Kalamu Yenye Siri ya Damu

Kalamu Yenye Siri ya Damu

NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069279

SEHEMU YA 12

Lengo lake kubwa la kwenda katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lilikuwa ni kuonana na mwanaume aliyeitwa kwa jina la Richard, alihitaji kumuona mtu huyo kwani alikuwa akisifika kwa kila mwanamke aliyekuwa akimfahamu.
Alirudi huko, kama kawaida akakutana na kijana ambaye alionana naye na kuhisi alikuwa Juma Hiza, alipomuona tu kama kawaida yake akamfuata kwa lengo la kuzungumza naye kwani siku hiyo alikuwa peke yake, hakuwa na wale wasichana.
Aliposimama mbele ya kijana huyo, akayainua macho yake na kumwangalia, alikuwa kijana yuleyule wa jana yake ambaye alimuita jina ambalo hakulifahamu, leo alimfuata kwa lengo la kutaka kuzungumza naye.
“Nataka tuongee,” alimwambia huku akimwangalia.
“Kuhusu nini?”
“Utajiri....mapesa mengi tu...utakuwa tayari kunisikiliza?” alijibu Chilo na kukaa pembeni yake.
“Kuna mtu asiyetaka kusikia habari ya mapesa?” aliuliza Miraji na kutoa tabasamu pana.
Chilo akaanza kuongea naye kuhusu lile alilokuwa amemfuatia chuoni hapo, Miraji alikaa kimya huku akimsikiliza mwanaume huyo, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, mipango alivyokuwa akiipanga ilionyesha kabisa hakuwa mtu wa kawaida, kichwa chake kilikuwa na mambo mengi mno.
Mpaka anamaliza, Miraji alikaa kimya, hakuzungumza kitu chochote kile, alikuwa akimwangalia mwanaume aliyekuwa pembeni yake huku kichwa chake kikiwa na maswali lukuki yasiyokuwa na majibu yoyote yale.
“Ulipata muda gani kuyajua haya yote?” aliuliza Miraji huku akimwangalia.
“Nafikiri umekutana na mtu mwenye akili kubwa tu,” alijibu Chilo na kuanza kucheka.
Kukubali kwa Miraji kulimpa Chilo matumaini makubwa ya kwenda kufanikiwa suala lake lililokuwa mbele yake, muda wote uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, aliamini kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ni lazima kufanikiwa kwa kile alichokuwa amekitaka.
Walizungumza mambo mengi na kubwa zaidi aliloambiwa na Miraji ni kutafuta mastaa ambao wangewezesha kuutangaza ukurasa wake wa hadithi huko Facebook ambapo alipenda sana kuona safari yake ikiwa inaanzia hapo.
Kwenye kumshauri huko akamwambia lingekuwa jambo zuri kama angekutana na msichana aliyejulikana kama Video Vixen na baadaye kujiingiza kwenye muziki, msichana huyo aliitwa Natasha (Umemsoma kwenye Dili la Dola Bilioni Nne).
Kumpata Natasha halikuwa jambo jepesi, muda mwingi msichana huyo hakuwa akionekana chuoni hapo, alikuwa na mambo mengi nje ya masomo yake, Chilo alipata kazi kubwa ya kumtafuta mpaka kuonana naye, ilimchukua mwezi mzima.
Alisimama mbele ya msichana huyo aliyeonekana kuwa na furaha tele, walikuwa canteen na hakujua alikuwa akifurahia jambo gani, pembeni yake alikuwa msichana mmoja mrembo, na kwa mbali alibahatika kumuona yule Richard akiondoka zake, alitoka kwenye meza ile aliyokaa Natasha na rafiki yake.
“Samahanini!” alisema Chilo huku akimwangalia msichana huyo.
“Bila samahani!”
“Nilikuwa nahitaji kuzungumza na wewe kidogo!” alisema Chilo huku akimwangalia Natasha.
“Kuzungumza na mimi? Kuhusu nini?” aliuliza msichana huyo, alitoka kuongea na Richard, mwanaume aliyekuwa akijulikana kwa sura nzuri, baada ya kuondoka, sasa alikuja mtu kama Chilo, alibaki akishangaa, yaani ilikuwa ni sawa na kumaliza kula pilau lililokuwa na nyama ya kuku, kachumbari na mchuzi mzito halafu ukaletewa sahani ya ugali na mlenda.
“Kuhusu kitu kidogo tu!”
“Kipi? Naomba nitafute muda mwingine!” alisema msichana huyo, alikuwa na nyodo kupita kawaida.
Yeye na rafiki yake wakasimama na kuanza kuondoka mahali hapo, Chilo alikasirika moyoni mwake lakini hakuwa na cha kufanya kwa kuwa kukubali kuongea naye ama kukataa yalikuwa ni maamuzi ya mtu binafsi.
Kwa kuwa hakuwa mwanafunzi wa hapo chuoni, akawasiliana na Miraji na kumwambia kuhusu msichana huyo, kwenye mipango yao mingi ilikuwa ni lazima na huyo apitishwe kwani kupitia jina lake aliamini akaunti yake ingekuwa na wasomaji wengi na hivyo kupata jina zaidi mitandaoni.
