Waraka wa Mbunge Luhaga Mpina kwa Watanzania: Tumeonewa kiasi cha kutosha sasa tunataka Mapinduzi ili tusionewe tena

Pfizer

JF-Expert Member
Mar 25, 2021
304
518
SALAMU ZA MBUNGE WA JIMBO LA KISESA MHE. LUHAGA JOELSON MPINA KWENYE KILELE CHA SHEREHE ZA MIAKA 60 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR ALIPOZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KATIKA UWANJA WA NEW AMAAN COMPLEX ZANZIBAR TAREHE 12 JANUARI 2024
1-28.jpg
1. UTANGULIZI
Ndugu Wanahabari
, Asanteni sana kwa nafasi mliyonipa kuzungumza machache kuhusu tukio hili muhimu la kitaifa, nimshukuru sana na kumpongeza Mhe. Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Serikali yake kwa salamu zake ambazo zimesisimua sana halaiki na maandalizi mazuri ya sherehe hizi ambazo zimefana sana.

Pia niwapongeze waandaaji wa Kauli Mbiu ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 2024 inayosema “Tuimarishe Uchumi, Uzalendo, Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu”. Kauli mbiu hii imekuja muda muafaka na imekonga mioyo ya watanzania na ndiyo maana imeshangiliwa sana uwanjani.

Sote tumeshuhudia gwaride la kijeshi lilivyopigwa kwa uhodari mkubwa na majeshi yetu ikiwa ni kielelezo cha uimara na umahiri wa majeshi yetu na kwamba yako tayari kuendelea kulinda Uhuru na Mapinduzi ya nchi yetu na kukabiliana na adui wa aina yoyote wa ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. HONGERA SANA MAJESHI YETU.

Pia kwa namna ya kipekee nimshukuru na kumpongeza sana Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulipa umuhimu mkubwa tukio hili na kutenga muda wa kutosha kushiriki kikamilifu licha ya majukumu makubwa aliyonayo ya kitaifa na kimataifa. Pia Sherehe hii imekuwa ya kipekee kwani imehudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Nchi jirani za Uganda, Rwanda, Kenya na Burundi. Umoja na mshikamano mnaotuonyesha Viongozi wetu wa kitaifa na kikanda unatutia nguvu na matumaini zaidi katika kuwatumikia watanzania na wa Afrika kwa ujumla.

Ndugu Wanahabari, kama mnavyofahamu leo tumekusanyika hapa katika Viwanja vya New Amaan Complex visiwani Zanzibar kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni siku muhimu sana kwa Ndugu zetu Wazanzibar walijitwalia Uhuru wao baada ya kuuangusha utawala wa Sultan kwa njia ya Mapinduzi yaliyo ongozwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na wazalendo wenzake 14 waliokuwa mstari wa mbele kudai Uhuru wa Zanzibar uliopatikana rasmi tarehe 12 Januari 1964.

Ndugu Wanahabari, hatujasahau na hatutasahau namna Mwasisi wa Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na wenzake walivyopigania kuuondoa na kuung’oa ukoloni wa kila aina unaofahamika na usiofahamika na hatimaye kupatikana kwa uhuru wa wananchi wa Zanzibar ambapo pia ilienda pamoja na kukomeshwa kwa dhuluma na unyonge waliofanyiwa wananchi kwa kipindi kirefu.

Wazee wetu hawa walijitoa mhanga hadi uhai wao kuhakikisha kuwa wanawakomboa wanyonge kutoka utumwani mwa Sultani na Serikali yake ya kidhalimu. Hawakuwa na silaha za kisasa wala Teknolojia ya kisasa zaidi walitumia silaha za jadi kama vile marungu, mapanga na mishale kufanya Mapinduzi. Wengine walipoteza maisha lakini haikuwarudisha nyuma wala kuwakatisha tamaa zaidi ilichochea hamasa ya kuendeleza mapambano. Daima tutaendelea kuenzi mchango wao mkubwa katika Taifa letu.

