Ballali alikiona kifo
na Kulwa Karedia na Salehe Mohamed
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MAELEKEZO ya kuzikwa Washington nchini Marekani kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), yalitolewa na yeye mwenyewe, siku kadhaa kabla hajafikwa na mauti, Ijumaa ya wiki iliyopita.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka kwa ndugu wa karibu wa Ballali aliyeko katika msiba huo Washington, zinaeleza kuwa, gavana huyo wa zamani wa BoT alifikia uamuzi wakati hali yake kiafya ilipokuwa ikizorota kutokana na kuumwa.
Mmoja wa wanafamilia ya Ballali aliyezungumza na Tanzania Daima jana, kutoka Washington, Marekani uliko msiba huo, alisema Ballali alitangaza uamuzi huo mbele ya jamaa zake, akiwamo mkewe Anna Muganda.
Kwa mujibu wa mwanafamilia huyo ambaye juzi alikuwa mmoja wa watu walioithibitishia Tanzania Daima kuhusu kifo hicho cha Ballali, hata kusababisha kuwa chombo pekee cha habari kilichoandika taarifa hizo jana, Ballali alifikia uamuzi huo kutokana na kufadhaishwa na namna jina lake lilivyokuwa likihusishwa na tuhuma nzito za ufisadi.
Yeye mwenyewe ndiye aliyeamua azikwe huku Washington. Siku zote amekuwa akitueleza namna alivyokuwa akifadhaishwa sana kutokana na kuchafuliwa kwa jina lake, hata baada ya kuitumikia nchi yake kwa juhudi kubwa, moyo mkunjufu na kwa uadilifu wa hali ya juu.
Alitueleza hapa kwamba hajapata kuiibia nchi yake hata senti moja. Hapo ndipo aliposema akifa angetaka azikwe huku huku Washington na si nyumbani, ambako alihusishwa na kila aina ya tuhuma, alisema mwanafamilia huyo ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini, akisema yeye hakuwa msemaji.
Mwanafamilia huyo alisema kwamba, katika mazishi yake, Ballali atazikwa bila ya kuwapo mama yake mzazi, aliyepo hapa nchini, ingawa atasindikizwa na dada zake wawili ambao walikwenda kumjulia hali huko Washington hivi karibuni.
Inavyoonekana mama yake hataweza kuwahi mazishi. Hata hivyo dada zake wawili, Elizabeth na Margaret, wote tunao hapa msibani na hao ndio watakaoiwakilisha familia yake katika mazishi, alisema mtoa habari wetu huyo.
Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka kwa jamaa wa Ballali walio Dar es Salaam zinaeleza kuwa, ingawa dada zake hao wawili walikwenda kumjulia hali kaka yao, waliwasili Washington, Marekani wakiwa wamechelewa na kumkuta ameshafariki dunia.
Mtoa habari wetu kutoka Washington aliieleza Tanzania Daima kwamba, ndugu hao wawili wa Ballali walikuwa wakitarajia kurejea nchini wakati wowote kuanzia Jumatatu ijayo.
Pengine msiniulize mimi hapa maswali mengi. Mpango uliopo hapa ni kwamba hawa dada zake wawili, Eliza na Maggy, wanatarajia kuitisha mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam na kutoa taarifa kamili kuhusu kifo cha kaka yao, alisema ndugu huyo wa Ballali.
Alisema alikuwa na imani kwamba, katika mkutano wao huo na waandishi wa habari, unaotarajiwa kufanyika wakati wowote wiki ijayo, maswali yote kuhusu nini hasa kilimpata Ballali hata kufikwa na mauti hayo kitawekwa hadharani.
Habari nyingine kutoka Boston na Washington zinaeleza kwamba, kulikuwa na taarifa zilizokuwa zikisema kwamba, Ballali alikuwa akisumbuliwa na aina moja ya saratani kwa muda mrefu sasa.
Hata hivyo wakati kukiwa na taarifa hizo, baadhi ya ndugu, marafiki na jamaa zake wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kwamba, Ballali alilishwa aina fulani ya sumu isiyojulikana, siku kadhaa kabla hajakimbizwa Marekani kwa matibabu.
Taarifa hizi za kulishwa sumu zimekuwa zikienea kwa haraka katika maeneo tofauti, mbali ya Tanzania Daima pekee kuligusia jambo hilo jana, likimkariri ndugu mmoja wa Ballali aliyekiri kuwapo kwa wasiwasi huo miongoni mwa wanafamilia.