Miraji akapewa kazi ya kumtafuta msichana huyo na kuzungumza naye. Kila siku hiyo ndiyo ilikuwa kazi yake, alipokuwa akifika chuoni, mtu wa kwanza kumtafuta baada ya masomo alikuwa huyo Natasha, lilikuwa jambo gumu kumpata kwani si muda wote alikuwa akija chuoni na alipokuwa akienda basi alionekana kuwa bize sana.
Baada ya wiki kama mbili ndipo Miraji akafanikiwa kuonana na msichana huyo, akamsimamisha na kumwambia alihitaji kuzungumza naye kidogo, akamruhusu, alichomwambia ni kwamba kulikuwa na rafiki yake alihitaji sana kuzungumza naye, hivyo alihitaji kuonana naye.
“Ni nani?” aliuliza Natasha.
“Anaitwa Chilo!”
“Ndiye nani na anataka kuongea nami kuhusu nini?” aliuliza maswali mawili mfululizo.
“Ni mwandishi wa vitabu vya simulizi!”
“Sawa! Ila nafasi yangu ni leo tu, akinikosa leo mpaka mwezi ujao,” alisema msichana huyo.
Miraji akampigia simu Chilo na ndani ya dakika chache akafika chuoni hapo na kuanza kuzungumza naye, alimwambia kuhusu suala lake, alihitaji kutangaziwa kurasa zake za mitandaoni, alihitaji kuona akipata wafuatiliaji wengi wa simulizi zake.
“Sawa! Nitakusaidia kwa sababu mwanachuo mwenzangu!” alimwambia, hakujua kama Chilo hakuwa mwanachuo.
“Sawa!”
“Ila mpaka nipate ruhusa!”
“Ya nani tena?”
“My baby! Richard!” alijibu kwa maringo kidogo.
Walibadilishana namba za simu na baada ya hapo wakaagana, kazi ikawa kwenye kutafutana tu. Chilo akawa anapiga simu mara kadhaa lakini haikuwa ikipokewa, hilo lilimkasirisha lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kuendelea kumtafuta msichana huyo kwa kuwa alikuwa msaada mkubwa kwake.
Zilipita wiki mbili nyingine, akampigia simu, ikapokewa na rafiki yake Natasha na kuomba kuongea naye, alichomwambia ni kuwa asingeweza kwa kuwa alikuwa kwenye matatizo makubwa mno kipindi hicho.
“Matatizo gani?” aliuliza.
“Wewe jua makubwa!”
“Ila naweza kumsaidia!”
“Hutoweza!”
“Niamini! Nitaweza,” alisema na msichana huyo kuomba kuonana naye huko Sinza.
Hakuchukua dakika nyingi akakutana na rafiki yake huyo ambaye alimchukua mpaka alipokuwa akiishi Natasha, alipofika na kumwangalia tu akajua msichana huyo alikuwa kwenye matatizo makubwa, akaomba kuzungumza naye, asimfiche na yeye angejua ni kitu gani alitakiwa kufanya.
“Picha zangu za utupu zimevuja,” alisema msichana huyo huku akifutafuta machozi yake.
“Zimevujaje?” aliuliza Chilo.
“Yaani sijui! Nimepigiwa simu na mtu na kuambiwa ana picha zangu za utupu! Mungu wangu nitafanya nini wenyewe wakijua?” aliuliza msichana huyo huku akilia.
“Wenyewe akina nani?”
“Wewe jua wenyewe tu!”
Hakutaka kumwambia kuhusu hao wenyewe ambao mkasa mzima uliandikwa kwenye kitabu cha Dili la Dola Bilioni Nne. Chilo hakutaka kujali sana lakini alihisi kabisa kulikuwa na mtu ambaye alihusika kwenye tukio hilo la kuvujisha picha hizo.
“Lakini simu si ilikuwa yako! Kuna mtu ulimpa?” aliuliza huku akimwangalia.
“Hakuna!”
“Sasa ilikuwaje mtu aidukue iPhone? Hicho ni kitu kisichowezekana kabisa,” alimwambia.
“Sasa amezipataje hizo picha?” aliuliza Natasha, yaani alichanganyikiwa.
“Kwani hukuwahi kumpa mtu simu yako?”
“Hapana!”
“Si kweli! Hebu kumbuka!”
Natasha akakaa kimya na kuanza kukumbuka kama aliwahi kufanya kitu kama hicho, hapo ndipo alimkumbuka Richard, alikuwa mwanaume pekee ambaye alimpa mpaka namba ya siri ya akaunti ya iCloud.
Japokuwa alikumbuka hivyo lakini bado hakuamini kama Richard angeweza kufanya jambo kama hilo, yaani alimpenda mno kiasi kwamba alihisi kumuhisi kwenye ubaya namna hiyo ilikuwa ni sawa na kumuonea.
“Nilimpa mpenzi wangu tu!”
“Basi ndiye aliyefanya hivyo!”
“Haiwezekani!”
“Hebu niambie zaidi kuhusu huyu Richard, nadhani anajua kila kitu!” alimwambia.
Natasha akaanza kumwambia Chilo kuhusu Richard. Hakujua ni kwa sababu gani alimwamini kwani kwa muda huo alihitaji kuufahamu ukweli tu, alichukua dakika kadhaa kusimulia kila kitu, halafu akanyamaza.
“Sasa huo upenzi wenu upo wapi?” aliuliza Chilo baada ya kusikia simulizi yake.
“Kivipi?”
“Siku zote hizo hamkuwahi kufanya mapenzi! Inawezekana vipi?” aliuliza.
“Aliamua tu!”
“Na nikisema Richard alitumwa kuwa na wewe utasemaje?”
“Alitumwa na nani?”
“Sijajua! Ila nahisi alitumwa.”
“Kivipi?”
