Sio siri Mkapa alikuwa na matatizo yake ila alikuwa Rais mwenye maamuzi na msimamo. Hakuwa indecisive kama huyu tuliye nae. Natoa tu mfano mmoja. Kuna wakati Valambia aliishtaki serikali kuhusu rada na mahakama kuu ikaamrisha serikali ilipe shilingi bilioni 50 plus interest. Mkapa alikataa akasema mkataba ulikuwa wa hila na mkawaambia waziri wa fedha, gavana na mwanasheria mkuu kuwa kama pesa ikilipwa nao wajiuzulu. Ilibidi wapeleke sheria bungeni kuzuia mtu kushika mali za serikali. Pesa haikulipwa hadi leo na Valambia mwenyewe na mwanasheri wake Maira wameshafariki. Huyu ndie rais anayejua kuwa maslahi ya mafisadi hayawezi kuwa juu ya maslahi ya nchi. Kwanini Kikwete asifanye hivyo? Narudia, hii hela ikilipwa serikali itaanguka.
AA, mi sina la kuongea ila msome huyo Rais wako wa awamu ya pili jinsi alivyokuwa mkweli na muazi:
KAMA kuna mtu katika Taifa letu ambaye anaamini kuwa Rais mstaafu na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Mapinduzi Benjamin Mkapa alikuwa kiongozi bora basi mtu huyo itampasa afungiwe jiwe la kusagia shingoni na "kwenda kutupwa Baharini".
Kama kuna yeyote ambaye anaamini kuwa mambo yanayosemwa juu ya uongozi wa Rais wetu huyo wa awamu iliyopita ni "wivu, chuki, masimango" binafsi dhidi yake basi na huyo naye tutamuongezea na jiwe la kukobolea.
Na iwapo kuna kundi la watu ambao wanaamini kabisa kuwa Tanzania ilifanya vizuri wakati wa Rais Mkapa na hivyo tujipange kwa kupiga magoti na kutoa shukrani zetu kwake basi kundi hilo na watetezi wa uongozi wa awamu ya tatu ningekuwa na uwezo ningehakikisha wanafutwa wote kwenye kitabu cha historia yetu.
Kwa karibu miaka miwili sasa nimekuwa nikiandaa ripoti yangu ya tatu ambayo itaangalia kwa undani ushahidi wa ubovu, uzembe, kutokuwajibika na mfano mbaya kabisa wa uongozi wa taifa wakati wa utawala wa Rais Mkapa.
Nitaangalia yale "mazuri" ambayo yanatajwa na kuonyesha kuwa ni uzuri wa mapambo tu ambao unaweza kusifiwa. Hata hivyo nikiwa nasubiri wakati muafaka wa kuitoa ripoti hiyo ikiwa ni baada ya zile mbili za kwanza (ile ya Matumizi ya Tanzania katika usafirishaji wa silaha haramu na ile ya Meremeta) nimeona niandike kwa namna ya makala tu kupinga utukuzaji wowote ule ambao umeanza wa utawala wa Rais Mkapa na zaidi kupinga jitihada zake za hivi karibuni kujaribu kutufanya wakosoaji wake tujisikie hatia kwani tunamuonea!
Ukweli na usemwe
Lengo langu si kudai kama baadhi ya wengine kuwa utawala wa awamu ya tatu haukufanya lolote. Kama nilivyoandika wakati wa suala la kupaa kwa ndege ya Lowassa ni kutokuwa mkweli kwa historia na dhamira kama kuna mtu atadai kuwa Serikali haijafanya lolote.
Mimi si mmoja wa wale waliofumba macho ambao hawaoni madaraja, barabara, mashule, zahanati, hospitali n.k ambazo zilijengwa chini ya utawala wa Rais Mkapa. Yeyote anayetaka kufuatilia mafanikio hayo anaweza kutembelea tovuti ya CCM ya ccmtz.org ambako anaweza kujisomea andiko la "mafanikio ya utawala wa awamu ya tatu -1995-2005".
Nitakuwa mjinga endapo nitaanza kubishana kama barabara ilijengwa au haikujengwa, daraja lilijengwa au halikujengwa, uwanja wa kimataifa wa mpira wa hadhi ya Kimataifa ulijengwa au la; Kama wahenga walivyosema "mwenye macho haaimbiwi tazama".
Hivyo, mgongano wangu na utawala wa Rais Mkapa siyo wa kitu gani kilifanyika au hakikufanyika hasa bali ni namna ya utawala wake ulivyotengeneza mazingira ya kifisadi ambayo leo sisi kama taifa tunayalipia gharama kubwa sana.
