NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269
SEHEMU YA 06
Ilikuwa ni lazima Chilo aangalie ni kwa namna gani biashara ya kitabu alichopanga kukiweka kwenye Mtandao wa Amazon kinakuwa na mvuto na hata kusomwa na watu wengi.
Haraka sana akawasiliana na Kindo Emmanuel ambaye alikuwa mbunifu wa makava na kuanza kuzungumza naye, ilikuwa ni lazima atengenezewe kavaa ambalo litamvutia kila mtu ambaye angekiona.
Hakutaka kubaki na jambo hilo kichwani mwake, haraka sana akampigia simu na kuanza kumwambia kuhusu kitabu hicho, alikipa jina la There is No God At All yaani Hakuna Mungu kabisa.
Mara ya kwanza Kindo kusikia jina la kitabu hicho akashtuka, hakuamini kama kungekuwa na mwandishi ambaye angediriki kuandika kitabu cha namna hiyo. Alikuwa na maswali mengi ya kuulizwa, kwa mtu kama Chilo, Mwafrika ambaye alimpenda Mungu na kumuabudu lisingekuwa jambo jepesi kuwa na kitabu chenye jina kama hilo.
“Sasa Chilo ndugu yangu wewe si mtoto wa mchungaji?” aliuliza Kindo huku sauti yake tu ilivyokuwa ikisikika ilionyesha alikuwa na hofu.
“Ndiyo!”
“Na si ulisoma Seminary?”
“Ndiyo!”
“Na kanisani ukawa unakwenda?”
“Tena sana tu! Ile shule hatari, asubuhi kanisani, mchana kanisani na usiku kanisani!” alimjibu.
“Na unamwabudu Mungu kwa asilimia mia moja?” aliuliza Kindo.
“Maswali yamekuwa mengi sana, mengine bakiza utaniambia siku nyingine. Hilo kava linatengenezwa lini?” aliuliza Chilo, aliona maswali yanakuwa mengi sana.
“Umekengeuka mshikaji wangu!” alisema Kindo.
“Hapana! Hebu niambie, inawezekana ama?”
“Itawezekana! Ngoja niingie Google kutafuta picha,” alisema Kindo.
“Hapana! Hiki kitabu kitauzwa kimataifa, kama ni picha, nitamtafuta msichana kwa lengo la kupiga picha ambayo tutaitumia,” alisema Chilo.
“Sawa. Mkishapiga nitumie!”
“Haina shida.”
Kazi ikabaki kwa Chilo, ilikuwa ni lazima kutafuta msichana ambaye angekwenda kupigwa picha kwa lengo la kutumika kwenye kava la kitabu hicho. Haraka sana akaingia Facebook na kuangalia picha kadhaa za msichana aliyekuwa akimtaka.
Kwa sifa ya msichana aliyemwandika kwenye kitabu hicho alikuwa mwembamba, mweusi kidogo lakini aliyekuwa na uzuri wa kumvutia kila mtu ambaye angemwangalia, kwenye kuangalia huko macho yake yakatua kwa msichana aliyekuwa akijiita kwa jina la Pearl Mk.
“Huyu atafaa! Ila atakubali?” alijiuliza.
Hakutaka kuchelewa, haraka sana akamtumia meseji na kuanza kuwasiliana naye, alichomwambia ni kwamba alihitaji kuonana naye kwa lengo la kuzungumza kidogo.
Msichana huyo hakujiamini, hakuwahi kuongea na Chilo, alimuogopa, mawazo yake yalifikiria ni mwanaume mtu mzima, mwenye mwili mkubwa, simulizi alizokuwa akiziandika zilimtisha na kuhisi alikuwa mtu ambaye hakustahili kuonana naye.
“Uonane na mimi?” aliuliza msichana huyo kwenye simu.
“Ndiyo! Ninahitaji kuzungumza na wewe!” alimwambia.
“Kuhusu nini?”
“Labda nakutaka!” alisema na kuanza kucheka.
“Unanitaka mimi?”
“Hahaha! Mbona hujiamini bhana! Una nafasi kwa kesho?” aliuliza.
“Mh!”
“Mh nini sasa na wewe!”
“Yaani! Jamani! Sasa mbo...”
“Pearl acha masihara bhasi!”
“Wewe ndiyo umeanza masihara, yaani uonane na mimi! Kuna shida gani?”
“Jambo dogo tu! Halafu jepesi sana! Naomba kuonana nawe kwa kesho. Unatoka chuo saa ngapi?” aliuliza.