Hayati Sheikh Abeid Amani Karume mara tu baada ya Mapinduzi kesho yake asubuhi alisafiri kwenda Dar es Salaam kukutana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Tanganyika wakati huo, hii inaonyesha kuwa Viongozi hawa walikuwa na ushirikiano mkubwa na nchi hizi mbili zilikuwa na uhusiano wa karibu hata kabla ya Muungano wa Aprili 1964. Vijana hawa wa kiafrika waliamini kuwa Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Ndugu Wanahabari, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Karume mara tu baada ya nchi yetu kupata Uhuru na Mapinduzi kufanyika kwa nyakati tofauti tofauti walionyesha kukerwa sana wakikumbuka dhuluma, ubaguzi, ukandamizaji, maonevu na manyanyaso waliyotufanyia wakoloni, wakikumbuka umiliki na uhamishaji wa raslimali za nchi, wakikumbuka namna walivyo wageuza watanzania kuwa watumwa ndani ya nchi yao na wakaligeuza taifa letu kuwa dampo la kuuzia bidhaa zao.

Hapa nanukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere alisema,

“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na tupuuzwe. Sasa tunataka Mapinduzi, Mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na tusipuuzwe tena” mwisho wa kunukuu.

Ndugu Wanahabari,
Kwa ujumla waasisi wetu hawa walichukizwa sana utawala wa kikoloni ndiyo maana mara baada tu ya Uhuru walitangaza kutumia nguvu zao zote kukomesha aina zote za dhuluma, wizi, rushwa na ufisadi wa mali za umma. Waasisi wetu hawa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume waliamini kuwa kama mambo hayo maovu yataendelea kufanyika katika taifa letu hakutakuwa na maana na Uhuru na Mapinduzi.

Ndugu Wanahabari, kutokana na msimamo huo wa waasisi wetu walitangaza maadui 3 wa Taifa letu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini na baadaye likatangazwa Azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo pia iliwekwa Miiko ya Viongozi wa Umma ili kukataa dhuluma na kuhakikisha kuwa wizi, rushwa na ufisadi wa mali za umma unakomeshwa nchini. Pia njia kuu zote za uchumi zilirejeshwa mikononi mwa wananchi.

TATHMINI YA MAPINDUZI NA UHURU
Ndugu Wanahabari,
Tunaposherehekea Mapinduzi ni muhimu kufanya tathmini kama Taifa tumeenzi na kulinda maono ya waasisi wetu ya kudai Uhuru na Mapinduzi kama ilivyokusudiwa au tumeenda nje ya malengo?

Ni muhimu kama taifa tufanye tathmini ya mafanikio na changamoto tulizopata katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Miaka 62 ya Uhuru wa Taifa letu ili kuweka uelekeo sahihi kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.

MAFANIKIO YALIYOPATIKANA TANGU MAPINDUZI NA UHURU
Ndugu Wanahabari,
ni ukweli usiopingika kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar. Maendeleo na mageuzi makubwa ya Kiuchumi yanaonekana dhahiri, Tanzania inajua, Afrika inajua na Dunia inajua mafanikio tuliyopata. Baadhi ya mifano ya maeneo machache ni pamoja na:-

Ulinzi, Amani, Usalama na mahusiano ya kimataifa

Katika kipindi chote cha miaka 62 ya Uhuru na Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kuwa kisiwa cha amani kutokana na uongozi bora na uimara wa vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama.

Tanzania imekuwa nchi ya kupigiwa mfano Duniani kote katika kuitunza na kuilinda amani tunashuhudia majeshi yetu na Viongozi wa nchi yetu wakiteuliwa katika misheni mbalimbali za kimataifa za usuluhishi wa migogoro, kulinda na kurejesha amani katika mataifa mbalimbali Duniani, Taifa letu tangu Uhuru limeendelea na msimamo wake kimataifa na sera ya mambo ya nje ya kutofungamana na upande wowote, sera ambayo imeifanya nchi yetu kupata marafiki kila kona ya dunia.

Utoaji haki na Hali ya Muungano
Muungano wetu umeendelea kuwa imara na kero za muungano zimekuwa zikitatuliwa siku hadi siku tangu awamu ya kwanza hadi sasa awamu ya sita. Mahakama zetu zimeendelea kutoa haki kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za nchi.