“Kwa sababu wewe ni staa, hivyo watu wanakuwinda, wanataka kujua mengi kuhusu wewe, hizo picha na mambo mengine! Hebu leo tujifanye kama FBI, tuanze kumfuatilia huyu Richard, kama utashindwa, naiomba kazi hiyo! Kuna mengi nataka kuyafahamu kuhusu huyu mtu,” alisema Chilo huku akimwangalia Natasha ambaye ni kama hakuwa akielewa kilichokuwa kikiendelea.
“Umfuatilie?”
“Yeah! Nisaidie kwa hilo, nadhani nikijua machache kuhusu yeye, basi naweza kuandika moja ya kitabu bora kabisa,” alimwambia.
“Kuandika kitabu tena?” aliuliza msichana huyo huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo!”
“Kitabu kuhusu nini?”
“Mambo mengi likiwemo la hii sura ya Richard inayowachanganya wanawake, inayokuchanganya mpaka uhisi hawezi kukufanyia ubaya wowote ule,” alijibu Chilo huku akiachia tabasamu kama kawaida yake.
“Sawa haina shida.”
“Ila utatakiwa kulipia!”
“Kivipi?”
“Kutangaza ukurasa wangu wa Facebook! Unaitwa Simulizi za Chilo!” alimwambia.
“Haina shida, ila nitahitaji unipe matokeo baada ya uchunguzi wako,” alimwambia.
“Haina shida.”
Chilo akaondoka mahali hapo, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alijiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu yoyote yale, alichohisi ni kwamba Richard alihusika kwenye ishu ya zile picha na hakujua alitaka nini mpaka kuchukua hizo picha.
Kesho yake akaenda chuoni na kuanza kumfuatilia Richard kwa siri sana, mara nyingi aliwaona akiwa na marafiki zake wawili, Robinson na Robert. Akahisi watu hao walikuwa pamoja kwenye kutekeleza yale mambo waliyokuwa wakiyafanya.
Alihitaji kuwajua zaidi watu hao wawili, hasa marafiki zake. Akaulizia kwa watu na kuambiwa kwamba huyo Robinsin alikuwa mtaalamu wa mambo ya kompyuta na huyo Robert kichwa chake kilikuwa hatari kwa kupanga mipango, hasa mambo ya biashara.
Chilo akajiongeza, suala la Natasha likaanza kumrudia kichwani kwa mara nyingine, akahisi inawezekana huyo Robinson ndiye aliyefanya mpango wa kuchukua picha kutoka kwenye simu ya msichana huyo. Yaani baada ya Richard kuchukua namba ya siri ya akaunti ya iCloud, Robinson akafanya mpango wa kuingia kwenye simu hiyo.
“Mh! Kama ni hivi! Hawa watu hatari sana, acha niendelee kuwafuatilia,” alisema.
Aliwafuatilia, baada ya siku kadhaa kwenye ufuatiliaji wake akamuona Richard akiondoka kuelekea Mwenge, hakutaka kubaki, alimfuatilia mpaka pale alipoingia chooni na kutoka huku akiwa na mavazi mengine ambayo yalimfanya kuonekana kama mtu wa mitaani, aliyepigwa na maisha.
Aliendelea kumfuatilia mpaka alipokwenda karibu na kituo cha mafuta cha TSN na kuingia kwenye mtaro mmoja. Chilo alibaki akishangaa, kile alichokuwa akikiona hakuweza kuyaamini macho yake, ilikuwaje Richard aingie humo? Alikuwa na jambo gani?
Hakutaka kuondoka, alibaki mahali hapo huku akiangalia ni kitu gani ambacho kingeendelea. Baada ya dakika chache akamuona Richard akitoka huku akiwa na mfuko ambao hakujua kwa ndani kulikuwa na nini.
“Hapana! Hapa kuna kitu!” alijisemea.
Hakutaka kumfuatilia, alichokifanya ni kuanza kuufuatilia mtaro ule kwa macho tu kwani kama angetaka kwenda kule alihisi kungekuwa na tatizo, aliufuatilia mpaka mahali kulipokuwa na pipa, akatulia kuona ni kitu gani kingetokea.
Baada ya dakika kadhaa akawaona wanaume wawili wakikimbia kuelekea kwenye pipa lile, wakaangalia ndani, kila mmoja alionekana kuchoka, haraka sana wakakimbia huku wakionekana kuwa na hasira, wakaanza kumtafuta mtu ambaye aliwachokoza lakini hawakupata kitu.
Baada ya kuona watu wale wameondoka, Chilo akaelekea kwenye pipa lile, macho yake yakatua kwenye karatasi nyingi kama uchafu, akazitoa ili kuangalia kulikuwa na nini, macho yake yakatua kwenye tundu kubwa lililokwenda mpaka kwenye mtaro, akabaki akishangaa.
Akapata picha kwamba ndani ya pipa lile kulikuwa na mfuko ambao Richard aliuchukua kwa siri, hakuuchukua kwa kulifuata lile pipa, bali alikwenda kule kupitia mtaro, bila shaka aliogopa kuonekana na watu wale waliokuwa wamesimama mbali muda mfupi uliopita.
“Kile ni kitu gani? Alibeba nini? Ni cha hawa watu ama cha nani? Kwa nini alitumia mtaro kwenda kukifuata?” alijiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu yoyote yale.
(Kufuatilia tukio lote hilo lilivyokuwa, limeandikwa kwa undani katika Kitabu cha Dili la Dola Bilioni Nne)

