NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269
SEHEMU YA 11.
Watoto hao mapacha waliendelea kukua kila siku wakiwa kwenye mikono ya watu tofauti, hapakuwa na yeyote ambaye alijua kama watoto hao walikuwa mapacha zaidi ya madaktari wale waliokuwa hospitalini.
Miaka ilisogea kama kawaida, Miraji akakua na kuanza darasa la kwanza, alisoma na kusoma mpaka alipohitimu kidato cha nne ambapo watu aliojua walikuwa wazazi wake, Amina na mzee Mrisho kufariki dunia baada ya kupata ajali ya gari na hivyo kubaki mwenyewe.
Maisha hayakuwa kama yalivyokuwa, yalibadika, yalikuwa magumu lakini alijitahidi kupambana nayo kama kawaida. Wakati huohuo naye Juma aliendelea kukua mkoani Kilimanjaro na baada ya kumaliza kidato cha nne akaamua kuondoka na kuelekea jijini Dar es salaam kusoma lakini lengo lake lilikuwa ni kuandika vitabu vya simulizi kwa sababu aljua alikuwa na kipaji cha uandishi lakini hakujua angeanzia wapi.
Alipofika huko, mtu wa kwanza kabisa kumtafuta alikuwa huyo Chilo, alisoma simulizi zake katika Mtandao wa Kijamii wa Facebook, alihitaji kujifunza kupitia kwake kwani aliamini kuna siku isiyokuwa na jina angekuwa na pesa nyingi, pesa ambazo zilipatikana baada ya kuandika vitabu kadhaa.
Akampigia simu mwandishi huyo na kuomba kuonana naye, halikuwa tatizo, wakaonana na kuanza kuzungumza. Juma hakujiamini, kila alipokuwa akimwangalia Chilo alihisi alikaa na mtu gani, kwa mbali kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka.
“Umesema umeandika simulizi! Zipo wapi?” aliuliza Chilo swali lililomfanya Juma kuchukua begi lake na kulifungua, akatoa daftari na kumuonyesha.
“Kwa hiyo unaandika kwenye daftari?” aliuliza huku akimwangalia.
“Ndiyo bro! Sijapata kompyuta!” alijibu.
“Unahisi kikifanyika kitu gani utaweza kufikisha ndoto zako?” alimuuliza huku akiwa amelichukua daftari hilo na kuanza kuliangalia.
“Kuandika kwenye magazeti!”
“Ili?”
“Nijulikane!”
“Tunahama huko! Tunahamia kwenye mitandao, kila kitu kimebadilika Juma, idadi ya wanunua magazeti imepungua, ni lazima tuwekeze kwenye mitandao,” alisema Chilo huku akimwangalia Juma.
“Sasa mimi nitafanyaje bro! Sina hata kompyuta!” alisema, alitia huruma, kwa jinsi alivyoonekana tu, ni kweli alihitaji msaada.
“Utaitumia yangu nitakapokuwa sipo bize! Unaishi wapi?”
“Temeke!”
“Duuh!”
“Kwani vipi bro?”
“Mbali kichizi!” alijibu Chilo na kuanza kutoa kicheko cha chini.
Waliongea kama marafiki ambao walikutana miaka mingi iliyopita, kila wakati Juma alipokuwa akimwangalia Chilo alitamani kuwa kama yeye, aandike simulizi kama zake, zije kupendwa na wasomaji wengi.
“Na nifanyeje ili nifanikiwe?” aliuliza Juma baada ya mazungumzo marefu.
“Tupo kwenye ulimwengu wa shida sana Juma! Tunapitia nyakati ngumu sana,” alijibu Chilo huku akimwangalia Juma, sasa wakawa wamesimama.
“Sijakuelewa!”
“Unajua kama wasomaji wana akili sana? Tena zaidi yetu?” aliuliza.
“Wasomaji wana akili zaidi yetu?”
