JOTO LA MAPENZI-9
ILIPOISHIA;
Mama uamuzi wangu ni huo, nimekuja hapa kukuelezea uamuzi wangu kuwa ninabadili dini na muda wowote nitafunga ndoa na Koleta.
Hiyo ndoa yako utaifanya peke yako, nakuapia kama kweli utabadili dini basi utafute wazazi na ndugu zako, lakini kwetu utakuwa umejivua.
ENDELEA...
Msimamo wangu uko palepale hata nitengwe na dunia nzima lakini siwezi kumpoteza Koleta kama amejitoa kwangu lazima na mimi nijitoe kwake.
Wee mtoto kwa nini ututie aibu, kumbuka baba yako kakutafutia mwanamke na mipango inakwenda vizuri.
Huyo mnayemtafuta ni wenu lakini wangu ni Koleta, kwa mara ya kwanza nilikosa heshima kwa kipenzi mama yangu.
Hebu nenda kajiulize tena nipo chini ya miguu yako usifanye hivyo ni aibu mwanaume kumfuata mwanamke tena ukiwa mtoto wa kiislamu.
Pamoja na yote aliyozungumza mama sikuwa na chochote cha kukibadilisha kwenye akili yangu. Niliondoka na kurudi kwangu, nakumbuka siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kutambulishwa kanisani kwa kumtambua Yesu ndiye Bwana na Mwokozi wa maisha yangu.
***
Majira ya jioni Koleta alinifuata na gari la kwao na kunipeleka kanisani, huko nilipokelewa na shangwe na vigelegele. Baada ya ibada nilitambulishwa mbele ya waumini waliokuwa wamejaa kanisani. Historia yangu iliwavuta wengi kutokana na kuhama dini yangu ya kuzaliwa ya uislamu na kuamua kumfuata Bwana Yesu kwa ajili ya Koleta.
Kwangu ilikuwa historia ambayo haikuwahi kutokea maishani mwangu, baada ya kutambulishwa, waumini walifanya harambee ya kunichangia fedha kwa ajili ya kujiunga na dini yao.
Fedha ya papo kwa papo nilipata milioni sita, baada ya utambulisho nilipewa jina la Godbless. Kwa kifupi jina langu niliitwa God, baada ya ibada nilirudi na familia ya mpenzi wangu hadi kwao kulikokuwa na sherehe ndogo ya kubadili dini.
Mzee Michael Mtoe baba mzazi wa Koleta aliahidi kusimamia kila kitu katika maisha yangu ikiwemo kutupatia nyumba na gari baada ya kufunga ndoa. Kazi yangu ilikuwa ya kuajiriwa, aliniahidi kunibadilisha na kunipeleka kusimamia miradi yake na kunilipa mara sita ya pesa niliyokuwa nikilipwa nilipokuwa nafanya kazi.
Baba mkwe aliniahidi baada ya wiki nitaianza kazi huku wakijipanga kwa ajili ya maandalizi ya ndoa yetu. Nilijiona kiumbe mwenye bahati ya mtende kuoa katika familia yenye uwezo, niliamini muda si mrefu nami nitaishi maisha niliyokuwa nikiyaota ndotoni ya kumiliki nyumba na gari.
Baada ya sherehe nilirudi nyumbani kupumzika kusubiri ahadi za baba mkwe, nikiwa nimejipumzisha nyumbani kwangu, nilipokea ugeni akiwemo baba, mama na baadhi ya ndugu zangu ambao walipata taarifa zangu za kubadili dini siku ile na kutambulishwa rasmi kanisani.
Huwezi kuamini siku ile nilirudi na cd za gospo ambazo nilikuwa nasikiliza huku nikisoma agano jipya kufuatia vipengele nilivyoelezewa na mchungaji nianze kuvisoma.
Ambe nini kimekusibu mwanangu? Baba aliniuliza huku akiangalia Biblia niliyokuwa nimeshikilia mkononi.
Tatizo nini? Niliwauliza huku nikikaa kwenye kochi na kuweka agano jipya pembeni.
Ni kweli umebadili dini? Mama aliniuliza.
Ndiyo.
Mwanangu nini kimekusibu, kwa ajili ya mwanamke?