Je nini kitaendelea?
 
NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269

Sehemu ya 13

Chilo hakutaka kuacha kufuatilia kuhusu Richard, moyo wake ulikuwa na furaha kwa kuwa aliamini huyo Richard alikuwa na akili kubwa ama alikuwa akiambatana na watu waliokuwa na akili hiyo.
Akaondoka na kuelekea nyumbani kwake, alipofika, akatulia kwenye kochi huku akiwa na kidaftari chake ambacho baada ya kujifikiria kwa dakika moja, akaandika maneno machache tu yaliyosomeka ‘DILI LA DOLA BILIONI NNE’
Alipenda kwa jinsi hali ilivyokuwa, yule Richard na wenzake walizidukua picha za utupu za Natasha, mbali na hivyo pia akamuona mwanaume huyo akienda sehemu kupitia mtaroni na kuchukua mfuko ambao aliamini ndani yake kulikuwa na pesa.
Moyo wake ulikuwa na chachu ya kuandika kitu kuhusu tukio hilo, alilifurahia mno lakini pia ilikuwa ni lazima aendelee kufuatilia kile ambacho kingetokea baada ya hapo.
Baada ya siku kadhaa akarudi chuo kikuu na kukuta kitu ambacho hakuwa akikielewa kabisa iliwezekana vipi. Akaambiwa kulikuwa na jambo lililomshtua kila mmoja, yaani msichana aliyekuwa na sura mbaya kuliko wote aliingia kwenye mapenzi na mvulana aliyekuwa na sura nzuri kuliko wote.
“Miraji! Unamaanisha nini?” alimuuliza huku akimwangalia.
“Unamfahamu Upendo?” aliuliza.
“Hapana!”
“Yule demu niliyekwambia ni mtoto wa kishua ila ana sura mbaya kama sokwe!” alimwambia.
“Yeah! Nakumbuka uliniambia!”
“Sasa bwana....”
“Kuna nini?”
“Eti anadate na Richard,” alimwambia.
Chilo alivyoambiwa hivyo akashtuka, picha ya Natasha ikaanza kuja kichwani mwake, akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Huyo Richard alitakiwa kuogopwa, kwa kutumia sura nzuri aliyokuwanayo alikuwa akiwadanganya wasichana na kuwatumia alivyotaka.
Kwa yeye kuwa na Upendo alihisi kulikuwa na kitu fulani, hakutaka kutulia, ilikuwa ni lazima kufuatilia jambo hilo kwa ukaribu zaidi. Na kweli alifanikiwa kuwaona wawili hao wakiwa pamoja, wakiyafurahia maisha huku watu wengine wakishangaa kile kilichokuwa kikiendelea.
“Natamani nijue kuna jambo gani!” alisema Chilo.
Kwa kipindi hicho Richard hakuwa na marafiki zake, hawakuwa wakionekana, walipotea, chuoni hawakuwa wakifika. Chilo alijitahidi sana kuwatafuta kila kona lakini hakufanikiwa (Ukisoma kitabu cha Dili la Dola Bilioni moja, kipindi hicho walikwenda nchini Kenya kushughulika na picha za tukio la ubakaji)
Aliamini kabisa kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea lakini hakugundua kulikuwa na kitu gani, moyo wake uliamini kulikuwa na mchezo mmoja hatari uliokuwa ukichezwa, alitamani kuufahamu lakini kichwa chake hakikugundua lolote lile.
Hakutaka kufuatilia tena, akaishia hapo na kurudi nyumbani. Alimpigia simu Miraji na kumwambia alitakiwa kujiandaa kwani baada ya miezi sita kuanzia hapo mpango wao ungetiki hivyo alitakiwa kukariri kila kitu ambacho alimwambia akariri.
Hapakuwa na tatizo, alipomalizana naye akampigia simu Juma Hiza na kutaka kuonana naye, ni ndani ya saa mbili, wawili hao wakaonana na kumwambia sasa ulikuwa ni wakati wa kuandaa kitabu hicho, alikuwanacho, alijitahidi kuandika kila aina ya codes kuhakikisha kinakaa sawa, kwa maana hiyo baada ya siku kadhaa angekiweka kwenye Mtandao wa Amazon kwani tayari alifanya kila aina ya mchakato.
“Kwa hiyo nitaitwa Williams?” aliuliza.
“Yeah! Kila kitu kitabadilika. Baada ya hapo, tukishatumiwa pesa, tunazihamisha na kuzileta kwenye akaunti zetu! Ila utatakiwa kukariri kila kitu nilichokwambia, yaani kariri hasa,” alisema Chilo.
“Sawa haina shida.”
Baada ya hapo, yakatokea yote hayo yalitotokea.
***
Kaburi, Afghanistan

Omar alibaki kimya, alimwangalia Miraji aliyekuwa mbele yake ambaye alimwambia yeye ndiye Juma Hiza kutokana na wawili hao kuwa mapacha. Hakujua ni nani alikuwa mkweli, kama ni Wamarekani ama kijana aliyekuwa mbele yake.
Kwa jinsi walivyokuwa, wawili hao walionekana kama mtu mmoja, walifanana kwa kila kitu. Alichokifanya ni kuwaambia vijana wake wamchukue kwani kulikuwa na kitu alichotaka kufanya.
Akachukuliwa na kupelekwa sehemu iliyokuwa ya wazi, akawaambia watafute kamera kwani alikuwa na ujumbe aliotaka kuwapa Wamarekani, walimpata mtu waliyeamini alikuwa Juma Hiza hivyo walitaka kufanya kila kitu walichotaka kufanya, hasa kuendeleza ugaidi nchini Marekani.
Kamera ikatafutwa na kuanza kuzungumza. Aliwaambia Wamarekani kwamba walitakiwa kujiandaa kwani kulikuwa na milipuko kadhaa ambayo ingetokea, na hiyo ilikuwa ni sababu ya kuwa na mtu ambaye waliamini alikuwa na akili kuliko binadamu mwingine yeyote yule.
Walimwamini Miraji, walitaka kumtumia kama daraja kufanikisha mipango yao. Omar alizungumza mbele ya kamera kwa kuwatisha Wamarekani kwamba sasa ulikuwa ni muda wao wa kuwapiga mpaka wakome.
Alitamba mbele ya kamera kwa dakika kumi na baada ya kumaliza, akamchukua Miraji na kuelekea naye ndani ya chumba kile kwa lengo la kuzungumza naye zaidi kuhusu mipango waliyotaka kufanya kuhakikisha Wamarekani wanalia.
“Nataka kuilipua Marekani,” alisema Omar huku akimwangalia Miraji.
“Haina shida. Unataka kulipua sehemu gani?” aliuliza Miraji.
“Daraja la Brooklyn!”
“Hapana! Hapo utakuwa unajisumbua tu, hutoweza kuua watu wengi,” alimwambia huku akimkazia macho.
“Kwa sababu gani?”
“Utaua watu ishirini tu, kwa kundi kama Al Qaida kumaliza watu ishirini ni jambo la kipumbavu sana,” alimwambia, alikuwa upande wao.
“Kwa hiyo unataka tufanye nini? Tulipue wapi?”
“Kwa nini tusilipue Chuo Kikuu cha Brooklyn?” aliuliza.
“Unahisi itawezekana?”
“Kabisa! Itawezekana!”
“Nipe mbinu.”