Uboreshaji wa huduma za jamii elimu, afya na maji
Tumepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu ambapo idadi ya watanzania wanaojua kusoma na kuandika imendeelea kuongezeka huku idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu ikiongezeka mara dufu huku miundombinu na vifaa vya elimu navyo vikiendelea kuboreshwa. Kwa kiasi kikubwa adui ujinga tumempiga.

Sekta ya Afya tumeshuhudia mageuzi makubwa katika kipindi cha miaka 62 ya Uhuru na miaka 60 ya Mapinduzi zikiendelea kuboreshwa ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa na Hospitali za Rufaa za Kanda hadi kufikia viwango vya ubingwa na kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Pia kwa kiasi kikubwa adui maradhi tumempiga.

Sekta za uzalishaji na miundombinu ya kiuchumi uboreshaji mkubwa umefanyika wa miundombinu ya barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege, meli, ndege, bandari, umeme ambapo imepelekea kupiga hatua kubwa za kiuchumi na maendeleo. Pia uzalishaji umeongezeka katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Misitu na wanyamapori. Raslimali za Taifa kama madini, gesi, mafuta nako tumepiga hatua na kusaidia kwa kiasi kupunguza umasikini.

4. CHANGAMOTO TULIZONAZO BAADA YA UHURU NA MAPINDUZI
Ndugu Wanahabari,
Licha ya Mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi cha miaka 62 ya Uhuru na miaka 60 ya Mapinduzi bado hatujafanikiwa kuwapiga na kuwashinda maadui hawa Ujinga, Maradhi na Umasikini kwa asilimia 100. Nitataja baadhi ya changamoto ambazo zinarudisha nyuma jitihada za nchi yetu kukuza uchumi na kujiletea maendeleo kama ifuatavyo:-

Raslimali za taifa Ardhi, gesi, mafuta, madini, misitu, bandari, wanyama, mazao ya uvuvi nk. kulinufaisha taifa kwa kiwango kidogo sana kutokana na Mikataba Mibovu inayoingiwa na Serikali, kuingia Mikataba ya siri na baadhi ya raslimali za nchi kukabidhiwa wageni kwa mlango wa nyuma kwa kisingizio cha uwekezaji. Hali hii inaifanya nchi yetu kukosa mapato ya kutosha kugharamia shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi huku raslimali zake zikinufaisha mataifa na makampuni ya kigeni.

Hatuwezi kujivunia kupambana na umasikini wakati Wizi, Rushwa na Ufisadi umetamalaki nchini, taarifa za wakaguzi zinaonyesha upotevu wa matrilioni ya fedha za umma kila mwaka, mfano Taarifa ya CAG ya mwaka 2021/2022 inaonyesha wizi na ubadhirifu wa fedha za umma zaidi ya Tsh. Trilioni 30 huku Taarifa ya Kitengo cha Udhibiti wa Fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi (FIU) ikionyesha miamala shuku ya zaidi ya Tsh. Trilioni 280.

Kwa mwendo huu hatuwezi kupata fedha za kutosha kugharamia maendeleo ya nchi na kujenga uchumi kwani sehemu kubwa ya fedha za umma zinaporwa na na kumilikiwa binafsi na baadhi ya Viongozi waliopewa dhamana.

Upande wa Sheria, licha ya Sheria kutungwa na Bunge lakini kumekuwepo na Sheria kandamizi, zinazoleta dhuluma na kurudisha maendeleo nyuma, mfano Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009 inayoruhusu askari wa hifadhi kutumia silaha za moto kwa mwananchi aliyeingia ndani ya hifadhi hata kama hana silaha, hajakataa kukamatwa au pengine anajaribu kukwepa kukamatwa. Leo tunashuhudia majeruhi na mauaji ya kutisha ya wananchi na mifugo yao kandokando mwa hifadhi.