Ni uamuzi tu, kwani kinachompeleka mtu peponi ni dini au matendo yake?
Ambe hayo ni maneno gani? Mama alizidi kuchanganyikiwa.
Sikilizeni wazazi wangu, uamuzi wangu si kuwavunjia heshima bali ni uamuzi ambao kwa upande wangu una faida kubwa kuliko hasara.
Sikiliza wewe mpumbavu kuanzia leo sisi siyo wazazi wako, pia nisikuone kwangu, baba alisema kwa hasira.
Baba alikuja juu, lakini maneno yake makali hayakulingana na huruma niliyoifanya kuokoa maisha ya mpenzi wangu. Nilikuwa nipo tayari kwa lolote kwa kuamini hata Mungu anajua kiasi gani nilivyoweza kuokoa uhai wa mtu. Sikuona umuhimu wa kungangania dini wakati nampoteza mtu muhimu maishani mwangu.
Waliamua kuondoka huku mama akinibembeleza kwa kunipigia magoti akitokwa na machozi. Lakini nilimshangaa kama angekuwa tayari Koleta afe kwa ajili ya dini.
Pamoja na kuumizwa na kitendo cha mama yangu mzazi kunipigia magoti bado sikuona sababu ya kuwasikiliza wao wakati uamuzi wangu ulikuwa ukiokoa maisha ya mtu. Baada ya kuondoka niliwapigia simu nyumbani kwao Koleta kuwaeleza familia yangu ilivyopokea. Mama yake Koleta alinipa moyo kwa kunieleza:
Mwanangu usiwe na wasiwasi waache wakutenge lakini nakuahidi hutajutia uamuzi wako wa kubadili dini pia kuokoa maisha ya mwanangu. Baada ya muda utakuwa na maisha mazuri, wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuja kukuomba radhi kurudisha uhusiano.
Maneno yale yalinitia moyo na kuamini pamoja na familia yangu kuamua kunitenga bado kuna nafasi ya kusameheana kwa kuamini hasira ndizo zilizotawala lakini kama wangekaa chini hasira zingewaisha na kuona jambo la kawaida.
***
Jioni Koleta alinifuata na kunipeleka kwao kutokana na wito wa baba yake, nilipofikishwa mbele ya mzee Michael Mtoe ambaye alinipa habari njema kuwa amenipatia kazi katika mmoja miradi wake ulio mkoani kama msimamizi mkuu na mshahara wangu ulikuwa mzuri pamoja na nyumba ya kukaa pia usafiri wa kutumia.
Kwangu ilikuwa ndoto ya mchana maisha yangu kubadilika ghafla kiasi kile.Katika maisha yangu sikuwaza kuna siku nitakuwa mtu mwenye heshima mbele ya watu kwa kutoa amri na kusikilizwa pia kutembelea gari langu, nyumba yenye kila kitu pia mshahara mara tano ya awali.
Mshahara wangu wa kawaida ulikuwa laki mbili na nusu. Lakini kwa kazi ya kusimamia mradi wa baba mkwe nililipwa milioni moja na nusu.
Nilikubaliana na maneno ya mama Koleta kuwa mafanikio yangu yatawafanya familia yangu kujirudi hata kuniomba msamaha. Niliamini ndani ya mwaka ningekuwa na pesa nyingi hata kumalizia nyumba ya familia iliyokuwa imesimama baada ya baba kustaafishwa kazi.
Huwezi kuamini maisha yetu yalianza kuyumba baada ya baba kustaafishwa kazi kiasi cha kushindwa kumalizia nyumba yetu ambayo ilikuwa ikikata mwaka wa saba ipo vile vile. Niliamini uwezo wangu wa kipesa utaweza kunirudisha kwa wazazi wangu.
Kuamua kubadili dini haikuwa kama siwapendi wazazi wangu la hasha, wazazi wangu nilikuwa nikiwapenda sana lakini baada ya kuzaliwa na kunilea ilifika hatua ya kujua zuri na baya. Wazazi wao walibakia kama walezi na washauri lakini uamuzi wa mwisho nilibaki nao mwenyewe.
