogo anisahaulishe lengo la safari yangu ya usiku ule, kwa jinsi alivyoonekana, licha ya kuwa alikuwa amevaa kandambili na kichwani akiwa amejitanda mtandio mwepesi kufunika nywele zake, lakini pia alikuwa amevalia gauni jepesi la kulalia, ambalo kiukweli lilionyesha vyema jinsi alivyo umbika, nilimtazama kwa mshaka maana jini ukisha muonyesha kuwa umemtambua huwa hakuachi salama hata kidogo, “Jesse pole kwa kutumia muda wako usiku huu, lakini nadhani unafahamu kilichonileta, naomba unieleze kila kitu kuhusu wewe na kwanini wanaume wawili uliokuwa nao walipoteza Maisha?” nilimuuliza Jessenia kwa sauti ambayo usingesema kuwa leo hii tumetoka kupeana utamu, “Eric nadhani nilikuomba uniahidi kuwa hutoniacha kwa kile nitakacho kuambia, na wewe ukakubali sivyo?” aliuliza Jessenia kwa sauti tulivu, “nakumbuka Jesse, lakini endapo utaniambia kila kitu bila kunificha” nilijibu Jessenia safari hii nikiifanya sauti yangu kuwa tulivu, “Eric nadhani nilikuambia kuwa wewe ndie mwanaume pekee ambae umenifanya niwe na furaha ya ukweli, na sasa inabidi utambue kuwa hiki ninacho kuambia hakuna mtu anaefahamu zaidi ya mimi mwenyewe, mjomba na shangazi na mwingine ni babu Mangeu mwenye kunisababishia” ndivyo alivyoongea Jessenia, wakati huo tulikuwa tume simama mita chache toka nyumbani kwao lakini upande wa mjini, sio kule nyumbani kwa Mangeu, “nashukuru umenipa ujasiri wa kukueleza hili, pengine naweza kupata msaada wako wa kuepukana na jini hili, maana umeonyesha dalili njema ulipokuwa mwanaume wa kwanza kwangu” alisema Jessenia, kwa sauti tulivu yenye masikitiko kidogo, hapo nikatega sikio ilikuweza kusikiliza simulizi ya Jessenia.*******
Ilikuwa hivi, Jesseni ambae alikulia katika familia ya kitajiri ya bwana Juma Mohamed Amour, ambae ni mjomba wake, ambayo ilikuwa na mtoto mmoja wakiume ambae ni Ussi, aliishi Maisha mazuri yenye upendo mkubwa kwake, alipewa kila kitu na kununuliwa kila alichohitaji, wakati mwingine ilikuwa zaidi ya binamu yake Ussi, ambae hakupata kitu chochote mpaka yeye alipopata kwanza, hata kwenye swala la kukosea na kuadhibiwa sio kwamba alikuwa mkosaji kama Ussi ambae alikuwa mtukutu sana hasa walipofikia kidato cha kwanza, lakini pia hata yeye alipo kosea hakuadhibiwa kwa bakora au kunyukuliwa (kufinywa) kama ilivyokuwa kwa Ussi, ambae alipewa kipigo kitakatifu toka kwa baba yake, swala ambalo kuna wakti lilizuwa ugomvi kati ya mjomba na shangazi yake Jessenia, lakini kupendwa huko hakukumfanya mschana huyo kuwa na kiburi wala tabia mbaya, alizidi kuwa mcha mungu na mwenye maadili mema katika jamii.
Kuna wakati Jessenia akaanza kuhoji kuhusu wazazi wake halisi, ni kutokana na watu kuanza kuhoji juu ya uhalisia wake, maana hakukuwa na siri kuwa yeye ni chotara wa kiarabu, hasa kutokana na muonekano wake, kitu ambacho kilifanya wanafunzi wenzake na majirani zake yani Watoto wenzie kuanza kuhoji juu ya wazazi wake, na ndipo yeye alipo anza kuhoji juu ya hilo, ambalo lilipingwa vikali sana na mjomba wake pamoja na shangazi yake, ambao walimsisitiza aache kuulizia habari hizo, lakini haikumfanya Jessenia kuacha kuhoji juu ya swala hilo, mpaka siku moja mjomba wake alipo mueleza kuwa mama yake alishafariki na baba yake hakuna alie kuwa anamfahamu.