“Ndiyo! Tena kubwa sana. Unaweza kuandika kuhusu nyumba kwa muonekano wa nje, wao wanajua mpaka muonekano wa ndani. Sasa ili uweze kwenda nao sawa ni lazima ujifunze, usome sana, ujitahidi kuijua dunia. Siku ukiandika kitabu ukazungumzia madaktari basi daktari fulani akikishika kitabu chako na kusoma aone kweli umeandika kama nawe ni daktari!” alijibu Chilo.
“Aiseee!”
“Hata kama hujawahi kukutana na mwanamke kimwili, ukiandika simulizi za chumbani, andika kama umetoka kucheza filamu za utupu!” alisema Chilo, Juma akaanza kucheka.
“Halafu bro bhana!”
“Najua mifano nikiitolea kwa wanawake lazima uonyeshe hali fulani hivi! Sikulaumu, sisi ngozi nyeusi tupo hivyo, kwanza tunapenda sana ngono! Lishike hilo na kuna siku nitakuuliza nilikwambia nini! Sisi ngozi nyeusi tunapenda sana ngono!” alisema Chilo.
“Utaniuliza siku moja?”
“Kila kitu ninachoongea nawe kuna siku nitakuuliza ama kitakuwa msaada mkubwa kwenye maisha yako! Huwezi kuendelea ukiwa unapenda sana ngono kupita kiasi!” alisema Chilo, kwenye suala hilo akaonekana siriazi.
“Hilo najua!”
“Bado hujajua ipasavyo! Ila nakuahidi kuna siku utajua! Kapande gari, tumeongea sana! Ila endelea kuandika,” alisema Chilo, wakaagana na Juma kuondoka mahali hapo.
Juma alijiona kuwa mwandishi wa kawaida lakini Chilo alipokuwa akimwangalia aliona kabisa kuna siku angekuja kuwa na uwezo mkubwa mno. Aliagana naye lakini kichwa chake hakikuacha kumfikiria hata kidogo.
Aliporudi nyumbani kwake, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuchukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika kama kawaida yake. Alikuwa na mipango mingi sana, aliigawa na ilikuwa ni lazima ifanyike, hata kama ingeshindikana lakini siku akikaa chini aseme nilijaribu kufanya kitu fulani lakini kilishindika. Kwenye kidaftari chake aliandika hiviiiiii...
1. Nitaandika filamu Hollywood: Ili kufika huko ni lazima kichwa changu kifkirie zaidi ya watu wengine, nipanue mawazo yangu zaidi ya watu wengine, nisome sana kwenye mitandao kuliko watu wengine.
2. Nitaandika kitabu na kuingiza pesa sana: Na hili nifike hapo ni lazima nifikirie kuhusu kitabu changu kimataifa. Niwe kama akina Ngugi wa Thiongo lakini niwe kidigitali zaidi, kwa hapa ni lazima nitumie mitandao ikiwemo Amazon. Jina nitakaloliweka ni THERE IS NO GOD AT ALL yaani HAKUNA MUNGU KABISA. Nitaliweka jina hili kwa sababu ya kuwafanya watu wasome ili waone kwa nini nimeandika jina hilo.
3. Kwa sababu nitakuwa na mipango mingi, nitamtumia Juma Hiza kukamilisha ndoto zangu! Tutasaidiana, wakati yeye anataka kukamilisha ndoto zake, anitumie kama daraja na mimi nimtumie kama daraja. Ni kama jinsi mwajiri anavyomtumia mfanyakazi wake kuwa daraja la kutimiza ndoto zake.
4. Kitabu nitakachoandika ni lazima niwasumbue akili Wazungu kama jinsi ambavyo Snowden alivyowasumbua Wamarekani. Wanaogopa sana ugaidi, nitaitumia hofu yao kutimiza malengo yangu. Wazungu walipokuja Afrika, walitutisha mno, tukaogopa, kupitia hofu zetu, wakachukua mali zetu na kubaki tulivyo, sasa ili kutimiza ndoto zako, wakati mwingine unatakiwa kuwatisha watu fulani, watakapotishika, unakamilisha ndoto hizo harakaharaka.
Chilo aliandika mambo mengi na baada ya kumaliza, akafunga daftari lake na kuendelea na mambo mengine. Ukaribu wake na Juma uliendelea kama kawaida, waliendelea kuwasiliana na kumsisitiza sana kuhusu uandishi huo wa simulizi ambao aliamini kuna siku ungemfanya kutoka na kuwa sehemu nyingine kabisa.
