YAMETIMIA. Hatimaye safari ya serikali kuelekea makao makuu ya nchi imeanza. Ofisi za serikali zinaendelea kufungasha virago tayari kwa kuhamia katikati ya nchi.
Hatimaye, safari iliyopangwa takribani miaka 42 iliyopita, inaanza rasmi mwaka huu. Itakumbukwa mwaka 1973, Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza azimio la kuhamia Dodoma. Halmashauri Kuu ya chama ilipitisha azimio la kubadili makao makuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Jiji la Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Dodoma uliopo katikati ya nchi. Sasa watendaji na viongozi mbalimbali wanaendelea kufungasha mizigo yao tayari kwa kuaga Jiji la Dar es Salaam; ambao ndiyo mji muhimu na wa kwanza kwa biashara nchini.
Wakati ilidhaniwa kuhamia Dodoma ni suala lililobaki kuwa nadharia na mtaji wa kisiasa kutokana na ahadi zisizoisha, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Magufuli, imefanya kweli. Baada ya Magufuli kutangaza kuwa kabla ya kipindi chake cha uongozi cha miaka mitano kuisha, serikali itakuwa imehamia Dodoma, kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametangaza kuwa ifikapo Septemba atakuwa amehamia na ametaka wizara zote zimfuate.
Hii ni habari njema kwa mkoa huu na wenyeji wake; ambao kabila kuu ni Wagogo ambao inaelezwa kwamba, idadi yao inakaribia nusu ya watu katika mkoa huo. Wagogo wanapatikana kwenye wilaya tano kati ya saba za mkoa wa Dodoma. Wilaya zinazokaliwa na kabila hili ni Dodoma, Kongwa, Mpwapwa, Chamwino na Bahi. Kwa upande wa wilaya ya Kondoa, kabila lililoenea zaidi ni Warangi wakati wilaya ya Chemba kabila lililoenea zaidi ni Wasandawe.
Hata hivyo mkoa huu uliozungukwa na mikoa minne, unatajwa kuwa umejaliwa utajiri wa makabila mengine mengi yanayopatikana kwenye maeneo mbalimbali. Makabila hayo ni Wanguu, Wazigua, Wakaguru, Waburunge, Wahadzabe, Wamasai, Wabarbaig, Wasukuma, Wanyamwezi, Wafyomi, Wapare, Wachaga na Waasi. Mikoa inayopakana na mkoa huo wenye eneo la kilometa za mraba 41,311 ni Manyara (Kaskazini); Morogoro (Mashariki), Iringa (Kusini ) na Singida ulio Magharibi.
Kwa waliozoea joto la Dar es Salaam, waende wakifahamu mkoa wa Dodoma umeinuka hadi meta 1,040 kutoka usawa wa bahari na una wastani wa nyuzi joto 22oC. Mvua ni za msimu mmoja ambazo ni za wastani wa milimita 500 ambazo hunyesha kuanzia Desemba hadi Machi/Aprili. Miongoni mwa fursa za kilimo zilizomo mkoani humo, ni pamoja na uwekezaji katika kilimo, ufugaji na viwanda. Wenye maono ya kuwekeza, wanaweza kujikita kwenye kilimo lakini kinacholenga mazao yasiyotegemea mvua.
Kwa jumla Dodoma haina mvua nyingi isipokuwa sehemu za wilaya za Mpwapwa na Kondoa. Hivyo mazao yasiyotegemea sana mvua yanayolimwa ni mtama na muhogo. Pia uwele, karanga, alizeti, ufuta na mazao ya jamii ya mikunde yanastawi. Dodoma ni pia kitovu cha uzalishaji wa zabibu zinazotengeneza mvinyo hapa nchini. Zabibu ambalo ni zao lililoanza kulimwa kibiashara miaka ya 1970 na 1980, ni miongoni mwa mazao ambayo yanatajwa kuwa na faida kubwa yakizalishwa kitaalamu kwa kuzingatia kilimo cha kisasa.
Zao hili limeupaisha mkoa kutokana na kupatikana zaidi humo kiasi cha kuwa kitovu cha uzalishaji wa mvinyo. Lakini usindikaji wa mazao hayo ya kilimo, mazao ya mifugo na asali ni fursa nyingine inayopatikana. Fursa nyingine iliyopo ni ufugaji wa wanyama mbalimbali.