Pia sheria hiyo inaruhusu utaifishaji wa mifugo kwa kukutwa tu ndani ya hifadhi wala si athari zilizosababishwa na mifugo. Lakini pia tumeshuhudia baadhi ya watumishi wa umma kutoza faini na adhabu nje ya Sheria. Aidha baadhi ya mawaziri wanatunga Sheria ndogo zinazokinzana na Sheria mama na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. hali hii inayopelekea uvunjifu wa amani, dhuluma na maonevu makubwa yaliyopitiliza kwa wananchi wanyonge.

DPP kuwa na mamlaka ya kuondoa mashtaka Mahakamani wakati wowote hata kama kuna ushahidi unaojitosheleza. Hali inayopelekea kuporwa haki na kufanya dhuluma kwa wananchi.

Ajira za watanzania hazina ulinzi, kuruhusu bidhaa hafifu, bandia, feki na zisizolipa kodi kuingia nchini pamoja na uagizaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Hali inapelekea kuua ajira na viwanda vya ndani. Pia Zabuni na kandarasi nyingi wanapewa wageni badala ya wazawa wenye fedha zao za kodi, hivi sasa wageni wanapata zaidi ya 61% ya thamani ya zabuni zote zinazotolewa na Serikali. Pamoja na upendeleo mkubwa unaofanywa kwa wageni wazabuni wazawa wamekuwa hawalipwi kwa wakati jambo linalowafanya kufilisika na kutumbukia kwenye ufukara na umasikini mkubwa. Kitendo hiki kinaua uchumi wa nchi na kuhamisha ajira za watanzania.

Misamaha na uanzishwaji wa Kodi zisizo na utafiti na tathmini za kina hali inayopelekea kuwa na kodi zisizo na usawa, kandamizi, upotevu wa mapato, kuua ajira na kuchochea umaskini kwa wananchi.

Kushindwa kukamilisha miradi kwa wakati, miradi iliyoligharimu taifa matrilioni ya fedha na bila sababu za msingi, mfano mradi wa SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere na baadhi ya miradi ya barabara, madaraja na miradi ya maji.

Wananchi kuuawa na kuporwa mali zao, katika siku za karibuni imekuwa ni jambo la kawaida wananchi kuuwawa na kuporwa mali zao kwa visingizio vya kusimamia sheria za uhifadhi, mfano katika maeneo jirani na hifadhi kunaripotiwa taarifa za wafugaji kuuawa, wanawake kuuawa wakiwa wanakusanya kuni kwenye misitu ya hifadhi. Wengine Mifugo yao kutaifishwa na kuuzwa kiholela na Serikali na hata wakishinda kesi mahakamani mifugo yao hawarejeshewi. Haya ni maonevu na dhuluma iliyopitiliza kwa wananchi wetu na ni kinyume kabisa na malengo ya Uhuru na Mapinduzi.

Wakulima kuuziwa mbegu, dawa na mbolea feki na kwa gharama kubwa. Imekuwa ni jambo la kawaida wananchi kuuziwa mbegu kwa gharama kubwa na bila Maelezo mfano kilo ya mbegu ya mahindi kuuzwa Tsh 10,000 wakati kilo ya mahindi inauzwa Tsh 600. Kuuziwa dawa feki za kupulizia mazao zisizoua wadudu

na badala yake zinanenepesha wadudu, kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na zisizo na ubora hali inayoathiri afya ya udongo na kushuka kwa mavuno ya Wakulima na kuwaingiza kwenye njaa na hasara kubwa.

Pia kuwepo makato makubwa ya fedha yasiyo na uhalali kwa kisingizio cha ununuzi wa pembejeo mfano Wakulima wa Pamba katika msimu wa kilimo wa 2022 walikatwa kiasi cha Tsh. 400 na mwaka 2023 walikatwa Tsh. 300 kwa kila kilo waliyouza. Makato haya hayana uhalali na ni dhuluma kwa Wakulima. Bei ya kilo moja ya pamba ni Tsh. 1,360 halafu mkulima anakatwa Tsh. 300 kwa kila kilo moja sawa na 22% kulipia pembejeo kwa maelezo ya aina yoyote suala hili halikubaliki.