‘MWANAUME MZURI KULIKO WOTE TANZANIA AONEKANA CHUO KIKUU KWA MARA YA KWANZA!’
Hicho kilikuwa kichwa cha bari kirefu kuandika katika Tovuti ya Michuzi, Chilo aliifungua na kutaka kuona picha ya mwanaume huyo, ilipofunguka, akabaki akiiangalia, alitamani kujua zaidi kuhusu mwanaume huyo, haraka sana akaanza kusoma maelezo yake, akabaini kwa jina, mwanaume huyo aliitwa Richard Mawelle, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Nahisi naweza kupata kitu kizuri hapa, acha niende huko chuoni nikajue mengi kuhusu mwanaume huyu,” alijisema Chilo huku akiyasoma maelezo zaidi kuhusu huyo Richard aliyekuwa na sura nzuri kuliko wanaume wote (Sifa zake kemkem zimeandikwa kwenye kitabu cha Dili la Dola Bilioni Nne).
****
Baada ya siku kadhaa, mapema sana Chilo akaelekea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku lengo lake kubwa likiwa ni kumuona kijana huyo, tayari kichwa chake kilikuwa na mambo mengi ambayo alitaka kuyaandika, hasa hadithi ambayo ingemuelezea mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama huyo ambaye alikuwa akienda kumuona.
Ndani ya daladala alikuwa akifikiria namna ya kuisuka simulizi nzuri ambayo ingemuhusisha mwanaume huyo aliyekuwa na uzuri wa sura, alihitaji kuandika simulizi ambayo ingemsisimua kila mtu ambaye angekwenda kuisoma siku moja.
Hakuchukua muda mrefu akafika chuoni na moja kwa moja kuelekea kwenye Ukumbi wa Nkurumah kwa lengo la kutulia kabla ya kuanza kumtafuta Richard, alikuwa na hamu ya kumuona na kadiri alivyokuwa akisubiri ndivyo alivyokuwa na hamu ya kutaka kumtia machoni mwake.
Akiwa humo huku akijifikiria kama alitakiwa kumuulizia mwanaume huyo, ghafla macho yake yakatua kwa kijana mmoja hivi, hakuwa mgeni machoni mwake, alimfahamu, alimuona siku chache zilizopita, kijana huyo alikuwa na wasichana wawili waliokaa katika meza moja wakizungumza.
“Juma Hiza...” aliita Chilo huku sura yake ikionyesha tabasamu pana.
Kijana huyo akayainua macho yake na kumwangalia Chilo, alikuwa akitabasamu, yaani kwa jinsi alivyokuwa akimwangalia ni kama aliwahi kumuona mahali fulani sehemu hivi. Si kijana huyo aliyekuwa akishangaa tu bali hata wale wasichana nao walikuwa wakishangaa.
“Mbona unashangaa sana?” aliuliza Chilo huku naye akivuta kiti na kutulia, jamaa yule akamwangalia Chilo kisha akawaangalia na wasichana wale aliokuwanao.
“Tunafahamiana?” aliuliza kijana huyo.
“Daah! Hiza bwana! Unanikataa mchizi wangu! Ndiyo yaleyale niliyokwambia, ukipenda sana hiyo kitu hutoendelea, sasa unanikataa kisa umekaa na wanawake!” alisema Chilo huku akitoa tabasamu ambalo lilionekana kama kumtaka kijana huyo akubaliane naye.
“Sijakuelewa!”
“Kwani wewe nani? Si Juma Hiza?”
“Hapana! Naitwa Miraji!”
“Miraji? Miraji gani? Acha masihara bwana!” alisema Chilo.
“Siriazi bro! Kwani wewe uliniona wapi?”
“Majuzi ulikuja ofisini kwetu pale Bamaga, ukaomba kuonana nami, wewe si ulisema unaandika hadithi, ama umesahau?” aliuliza Chilo.
“Mimi?”
“Yeah!”