“Saa kumi.”
“Saa kumi na mbili nitakuwa Pizza Hut hapo pembeni ya Serena Hotel!” alimwambia.
“Pembeni ya Serena Hotel?”
“Yaani umesikia hoteli ushaanza kuogopa. Basi acha niseme pembeni ya Jengo la Uhuru Heights! Naomba kuonana nawe. Saa kumi na mbili, usikose, ukishindwa niambie nimwambie msichana mwingine!” alimwambia.
“Nitajitahidi!”
Pearl, msichana mrembo hakuwa akijiamini, aliiangalia simu yake mara mbilimbili, hakuamini kama alipigiwa simu na Chilo. Alizoea kumuona mwanaume huyo kwenye mitandao, hakuamini kama kuna siku angempigia simu na kuomba kuonana naye.
Aliwahi kuzungumza naye mara moja tu, tena zamani alipohitaji kitabu, na bahati mbaya kwake, Chilo akamwagiza mtu ampelekee kitabu hicho huku yeye akidai kuwa bize. Ilimuuma lakini hakutaka kumwambia.
Leo hii mwanaume huyo alimwambia alihitaji kuonana naye, hakujua alitaka kitu gani kutoka kwake. Aliingia kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali kwa kuhisi labda kulikuwa na picha chafu zake ambazo mwanaume huyo alizinasa, hakufanikiwa kuziona, na hakuwahi kupiga picha za namna hiyo. Sasa alikuwa akimuhitajia nini?
Hakutaka kuwaza sana, kwa kuwa alimwambia walitakiwa kuonana Posta, hakuwa na jinsi, siku iliyofuata mapema sana akatoka Kigamboni na kuelekea huko huku akionekana kutokujiamini hata kidogo.
Alipofika hapo akatulia na kuagiza chakula na kula mdogo mdogo huku akimsubiri Chilo mahali hapo. Baada ya dakika kadhaa macho yake yakatua kwenye gari ndogo aina ya Vitz ambayo ilisimama na mwanaume huyo kuteremka.
Kitendo cha kumuona tu akahisi mapigo yake ya moyo yakiwa juu, hakuamini, alikuwa akitetemeka na kwa mbali kijasho chembamba kikaanza kumtoka, akatamani kukimbia mahali hapo.
Chilo akaingia na kuanza kuangalia huku na kule, macho yake yalipotua kwa msichana huyo, akamsogelea, akamsalimia na kuanza kuzungumza naye.
Pearl alitamani kutoa kamera yake na kumpiga picha, alitamani kumkumbatia, alitamani kufanya kitu chochote kile kuonyesha furaha aliyokuwanayo mara baada ya kumuona mtu ambaye alitamani sana angekuwa na uwezo kama wake, kuandika vitu vikubwa kama alivyokuwa akiviandika.
“Najaribu kuyatafakari hayo macho yako!” alisema Chilo baada ya mazungumzo marefu kidogo.
“Yamefanyaje?”
“Ni kwamba unanionea aibu ama unaniogopa?” alimuuliza.
“Kawaida tu!”
“Kwamba?”
“Wala sikuogopi!”
“Kumbe?”
“Basi tu!”
Chilo hakuzungumza kitu, akaachia tabasamu na kumkazia macho msichana huyo, Pearl alihofu, alitamani kumwambia alitaka kuondoka lakini akavuta subira na kusubiri alichoitiwa mahali hapo.
“Kuna kitabu nimeandika!” alimwambia.
“Kitabu gani?”
“Cha hadithi!”
“Unauza shilingi ngapi ninunue?” aliuliza kwa bashasha.
“Dola kumi!”
“Dola tena?”
“Yeah! Ila nitahitaji unisaidie kitu kimoja!”
“Kipi?”
“Nahitaji nikutumie kwenye kava la kitabu hicho!”
Ni kama Pearl hakuamini, alimwangalia Chilo mara mbilimbili, ni kweli alimaanisha kile alichokisema ama alikuwa akitania. Yeye kukaa kwenye kava, kila mtu amuone lilikuwa ni kama ndoto machoni mwake, hakuamini kama kuna siku picha yake ingetumika kwenye kava la kitabu.
Kukataa lingekuwa jambo jepesi sana lakini hakutaka kufanya hivyo. Hakutaka kujua sababu ya Chilo kumchagua yeye, kuwa kwenye kava hilo, tena kwa mbele kwake ilikuwa ni fahari kubwa mno. Akamkubalia.
“Gharama yako?”