Je, nini kitaendelea?
 
NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269
Sehemu ya 14

Miraji akaanza kuongea naye juu ya namna ya kulipua chuo hicho. Alimwambia kulikuwa na wanafunzi zaidi ya elfu ishirini na nane, lingekuwa jambo zuri kulipua na kuwamaliza hata wanafunzi elfu kumi tu.
Kwa nchi kama Marekani lingekuwa jambo la kuhuzunisha mno, kila mtu angelia na kwenye mitandao, televisheni, magazeti, kote huko kungekuwa na taarifa kwamba Al Qaida walifanya mambo yao, kundi lilirudi kwa kasi baada ya kifo cha Osama Bin Laden.
Mpango ulisukwa na Miraji ndani ya chumba hicho, alimwambia kila kitu na kumuonyesha baadhi ya maandiko kwenye kitabu kile, kwa jinsi alivyomuelezea Esta, jinsi alivyokutana na hao magaidi hapo Brooklyn ilikuwa ni alama ya kuwaonyesha kwamba hiyo ndiyo sehemu waliyotakiwa kuilipua.
“Safi sana!”
“Wasiliana na watu!”
Haraka sana mawasiliano baina ya kijana wa Omar aliyekuwa hapo Kabul na jijini New York yakaanza kufanyika, hayakuwa mawasiliano ya kawaida kwani waliogopa kudukuliwa na kugundulika kwamba walikuwa na mpango wa kuilipua Marekani.
Abdallah Issa alikuwa akiishi Brooklyn jijini New York nchini Marekani. Yeye na vijana wengine walikuwa wakifanya kazi chini ya kundi la Al Qaida lakini hawakuwa wakifahamika na mtu yeyote yule.
Shirika la Kipelelezi la FBI yaani Federal Bureau of Investigation lilifanya kazi kubwa kuwabaini watu hao lakini ilishindikana. Walijua kabisa ndani ya ardhi ya Marekani kulikuwa na Waarabu ambao walikuwa wakifanya kazi chini ya kundi hilo la kigaidi lakini hawakujua ni mahali gani watu hao walipatikana.
Kitendo cha kuibuka kwa gaidi aliyejulikana kwa jina la John iliwachanganya sana. Kijana huyo alikuwa wa Kizungu aliyekuwa akiishi hapohapo Marekani, alilipua katika kituo cha treni na kuua mamia ya watu na kufanikiwa kutoroka na kuelekea nchini Afghanistan.
Hilo likawafanya kugundua kwamba si Waarabu waliokuwa magaidi, na ugaidi haukuwa na dini kama walivyokuwa wakihisi kipindi cha nyuma, likazidi kuwapa ugumu kwani iliwafanya kuamini kwamba inawezekana kabisa kulikuwa na Wazungu waliokuwa wakifanya ugaidi na kushirikiana na kundi hilo.
Abdallah alikuwa mhimili mkubwa wa Al Qaida nchini Marekani, baada ya kupigiwa simu na Omar na kuambiwa kulikuwa na chuo walitakiwa kukilipua, haraka sana akawasiliana na vijana wake na kuonana nyumbani kwake.
Wakakaa na kupanga mipango, ilikuwa ni lazima kijana mmoja aende kujilipua kama kawaida, aue watu wengi. Walidanganywa kwamba wanapojitoa mhanga kwa kujilipua Mungu alikuwa akifurahia, watakapokufa basi wangekwenda peponi na kukaa na mitume, wafutwe machozi na kupongezwa kwa kazi nzuri waliyokuwa wameifanya duniani, kuua watu wasiokuwa na hatia yoyote ile.
Mafundisho waliyokuwa wakipewa yaliwaingia mioyoni mwao, walijiona kufanya jambo sahihi na kuona Mungu aliruhusu kujitoa mhanga na kuwamaliza watu wengine, hawakujali kwamba miongoni mwa watu waliokuwa wakiwaua kulikuwa na Wakristo, Waislamu, weusi, Wazungu, walichokuwa wakikijali ni kusimamia kile walichokuwa wameambiwa.
“Ten thousand souls will take you to our almight Allah...” (Roho elfu kumi zitakuchukua na kukupelekwa kwa Mungu wetu mkuu) alisema Abdallah huku akiwaangalia vijana hao aliowaita ambapo mmojawapo alitakiwa kuvaa bomu na kwenda kujilipua.
“Allah Akbar...” (Mungu mkubwa..) walisema kwa lugha ya Kiarabu.
Baada ya kuzungumza nao, simu ikapigwa mpaka kwa mwanaume aliyeitwa kwa jina la Mike Castro, Mzungu aliyekuwa akiichukia Marekani kuliko nchi yoyote ile japokuwa naye alizaliwa na kukulia nchini humo.
Mwanaume huyu alikuwa mwanabailojia, alikuwa na utaalamu mkubwa wa kutengeneza dawa na hata mabomu kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu. Alikuwa akitumika na Waarabu kwa siri kuwamaliza ndugu zake.
Alilichukia taifa hilo kutokana na uonevu aliokuwa amefanyiwa, alitengeneza dawa ya magonjwa ya kansa lakini bahati mbaya formula yake ikaibwa na mtu mwingine na hata alipofungua kesi, hakuonekana kuwa mkweli, mwanaume aliyemuibia, akashinda kesi na bahati nzuri kwake dawa hiyo haikuwahi kufanya kazi, kansa iliendelea kusumbua.