Jamaa mwingine wa Ballali aliyeko huko huko Washington Marekani, aliieleza Tanzania Daima kwamba, familia ilikuwa ikijiandaa kuwasiliana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani ili kesho aweze kuhudhuria misa maalumu ya kumuombea marehemu itakayofanyika kabla ya mazishi yake yanayopangwa kufanyika kesho hiyo hiyo.
Ndugu huyo wa Ballali alisema, walikuwa na imani kuwa serikali ilikuwa na taarifa kamili, baada ya wao kuwasilisha Ofisi ya Rais Ikulu na baadaye kwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, juzi hiyo jioni.
Wakati Ballali akitarajiwa kuzikwa kesho, uongozi wa BoT jana alasiri ulitoa taarifa rasmi ya kukiri kupokea taarifa hizo za kifo cha Ballali na kusema unaungana na familia yake katika kipindi hiki kigumu.
Akitoa taarifa hiyo ya maandishi kwa waandishi wa habari jana, Ofisa Mwandamizi wa Kitengo cha Habari cha BoT, Emmanuel Mwero, alisema ofisi ya Gavana (Ndulu) ilipokea habari hizo kwa masikitiko makubwa.
Ofisi ya Gavana imepokea habari za kusikitisha jana usiku (Jumanne) kuwa gavana wa zamani wa BoT, Daudi Ballali, amefarikia Ijumaa Mei 16, mwaka 2008 huko Boston, Marekani, ilisema taarifa hiyo wakati ukweli ni kwamba Ballali alikuwa amefia Washington.
Katika taarifa hiyo, Ballali anaelezwa kuwa alijiunga na BoT kama gavana Julai 14, 1998, nafasi aliyodumu nayo hadi Januari 8 mwaka huu, uteuzi wake ulipotenguliwa na Rais Kikwete, baada ya kupokea taarifa za ukaguzi wa EPA, uliofanywa na Kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya Enrst & Young.
Hata hivyo, si BoT wala serikali, ambayo ilikuwa mwajiri wa Ballali, iliyotoa taarifa ya ufafanuzi kuhusiana na mazishi ya Ballali, ambaye ni mmoja wa watu waliopata kushika nafasi nyeti za uongozi nchini.
Ndugu waandishi habari hii imejitosheleza, hivyo tunawaomba mkaitumie na kama kutakuwa na jambo lolote, Gavana Beno Ndullu atawaita, alisema Mwero.
Taarifa kutoka ndani ya benki hiyo zinasema kuwa, jana asubuhi wafanyakazi wote walisambaziwa kupitia anuani zao za e-maili, wakijulishwa kuhusu msiba huo.
Tanzania Daima ilipofika katika nyumba aliyokuwa akiishi wakati akiwa gavana, iliyoko Masaki Plot 387, jijini Dar es Salaam, hali ilikuwa ya utulivu, ingawa walikutwa walinzi wa Kampuni ya Ultimate Security.
Ni kweli hapa ni nyumbani kwa Gavana, lakini tangu Ballali alipoondolewa, nyumba imebaki wazi, tupo sisi na mfanyakazi wa ndani tu, alisema mmoja wa walinzi hao.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, jijini Dar es Salaam, Salvatory Rweyemamu, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo za msiba alisema yeye hakuwa msemaji na akamwita Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Kassim Mpenda aliyekuwapo hapo.
Mpenda kwa upande wake alisema serikali imepanga utaratibu juu ya taarifa hizo na kwamba msemaji mkuu ni Gavana wa BoT, Ndullu.
Ni kweli hata miye nimesikia kwamba Ballali amefariki dunia, sasa mimi siyo msemaji, kumbukeni serikali inafanya kazi kwa utaratibu, hivyo imemteua Dk. Ndullu kuwa msemaji mkuu wa suala hili, nawaomba mtafuteni, alisema Mpenda.
Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Ballali aliwahi kuwa mchumi wa BoT mwaka 1967-1976, kabla ya kufanya kazi katika Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Ndugu wa karibu wa Ballali alisema wanatarajia kufanya misa ya mazishi ya Ballali na kumualika Balozi wa Tanzania nchini Marekani, katika shughuli za mazishi zitakazofanyika kesho jijini Washington, Marekani.