“Yaani jamani! Mimi hata bure!”
“Hahaha! Hapana! Mjini cha bure ni salamu tu! Na unaponiambia bure, unanitia hofu!” alisema Chilo.
“Mh! Sasa jamani mimi nitasema kiasi gani?”
“Chochote kile!”
“Mh! Yaani hata sijui!”
“Basi nitakulipa. Sipendi nifanyiwe kazi bure, hasa kazi ambayo inakwenda kuniingizia pesa. Nitakutafuta kwa ajili ya kupiga picha. Umelipia chakula?” alisema na kumuuliza.
“Bado!”
“Basi shika hiyo utalipia. Naomba nikutakie jioni njema!” alisema Chilo na kusimama huku akimpa kiasi cha shilingi elfu ishirini.
“Asante!”
Chilo hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka na kuendelea na mambo mengine. Alipofika nyumbani, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufuatilia kwa kina kuhusu mtandao wa Amazon, ilikuwa ni lazima ajue namna ambazo kitabu chake kilitakiwa kuwa na kuingizwa humo.
Aliangalia kila kitu na kukubali kwamba ni lazima atumie jina la Williams McCannon. Alitaka kufanya hivyo kwa sababu alihitaji sana kitabu hicho kisomwe na watu wengi, hasa Wazungu ambao walipenda sana kusoma vitabu.
Kama angeliweka jina la Juma Hiza ingekuwa ni vigumu sana kitabu hicho kupakuliwa na kusomwa na ndiyo maana alihitaji kuweka jina lililoendana na majina yao ili iwe rahisi kununuliwa.
Alijifunza zaidi usiku huo na alipomaliza, akampigia simu Juma Hiza, wakaonana na kumwambia alitakiwa kujiandaa ilikuwa ni lazima kwenda kufungua akaunti kwenye Benki ya Barclays.
“Kufungua akaunti haina shida!” alisema Juma.
“Ila subiri kwanza! Hapa inabidi tucheze mchezo mmoja mkubwa sana, hutakiwi kufungulia akaunti nchini Tanzania, ni lazima iwe Afrika Magharibi!” alisema Chilo.
“Kwa maana ya Ghana, Cameroon, Nigeria, ama unataka wapi?” aliuliza Juma Hiza.
“Nigeria!”
“Sasa huko tutakwendaje?” aliuliza, Chilo akaanza kucheka.
“Vipi tena?”
“Tutafunguliwa akaunti huko!”
“Na nani?”
“Unawajua watu wanaitwa Yahoo Boys?” aliuliza Chilo huku akimwangalia Juma.
“Yahoo Boys? Ndiyo akina nani?”
“Hawa ni vijana kama sisi tu, wao wanadili na utapeli wa mitandaoni yaani Scammers, ni vijana wanaokaa na laptop vyumbani, wanakutapeli kupitia mitandao ya kijamii na sehemu nyingine. Ushawahi kutumiwa meseji Facebook msichana akajitambulisha yeye ni Christina ameachiwa pesa na baba yake tajiri, alihitaji kuja kuweka kwenye akaunti yako, sijui anakuamini, analelewa na mchungaji mmoja huko mbele?” aliuliza Chilo.
“Nishatumiwa mnooo!”
“Sasa waliokutumia hao ndiyo wanaitwa Yahoo Boys! Hao watu hatari, wanaongozwa na jamaa anayeitwa Ray Hushpuppi, ukipata muda utamcheki Instagram uone mwamba anavyokula bata,” alisema Chilo.
“Duuh!”
“Ninajua mambo mengi sana, ila nikwambie kitu kimoja usichokijua, mimi pia ni Yahoo Boy!” alisema Chilo huku uso wake ukiwa kwenye usiriazi na kile alichokuwa akikizungumza.
“Sijakuelewa!”
“Najua hujaelewa. Kwenye hii sekta unatakiwa kuwa makini sana, niliamua kuwa mmoja wa vijana wa Yahoo Boy miaka kama mitatu iliyopita, niliamua kuwa hivyo kwa sababu ya kufanikisha huu mpango wetu. Juma, huu ni mpango ambao niliupanga kabla ya kuonana nawe, ulikuwa kichwani mwangu na nilihitaji sana siku moja nije kupata mabilioni ya pesa,” alisema Chilo.
“Kwa hiyo na wewe ni Yahoo?”