Kuanzia siku hiyo hakutaka kusikia kuhusu Marekani, alilichukia taifa hilo kwa kuwa aliona lilijaa uonevu mkubwa, hicho ndicho kitu kilichopelekea kuamua kushirikiana na Waarabu kuwamaliza ndugu zake bila kujali lolote lile.
Baada ya dakika kadhaa Mike akafika nyumbani hapo na kupewa kazi ya kutengeneza bomu. Kwake, hilo halikuwa tatizo hata kidogo, akaanza kutengeneza bomu hilo na kuliweka kwenye nguo ambayo ilitakiwa kuvaliwa na mwanaume aliyekuwa na jukumu la kwenda kujitoa mhanga.
Alitumia saa tatu kutengeneza na baada ya hapo akaliweka kwenye nguo hiyo hivyo kusikiliza simu kutoka kwa Omar ambaye angewasiliana na Miraji kujua ni muda gani ungekuwa sahihi kufanya mlipuko huo.
Wakati simu inaingia, Omar alikuwa chumbani mwake akisoma kitabu kile kilichoonekana kuandikwa na mwanaume aliyejulikana kwa jina la Williams, kumbe kiliandikwa na Juma Hiza ambaye aliamini ndiye huyo aliyekuwa mbele yake.
Simu haikuita sana, akaipokea na kuipeleka sikioni, sauti ya Abdallah ikaanza kusikika kutoka upande wa pili. Alichomwambia ni kwamba kila kitu kilikuwa tayari hivyo alitakiwa kumwambia ni wakati gani alitakiwa kwenda kukilipua chuo hicho.
“Subiri...” alimwambia, akamwangalia Miraji.
“Muda gani tukalipue?” aliuliza.
“Mchana! Majira ya saa saba ndipo kunakuwa na watu wengi,” alimwambia, naye akamwambia Abdallah.
Kwa sababu ilikuwa ni usiku kwa nchini Marekani hakutaka kujali sana, wakasubiri mpaka siku iliyofuata ambapo majira ya saa sita, tayari kijana wake, Said alishajivisha nguo iliyokuwa na bomu kwa ndani na kuanza kwenda kwenye chuo hicho.
Njiani ndani ya gari alionekana kuwa na hofu tele, hakuamini kama alikuwa akienda kuyamaliza maisha yake. Aliahidiwa baada ya kufa familia yake ingelelewa na kundi hilo, ingelipwa kiasi kikubwa cha pesa kwa sababu aliifanya kazi kubwa ya Mungu.
Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, moyo wake ulikosa amani, hakuamini kama kipindi hicho alikuwa akienda kuyatoa maisha yake mhanga, alidanganywa kuitetea dini kumbe haikuwa hivyo, ni watu wenye roho mbaya kwa maslahi yao ndiyo waliomshawishi kufanya tukio hilo la kipumbavu.
Alipofika chuoni hapo akasimamisha gari na kubaki humo kwa muda, aliyafikiria maisha yake kwa ujumla na kile alichokuwa akienda kukifanya, hakika kilimsikitisha na kumuogopesha lakini hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima afanye kile alichotakiwa kufanya.
Baada ya dakika kadhaa akateremka na kuelekea ndani ya jengo la chuo kile, kila mtu alionekana kuwa bize, waliokuwa wakijisomea, walikuwa wakiendelea kujisome, waliokuwa wakifanya mambo yao walikuwa wakiyafanya pasipo mtu yeyote yule kujali lolote lile.
Mkononi mwake kulikuwa na kitufe ambacho kiliunganishwa mpaka kwenye lile bomu lililokuwa ndani ya nguo yake na endapo angekibonyeza kile kitufe basi bomu lingeweza kulipuka, alikishikilia mkononi vilivyo, alitakiwa kubonyeza tu.
Akapiga hatua na kuelekea ndani kabisa, sehemu iliyokuwa na ukumbi mkubwa na kukaa humo, kulikuwa na watu zaidi ya elfu moja ambao walikuwa wakiendelea na mambo yao kama kawaida.
“Don’t cry...Said, don’t cry...fight for your God, religion, fight for your brother and sister...fight for you country...” (Usilie...usilie Said...pambana kwa ajili ya Mungu wako, dini yako, pambana kwa ajili ya ndugu zako...pambana kwa ajili ya nchi yako...) alijisemea maneno hayo, kijasho kilikuwa kikimtoka.
Huku watu wakiendelea na mambo yao, hapohapo akasimama wima, akaangalia huku na kule, akainamisha kichwa chake na machozi kumtoka mfululizo. Akayainua macho yake na kusema kwa sauti ya juu.
“Allah Akbar....” (Mungu mkubwaaaa....) alisema huku kidole chake akikipeleka kwenye kitufe kile tayari kwa kukibonyeza.
Hapohapo mlipuko mkubwa wa bomu ukasikika na kuonekana kupitia kwenye televisheni mbalimbali duniani zikiwemo CNN, BBC, Aljazeera na nyinginezo.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne mahali hapahapa.
 