Badala ya kuwainua Wakulima tunawatia umasikini
Upande wa Masoko, Masoko ya ndani ya mazao kuhujumiwa na Masoko ya nje kukosa usimamizi hali inayopelekea wakulima kukosa masoko na bei nzuri ya mazao yao na kuendelea kubaki masikini.

Shughuli zingine za Kiuchumi, kuwepo migao na katakata ya umeme isiyo na sababu za msingi, kukosekana kwa dola, riba kubwa za mabenki, kupanda kiholela kwa bei ya nishati ya mafuta na bidhaa zingine muhimu kama mafuta ya kula, ngano, sabuni na vifaa vya ujenzi na kupelekea mfumko mkubwa wa bei na ugumu wa maisha, kuvuruga huduma za jamii na kuharibu uchumi wa nchi. Hatuwezi kuimarisha uchumi kama kuna usimamizi dhaifu na ufisadi mkubwa kiasi hiki katika maeneo nyeti.

Kuanzishwa kwa Sera mpya ya elimu ambayo inaruhusu mwanafunzi kusoma kuanzia shule ya awali hadi kidato cha 4 bila kuwepo na mtihani wa taifa uamuzi ambao ni mkakati wa kuua elimu nchini. Pia kukosekana mikakati madhubuti ya kutengeneza vijana wenye ujuzi mahiri katika fani mbalimbali. Pia hakuna tafiti zinazofanywa kubaini mahitaji ya soko la ajira.

Baadhi ya Madaktari na wauguzi kuripotiwa kutumia lugha chafu kwa wagonjwa na kutumia maeneo ya huduma za afya za Serikali kama eneo la kukutana na wagonjwa (meeting point) na baadaye kuwahamishia kwenye hospitali zao binafsi ambapo ndiko muda mwingi wanautumia huko. Vifaa Tiba vilivyoko kwenye hospitali za umma kama MRI, CT–Scan, X-ray nk. kutokufanya kazi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutofanyiwa matengenezo, kukosa wataalamu na wakati mwingine kuhujumiwa ili kuwezesha hospitali binafsi kupata biashara. Hali hii inapelekea wagonjwa wengi kukosa matibabu na kupelekea vifo ambavyo vingeweza kuzuilika.

Kutokufanyika kwa ukaguzi wa kimatibabu kulingana na vigezo vilivyowekwa na WHO ili kujipima viwango vya ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini. Hali hii inapelekea kushindwa kujua ufanisi wa utoaji huduma katika Hospitali za Serikali, kuchochea uzembe na kushindwa kuwajibika kikamilifu kwa mamlaka zinazohusika.

Hospitali za Serikali kuacha jukumu lake la msingi na kuanza kufanya kazi za anasa kama kuongeza ukubwa wa makalio badala ya kujishughulisha kikamilifu kutibu maradhi yanayosumbua wananchi.

Tunao uhaba mkubwa wa raslimali fedha katika kutatua matatizo ya huduma za afya. Mfano leo ni zaidi ya miaka 3 tumeshindwa kutoa mtaji kwa MSD wa takribani Tsh. Bilioni 500 kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba kutokana na ukosefu wa fedha. Hizi fedha za kununua mitambo na vifaa vya kuongeza ukubwa wa makalio zimetoka wapi?

Kuendelea kuripotiwa kwa vifo visivyo na Maelezo kwa wagonjwa hususan akina Mama wajawazito na watoto wakiwa eneo la huduma. Ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika maeneo ya utoaji wa huduma za afya za umma. Pia zaidi ya vijiji na mitaa 6,000 havina zahanati kote nchini tangu Uhuru jambo linalowafanya wananchi wa maeneo hayo kukosa huduma za afya ya msingi.

5. HITIMISHO
Ndugu Wanahabari,
Wakoloni tuliwang’oa na wakafungasha virago vyao wakaondoka tukashusha bendera yao na kupandisha bendera ya kizalendo kuashiria Uhuru kamili. (Complete Independence). Leo nani anaendesha dhuluma, nani anaendesha uonevu, wizi, rushwa na ufisadi wa mali za umma mambo ambayo tuliyakataa tangu siku ya kwanza ya kupata Mapinduzi Uhuru wa nchi yetu. ninaamiini sio mwananchi wa kijijini anayefanya haya isipokuwa ni sisi Viongozi tuliopewa dhamana.