“Yeah! Ongezea Boy kwa mbele ila sijawahi kutapeli! Niliamua kujiunga nao kwa ajili ya huu mchongo tu, kwenye mtandao huo nilifahamiana na washikaji wengi, wa kwanza anaitwa Usman Umar. Kuna stori nyingi sana kuhusu huyu jamaa, nisingependa kupoteza muda sana ila jua mchizi amemuoa manzi fulani anaitwa Lisa kutoka nchini Marekani. Huyu jamaa nilikuwa naye beneti mitandaoni na kitu nilichomwambia anifungulie akaunti kwenye Benki ya Barclays nchini Nigeria ikiwa na jina la Williams McCannon. Kazi hiyo itafanyika haraka sana endapo tutatuma picha yako,” alisema Chilo.
“Mh! Unamwamini jamaa? Sasa atanifunguliaje akaunti? Saini yangu vipi?” aliuliza Juma.
“Juma! Kuna matatizo mengi sana duniani, ila hakuna tatizo linaloitwa saini! Wadau wanasema ukienda pale Posta hata saini ya ikulu unaipata! Andika saini yako, nitatuma kwa jamaa na kila kitu kitafanyika!” alisema.
“Unamwamini mchizi?”
“Yeah! Hakuna tatizo lolote lile!”
Juma hakuwa akijiamini hata kidogo kufanya alichoambiwa na Chilo akifanye lakini hakuwa na jinsi, alikifanya na kila kitu kutumwa nchini Nigeria. Suala hilo lifanyika, hakujua Usman alilifanyaje lakini alifanikiwa na baada ya siku kadhaa alipokwenda kuangalia akaunti yake na namba ya siri aliyopewa, alishangaa kuona imekubali.
Yahoo Boys hawakuwa watu wa mchezo, walijua kufanya vitu kwa utalaamu mkubwa, duniani kulikuwa na watu wengi walikuwa wakilizwa, kuna wengine waliibiwa mpaka dola milioni mia moja na vijana hao ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kula bata tu.
Walinunua magari ya kifahari na majumba makubwa kwa pesa ndefu, walilala na wanawake waliokuwa wakiwataka, walifanya kila aina ya ujinga mpaka pale CIA walipoamua kuingilia kati na kuanza kumkamata mmoja baada ya mwingine.
Baada ya kukamilisha kila kitu, Pearl akapiga picha, kava likatengenezwa, kitabu kikapangwa na hatimaye kuingizwa sokoni huku namba ya malipo ikiwa ya akaunti ambayo ilifunguliwa nchini Nigeria.
Kwa siku ya kwanza tu kitabu kilipowekwa katika Mtandao wa Amazon kila mtu alishtuka, hapakuwa na mtu aliyeamini kama kungeandikwa kitabu kilichokuwa na jina kama lile lililokuwa mbele ya kava hilo ambalo kulionekana picha ya msichana mrembo aliyekuwa ameshika mkoba ambapo ule mkono ulioshikilia mkoba ule begani ukiwa na simu na kwa mbali yalionekana majengo ya WTC yaani World Trade Center yaliyokuwa jijini New York nchini Marekani.
Kava lilivutia machoni, jina lake ndilo lilikuwa chachu ya watu kutaka kufahamu hasa kilichokuwa kimeandikwa humo. Walipoanza kusoma tu, kila mmoja hakuamini, ilikuwa ni simulizi iliyoandikwa kwa mtindo wa flashback, yaani kuanza mwisho na kuja mwanzoni.
Ni ndani ya kurasa hamsini za mwanzo tu, kulikuwa na jumbe mbalimbali, maneno ambayo kwa namna moja yalionyesha ni kwa namna gani majengo hayo yalilipuliwa huku chanzo kikiwa ni msichana mmoja aliyejulikana kwa jina la Esta kutoka barani Afrika kuingia ndani ya jengo moja akiwa na simu ambayo iliweza kupeleka taarifa kwa Waarabu waliokuwa uwanja wa ndege wakisubiri kufanya safari zao za humohumo, simu ile iliweza kunasa sauti ya kila floo aliyokuwa akipita msichana huyo mpaka alipofika floo ya juu kabisa.
“Hiki kitabu..mh! Hebu subiri niendelee kusoma zaidi, nadhani kuna mambo nayaona kabisa yalijulikana kabla, nadhani kutakuwa na mengi ambayo mwandishi anajaribu kutuambiwa kwa mafumbo na kwa undani zaidi juu ya kile kilichokuwa kimetokea,” alisema Peter O’Brain, mwanaume aliyekuwa msimamizi wa maofisa wa CIA hapo Marekani.
Je, nini kitaendelea?