Mfumo wa Utawala wa kifisadi ulisimikwa chini yake
Jambo moja ambalo nina uhakika hakuna mtetezi yeyote Mkapa anaweza kusimama na kupinga ni ukweli kuwa Mfumo wa Utawala wa Kifisadi (MUK) ulipandwa wakati wa utawala wa Rais Mwinyi, lakini ulimwagiliwa, kupaliliwa, na kutiwa mbolea wakati wa utawala wa Mkapa. Leo hii katika utawala wa Rais Kikwete tunaanza kuvuna mavuno yake ya awali! Na bado hatujafikia hata nusu ya mbegu zilizopandwa!
Kutokana na maamuzi mbalimbali yaliyochukuliwa chini ya utawala wa Mkapa, mazingira yalitengenezwa ambayo yamefanya ufisadi kuwa ni mgumu kuushinda, yametoa kinga kwa mafisadi, na zaidi sana yamefungua mlango wa watawala kututawala wapendevyo.
Kuna mtu anabisha?
1996 - Sheria iliyounda Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS) na hivyo kwa mara ya kwanza kurasimisha shughuli za watu wa Usalama wa Taifa katika taasisi inayotambulika na kuongozwa na sheria na muundo wa kiutendaji.
Kati ya Sheria za Usalama wa Taifa duniani ya kwetu ni miongoni mwa sheria mbovu zaidi kabisa. Ni sheria iliyoweka mipaka ya ajabu kwenye idara hii na kuigeuza siyo idara ya usalama tena kama ilivyokuwa enzi za kina Mzena, Gama, Kombe na wengine waliolitumikia taifa hili. Kutumika kwa sheria hii kama nilivyoonyesha mara kadhaa huko nyuma kumechangia kwa kiasi kikubwa sana kwa ufisadi uliokubuhu kwenye taasisi zetu mbalimbali kiasi kwamba wapo wanaojenga hoja kuwa idara hii hutumika kama silaha ya kisiasa.
Mojawapo ya mambo ya ajabu kabisa katika sheria hii ni kuwakataza watu wa Usalama wa Taifa kutekeleza wao wenyewe jukumu la usalama na badala yake kuwa wakusanyaji, wachambuzi na habari za kiusalama na kijasusi na kutoa taarifa hizo kwa vyombo vingine (Ibara ya 2a) Yaani, wanaona mtu anaiba EPA, Richmond wanaingia, Dowans wanadanganya BRELA badala ya kuchukua hatua za kiusalama wao wenyewe wanabakia kwenda kuwaita Polisi. Rais Mkapa aliipitisha sheria hiyo Januari 20, 1997.
1997- Mwaka huu uliingiwa mkataba wa hatari sana kwa usalama wa taifa letu na ambao mrindimo wake tumeusikia miezi michache iliyopita ambapo Waziri Mkuu katika hali ya woga aliapa Bungeni kuwa hata kama wabunge wako tayari "kumsulubisha" na wamsulubishe lakini suala la Meremeta hatoligusa kwani ni kwa ajili ya "usalama wa taifa". Nimeonyesha katika ile ripoti yangu ni kitu gani hasa kilifanyika. Mkataba wa Meremeta uliingiwa chini ya Rais Mkapa! Mengine ambayo sikuyagusa kwenye ripoti ile yanasubiri wakati wake muafaka. Lakini leo wanataka tumshangilie!
1998 - Mwaka huo sheria mbili za ajabu kabisa ziliwahi kupitishwa na utawala wa Mkapa na wabunge wa CCM. Sheria hizi mbili ni kichocheo cha mfumo wa ufisadi katika sekta ya madini na vile vile ilitengeneza mwanya mkubwa wa maadili ya kiuongozi.
1997 kuanza kutumika kwa sheria ya Madini ya mwaka 1998 kulifungulia chini ya utawala wa Rais Mkapa uporaji mkubwa wa raslimali na utajiri wa nchi yetu. Kwa mara ya kwanza watawala wetu walitengeneza mfumo wa kufungua urithi wa watoto wetu kwa wageni kwa mtindo wa kuchota maji kisimani kama vile kisima ni chao. Utawala wa Rais Mkapa unaotaka kusifiwa leo kwa "uongozi bora" ulifungulia mlango wa "wawekezaji" kwa kile walichokiita "kuvutia uwekezaji" katika sekta ya madini.
Ndipo tukaona yaliyotokea katika sekta hiyo hadi kufikia suala la Buzwagi katika miezi ya mwanzo ya utawala wa Rais Mkapa. Migogoro mingi katika sekta ya madini na kile tunachokiita "mikataba mibovu" msingi wake ni sheria hii mbovu. Rais Mkapa aliipitisha kuwa sheria Julai 1, 1998.