Kibao kiligeuka wakiwa kidato cha pili mwishoni, wakati ambao Jessenia alikuwa amesha vunja ungo, kipindi ambacho Ussi nae alikuwa amesha barehe, ni wakati ambao Ussi alianza kudekezwa sana akipewa kila alichohitaji, ikiwa ni pamoja na kuachiwa gari kufanya kila anachotaka, hakuna aliemuuliza kuhusu tabia yake mpya ya kuanza kunywa pombe na kuvuta sigara akiwa kidato cha tatu, na hata aliposema kuwa anaacha shule na kutaka kufanya biashara, hakuna aliejaribu kumzuia, zaidi mzee Juma Mohamed alimpatia kiasi fulani cha fedha ambazo alinunua mashine tatu za boti ya uvuvi na yeye Ussi kuanza kufanya biashara ya uvuvi, akiwa ameajiri vijana sita, ambao wange simamia vyombo hivyo vitatu ya uvuvi.
Tofauti ikiwa kwake ambae sasa alianza kuchungwa kweli kweli, akiwekewa ulinzi mkali sana kila anakoelekea pasipo yeye mwenyewe kujuwa, na kila alipoonekana akiongea na mwanaume au kuzoweana nae, pasipo kujuwa zimefikaje habari, angekalishwa kitako na shangazi au mjomba na kuanza kusema vibaya sana huku akitishiwa kufukuzwa nyumbani endapo angerudia tena, na sio hivyo tu, hata Ussi hakuwa mbali na hilo, na yeye ndio ilikuwa balaa zaidi, maana yeye alikuwa anamaliza hapo kwa hapo endapo akimkuta kijana yoyote amesimama na binamu yake, basi angepigana sana na huyo kijana, ilifikia wakati akawa anawatumia wale vijana wake wavuvi kuwavizia wote wanao mvizia binamu yake na kuwashambulia vikali, mara kadhaa alishafikishwa kituo cha madungu, kwa kesi za kushambulia na baba yake kwenda kumtoa, wivu wa Ussi uliwashangaza sana watu, maana yeye hakujali alichokuwa anakifanya yeye kwa wadada wa wenzake, ila alimchunga dada sana dada yake, kitu ambacho hakuthubutu ni kumshambulia dada yake huyo, aliishia kumsema na kumsimanga, lakini licha ya yote hakupunguziwa mahitajio yake, ambapo sasa alikuwa anapewa fedha kwaajili ya kununua kile alichotaka, ikiwa ni pamoja vile ambavyo yeye alivipa kipaumbele, yani mavazi mazuri vito vya thamani na manukato.
Kuna wakati Jessenia alipokuwa na miaka kumi saba, akiwa kidato cha tatu, siku moja alijitokeza kijana mmoja mtoto wa mzee Nasoro, baba yake alikuwa anawadhifa fulani pale chake chake, (siwezi kuutaja) alikuwa kijana ambae alitokea katika Maisha ya kitajiri, mwanafunzi ambae waschana wengi walikuwa wanampenda na kumuhitaji kuwa nae, sijui wao walikuwa wanafanyaje mambo yao, maana unaweza kushangaa kuwa moja mambo ambayo yalizingatiwa katika jamii hii ni mschana kuolewa akiwa na uschana wake.
Ukweli kijana Ali Nasoro, alimfikia Jessenia ambae ndie alikuwa mschana mzuri kuliko waschana wote pale shuleni Madungu, ambae alitamaniwa na wanafunzi wote na wanafunzi wenzie, ilikuwa kazi ngumu kidogo kwa Ali kukubaliwa kuwa mpenzi wa Jessenia, naweza kusema hata jibu lake hakuwahi kulipata, ilikuwa hivi, siku ambayo Ali alipewa ahadi ya kupewa jibu, ilikuwa ni juma tano mida ya saa tisa jioni, mida ambayo walitakiwa kuelekea majumbani mwao, ndio siku ambayo Alli na mwenzeia Saidi walisindikizana kwenye miadi, ambayo ilikuwa ifanyike kabla ya wao kwenda majumbani mwao, sehemu ya ahadi ilikuwa ni nyuma ya majengo ya shule, ambako kiulikuwa na kichaka hafifu na wao waliwahi sehemu ya tukio mapema sana, ikiwa ni dakika kama kumi na tano kabla ya muda uliopangwa, lakini Jessenia alipofika eneo la tukio alichokiona alikishangaa sana, hakuamini macho yake, maana aliwakuta vijana wale wote wawili wakiwa wamelala chini wamekauka vibaya sana huku wamekuwa weusi kama mikaa au wameungua na moto, yeye akatimua mbio pasipo kumuleza mtu yoyote zaidi ya mjomba wake, ambae alibashiri kilicho tokea, “lazima mulikuwa muna taka kufanya uzinifu sivyo” ukweli Jessenia hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali, maana ukichukulia kwamba hakujuwa siri imefikaje kwa mjomba wake ambae, alimsisitiza kuwa asimueleze mtu yoyote juu ya tukio lile, na pia hakutakiwa kufanya jambo kama hilo na mtu yeyote, maana alikuwa ana jini baya sana ambalo alimruhusu kufanya uchafu kama huo, mwanzo shariti lile halikuwa gumu sana kwa Jessenia, japo alipata wakati mgumu sana kila alipokumbuka vifo vya Alli na mwenzie Saidi, lakini alijitahidi kukaa na siri ile pasipo kuitoa kwa mtu yoyote, huku akikaa mbali na wavulana, kuwaepusha wasije kupatwa na kifo cha jini.
