SEHEMU YA 25...
Kansa iliendelea kumtesa Juliana, hakuwa na furaha, muda wote alikuwa akilia, alimuomba Mungu kumponya kansa ile au kubadilisha kila kitu na mwisho wa siku kugundua kwamba kila kilichoendelea kilikuwa ndoto.
Alimpenda sana mume wake, Gideon lakini kwa kipindi hicho mwanaume huyo alikuwa bize na mambo yake, upendo uliondoka, akawa anachelewa kurudi nyumbani, hakutaka kabisa kuona akiendelea kuwa na mwanamke mgonjwa kama alivyokuwa Juliana.
Moyo wa mwanamke huyo ulimuuma kupita kawaida. Bado aliendelea kutoka damu sehemu za siri, aliumia, alihitaji msaada kutoka kwa mume wake lakini mwanaume huyo hakuwa na muda naye.
Wakati mwingine akawa anampigia simu, hakuwa akipokea na hata alipomtumia ujumbe kwenye simu yake mwanaume huyo hakuwa anajibu kitu kilichomfanya kujisikia vibaya mno.
Wakati Juliana akiteseka kitandani, Gideon alikuwa kwenye penzi la mwanamke mwingine aliyeitwa Juliet. Lilikuwa penzi jipya, penzi lililochipukia kwa kasi kubwa, penzi ambalo lilimfanya kuanza kumsahau mke wake.
Alihitaji faraja, alihitaji kulala na mwanamke, mkewe hakuwa akiweza kufanya kitu chochote kile, alionekana kama sanamu hivyo kwa hali aliyokuwa akipitia ilikuwa ni lazima kutafuta mwanamke mpya ambaye angeufanya moyo wake kuwa na furaha muda wote.
Akawa akitoka na Juliet kwenda sehemu mbalimbali, alikuwa na pesa, alitumia pesa zake kumfurahisha msichana huyo pasipo kumkumbuka mwanamke ambaye alichuma naye.
Kila alipokuwa na Juliet, Juliana alikuwa akipiga simu, aliichukua simu yake na kuangalia, alipoona jina la mke wake, alicheka sana na kumuonyeshea Juliet ambaye alimwambia amsahau mwanamke huyo kwani hakuwa chochote kile.
“Achana naye!” alisema Juliet.
“Ndiyo ninachofanya. Unajua namchukia sana yule mwanamke,” alisema Gideon huku akionekana kuwa na hasira.
“Jamani! Basi tukampoteze,” alishauri Juliet.
“Tumpotezaje?”
“Tumuue!”
“Sawa. Ngoja nikafanye mipango, mwanamke yule hatakiwi kuishi. Kwanza pale alipokuwa tayari maiti,” alisema Gideon.
Itaendelea.