Kupitia Kauli mbiu ya Miaka 60 Mapinduzi Zanzibar 2024 inayosema “Tuimarishe Uchumi, Uzalendo, Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu” tukafanye tathmini na kubaini mahala tulipokosea na kurekebisha changamoto zilizopo ili taifa na wananchi waendelee kufurahi na kufaidi matunda ya Mapinduzi na Uhuru kama yalivyokuwa malengo ya waasisi wetu.

Kamwe tusikubali dhuluma, wizi, rushwa na ufisadi kuendelea katika taifa letu na wale wote wanaojihusisha na maovu haya washughulikiwe bila huruma kama sehemu ya kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Uhuru wa nchi yetu.

Naamini inawezekana kwani penye nia pana njia, The most frustrating things is not the size of the challenge but the size of the opportunity.

Asanteni kwa kunisikiliza,
……………………………..

Luhaga Joelson Mpina (Mb) Mbunge wa Jimbo la Kisesa
 
Mpina amejipambanua vizuri sana kwa wakati huu ndani na nje ya bunge, ameamua kwa dhati kuitumia akili yake kikamilifu kuangaza maeneo tofauti yenye kero kwa jamii yetu, na kuyataja pamoja kero husika bila hofu wala woga wowote.

Ameamua kufanya kazi ya upinzani ndani ya lile bunge la chama kimoja bila aibu, hofu, wala woga, na anaifanya kikamilifu, huyu anastahili pongezi toka kwa wote wanaolitakia mema hili taifa, bila kujali itikadi zao.

Kumkejeli au kumtolea kasoro yoyote kunaonesha vile wengine walivyozama kwenye lindi la ujinga tuliopewa na serikali ya CCM na itawachukua muda mrefu sana kutoka huko, matatizo yetu lazima yasemwe ili wahusika wayafanyie kazi, na hilo sio jukumu la wapinzani peke yao, ni jukumu letu sote.

Sent from my SM-G900H using JamiiForums mobile app
 
Huyu jamaa probability ya kuchanganyikiwa ni kubwa sana, alichotufanyia wavuvi enzi zile mungu anamuona, akae kwa kutulia, huyu jamaa alikuwa akifika sehemu anasema changeni kiasi kadhaa cha fedha ili nyavu zenu zisikamatwe au kuchomwa moto,huyu mtu ana tembea na laana za wavuvi,

Apuuzwe kwa nguvu zote.
 
Mpina amejipambanua vizuri sana kwa wakati huu ndani na nje ya bunge, ameamua kwa dhati kuitumia akili yake kikamilifu kuangaza maeneo tofauti yenye kero kwa jamii yetu, na kuyataja pamoja kero husika bila hofu wala woga wowote...
Ni Mnafiki tu huyo hana lolote, kakosa uwaziri ndio maana anamaliza frustration tu wala hana hoja za msingi. Sasa GDP ya Tanzania ni Trillion kama 150 pekee sasa kivipi kuwepo miamala ya Trillion 280!! Yaani miamala shuku ni mingi mara mbili ya GDP!! sasa kama ni shuku pekee ina maana kuna miamala mara 7 ya GDP ya Tanzania?

Kingine anadai ripoti ya CAG kuna ufisadi wa Trillion 30 kwa mwaka 2021/22 pekee!! Yaani Bajeti Trillion 40 ila 30 zimeibiwa, sasa mishahara pia iliibwa?

This guy is delusional hata akija upinzani hana la kutusaidia.
 
Ni Mnafiki tu huyo hana lolote, kakosa uwaziri ndio maana anamaliza frustration tu wala hana hoja za msingi. Sasa GDP ya Tanzania ni Trillion kama 150 pekee sasa kivipi kuwepo miamala ya Trillion 280!...
Suala la hizo Trillions MPINA alifananua Bungeni kimahesabu mpaka kufikia hapo

MPINA hapiki takwim, Bali hutumia Takwimu za Wataalam Kisha yeye anazichambua na kuja na kitu kinachoeleweka.