Niliamini kabisa suala nimuoe mwanamke wa aina gani lilibaki kwangu, sikuamini kabisa dini ni kigezo cha kumpoteza mpenzi wangu ambaye alikuwa tayari hata nimtoroshe ili asinipoteze. Bado niliendelea kuwaheshimu wazazi wangu japo walinisusa kwa uamuzi wangu wa kubadili dini.
Lakini niliamini ipo siku watakubaliana na uamuzi wangu na kuniona nilichokifanya kilikuwa sahihi.
****
Nilipewa wiki ya kujiandaa kabla ya kuondoka, lakini ajabu muda wote huo sikupata nafasi ya kuwa karibu na mpenzi wangu ili tupange baada ya kuondoka kipi kifanyike. Kingine kilichonishangaza kilikuwa baada ya kuondoka kwenda mkoa wa mbali ambao ni zaidi ya saa kumi na saba kwa basi toka pale.
Swali lilikuwa harusi yetu itakuwaje kama nitakuwa mbali na mwenzangu ambaye sikuruhusiwa kwenda naye kwa vile alikuwa bado mchumba wangu. Lakini niliamini huenda nakwenda kuzoea mazingira ya kazi kisha ndipo mipango ya harusi ifuate.
Sikutaka kuuliza maswali yoyote juu ya harusi yangu kwa kuamini wenyewe ndio wanaojua kila kitu. Niliamini mpaka kunipa kazi nzuri tena yenye mshahara mzuri kulikuwa na mipango mizuri iliyokuwa mbele yangu hivyo sikutaka kula na kipofu nikamshika mkono.
Pamoja na mipango yao mizuri bado nilitakiwa niwe karibu na mwenzangu hasa kipindi kile ambacho nitakuwa naye mbali kwa kipindi kisichojulikana. Sikuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana lakini nikiwa katika kipindi kigumu cha kutomuona mpenzi wangu hata kuja kuniaga.
Siku moja kabla ya kuondoka nilipewa pesa za kijikumu ninapokwenda, kwa kweli zilikuwa pesa nyingi sana ambazo kwangu niliona kama ni ndoto kushika pesa nyingi kama zile. Usiku majira ya saa nne baba mke mzee Michael Mtoe alikuja nyumbani kwangu kuja kuniaga. Baada ya kukaa alinieleza:
Kijana kesho ndiyo siku yako ya kwenda kuanza kazi niliyokutuma pia kutengana na mpenzi wako. Katika hali ya kawaida najua utakuwa na upweke pia majonzi ya kuwa na mwenzako mbali. Lakini nimefanya hivyo kwa maana kubwa moja kukuandaa kimaisha ili uweze kuishi na binti yangu katika mazingira mazuri.
Kumbuka leo nipo kesho sipo hivyo nakufundisha ili siku moja uweze kuiongoza familia yako bila kutegemea msaada wa mtu. Nakuomba kitu kimoja unapokwenda huko kama mwanaume ondoa mawazo ya nyumbani tafuta maisha kwa nguvu zako zote ili uonekane mwanaume mbele ya wanaume.
Hata nikikubali muoane leo bado mtakuwa tegemezi kwa vile huwezi kumlea mwanangu kama nimleavyo kwa vile huna fedha za kutosha. Kazi niliyokupa na masilahi mazuri baada ya muda utaweza kusimama wewe kama wewe.
Hivyo basi nakuomba ukiondoka hakikisha huwasiliani na mwenzako mpaka upate ruhusa yangu. Kama utakwenda kinyume na maagizo yangu utanitafuta ubaya, naomba kipindi ninachowaandalia maisha yenu kaa mbali na mwanangu najua huwezi kuwatumikia mabwana wawili mapenzi na kazi siku zote mapenzi huchukua nafasi na penzi siku zote ni kitovu cha uzembe.
Hivyo nakuomba kipindi chote msahau Koleta mpaka hapo utakapokuwa tayari kummiliki kama mke ruksa kurudi na kumuoa siwezi kuyaingilia maisha yenu vile ninyi wenyewe mmechaguana.
Kila tatizo lolote la pesa au ushauri wasiliana na mimi tu hata mama yako hana ruhusa ya kuwasiliana na wewe. Nina imani umenielewa?
Nimekuelewa.
