Nimepitia kwa kituo maoni mbalimbali ya wachangiaji wa makala yangu ambayo thread yake imetumwa jana. Kimsingi nayaheshimu mawazo mbalimbali yaliyotolewa na Watanzania ambao wameonyesha namna wanavyoguswa na masuala mazito ya kitaifa.
Hata hivyo ni jambo la bahati mbaya sana kwamba baadhi ya maoni yaliyotolewa na wachangiaji yamechukua mwelekeo wa kebehi, kashfa, uzushi, matusi na mambo yanayofanana na hayo. Hayo yamenisikitisha.
Siku zote naamini hoja hujibiwa na hoja na ndiyo maana nimekuwa tayari kuanzisha mijadala mbalimbali katika magazeti lengo likiwa ni kujua mitazamo ya Watanzania wenzangu katika mambo mbalimbali yanayohusu hatima ya taifa letu.
Nimeona nifanye juhudi za makusudi kuweka sawa baada ya mambo ambayo yameibuliwa katika mawazo ya Watanzania ambao naamini yametolewa kwa nia mbaya.
Kwanza si kweli kwamba makala ile imeandikwa kwa malengo ya kumfurahisa, kujipendekeza au kujikomba kwa Mbowe kama ambavyo imetakwa iaminiwe na baadhi ya wachangiaji wa JF.
Naamini Zitto mwenyewe angekuwa mkweli na muwazi angeweza kuwathibitishia wana JF wengine kuhusu maoni yangu katika masuala mbalimbali ya kisiasa likiwamo hili ambalo linamgusa yeye moja kwa moja.
Niseme wazi kwamba siku zote nimekuwa nikimtakia mema Zitto na wanasiasa wengine mbalimbali vijana ambao wamesambaa katika vyama mbalimbali kwa sababu nina imani kuwa, Vijana ni Taifa la Leo. Kwa sababu hiyo basi hoja yangu kuhusu Zitto haikugusia umri wa Zitto bali uchanga wake katika masuala mbalimbali ya siasa. (Huo ni mtazamo wangu).
Uamuzi wangu wa kuandika makala hii na kueleza 'maono yangu ya kisiasa' kuhusu anguko la Zitto ninaloliona, halimaanishi hata kidogo kuwa ninamuombea mwanasiasa huyo kijana baya lolote, zaidi ya tu ya kumtaka atambue uzito wa wajibu ambao anaelekea kuuchukua.
Napenda kusema bayana kwamba anguko naloliona likimkabili Zitto si la kushinda au kushindwa katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa taifa wa Chadema. Anguko ninaloliona kwa Zitto litakuja akishindwa na hata akishinda wadhifa huo anaogombea.
Ni kwa sababu hiyo katika makala hiyo nilimtaja James Mbatia ambaye alipoamua kugombea uenyekiti wa NCCR akiwa na lengo la kupambana na Marando kwa sababu tu ya makosa kadha wa kadha ya kimaamuzi ambayo Marando aliyasimamia na kukiletea matatizo chama hicho, aliishia kukiingiza shimoni kabisa chama hicho na hata baada ya kushinda wadhifa huo.
Nilitegemea wachangiaji wangempima Zitto wa Chadema kwa kumlinganisha na Mbatia na Marando wa NCCR Mageuzi kwanza, kabla ya kukimbilia na kumlinganisha Nyerere aliyeshika madaraka akiwa mdogo wa miaka 32 ndani ya Tanu na miaka 39 akiwa rais wa Tanzania.
Kwa mantiki hiyo hiyo, nilitarajia kusikia wachangiaji wakijenga hoja yao ya anguko la Zitto kwa kuangalia mahitaji ya vyama vya siasa vya upinzani wakati huu, ukiwa ni mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Aidha matarajio yangu yalikuwa ni kuona watu wakimpima Zitto kwa kuangalia vigezo vya namna anavyoweza kuwaongoza watu na si kujiongoza mwenyewe kwa namna ya kuonyesha njia chini ya msingi imara wa uwajibikaji wa pamoja na si wa kila mtu kujitafutia umaarufu wake binafsi.
Kwa kusema hivi sina maana hata kidogo kwamba, Zitto hana uwezo wa kiuongozi bali kwa namna ninavyomfahamu nimetumia neno 'mwanasiasa mchanga' nikimaanisha kuwa ni mtu anayepaswa kujifunza masuala mengi katika kuongoza.
Katika hili ni makosa kulinganisha umri wa Zitto na wa Nyerere na kuishia katika kigezo hicho na kusahau ukomavu, nidhamu na namna viongozi hao wawili wanavyotofautiana katika medani ya kiuongozi.
Pengine ni wale tu tunaomfahamu Zitto vizuri ndiyo tunaojua namna alivyo tayari kujenga hoja zake binafsi pasipo kujali msingi wa msimamo wa chama chake katika jambo hilo hilo tena hadharani, Je mtu wa namna hiyo anafaa kuwa Mwenyekiti wa Chama.
Zitto ni shahidi kwamba siku zote amekuwa akihimizwa kutambua dhana ya uwajibikaji wa pamoja ndani ya chama chake akiwa mbunge jambo ambalo hadi leo hii kijana huyu anaonekana kulipuuza (huo ni mtazamo wangu).
Ni kwa sababu hiyo nilimuita mchanga na kuona anao muda wa kujifunza zaidi masuala kadhaa ya kiuongozi kabla hajapewa dhamana kubwa ya kuwa mwenyekiti na hivyo kuishia akianguka.
Ukiacha hayo, nimesikitishwa na wachangiaji ambao wamefikia hatua ya kunihusisha na ufisadi hata kutunga uongo kwamba eti mimi na Muhingo Rweyemamu tumenunuliwa magari yanayofanana na ambayo yanafuatana namba. Hakika huu ni upuuzi na uongo.
Ni kweli mimi na Muhingo tuna magari yanayofanana. Mbali ya kuwa kaka yangu, Muhingo ni rafiki yangu mkubwa. Nilinunua gari kwa fedha zangu na nyingine nikapewa kwa nyakati tofauti na mwajiri wangu.
Nikiwa nimeshalitumia gari langu kwa miezi mitatu, Muhingo alilipenda na nikampeleka kwa watu ambao waliniuzia kwa kuliagiza kutoka Japan. Alipofika pale akasema anahitaji gari kama langu na wakati huo namba za usajili zilikuwa zimesogea sana. Ni kwa nini Watanzania tumejenga tabia ya kusema hata kabla hatutafanya uchunguzi wa kutosha? Haya ni maradhi ambayo mara nyingi nimekutana nayo JF. Hata hivyo siku zote ukweli utasimama.
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba, hivi sasa mtu anapotoa maoni yake ambayo huonekana kuwa tofauti na mawazo ya wengi basi mtu huyo hupewa majina mengi machafu; ametumwa, amehongwa au anajipendekeza.
Huku tukijua umuhimu wa watu kuheshimu maoni tofauti ya watu kwani ndiyo msingi wa maendeleo, wengi wetu tumekuwa tukikimbilia kuwahukumu wenzao. Nimefikwa na hali hiyo mara nyingi tu na hata Zitto mwenyewe amekuwa majeruhi wa tuhuma hizo hizo.
Kwa kusema hivyo simaanishi hata kidogo kwamba watu hawatumiwi au hawatumwi au hawajipendekezi, la hasha ninachotaka kusema hapa ni kutokuwa wepesi kuhukumu watu kwa sababu tu ya hisia. Haya ni maradhi ya hatari na ambayo kwa kiwango kikubwa yamekuwa yakiwakatisha tamaa wachambuzi wengi wenye mioyo dhaifu.