Siku zilienda, Jesseni akishuhudia wenzie wakijipatia wanaume na kufurahi nao, japo haikuwa sawa kwa waschana asieolewa kuwa na mwanaume, yeye alipambana na hali yake mpaka kipindi ambacho alikuwa amemaliza Kidato cha nne, kipindi ambacho alianza kufikiria kuwa na familia yake ili aweze kujipatia Watoto, ambao, wangeweza kumliwaza na kumuondolea upweke wakukosa baba na mama.
Naam, ilikuwa siku ya Idd ya mfungo moss, siku ambayo Jessenia hatoisahau katika Maisha yake, ni siku ambayo Jessenia alitoka nyumbani kwao pamoja na binamu yake Ussi, kwenda matembezi kama ilivyo kawaida kwa siku za sikukuu, kwa watu kujikusanya kwenye viwanja vya siku kuu, yaani Tibirinzi, ambako wakazi wa chake chake, napengine toka wete na mkoani, huwa wanakusanyika na kuja kusherehekea hapa, ambapo pana kuwa na michezo na burudani ambali mbali, ndiko Jessenia alikokutana na Hamduni, ambae ni kijana aliemuacha Jessenia shuleni pale madungu, Hamduni akimaliza shule na kumuacha Jessenia kidato cha kwanza, walijikuta wakianza urafiki wa ghafla siku ile, japo hapo zamani hawakuwahi kuwa karibu, na kitu ambacho leo kilimfanya Jessenia aamini kuwa sasa ni mkubwa ni baada ya kuona binamu yake Ussi akiwa anaendelea na mambo yake bila kujari ukaribu wake na Hamduni, ambae katika maongezi yao walikubaliana kuwa wapenzi.
Makubaliano yao yalikuwa kama sumu kwao, maana kuna wakati Hamaduni alienda chooni, ambako hakurudi tena, na baada ya muda mfupi watu wakaanza kukimbizana, huku na huko hofu zimewajaa, kelele nyingi zikisikika, kuwa kuna mtu kafa kuna mtu kafia chooni, na baada ya polisi kufika ndipo Jessenia alipobaini kuwa alie uwawa ni Hamduni, na kifo chake kina fanana na vifo vya kina Alli na Saidi,
Ukweli mpaka hapo Jessenia alitambua kuwa lile Jini bado lilikuwa lina muandama, Jessenia aliogopa sana na kuingiwa na simanzi, maana aliona kuwa Maisha yake yanaelekea kuwa magumu ya upweke, kwasababu aliona wazi uwezekano wa yeye kuto kuolewa wala kupata mwanaume yoyote wa kumpatia mimba angalau apate mtoto wa kumliwaza.
Jessenia alirudi nyumbani, moja kwa moja akaongea na shangazi yake, akimtaka kumsaidia kupata ufumbuzi juu ya jambo hili, ikiwa ni kwenda kusomewa kisomo ambacho kita muondoa jini linalomsumbua, na yeye aweze ukuishi Maisha ya kawaida na hapo ndipo mjomba wake alipompeleka kwa shekhe mmoja wa msikiti wa Mchanga Ujuma, na kumfanyia kisomo kikubwa sana kisomo ambacho kilifanywa kwa siku tatu, kisomo ambacho kilimfanya Jessenia aamini kuwa sasa amesha ondokana na lile Jini, lakini ukweli alikuwa anajidanganya, maana tatizo lilikuwa pale pale, na sasa ikafikia wakati Jessenia alianza kumtilia mashaka babu Mangeu, ambae ni jirani yao pale msingini…….. Itaendelea