Nilijibu kwa mkato kwa vile sikuwa na kuuliza kutokana na maneno yote kumaliza japo niliamini kabisa kanipa mtihani mkubwa maishani mwangu. Kukaa mbali sawa lakini hata mawasiliano. Mmh! Nilijiuliza hata kutafuta maisha kwa jasho la damu bado nilitakiwa kuwasiliana na mpenzi wangu ambaye angekuwa ni sehemu ya kichocheo changu kutafuta maisha kwa nguvu zote.
Nikikumbuka nimemuacha mpenzi wangu aliyekuwa akinisubiri kwa hamu ili tuishi maisha tuliyo yasubiri kipindi kirefu.
God...God,baba Koleta aliniita zaidi ya mara mbili.
Eeh...Aah! Naam, nilijikuta nikichanganya majibu kutokana na kuhama kwenye dimbwi la mawazo mazito.
Najua bado jina hujalizoea lakini utalizoea tu.
Mzee Michael alisema bila kujua mwenzake sikubabaikia jina bali mtihani mzito, niliamini kubadili dini ni kuwa karibu na mpenzi wangu lakini yalizuka mapya ya kwenda mbali kufanya kazi kisha nisiwasiliane na mpenzi wangu. Upande wa pili niliona sawa kwa vile muda si mrefu nitakuwa nimejipanga kimaisha.
Ndi..ndi..yo mzee.
Nashukuru kwa kunielewa ila ukienda kinyume unaweza kupoteza hata uhai wako.
He! Makubwa nikienda kinyume naweza kupoteza maisha, kwa kweli kwa kauli ile ilinifanya niulize:
Mzee mbona kama safari imejaa vitisho?
Siyo vitisho, kumbuka sikutaka umuoe mwanangu lakini umetumia hila za kubadili dini ili uihadae familia yangu. Hilo kwangu halikunishtua sana kwa kuamini baada ya kuoa unaweza kubadili dini na kurudia dini yako. Upande wa hila zako naamini umenishinda kwa vile sina uwezo wowote wa kukuzuia.
Nachotaka ni kuyatengeneza maisha yako na mwenzako ili msimame hata kama sipo.
Sasa mbona unanitishia maisha?
Si kwanza nakutisha bali sitaki kuona mwanangu akiishi maisha ya kubahati na kama utafanya kwa jeuri yako sitasita kuchukua uamuzi wowote kwako.
Basi mzee wangu kama tunaelekea kutishana maisha basi naomba nirudi katika dini yangu nikuache na mwanao.
Kijana unataka mke wangu nimwambie nini, kipi kibaya nilicho kifanya kitakacho kurudisha dini yako au unataka Koleta ajiue?
Sipo tayari kumuona Koleta akifa, lakini naomba usiniwekee vitisho kwani kila kitu nimekifanya kwa faida yenu ili tu niwe na Koleta.
Basi nimekuelewa, nakuomba tuliyozungumza yabakie siri yetu tulikuwa tukizungumza wanaume wawili. Na kuahidi kama utanisikiliza harusi yako na Koleta inakuwa ya kihistoria pia mtaishi maisha ya peponi.
Nimekuelewa baba.
Basi kesho alfajiri nakutakia safari njema.
Nashukuru baba yangu.
Jana ulipewa kiasi gani cha kujikimu kimaisha.?
Milioni mbili.
Sasa hivi nitakuongezea milioni tatu jumla utakuwa na milioni tano.
Asante baba.
Hujui tu, nina mpango mzito na wewe ya kukufanya siku moja uishi kama mfalme hata kuuvuka mara kumi utajiri wangu.
Nitashukuru baba.
Furaha ya pesa ilinifanya nisahau yote tuliyozungumza na kumuona mzee Michael Mtoe ni binadamu mwenye utu na mwenye kujua thamani ya maisha ya mtu.
Sasa nikuache upumzike, kesho utapitiwa na gari majira ya saa tisa na kuanza safari yako nina imani mpaka saa kumi na mbili au saa moja jioni bila matatizo utawasiri. Kila kitu nimekwisha kipanga ukifika utapelekwa moja kwa moja nyumbani kwako.
Kuna mfanyakazi wa kike ambaye atakusaidia kwa kazi ndogo ndogo, nina imani utainjoi maisha. Pesa za matumizi zikiisha nijulishe hazihusiana na mshahara wako. Nina imani umeona kiasi gani ninavyoonesha kukujali kwa vile umejitolea kuyaokoa maisha ya mwanangu.
