Serikali imeamua "kupoza mambo"...
Mchakato Mahakama ya Kadhi kukamilika Oktoba
Na Theodatus Muchunguzi, Dodoma
WIZARA ya Katiba na Sheria inalishughulikia suala la kuanzishwa Mahakama ya Kadhi na sasa litakuwa tayari Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kwenye majumuisho ya Katiba na Sheria, Waziri Mary Nagu alisema Wizara yake ililikabidhi suala hilo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Oktoba mwaka jana na kwamba inatarajia kukabidhiwa ripoti ya suala hilo kabla ya Oktoba mwaka huu.
"Tunayo miezi miwili kuanzia sasa tu kabla ya kukamilisha suala hilo, hivyo kwa kuzingatia maslahi ya taifa na ya watu wetu wa imani zote nina imani Tume italishughulikia.. tuvute subira, suala hili limo katika ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), "alisema.
Awali suala hilo la kuanzishwa mahakama ya kadhi liliibuliwa tena bungeni na kambi ya upinzani kwa kuihoji serikali sababu za kushindwa kutekeleza ahadi yake.
Hoja hiyo iliibuliwa jana na Waziri Kivuli wa Wizara ya Katiba na Sheria, Fatma Maghimbi (CUF), wakati akiwasilisha hotuba yake ya makadirio na mapato ya wizara hiyo kwa mwaka 2007/08.
Maghimbi alisema muda mrefu umepita tangu serikali ilipotoa tamko kuhusiana na suala la mahakama za Kiislamu na kwamba kambi
ya upinzani haijaona nia ya dhati ya serikali kutatua suala hilo, ambalo linagusa mustakabali wa taifa.
Aliyataja mambo makuu mawili yaliyotolewa katika tamko la serikali lililowasilishwa na Waziri wa Sheria kuwa ni kuwataka wananchi wafunge mjadala kuhusiana na suala hilo na pili, serikali iliahidi kuendesha mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa wananchi.
Maghimbi alisema: "Tamko la serikali lilikuwa
likijipinga lenyewe kwa maana huwezi kufunga mjadala wa wananchi kuhusiana na suala la mahakama ya kadhi na wakati huo huo ukaahidi kukusanya maoni kutoka kwao."
"Je maoni yatapatikana bila mjadala? Lengo la serikali kuutaka umma wa Watanzania kutojadili suala hili. Au nia ya serikali ni kuzima ili lisisikike?" alihoji. Maghimbi, ambaye ni Mbunge wa Chakechake.
Maghimbi alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 iliahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo lakini hadi leo, hakuna jambo la msingi lililofanyika zaidi ya kuitishwa kwa kongamano moja kujadili suala hilo.
Shoka Khamis Juma (Micheweni-CUF), alisema suala la mahakama ya kadhi limesubiriwa muda mrefu bila kutekelezwa na kwamba sasa ni wakati muafaka.
Alisema kamati mbili za Bunge ziliwahi kuundwa kufuatilia suala hilo, moja ikiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe, Alicardo Ntagazwa na Mbunge wa Kisarawe, Athumani Janguo kwa kutembelea nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Msumbiji, kuona zinavyoendesha mahakama hizo.