Mama huyo, akiwa na simanzi ya kudumu usoni, aliwaambia waandishi wetu kuwa, siku ya Bonanza hilo hakutaka kufungulia Tv kwani aliamini kuwa, kwa kumwona mwanae (Nguza) na wajukuu zake watatu (Francis, Mbangu na Papii Kocha) angeumia sana kwani mara nyingi hutoa machozi anaposikia lolote linalohusu familia hiyo iliyoko jela maisha.
Huku akiwa amemkumbatia mikononi mjukuu wake ambaye alisema ni mtoto wa mwanae mkubwa (kaka wa Nguza), mama huyo aliendelea kusema kuwa, amekuwa akiishi bila imani kuhusu kufungwa kwa mwanae na wajukuu zake hasa baada ya baadhi ya vigogo Serikalini (alikataa kuwataja majina) kukataa kuwapa uhamisho akina Nguza kutoka kwenye Gereza la Ukonga waliko sasa kwenda kwenye Gereza moja nchini Kongo ambako ndiko kwenye asili yao.
Alisema hilo lilijitokeza muda mfupi baada ya familia yake hiyo kuhukumiwa ambapo Rais wa Kongo, Joseph Kabila aliiomba nchi kuwahamishia wafungwa hao katika Gereza moja la nchi hiyo. Lakini alikataliwa.
Aidha, mama huyo alisema kuwa, inavyoonesha kuna mchezo mchafu unafanywa ili kuendelea kuwaweka gerezani watoto wake lakini anaamini Mungu yupo, siku si nyingi watatoka kutokana na maombi anayofanya kila siku.
Naamini kuna mchezo mchafu ambao unachezwa na baadhi ya viongozi wa Serikali watoto wangu wasitoke, lakini naamini kwa uwezo wake Mungu ninayemuomba kila siku watatoka tu, na watatoka kishujaa kwani kuna mpango wa kukata rufaa kwa mara nyingine na safari hii tunaamini tutashinda na watakuwa huru, alisema mama wa Babu Seya.
Hakuishia hapo, mama huyo aliongeza kuwa, iwapo mwanae na wajukuu zake watatoka hawatakaa tena nchini kwani mpango wao ni kurudi kwao (Kongo) ambapo wanatarajia kuwa na msafara mkubwa ambao utapokelewa na idadi kubwa ya wakongo na kufanyiwa sherehe ambayo haijawahi kutokea.
Iwapo Nguza na wanawe watafanikiwa kutoka Gerezani, tutaondoka kurudi nyumbani kwetu Kongo ambako tutakuwa na msafara mkubwa. Tukifika huko watatupokea kwa shangwe na kufanya sherehe kubwa kwani Nguza anafahamika sana kwasababu baba yake alikuwa ni mfalme, hivyo kila mtu ana hamu ya kumuona na siku hiyo patakuwa hapatoshi, alisema kwa masikitiko makubwa mama wa Nguza.
Katika hali iliyoonesha kusikitishwa sana na kifungo hicho cha mwanae na wajukuu zake, mama huyo alisema siku watakapohama hawataacha hata vifaranga, achilia mbali kuku wenyewe.
Hili ni tamko kubwa kulitoa mama huyo toka wanae hao wahukumiwe kifungo cha maisha jela mwaka 2005 kwa kosa la kuwanajisi watoto.
Bonanza la Wafungwa liliandaliwa na Kampuni ya Global Publishers inayotoa magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Championi, Amani na Risasi.