Nashukuru mzee wangu nakuhakikishia kuyafanya yote uliyonieleza.
Utaona nitakupa kitu gani katika harusi yako ni zawadi ambayo hutaisahau maishani mwako.
Nakuhakikishia kuzingatia yote ili niipate hiyo zawadi.
Baada ya mazungumzo yaliyoishi saa sita usiku, mzee Michael Mtoe aliniaga na kuondoka. Baada ya kuondoka nilijikuta nikisahau mazungumzo yote zaidi ya kuingia chumbani na kuzimwagia fedha zote kitandani na kuanza kuzihesabu. Niliyaona maisha yangu kama ya hadithi ya mtu kuhadithia kwa muda mfupi kisha hadithi kwisha kwa muda huo mfupi mtu alikuwa maskini na baadaye kuwa tajiri. Niliona hadithi hiyo ilinigeukia mimi, kwa mwezi mmoja nilitengeneza zaidi ya milioni kumi toka mchango wa kanisani na pesa za kijikimu katika maisha yangu mapya pia mama Koleta alinipa milioni mbili za siri mzee asijue.
Nilijikuta nikisahau hata mazungumzo yangu na mzee Michael baba yake Koleta na kuzichukua zile fedha alizonipa na kwenda kuzimwaga kitandani ili nizihesabu. Ile kwangu ilikuwa ndoto ya mchana sikuwahi kuwaza kuna siku nitashika milioni mkononi, lakini siku ile nilikuwa na milioni zaidi ya kumi.
Nikiwa katikati ya kuzihesabu maburungutu ya fedha, mlango uligongwa. Niliacha kuhesabu na kuzirudisha haraka fedha zote kwenye begi na kuziweka kwenye kabati na kutoka hadi sebuleni na kupaza sauti kuuliza:
Nani?
Mimi.
Wewe nani?
Ambe leo unaniuliza mimi nani, hebu fungua mlango.
Mmh! Sauti ile ilinishtua baada ya kuishitukia.
Koleta, niliita.
Kuna mwingine tena zaidi yangu anayeingia ndani mwako?
Sikuhitaji kuongeza neno lolote zaidi ya kufungua mlango, nilishtuka kumuona muda ule, wazo la haraka labda alifuatana na baba yake.
Karibu mpenzi.
Asante.
Mbona usiku sana?
Nimekuja saa mbili zilizopita.
Ulikuja na baba?
Hapana peke yangu.
Koleta mbona ulitoweka kwenye mboni za macho yangu ghafla?
Ambe, aliniita jina langu la zamani.
Niite jina langu jipya.
Hilo jipya watakuita wao sio mimi, moyo wangu huchanua kulitaja jina lako halisi nilililolizoea hata ndani ya ndoa yetu sitakuita God, nitakuita Ambe mpaka pumzi zangu zitakapogota.
Mmh! Hebu nijibu swali langu.
Ambe hata sielewi kuna kitu gani kilichopo ndani ya familia yangu.
Kwa nini?
Kumekuwa na vikwazo vingi eti natakiwa kuwa karibu na wewe baada ya kuoana. Niliwaeleza basi hata univishe pete ya uchumba kabla ya kuondoka ili niweze kuwa karibu na wewe hata mara moja. Lakini hata hicho wakimekikataa kwa kweli hata sielewi wana lengo gani katika penzi letu.
Koleta nimezungumza muda mfupi na baba japo nilikuwa vigumu kumuelewa haraka nia na madhumuni yake kwetu, lakini baada ya muda nilielewa lengo lake la kutuweka mbali kwa muda.
Ambe mimi siamini kama lengo la baba ni zuri kwetu.
Kwa nini?
Mmh! Hebu nenda kwanza sijapata uhakika wa kitu nilichokiwaza kama ndicho usishangae kuniona nimekufuata huko huko.
Kuna nini tena? Kauli ya Koleta ilinishtua.
Nina wasiwasi safari yako ikawa mwisho wa mapenzi yetu.
Una maana gani? Kauli ile ilizidi kunishtua.
