Joto la mapenzi

Mkuu, hongera sana. Yaani ni bonge la story kifupi umekumbusha mbali enzi zile tulikiwa tunasoma/fuatilia riwaya za magazetini.
Big up mkuu kwa burudani tosha. Nasubiria mwendelezo.., but dont keep us waiting for too long pls!

Je unatunga kwa kutifurahisha au unaandika vitabu pia kwa ajili ya kunufaika na jasho lako..?
 
Soriii wakuuuu mishe mishe zinabana kidogo ila tuko pamojaa
 
JOTO LA MAPENZI-25

ILIPOISHIA

“Binafsi namuona kama baba yangu mzazi hivyo basi kwa umri wake tunatakiwa kumtunza kama mboni ya jicho letu. Najua mimi sijawa vizuri lakini kwa mazoezi na dawa ninazotumia muda si mrefu tutakuwa pamoja.”
ENDELEA NAYO…


“Ni kweli Mabina, kupitia kwa mzee huyu tumezaliwa na kuwa ndugu wa damu kwa hiyo la kwako litakuwa langu na langu litakuwa la kwako.”


“Ni kweli kabisa Ambe tumekuwa pamoja tangu gerezani nina imani mzee Yamungu ameongeza uzito katika urafiki wetu.”


Baada ya kubadilisha mawazo walijiandaa kwa chakula cha mchana ambacho siku ile kilikuwa viazi vitamu vya kuchemsha na maziwa ya mgando.


MIEZI MITATU BAADAYE


Siku moja asubuhi Ambe kama kawaida aliwahi kuamka na kumuamsha Mabina kwa ajili ya mazoezi kwani waliamua kujiandaa kabla ya kuingia vitani kulipa kisasi wakiwa kamili.


Walipokwenda chumba cha mzee Yamungu alishangaa kukuta mzee huyo akikoroma mkoromo usio wa kawaida. Alipomsogelea alimkuta akikoroma kama mtu anayetaka kukata roho, alijaribu kumwita lakini hakukuwa na jibu.


Alimwita Mabina aliyekuwa tayari amekwishatoka nje.


“Mabina hebu njoo.”


Mabina aliingia ndani na kupokelewa na mkoromo usio wa kawaida.


“Vipi mzee anaumwa?”


“Hata sijui, yaani nimeingia nimemkuta hivihivi.”


“Sasa tutafanyaje?”


“Hebu kimbilia yale majani ya nyuma ya nyumba ili tujaribu kumnywesha.”


Kabla hajanyanyua mguu mzee Yamungu alivuta mkoromo mmoja kisha alitulia, hali ile iliwatisha walimsogelea ili kujua alikuwa na tatizo gani.


Ambe alimtuma Mabina afuate majani ambayo walielekezwa na mzee Yamungu mtu akiwa katika hali isiyoeleweka kama ukimnywesha lazima atapata nafuu fulani. Mabina alikimbilia mara moja nje na kuchuma majani ambayo waliyasaga na kuyachanganya na maji na kujitahidi kumnywesha.


Lakini dawa haikuingia hata kidogo, kwani meno tayari yalikuwa yameshikana. Walijitahidi kuyafungua kwa kijiti na kuingiza dawa ambayo ilitoka yote kuonesha hakukuwa na mawasiliano kwenye mwili wa mzee Yamungu.


“Sasa hii itakuwa nini?” Mabina aliuliza akiwa ameshikilia kikombe cha dawa.


“Hata mimi sijui.”


“Mbona kama ahemi?”


“Wewe unafikiria nini?”


“Asiwe amefariki?” Mabina alisema huku akiweka mkono kifuani ambako hakukuwa na dalili za mtu kuhema.


“Mmh! Itakuwa vigumu kwani mzee ameumwa ugonjwa gani uliomfanya afariki ghafla?”


“Sasa unafikiri hiki nini?”


“Tusiwe na haraka ya kufikiria mbali tufanye subira ya kuangalia afya yake baada ya muda.”


“Kwa hiyo unanishauri tumwache kwanza?”


“Hilo la muhimu hata wewe kama mzee angekuwa na haraka angekuzika ukiwa hai.”


“Basi tumlaze tumwache apumzike baadaye tutarudi kuangalia hali yake.”


Walitoka nje kuendelea na mambo mengine. Ambe hali ya mzee Yamungu iliendelea kumpa wasiwasi kutokana na tukio lile kuwa ndilo mara ya kwanza kutokea.


