KESI YA MKE WA BILIONEA MSUYA: Shahidi askari ayakana maelezo yake

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
Dar es Salaam. Shahidi wa 16 katika kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; ameyakana maelezo yanayodaiwa aliyaandika kuhusiana na kesi hiyo.

Shahidi huyo, Askari Polisi kutoka kitengo cha ukaguzi wa matukio cha Polisi Reli, WP 2920 DS Elentruda 53, aliyakana maelezo hayo jana wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko baada ya kubaini kuwa yana kasoro kutokana na kutofautiana na ushahidi alioutoa mahakamani kwa mdomo.
Kutokana na hali hiyo, Wakili Nkoko aliiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inayosikiliza kesi hiyo iyapokee yawe kielelezo cha upande wa utetezi ili mahakama iweze kuzingatia mkanganyiko huo kati ya ushahidi alioutoa mahakamani na maelezo yake hayo ya maandishi, wakati itakapoandika hukumu.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga maombi hayo ya upande wa utetezi ukidai hayajatimiza vigezo vya kisheria.
Jaji Edwini Kakolaki anayesikiliza kesi hiyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake alikubaliana na pingamizi la upande wa mashtaka na kukataa kuyapokea maelezo hayo kuwa kielelezo cha upande wa utetezi, akisema hajayakidhi vigezo vya kisheria.
Miriam Steven Mrita, anakabiliwa na shtaka la mauaji ya wifi yake, Aneth Msuya, akidaiwa kushirikiana na mshtakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.
Aneth aliuawa Mei 25, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, miaka mitatu baada ya kifo cha kaka yake, Bilionea Msuya aliyeuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi katika eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Kesi hiyo namba 103 ya mwaka 2018 inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake alioutoa akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Peter, shahidi huyo alieleza mahakama kuwa ndiye aliyepokea vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio la mauaji na kukabidhiwa sampuli ya mpanguso wa kinywa cha mshtakiwa wa pili, Muyella kuvipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa vinasaba.
Baada ya maelezo hayo ya ushahidi, alihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa washtakiwa Peter Kibatala na Nehemia Nkoko kuhusu utaratibu wa kuhifadhi vielelezo hivyo kisheria, hatua kwa hatua mpaka kufikishwa mahakamani kuona kama matakwa ya kisheria yalizingatiwa.
Wakati akihojiwa na Wakili Nkoko, kwanza alimpatia nakala kivuli ya maelezo yake akasoma kimyakinya. Kisha akamuuliza kama ni yake naye shahidi akakubali.
Hata hivyo, baada ya Wakili Nkoko kuanza kuonyesha tofauti kati ya ushahidi wake kizimbani na maelezo hayo, ndipo shahidi huyo alipoyakana maelezo hayo kuwa si yake, akidai kuwa yeye aliandika kwa mkono, lakini hayo yaliyochapwa yana upungufu.
Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo na Wakili Nkoko yaliyosababisha shahidi huyo kuyakana maelezo yake ni kama ifuatavyo:
Wakili Nkoko: Utakubaliana na mimi kwamba maelezo yote uliyoyasema hapa ni ya uwongo maana hayapo katika maelezo yako uliyoyaandika tarehe 30/8/2016?
Shahidi: Si kweli, niliyoyaeleza hapa ni sahihi, hayo maelezo siyo niliyoandika mimi. Mimi niliandika kwa mkono si kwa kuchapa.
Nkoko: Ukisoma haya maelezo, jina na saini iliyoko hapa yanafahamika kuwa ni ya nani?