“Hapana! Labda umenifananisha! Mimi na hadithi wapi na wapi!” alisema, wasichana wale wakaanza kucheka.
“Siwezi kufananisha kiasi hiki!”
“Bro! Utakuwa umenifananisha!”
Chilo alikuwa na uhakika hakuwa amemfananisha kijana huyo, alijua dhahiri alikuwa Juma Hiza ila alitaka kumkataa tu kwa sababu alikuwa na wasichana mahali hapo.
Alichotaka ni kuuona uongo wa kijana huyo, si alikuwa na namba yake, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kumpigia Juma Hiza huku akiwa mbele ya watu hao, simu ikapokewa na sauti ya Juma kuanza kusikika.
“Niambie bro!” alisikika Juma Hiza kutoka upande wa pili, Chilo akashtuka.
“Upo wapi?”
“Nipo home bro! Kuna ishu?”
“Hapana! Nitakucheki!” alisema Chilo na kukata simu.
Akabaki kimya, akaendelea kumwangalia Miraji, kwa jinsi alivyokuwa akionekana, hakuwa na tofauti yoyote ile na Juma Hiza, yaani walifanana kwa kila kitu, kwa jinsi alivyokuwa akiongea, kutabasamu na hata kucheka.
“Basi poa!” alisema Chilo na kuondoka mahali hapo.
Kilichokuja kichwani mwake ni kwamba kijana aliyekuwa amemuona na Juma Hiza inawezekana kabisa walikuwa mapacha wasiofahamiana kwani hata kama kufanana hakudhani kama kungekuwa na watu waliokuwa wakifanana kiasi kile.
Alihitaji kumfahamu kijana huyo, mbali na jina lake kumwambia lakini alitaka kujua alipokuwa akiishi, inawezekana kwa kufahamu hilo angeweza kufahamu baadhi ya mambo.
Hakutaka kumshirikisha Juma Hiza kwanza, alitaka kuwa siri kwani endapo watu hao walikuwa mapacha basi alitakiwa kwenda kuandika script nyingine nyumbani kwa kile ambacho alitaka kukifanya na kujikuta akiwa bilionea kwa kuuza vitabu tu.
Hakurudi nyumbani, akaenda sehemu na kutulia huku macho yake yakiwa makini kuangalia mlango wa ukumbi ule, alihitaji kumfuatilia Miraji na kufahamu kila kitu.
Baada kama ya masaa mawili hivi, akamuona akitoka na wasichana wale na kuanza kuelekea kwenye kituo cha daladala cha Utawala hapo chuoni, naye akaelekea huko, walipofika, wakaingia, na yeye akaingia.
Gari likaondoka mpaka Mawasiliano ambapo wakateremka na kuelekea kwenye sehemu iliyokuwa na daladala za Mabibo, naye akaenda na kupanda, tayari kigiza kilianza kuchukua nafasi yake na kwa sababu kulikuwa na watu wengi hawakuweza kumgundua.
Gari likawashwa na kuondoka mahali hapo mpaka katika kituo cha External, Miraji akateremka na Chilo naye kufanya hivyo, akaanza kuelekea upande mwingine kabisa kumzuga kijana huyo endapo angemuona, alipofika mbali kidogo, akageuka na kuanza kumfuata Miraji upande mwingine.
Alimfuatilia mpaka alipomuona kijana huyo akiingia ndani ya nyumba moja nzuri, akahisi hapo ndipo alipokuwa akiishi, hivyo akaridhika na kuondoka zake.
Alipofika nyumbani akachukua daftari lake na kuanza kuchora ramani kama ilivyotakiwa kuwa. Alimuweka Juma Hiza lakini uwepo wa mwanaume mwingine mahali hapo ulimaanisha alitakiwa kufanya kitu kingine cha ziada ambacho kingekuwa kikubwa sana.
Aliandika na kuandika, alipomaliza, akalala, asubuhi ilipofika akaendelea na mambo yake mengine huku kila kitu alichokuwa akikifikiria mahali hapo kilionekana tu kingekwenda kuwa na mafanikio makubwa huko mbeleni.
Je, nini kitendelea?