Kuna njama za kulivunja penzi letu kwa nguvu zote.
Mbona sikuelewi!
Ndio maana nikamkwambia wewe nenda lolote litakalotokea nitakujulisha.
Na mbona upo hapa usiku wote huu?
Ambe unaondoka lini?
Saa tisa usiku wa leo.
Ulitaka nikuage lini kama si muda huu?
Kwa nini usije mchana?
Ambe naomba uende lakini nitakupa jibu la kile ambacho nakiona.
Kipi hicho? Maneno ya Koleta yalionesha ana siri nzito moyoni mwake.
Kuwa muelewa nikisema leo naweza kusema ikawa sivyo ni mawazo yangu niache nipate ushahidi kamili.
Koleta kuna nini mpenzi wangu? Mbona leo umekuwa na maswali akilini mwangu kuliko majibu.
Unajua siamini kama kweli baba yangu amekubali kwa moyo wake tuoane.
Kwa nini?
Mbona ananiwekea mipaka hata simu hataki tuwasiliane hapo unaona kuna nini?
Najua utasema hivyo hata mimi nilijua kama unavyowaza wewe, lakini baadaye nilimwelewa. Nia yake ni mimi kusimama ile tuweze kuoana.
Sawa anataka usimame, kwa nini tusiwasiliane? Mbona mwanzo sikuwa na mipaka kama sasa?
Nakuomba uvumilie muda si mrefu tutaishi yale maisha tuliyokuwa tukiyaota ndotoni. Amini baada ya mwaka mmoja tutakuwa watu wengine.
Yaani tuoane baada ya mwaka mmoja?
Hapana ila naamini kwa mimi nitakuwa nimesimama vizuri.
Ambe nataka kukuambia kitu, kuna siri ipo nyuma ya moyo wa baba ambayo nina wasiwasi nayo sana.
Nakuomba niamini nikwenda kutafuta maisha nikirudi tutaishi maisha ya raha.
Ambe nilikupenda ulivyo sikukupenda kwa mali, yote haya yametokea wapi?
Mmh! Lilikuwa swali gumu sana kulijibu.
Ambe nakueleza ukweli kuwa safari yako ya kuwa mbali na mimi ni njia ya kulipunguza nguvu penzi letu.
Koleta nakuahidi mpaka kubadili dini na kukosana na familia yangu hakuna kitu kitakacho kuondoa moyoni mwangu, hata kifo kitauondoa mwili wako lakini si upendo wako moyoni mwangu.
Hilo nalijua mpenzi wangu, lakini penzi letu lipo kwenye vita nzito.
Hata kama ipo kwa vile sisi wenyewe tumependena pasipo ushawishi wa mtu tutashinda.
Ambe kwangu nilikufungia moyoni mwangu kisha ufunguo nikautupa bahari, nakuomba huko unapokwenda ukigeuka basi pembeni yako unione mimi.
Hilo nalijua mpenzi wangu, toka nilipojua kupenda jicho langu la kwanza kuona mwanamke mzuri lilitua usoni kwako. Nimekuwa kipofu toka nilipokuona sioni mwingine zaidi yako.
Ambe chochote ukisemacho nakikubali kwa vile umenionesha penzi la vitendo, nakuombea uende salama ili tupate tulichokitafuta kwa jasho la mioyo yetu?
Amini baada ya mioyo yetu kupata joto la mapenzi tutapumzika kwenye kivuri cha furaha ya mioyo yetu.
Naomba nikuage mpenzi wangu kabla hujaondoka ili niwahi nyumbani.
Kwa kweli sikuwa na kipingamizi nilimkubalia mpenzi wangu, lakini ajabu siku ile hakutaka tutumie mpira wa kinga kama ilivyo kawaida yetu. Nilipomuuliza kwa nini siku ile hataki tutumie mpira wa kinga.
Sioni umuhimu wa kuutumia kwa vile hiyo ndoa kwangu bado naiona ndoto.
Je, ukipata mimba?
Mimba si yako?
Lakini si tulipanga tuzae mtoto ndani ya ndoa yetu.
Nikimsubiri huenda nisimpate ndoa bora nipate mtoto kuliko kukosa vyote.
Kwa nini?