Ni Mpumbavu tu na mjinga wa akili ,ndo anaweza Kumpinga mpina.

Hata hivo Duniani hapa, Sisi wenye akili nyingi, Huwa tunachukiwa na Wajinga na sisi wenye kuchapa kazi Huwa tunachukiwa na wavivu,wazembe !!
 
Waraka mzuri sana, na umebeba ujumbe wenye maudhui muhimu sana kwa wakati huu wenye watawala wenye hulka na haiba zote za kikoloni.

Waasisi wa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar hawakuwa na "elements" za kikoloni hata kidogo, lakini watawala wa sasa ni wakoloni weusi ila tu kiunafiki wamejificha nyuma ya sifa nzuri za kihistoria za waasisi wetu.

Ni vyema watu wakamwelewa Mh. Mpina kwa msimamo wake na kile ambacho anachojipambanua nacho kutokana na uzoefu wa kiuongozi ndani ya chama chake. Anaonyesha ni kada ambaye alitamani sana kuiona falsafa na njozi ya JPM ikitimia ifikapo mwaka 2024.

Ni mtu ambaye kutokana na tathmini yake mwenyewe, ambayo inahakisi ukweli na uhalisia wa nyakati, anaona kila kitu ambacho kilikuwa ni kipaumbele kwa miaka michache iliyopita kimefanyiwa usaliti, tena na watu wale wale ambao walioshiriki kukijenga.

Watawala wa sasa wamebadili ajenda waliyoshiriki kuiasisi na kuiishi, na hivi sasa badala ya mafisadi kuishi kama mashetani, kibao kimebadilika umma wa maskini wa Kitanzania ndiyo unaishi kama mashetani na kwa kulimia meno yao.

It is plain reality that despite of the size of challenges, the size of opportunity is also worthy to mention.
 
Kibaya zaidi mawazk mazuri na makubwa huwa hayaeleweki kirahjsi kwa wajinga, wezi, wapinga pambio n.k

Luhaga is another level.

Anafaa kuwa Super youth president.

Kama unaskma huu uzi mheshimiwa mpina, keep it up
Kila mtu anatambua Mpina alikuwa mojawapo wa wanafumzi watiifu sana kwa JPM. Kinachowatisha wengi wa mahasimu wake wa kisiasa ni kutokana na ukabila na ukanda wake.

Huyu anaonekana ni tishio kubwa sana kwa mafisadi na vibaraka wao. Kila kauli itokayo katika kinywa chake ni kama vile moto ulao. Hongereni sana ndugu zetu Wasukuma kwa kuzaa, kulea, na kuandaa vijana wenye uthubutu kuukemea uovu pasipo kupepesa macho, na uzalendo wa kweli na usiokuwa na shaka yoyote ile
 
Pamoja na kuwa kaamua kujipambanua baada ya kukosa uwaziri ila hotuba yake ni nzuri na kweli.

Ninavyokifahamu chama chake kilivyo hakitaki kinyoshewe kidole na mwanachama wa humo humo,ila huyu ajiandae kuliwa kichwa.

2025 ccm lazima mpasuko utokee tu! Mafisi
 
Serikali ya CCM na vibaraka (chawa) wake hawataki wabunge wa aina hii. Si ajabu 2025 huyu Mpina atapata shida sana kupitishwa kuwa mgombea.

Kuongea ukweli ndiyo kilichomfanya jiwe awaenguwe wale wote aliohisi watampa challenge hata kama walipita kwenye kura za maoni na kumalizia kwa kuwapiga chini kiaina wagombea wa vyama vya upinzani hasa Chadema.

Wabunge wanaotakiwa CCM ni wale wenye uwezo wa kusema ndiyoooo hata pale panapoitajika kusema hapana. Hongera mh. Mpina ukweli umuweka mtu huru no matter what.
 