Mkoa huu unatajwa kuwa wa tatu nchini kwa kuwa na mifugo mingi hususan ng’ombe na mbuzi. Hata hivyo kutokana na mifugo kudaiwa kuongeza mmomonyoko wa ardhi katika maeneo mbalimbali mkoani humo, wale wanaopanga kufuga wanapaswa kuendesha shughuli hiyo kisasa.
Biashara na shughuli nyingine zihusuzo usafirishaji pia zina nafasi kufanyika kwa kuzingatia kwamba, mkoa huu una mawasiliano mazuri ya barabara za lami kuanzia mji wa Dodoma kwenda Morogoro, Dar es Salaam, Iringa, Mwanza, Arusha na hata nchi jirani za Rwanda na Kongo. Reli ya Kati ambayo inatarajiwa kuboreshwa kwa kiwango cha ‘standard gauge’ kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza ikipita Dodoma ni fursa nyingine ya kiuchumi na kijamii.
Dodoma ilikotoka Mkoa huu wenye idadi ya watu wapatao 2,083,588 (kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012), jina lake linaelezewa kwa simulizi mbalimbali. Lakini simulizi ambayo imekubalika na wengi ni hii: Tembo alikuja kunywa maji katika Kijito cha Kikuyu na akakwama matopeni. Baadhi ya wenyeji waliomwona walipiga mayowe na kusema ‘yadodomela’ ambayo kwa lugha ya Kigogo maana yake ‘amezama’.
Inaelezwa kwamba, tangu wakati huo, mahala hapo pakawa panajulikana kama Idodomya kwa maana ya kwamba ‘ mahali alipozama yule tembo’. Ingawa haijulikani ni lini jina lilianza kutumiwa, inakisiwa kwamba lilianza tangu mwaka 1860 huku mpelelezi wa kizungu, Henry Stanley akihusishwa. Anatajwa kwamba alipitia sehemu hiyo mnamo mwaka 1874 na kuita eneo hilo Dodoma. Inasisitizwa kwamba, hakuna kumbukumbu ya kimaandishi ya zamani zaidi kuhusu jina hilo lilivyopatikana.
Mwaka 1890 Utawala wa Kijerumani uliingia mkoani Dodoma. Na miaka 18 baadaye yaani mwaka 1912, eneo la Dodoma likawa eneo la Utawala wa Wilaya. Mji wa Dodoma ukiwa makazi ya kudumu, ulianzishwa mnamo mwaka 1910 kwa ujio wa reli Kuu ya Kati ambayo iliufanya ukue. Dodoma ilianzishwa wakati wa ukoloni wa Kijerumani kama kituo chenye reli ya kati na karakana ya reli.
Tangu 1912 imekuwa makao makuu ya mkoa. 1913 Dodoma ilikuwa na posta, simu, hoteli na maduka 26 ambayo moja lilikuwa la Mzungu na mengine ya Wahindi na Waarabu. Kabla ya Tanganyika kupata Uhuru, mkoa huu ulikuwa sehemu ya Jimbo la Kati kabla ya mwaka 1963 kugawanywa na kupatikana mikoa ya Dodoma na Singida. Ulianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na.450 la Septemba 27, 1963. Awali ulikuwa na wilaya tatu za kiutawala ambazo ni Dodoma, Kondoa na Mpwapwa.
Mabadiliko ya kwanza yalifanyika mwaka 1973 ambayo Wilaya ya Dodoma iligawanywa na kuwa Dodoma Mjini na Dodoma Vijijini. Aidha, mwaka 1995, wilaya ya Mpwapwa iligawanywa na kuwa wilaya mbili za Mpwapwa na Kongwa. Mwaka 2005, wilaya ya Dodoma Vijijini nayo iligawanywa na kuwa na wilaya mbili za Bahi na Chamwino. Vile vile mwaka 2010, wilaya ya Kondoa iligawanywa na kupata wilaya za Kondoa na Chemba.
Pamoja na wilaya zake saba, una tarafa 28, kata 190 na vijiji 540 vilivyoandikishwa kisheria Kwa ujumla, hii ndiyo Dodoma; ambayo umaarufu wake kisiasa ulichagizwa na Bunge kuendesha vikao vyake vyote humo. Sasa inaendelea kung’ara hususani pale Ikulu halisi ya rais sanjari na taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo wizara zitakapohamia na kuuacha mji wa Dar es Salaam kubaki kuwa mji mkuu wa biashara.