Ambe hilo swali usiniulize leo ipo siku utajua leo nazungumza nini.
Majibu ya Koleta yalionesha kuna siri nzito moyoni mwake, sikutaka kuuliza maswali mengi nilimpa haki yake mpaka tuliposhtuliwa na honi ya gari kunijulisha safari imeiva. Niliamka kujiandaa huku Koleta akioniomba nimuache alale ataamka asubuhi.
Baada ya maandalizi yote nilimuaga Koleta ambaye muda wote alikuwa akibubujikwa na machozi.
Ambe usinigeuke kumbuka wewe ndiye mabawa yangu ukiniacha sitaruka milele.
Nakuahidi kutimiza ahadi yetu ya muda mrefu.
Asante mpenzi wangu nenda salama.
Na wewe bakia salama.
Tulikumbatiana kwa muda kisha tuliachiana na mimi kwenda ndani ya gari na safari ya kuniweka mbali na mpenzi wangu ilianza.
Nje nilikuta Toyota Land Cruser Vx V8 likinisubiri, ndani ya gari kulikuwa na dereva tu mzee wa makamo kidogo. Niliingia ndani ya gari na safari ilianza.
Vipi mzee, za asubuhi? nilimsalimia dereva.
Nzuri tu kijana, sijui zako?
Namshukuru Mungu, hivi hiyo sehemu ninayokwenda umeshawahi kufika?
Mara nyingi tu.
Mazingira yake yapoje?
Ni pazuri hasa kutokana na cheo chako, vipi umeoa?
Aah! Mzee huna habari kuwa mimi ni mchumba wa mtoto wa mzee Mtoe.
Unamuoa nani?
Koleta.
Mmh! Mbona nasikia Koleta ana mchumba wake mwingine sijui mtoto wa waziri kama sikosei.
Hapana utakuwa umesikia vibaya, Koleta ni mchumba wangu mimi ambaye nimebadili dini kwa ajili yake.
Ha! Kijana ina maana wewe umebadili dini kwa ajili ya mwanamke? Dereva aliniuliza.
Sikuwa na jinsi kwa vile hatua aliyofikia mpenzi wangu haikuwa na njia nyingine zaidi ya kukubali kuikana dini yangu.
Kijana unawajua wanawake walivyo vigeugeu, una wazazi?
Ndiyo.
Wameshiba dini?
Ndiyo.
Si kweli siamini mzazi wa Kiislamu kumuachia mtoto wake kuingia ukristo.
Ni kweli wazazi wangu hawakukubali.
Kama hawakukubali nani aliyekupa ruhusa ya kufanya hili.
Ni mimi mwenyewe bila hivyo Koleta angejiua.
Mmh! Siwezi kukuingilia uamuzi wako kwa vile wewe ndiye uliyebeba mzigo, uzito wake unaujua mwenyewe.
Lakini mzee hata ungekuwa wewe ungechukua uamuzi huu, familia zetu zote ziliweka ngumu kuturuhusu kuoana kwa kila mtu na dini yake.
Baada ya kubadili dini nini kimefuata?
Nimetengwa na familia yangu.
Kwa hiyo umeona mapenzi matamu kuliko familia yako?
Najua familia yangu ndiyo muhimu lakini umuhimu wa jambo hili ni mkubwa kuliko kutengwa na familia yangu.
Sasa unasema ulibadili ili umuoe mbona umeondoka bila kuoa?
Amesema kunipeleka kule ni kujijenga kimaisha kabla ya ndoa, lakini ajabu amesema nisiwasiliane na mpenzi wangu.
Kijana mbona mnafanya mchezo wa kuigiza itakuwaje uwe mbali na mpenzi wako kisha msiwasiliane?Hata mimi nashangaa, mzee Mtoe amenitishia kama nitakwenda kinyume tutaelewana vibaya.
Mdogo wangu kuna kitu kina siri nzito, nenda lakini kuna siku utaniambia.
Je, Koleta na Ambe watafanikiwa kufunga ndoa na kutimiza ndoto yao? na Baba yake koleta ana mpango gani juu ya hatima ya ndoa ya mwanae? tuungane jioni mnamo wa kuanzia saa moja ili kujua nini kiliendelea nashukuru kwa uvumilivu wako have a nice time