Dah! Speechless

Hawa wakoloni weusi wangepitia kwanza huu waraka ulioshiba,ni articulate
 
Mpina watakukata jina lakini wewe unajiamini na Watanzania wanakuheshimu
 
la hizo Trillions MPINA alifananua Bungeni kimahesabu mpaka kufikia hapo
Be serious alisema ni accumulated "ufisadi" wa miaka mingi ila hapo kwenye waraka anasema ni bajeti ya 2021/22!! Sasa Bajeti ya Trillion 40 unaibaje Trillion 30!!

Kingine audit query sio ufisadi maana yake ni fedha zenye malipo yasiyo na risiti au mali ambazo hazijathaminishwa. Na ndio maana ripoti ya PAC huwa inachambua na kuainisha kipi kiliipwa kipi hakikuibwa so ni mjinga pekee anatumia ripoti ya CAG bila kuoanisha na majibu ya ripoti ya PAC!!
MPINA hapiki takwim, Bali hutumia Takwimu za Wataalam Kisha yeye anazichambua na kuja na kitu kinachoeleweka.
Takwimu za wataalamu gani zinasema Miamala shuku ni mingi kuliko GDP ya nchi? Hivi mnatuonaga wote ni wajinga ama? Yaani Tanzania ina miamala ya Trillion 700 wakati GDP ni Trillion 150?? Embu nitafutie ripoti yenye hiyo takwimu.
Mpumbavu tu na mjinga wa akili ,ndo anaweza Kumpinga mpina.
Mimi siwezi ingia mtego wa kumsikiliza mtu ambaye leo anakosoa vitu ambavyo alivitetea alipokua waziri. Mfano alidai katiba mpya sio takwa la wananchi cha ajabu leo kakosa uwaziri anaona katiba mpya ni muhimu.

Kipindi akiwa waziri hatukupewa fedha za Acacia ila alikaa kimya, kakosa uwaziri ndio anajifanya kuhoji kwanini hatujalipwa!!

Ni mnafiki tu asiyejua lolote kuhusu uchumi wala takwimu kafanikiwa kuwachota wajinga msio na shule kama wewe!! Mnamuona mzalendo wakati kakosa tu uwaziri!! Kesho akiteuliwa na Samia utashangaa atakavyokana haya maneno yake.

Huo muda ukifika nitarudi kufufua hizi nyuzi zenu za kishamba.

Cc joseph1989
 
Mpina watakukata jina lakini wewe unajiamini na Wtz wanakuheshimu
Hakuna mtanzania ana time na huyo mnafiki. Pia alikatawa ujumbe wa NEC taifa na mkoa na wala sikuona kelele yoyote means watu wamempuuza rasmi.
 
Kibaya zaidi mawazk mazuri na makubwa huwa hayaeleweki kirahjsi kwa wajinga, wezi, wapinga pambio n.k

Luhaga is another level.

Anafaa kuwa Super youth president.

Kama unaskma huu uzi mheshimiwa mpina, keep it up
Alipokua waziri alifanikisha kipi? Au urais anafaa kisa anakosoa mambo aliyoshindwa kuyatekeleza akiwa serikalini?
 
Hakuna mtanzania ana time na huyo mnafiki. Pia alikatawa ujumbe wa NEC taifa na mkoa na wala sikuona kelele yoyote means watu wamempuuza rasmi.
2025 sio mbali.


Kama Mkuu wangu Paul Makonda, karudishwa na Nchi.

MPINA ndo akatwe ??? THUBUTU.

yaan Kichwa Cha Mpina kikatwe, ulete mabichea hewa ya Akina Nape???.
 
Ndugu Wanahabari, hatujasahau na hatutasahau namna Mwasisi wa Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na wenzake walivyopigania kuuondoa na kuung’oa ukoloni wa kila aina unaofahamika na usiofahamika na hatimaye kupatikana kwa uhuru wa wananchi wa Zanzibar ambapo pia ilienda pamoja na kukomeshwa kwa dhuluma na unyonge waliofanyiwa wananchi kwa kipindi kirefu.
Hapa tu kuna Uongo....siendelei kusoma tena
 
Back
Top Bottom