Pc Imezingua...nairekebisha halafu tutaendelea kama kawaida wadau

Najua unapitia wakati mgumu maana kwa waandishi hili tatizo la kuharibikiwa vifaa linasumbua haswaa. Wakati fulani virusi vilitfuna riwaya zangu zote ikanipasa kuanza upya kuandika. Na unafahamu kuanza upya unajikuta umepoteza mtililiko wako wa kwanza na huenda ukakosa ladha ya mwanzo kama ilivyo kuwa. Mi nitakuwa mvumilivu hadi uwe tayari. Maana umesha toa ahadi ya kuimaliza hapa hapa. Natumaini ahadi itatimia hata miaka 1000 ipite ipo siku utaimaliza.
 
Najua unapitia wakati mgumu maana kwa waandishi hili tatizo la kuharibikiwa vifaa linasumbua haswaa. Wakati fulani virusi vilitfuna riwaya zangu zote ikanipasa kuanza upya kuandika. Na unafahamu kuanza upya unajikuta umepoteza mtililiko wako wa kwanza na huenda ukakosa ladha ya mwanzo kama ilivyo kuwa. Mi nitakuwa mvumilivu hadi uwe tayari. Maana umesha toa ahadi ya kuimaliza hapa hapa. Natumaini ahadi itatimia hata miaka 1000 ipite ipo siku utaimaliza.
Kabisa kaka! Ila mimi huwa nazihifadhi kwenye dropbox hivyo huwa ni rahisi kuwa nazo hata mashine ikiharibika kabisa. Ikiwezekana nitairekebisha leo ama keaho. Ila nahisi mpaka Jumatatu inaweza kuwa tayari.
 
NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269

SEHEMU YA 15.