Shahidi: Jina ni langu, mimi Elentruda maana nafahamika ndiye mtunza vielelezo, lakini haya maelezo yana mapungufu, mimi sikuandika haya.
Nkoko: Katika hii statement imeandikwa kuwa yote uliyoyasema ni ya kweli tupu na kama ukisema uwongo unaweza ukashtakiwa.
Shahidi: Hauko sahihi, maana yana mapungufu.
Nkoko: Mheshimiwa Jaji naomba chini ya kifungu cha 154 na 164 (1) (c), Sheria ya Ushahidi mahakama ipokee maelezo haya kama kielelezo cha upande wa utetezi ili mahakama ione contradiction (utata) hizi zilizopo.
Wakili wa Serikaki Yasinta anasimama: Kwa upande wetu tunapinga maelezo haya yasipokewe, kwanza ni nakala, pili, hayajasomwa, tatu, anayeomba kuyatoa ni wakili, si shahidi na wala shahidi hajaombwa ayatoe yeye. Shahidi pia hajathibitisha kama ni maelezo yake.
Pia yana upungufu wa vigezo vya kisheria kuweza kutolewa kama kielelezo na Mahakama ilishatoa maelekezo katika changamoto kama hiyo kuhusiana na nani ana nguvu ya kutoa kielelezo na lazima yasomwe.
Na sheria imetoa mwongozo wa nani ana mamlaka ya kutoa kielelezo kwamba lazima awe aliyekitengeneza au anayekitunza
Badala yake anataka kuyatoa wakili ambaye siye mwenye kielelezo wala mhifadhi wake.
Kutokana na maelezo hayo na kwa vifungu alivyovitumia wakili, sisi tunaona maelezo hayo ambayo wakili anataka yapokewe, yasipokewe kwa sababu hayajakidhi vigezo vya kisheria na tunaomba maombi ya wakili msomi yatupiliwe mbali.
Nkoko: Nadhani hapa kuna kuchanganya taratibu. Wakati wa upande wa mashtaka unapokwa unatoa ushahidi, ndipo hizo taratibu zote zinatakiwa zifuatwe, lakini katika dodoso shahidi anaweza kubanwa wakati wowote.

Wenzetu wangekuwa wanafanya kesi za madai hili lisingekuwa tatizo, wangekuwa wanaelewa na kanuni hii inatumika kwenye kesi zote.
Mwanzoni nilimwonyesha na kumuuliza shahidi kama ni maelezo yake akasoma kimyakimya, kisha akasema ni yake. Nilipoanza kumuonyesha utata ndiyo akaanza kusema si ya kwake.
Kwa hiyo, hatua zote zimefuatwa na hii nyaraka imetoka kwao (upande wa mashtaka) wametupa leo na walitupa wakati wa kutoa maelezo ya awali.
Kwa hiyo tunaomba hoja yao kwamba yasipokewe isikubalike.
Tumeomba mapema nakala halisi wakasema hawana na wakasema wana nakala tu, wakatupatia na sasa inataka kutolewa wanasema hapana.
Sisi tunaendelea kusisitiza ushahidi wa upande wa utetezi haujafunguliwa na hawana shahidi kwenye kizimba, hivyo hata wakili anaweza kutoa kielelezo na ili mahakama ipate ukweli lazima wakitoe mawakili.
Wakili Yasinta: Sisi tunaendelea kupinga. Kifungu cha Sheria alichokitaja kinataka kielelezo kutolewa kwanza kwa notisi. Notisi haijatolewa na wala hajathibitisha kwamba sisi hiyo nakala halisi tunayo mahakamani.
Japo wakili amesema shahidi aliyeko kizimbani si shahidi wao, lakini utaratibu wa kutoa vielelezo ni uleule. Ingawa shahidi wetu yuko kizimbani lakini hajaombwa kuyatoa maelezo hayo. Kutokuwepo kwa shahidi wao kizimbani hakumpi wakili haki ya kuwa shahidi na kuomba kuyatoa maelezo yeye.
Jaji Kakolaki katika uamuzi wake alisema kuna vigezo vitatu vya kielelezo kupokelewa, kwamba katika kigezo cha kwanza cha na cha tatu havikutimizwa.
Jaji alisema japo ni kweli kwamba nyaraka hiyo inahusiana na kesi, lakini mwenye mamlaka ya kutoa kielelezo mahakamani ni shahidi aliyekiandaa au aliyeshughulika nacho au kukitunza na kwamba katika sheria hatajwi wakili, hivyo ombo la utetezi likatupwa.

CREDIT:MWANANCHI
 
Shahidi huyo, Askari Polisi kutoka kitengo cha ukaguzi wa matukio cha Polisi Reli, WP 2920 DS Elentruda 53, aliyakana maelezo hayo jana wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko baada ya kubaini kuwa yana kasoro kutokana na kutofautiana na ushahidi alioutoa mahakamani kwa mdomo.
Kutokana na hali hiyo, Wakili Nkoko aliiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inayosikiliza kesi hiyo iyapokee yawe kielelezo cha upande wa utetezi ili mahakama iweze kuzingatia mkanganyiko huo kati ya ushahidi alioutoa mahakamani na maelezo yake hayo ya maandishi, wakati itakapoandika hukumu.

Imeisha hiyo ,watu washakula fungu wanaandaa mazingira mtuhumiwa aachiwe huru.
 
Back
Top Bottom