Nguvu za kufanya kazi kwa siku ile hakuwanazo, uchovu ulitawala kuliko kawaida aliamua kumweleza mwenzake wasiwasi wake.


“Mabina hata akili yangu leo siielewi.”


“Kivipi best?”


“Kuhusu hali ya mzee.”


“Kwani umewaza nini?”


“Ninaweza kukubaliana na mawazo yako.”


“Mawazo gani?”


“Huenda amefariki.”


“Ambe usiwaze hivyo tusifike huko, kwa nini tusisubiri baadaye turudi kumjulia hali yake?”


“Mabina, kwa hali ile bado moyo wangu una hofu kubwa.”


“Sasa tutafanyaje?”


“Kuna kitu nataka tukaangalie kitatujulisha hali ya mzee.”


“Kitu gani hicho?”


“Kuna sehemu alinielekeza ukiishika itakujulisha ni mzima au amekufa.”


“Sehemu gani?”


“Twende nikakuoneshe hata mzee alipokuokota kuna sehemu alishika na kugundua hujafa japo ulikuwa hupumui.”


“Mmh! Hebu twende tukamuangalie ili tujue cha kufanya.”


Waliongozana mpaka ndani alikokuwa amelala mzee Yamungu ambaye bado hakuonesha mabadiliko yoyote kwani alikuwa kama walivyomuacha, shingo ilikuwa imelalia upande. Ambe alimshika sehemu aliyoelekezwa na mzee Yamungu katika kutambua uhai wa mtu kama amekufa au yupo hai.


Alimshika sehemu ile kwa kuiminya kwa nguvu, sehemu ilikuwa imetulia, alirudia zaidi ya mara nne lakini jibu lilikuwa lilelile kuwa mwili wa mzee Yamungu haukuwa na uhai.


Ambe alishusha pumzi nzito zilizomfanya Mabina ashtuke na kuuliza:


“Vipi?”


“Mtihani ndugu yangu.”


“Mtihani upi?”


“Wa kuishi peke yetu porini.”


“Una maana gani?”


“Mzee amefariki.”


“Usiniambie?” Mabina alishtuka kusikia vile.


“Kweli, wasiwasi wangu ulikuwa kweli,”


“Upi huo.”


“Pale alipovuta mkoromo mrefu na kutulia ilikuwa kweli anakata roho.”


Mabina alianza kulia kilio cha kwikwi kwani mzee Yamungu kwake alikuwa zaidi ya baba yake mzazi bali Mungu wake wa pili aliyeyaokoa maisha yake. Kifo chake kilikuja ghafla sana kwani moyoni alipanga kumfanyia kitu kikubwa kama asante baada kuyaokoa maisha yake, ambayo hakuna mtu ambaye angekuwa radhi kuushughulikia mzoga wa mtu asiyemjua hata kujua upo hai au umekufa zaidi ya kuupita uliwe na mnyama.


“Mabina huu si muda wa kulia,” Ambe alimweleza rafiki yake.


“Ambe inaumwa, mzee huyu ni mtu muhimu sana katika maisha yangu.”


“Hilo najua, hata mimi kungekuwa na mtu wa kumshughulikia mzee wetu, ningelia zaidi ya mwaka mzima bila kunyamaza. Mzee alikuwa kiumbe wa ajabu ambaye si rahisi kwa mwanadamu wa dunia ya sasa kufanya aliyofanya.”


“Ambe najiona kama nimepasuliwa moyo kwa kisu butu bila ganzi, maumivu ninayosikia ni makubwa sana niache nilie.”


“Si wewe tu, la muhimu tufanye taratibu zote tumzike.”


Walikubaliana mwili wa mzee Yamungu kuuzika ndani ya chumba chake. Walichimba kaburi kisha kila mmoja kwa imani ya dini yake alimuombea mzee huyo apumzike kwa amani kisha walimzika.


Baada ya kumzika walijikuta wakiwa njia panda kwani hawakuwa wamejipanga lolote baada ya kifo cha mzee Yamungu wafanye nini.


“Sasa tutafanya nini baada ya kifo cha mzee?” Ambe aliuliza.


“Kilichobakia ni kujipanga kuhakikisha tunaondoka hapa na kuhamia mjini.” Mabina alijibu.


“Lakini si unajua tunatafutwa?”


“Ni kweli, lakini bado tuna deni la uonevu juu yetu.”
 
Back
Top Bottom