Ni kama Peter alichanganyikiwa, hakuamini alichokuwa akikione, kwenye kompyuta ile alimuona mtu ambaye alitambulishwa kama Juma Hiza lakini kitu cha ajabu kabisa mbele yake alikuwepo kijana mwingine ambaye naye aliitwa Juma Hiza.
Hakujua yupi ni yupi! Huyu aliyekuwa naye alimwambia mambo mengi, jinsi maneno yaliyotumika kwenye kitabu kile yalivyoweza kufanyiwa kazi na milipuko kadhaa kutokea katika ardhi ya Marekani lakini kitu cha ajabu kabisa naye yule Omar aliyekuwa nchini Afghanistan naye alikuwa na kijana aliyemtambulisha kama Juma Hiza.
Hakujua huyo mwandishi alikuwa yupi kwani hali ilionekana kumchanganya kila mmoja. Alimuuliza Juma lakini naye alionekana kushangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea. Alimwangalia yule kijana ambaye Omar alisema alikuwa yeye, ni kweli alionekana kama yeye, yaani walifanana kwa kila kitu.
Lingekuwa jambo jepesi kusema alikuwa pacha wake lakini alishindwa kuwaza hilo kwa kuwa hakuzaliwa na pacha, kama angekuwa na pacha basi ilikuwa ni lazima wazazi wake wamwambie, sasa yule aliyekuwa akimwangalia alikuwa nani?
Huku akijiuliza, naye Peter alikuwa na mawazo tele, kichwa chake kilikuwa na maswali mengo, wakati mwingine alihisi kama kugeukiwa kwamba inawezekana huyu Juma alionana na Omar halafu baadaye kwenda Tanzania na kumchukua, yaani kwa maana nyingine ni kwamba ile video aliyokuwa akiiangalia ilirekodiwa siku kadhaa zilizopita.
“Hii habari ilikuwa ni ya moja kwa moja?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo bosi!”
“Haijarekodiwa siku chache zilizopita?” alimuuliza kijana wake.
“Hapana!”
“Sasa huyu ni nani?” aliuliza.
Hakujua jibu la swali hilo, akamuuliza maswali Juma kama alikuwa akimfahamu mtu aliyekuwa pembeni ya Omar lakini naye alisema hakuwa akimfahamu hata kidogo na ndiyo kwanza alikuwa akimuona siku hiyo.
Wakahisi kwamba inawezekana Omar alifanya mchezo kucheza na akili zao, yaani alimchukua mtu mwingine, akatengeneza sura ya Juma Hiza na kumvalisha hivyo haraka sana akawasiliana na watu wa kitengo cha facial na kuwauliza kuhusu ile picha iliyokuwa ikionekana.
Haraka sana watu hao wakaivuta picha ya Miraji na kuangalia, endapo ingekuwa sura ya bandia, kwa utaalamu wao ingekuwa rahisi sana kuligundua hilo, wakaiangalia na jibu lililokuja ni kwamba haikuwa sura ya bandia.
“Sasa ni nani yule?” aliuliza.
Hakutaka kukubali, alichanganyikiwa, si yeye tu bali kila mtu aliyekuwa ndani ya jengo hilo lililokuwa Langley alichanganyikiwa vilivyo. Walitakiwa kudili na jambo hilo mapema kwani endapo wangelipuuzia, baadaye roho za Wamarekani wengi zingeweza kutoka.
Wakasahau ishu ya bomu lililotakiwa kulipuliwa siku inayofuata, ilikuwa ni lazima kwanza wamalizane na suala hilo ili kujua ukweli. Wakawasiliana na kituo cha Televisheni cha CNN na kuuliza kama ile video iliyokuwa imerushwa ilikuwa ni ya moja kwa moja ama ilirekodiwa, wakawajibu ilirushwa moja kwa moja kwani nao waliunganishwa na Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera.
Hawakuishia hapo, napo wakawasiliana na Al Jazeera na kuwauliza kilichokuwa kimetokea, nao walisema ilikuwa ni video ya moja kwa moja kwani walirushiwa na mtu ambaye walikuwa na uhakika naye kwani ndiye alikuwa akiwatumia video mbalimbali za kundi la Al Qaida.
“Kwa hiyo huyo hajulikani?” aliuliza Peter.
“Ndiyo! Na mbaya zaidi hatujui Juma Hiza ni yupi!” alisema mwanaume mmoja ndani ya jengo hilo.
Vichwa viliuma mno, hawakujua ni yupi sasa alitakiwa kuaminika kwamba alikuwa Juma Hiza. Peter akarudi ndani ya chumba kile na kumwangalia kijana huyo. Moyo wake ulimwambia kuwa huyo ni Juma Hiza lakini upande mwingine ulikataa na kumwambia hakuwa yeye bali yule mwingine ndiye alikuwa mwenyewe.
Akamsogelea Juma kwa lengo la kumuuliza maswali kadhaa, alihitaji kufahamu kuhusu jambo hilo, walitakiwa kumalizana nalo haraka kwa kuwa kulikuwa na suala la bomu ambalo nalo lilitakiwa kumalizwa haraka sana.
“Una uhakika kwamba hamkuzaliwa mapacha?” aliuliza Peter huku akimwangalia Juma Hiza.
“Ndiyo!”
“Una uhakika kabisa?”
“Ndiyo!”
“Sasa yule ni nani?”
“Hata mimi nashangaa! Labda amevishwa sura ya bandia!”
“Hapana! Ile ni sura halisi, tumefuatilia kila kitu, yule ni sura yenyewe kabisa!”
Juma alitamani kujua ukweli juu ya mtu huyo lakini hakufahamu lolote lile. Alichokijua ni kwamba inawezekana Chilo alifahamu kila kitu lakini kitendo cha kulitaja jina lake mahali hapo haikuonekana kuwa kitu kizuri, alijitahidi kulinyamazia lakini alihitaji kufahamu zaidi juu ya yule aliyekuwa akimwangalia kwenye kompyuta ya Peter.
“Turudi kwenye bomu! Kuna saa kadhaa litalipuka,” alisema Juma, alitaka kwanza kuwahamisha kwenye suala hilo, lilikuwa zito na gumu kulizungumzia mahali hapo.
“Aya! Tuambie ni mahali gani ambapo bomu linakwenda kulipuka!” alisema Peter.
“Hebu soma kitabu vizuri! Niambie kuhusu Esta, alikwenda kuonana na hao Waarabu hapo Brooklyn, ni lazima nitakuwa nimeandika kwa mafumbo, nataka kabla ya kukwambia, nahitaji msumbue vichwa vyenu,” alisema Juma huku akimwangalia Peter.
“Kwa maana gani?”
“Nimeandika mahali ambapo bomu hilo linakwenda kulipuliwa, hebu soma vizuri!” alisema Juma.
Peter akafungua kitabu kile na kuanza kuangalia kwenye ule ukurasa uliokuwa ukimzungumzia Esta kukutana na Waarabu wale, alijaribu sana kuangalia ni mahali gani ambapo paliandikwa mahali walipokuwa wakienda kulipua lakini hakubahatikana kupaona.
Hakutaka kusumbuka peke yake, alichokifanya Peter ni kuwashirikisha na wenzake, walisoma kwa makini, mahali ambapo palikuwa wazi kabisa kupagundua palikuwa ni pale kwenye park ya kupumzikia.
“Bila shaka kwenye hii park,” alisema Peter huku akimwangalia Juma Hiza.
“Kwa staili hii hatutoweza kupata majibu ya maswali yetu! Ukisoma hiki kitabu ni kwamba nimekiandika kwa mafumbo mengi mno, sasa mnaposhindwa kujua mahali mabomu yatakapokwenda kulipuka, nashangaa sana,” alisema Juma huku akionekana kukata tamaa na hao CIA.
“Ila hukuandika eneo!”
“Nimeandika kimafumbo!”
“Wapi?”
“Kwenye kitabu! Hebu soma ukurasa wa 87 aya ya nne,” alisema Juma na Peter kuanza kusoma.
“Esta alikuwa akiogopa, mwili ulitokwa na jasho chembamba kiasi cha kutaka kuyaangusha madaftari yake. Aliwaangalia wanaume waliokuwa kwenye kiti ndani ya park ile, walionekana kuwa na roho mbaya, suala la kuua halikuonekana kuwa gumu hata kidogo. Walimuita mahali hapo kwa lengo la kumpa maelekezo ni jambo gani alitakiwa kufanya,” alisema Peter, akaimaliza aya.
“Sasa si umeona! Nimeitaja sehemu!”
“Wapi? Mbona sijaiona!” alisema Peter, akaanza kujisomea.
“Peter! Hiki kitabu kinahitaji akili kubwa sana! Esta alishika nini?” aliuliza.
“Madaftari!”
“Kwani madaftari huwa yanasomwa wapi?”
“Shuleni!”
“Esta alikuwa akisoma shule gani?”
“Alikuwa akisoma chuo!”
“Chuo gani?”
“Brooklyn!”
“Yeah! Hapo ndipo bomu linapokwenda kulipuliwa. Sikuandika jina la chuo, nimekiwakilisha chuo kwa kuyaandika yale madaftari! Kama madaftari yasingekuwa na maana yoyote ile, ningesema alikwenda akiwa na simu yake mkononi! Kila ninachokiandika kina maana,” alisema Juma huku akimwangalia Peter aliyeonekana kuwa hoi kwa kile alichoambiwa.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumapili hapahapa.
Kwa watakaotaka kukisoma kitabu hiki, wajiandae, kitatoka mwisho wa mwezi huu.
 
Back
Top Bottom