SEHEMU YA 31...
Juliana hakuwa na furaha, moyo wake ulikuwa umeumia kupita kawaida, alilia usiku na mchana, alikuwa kwenye mateso makali, kansa ilimuumiza, wakati akiyaugulia maumivu hayo, upande mwingine mtoto wake alikuwa mgonjwa.
Hakujua amlilie nani, hakujua sababu ya Mungu kuamua kumuadhibu kwa namna hiyo. Hakuwa na raha, hakula chakula chochote kile, kila wakati alikuwa mtu wa kusikitika na kumuuliza Mungu kwa nini yeye?
Japokuwa alikuwa nyumbani lakini kila siku asubuhi alikuwa hospitalini kwa ajili ya kumuona mtoto wake, Jesca. Kila alipokuwa akimuona kitandani, alihisi moyo wake kuwa kwenye maumivu makali, hakupenda kumuona katika hali hiyo, ilimuumiza mno kiasi kwamba wakati mwingine alihisi kama angepata ugonjwa wa presha.
“Mungu! Naomba usimchukue mtoto wangu, itaniuma sana Mungu,” alisema Juliana huku machozi yakimtoka, wakati huo alikuwa mbele ya kitanda alicholala mtoto wake, kwa jinsi alivyokuwa kimya kitanani pale, alionekana kama tayari alikwishafriki dunia.
“Mke wangu! Acha kulia, Jesca atapona tu,” alisema Gideon huku akimwangalia mke wake.
“Inaniuma! Kwa nini Mungu anataka kumchukua mtoto wangu? Ninamuhitaji, yeye ni faraja yangu, yeye ni kila kitu kwangu,” alisema Juliana huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
“Usilie mke wangu! Ninaamini Mungu atafanya jambo,” alisema Gideon.
Alijaribu kumfariji sana mke wake lakini mwanamke huyo hakufarijika, kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, kila alipomuona mtoto wake kitandani pale, moyo wake ulichoma na kuchoma.
Siku zikakatika, baada ya siku tatu ndipo Jesca akarejewa na nguvu na kuanza kuzungumza tena. Kila mmoja alifurahi, nyuso zao zikatawaliwa na tabasamu pana, kwao, kwa kile kilichokuwa kimetokea ilikuwa kama muujiza fulani mkubwa.
“Unajisikiaje?” aliuliza Juliana huku akimwangalia mtoto wake.
“Tumbo linauma mama!”
“Pole sana! Mungu ni mponyaji, atakuponya tu,” alisema Juliana huku akimwangalia mtoto wake.
“Kweli mama?”
“Ndiyo! Unakumbuka mwalimu wa Sunday School alisemaje?”
“Mungu ni mponyaji!”
“Basi jua atakuponya tu!”
Itaendelea.