1998 Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilipitishwa nayo mwaka huo huo na ilikuwa na lengo la kuweka maadili katika uongozi wa umma. Sheria hiyo ilikuwa inamhusu kuanzia Rais hadi wabunge. Lengo la sheria hiyo ilikuwa ni hatimaye kujaribu kuziba pengo la kile kilichofanywa kule Zanzibar walipoliua Azimio la Arusha na kuisigida miiko ya uongozi iliyoanishwa ndani ya Azimio lile. Cha kuudhi katika sheria hiyo ni kuwa yeye mwenyewe Rais Mkapa na aliyekuwa Mwanasheria wake Mkuu Andrew Chenge ninaamini walikuwa ni wa kwanza kuivunja sheria hiyo bila kujali matokeo yake (with impunity). Leo hii wanaendelea kunesanesa na hakuna mtu mwenye uthubutu wa kuwachukulia hatua.
Mkapa kwa kutumia nafasi yake na kuanza biashara akiwa Ikulu na uthubutu wake wa kutumia taarifa za ndani (inside information) kuhusu Kiwira na hatimaye kujiuzua mgodi huo yeye na Waziri wake wa Nishati. Kikatiba alitakiwa aondolewa madarakani wakati ule ule kwani Katiba inasema Rais anaweza kuondolewa endapo itathibitika amevunja sheria ya maadili. Lakini nani ana ubavu huo!?
Niseme nini tena; niendelee kuchambua jinsi utawala wa Mkapa ulitengeneza mfumo wa mafanikio ya utawala wa kifisadi? Nijadili sheria ya fedha ya 2001 na 2004? Niandike juu ya sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa ya 1999? Nizungumzie mfumo wao wa ubinafsishaji wa makampuni yetu? Nielezee kama marudio yaliyotokea NBC, Tanesco, Posta na Simu, na kwingine?
Nije nizungumzie yale tunayoyajua ya ufisadi katika Benki Kuu? Nirudi na kuchambua ajira ya Gavana Ballali? Nizungumzie uanzishwaji wa makampuni feki? Nielelezee kama kichaa mmoja jinsi utawala wake ulijitahidi kuua kila kizuri cha "kwetu" kwa kukimbilia cha "wageni" kwa vile wanataka kuja kutuokoa?
Mnataka nirudi kugusia yale yaliyotokea kwenye sekta yetu ya utalii, uwindaji na elimu? Kweli tunatakia kusahau haya yote na kushangilia uwanja wa mpira, daraja la Mkapa, na barabara tu?
Mnataka niseme kuhusu yale mabadiliko ya Katiba ya 2005 ambayo yalimtengenezea nafasi Lowassa ya kukaimu kiti cha Urais na kumuondoa Spika wa Bunge la Muungano? Mnafikiri hatukuyaona wakati ule? Mnataka tugusie ya Mwembechai na mauaji ya Pemba? Au mnafikiri nayo tumeyasahau?
Basi na wasimame watetezi wa Mkapa leo! Wasimame au asimame yeye mwenyewe kujitetea juu ya ya ufisadi uliokubuhu uliofanyika mbele za macho yake ambao ninadai ulitengenezwa kitaalamu na kuundiwa sheria mbalimbali ambazo zimeufanikisha!
Wanaotaka kumsifia wamsifie kwa madhara yao wenyewe; wanaotaka kucheza chioda na lizombe kumshangilia basi na wafanye hivyo! Wale wana CCM wanaotaka kumshangilia kuwa alikuwa ni kiongozi bora basi wafanye hivyo.
Lakini wakumbuke kuwa siyo wana CCM wote wamezugwa, siyo wananchi wote wamefumba macho na siyo vizazi vyote vitaaamini uongo hata upambwe kwa bendera, maneno ya ukali na vitisho vya madhara.
Ushauri wangu ni kuwa Mkapa aendelee kukaa kimya tu. Natoa hoja na watetezi wake wasimame sasa waseme au wanyamaze milele! Siku moja watasimama watawala kati yetu ambao watayafunua haya yote kwa wote kuona na ndipo tutakapojua kuwa uongo hata upambwe kwa saluti haugeuki kuwa ukweli!
Haya, niache kuandika kabla sijaambiwa "anapandikiza mbegu za chuki, dharau, na analeta mgawanyiko katika jamii"
Mwandishi wa makala hii ni amejitambilisha kuwa ni msomaji wa Changamoto