SoC03 Jinsi jeshi la Magereza na Jamii kwa ujumla zinavyopelekea wafungwa kurudia uhalifu pindi wanapomaliza vifungo vyao

Stories of Change - 2023 Competition

Lidafo

JF-Expert Member
Sep 26, 2019
551
747
Tatizo la wahalifu waliohukumiwa wanapomaliza vifungo na kurudi mitaani kisha kuendelea na uhalifu ni moja ya changamoto katika jamii zetu pamoja na kazi nzuri inayofanywa na jeshi la magereza ya kuwarekebisha wafungwa waliohukumiwa ili watoke wakiwa raia wema lakini bado jukumu hili halitekelezwi kwa kiwango cha juu.

Sababu zinazopelekea wafungwa wengi kurudi mitaani na kuendelea na uhalifu zimegawanyika katika sehemu mbili moja ni Jeshi la Magereza lenyewe na sabubu ya pili ni jamii jinsi inavowapokea wafungwa walio maliza vifungo vyao.

1. Jinsi Magereza zinapelekea wafungwa kurudia uhalifu pindi wanapomaliza vifungo vyao.

  • Kutokufundishwa ujuzi kwa wafungwa wasio na ujuzi wanaotumikia vifungo vya muda mfupi
kuna wafungwa ambao wamehukumiwa miezi mitatu, sita au mwaka mmoja na hawana ujuzi wowote aina hii ya wafungwa mara nyingi hufundishwa ujuzi kwa kiasi kidogo hali hii inapelekea wao kurudia uhalifu wanapo rudi miataani, Kundi hili linatakiwa kufundishwa ujuzi kama wa kushona, kujenga na kuchomelea kwa nguvu kubwa sana ili wale waliofanya uhalifu kwa sababu ya kukosa kipato na ugumu wa kazi iwe rahisi kwao kufanya kazi wanapo rudi mitaani.

  • Idadi ndogo ya wataalamu wa saikolojia na madaktari wa afya ya akili ndani ya jeshi la magereza
Kitendo cha mtu kufungwa kina kuja na matokeo hasi katika saikolojia ya mfungwa, Jambo hili linaweza pelekea badala ya mfungwa kutoka na tabia njema akatoka na tabia mbaya zaidi hii ni kutokana na ukweli kwamba sio wote wanaofungwa wanakuwa na hatia lakini pia kuna wanaofanya uhalifu kwa kuwa na historia ya kumbukumbu mbaya katika ukuaji wao, Visasi na wengine saikolojia yao ya akili tayari inashida, Hivyo basi jeshi la magereza linabidi kuwa na askari wasomi wa maswala ya afya ya akili na saikolojia ili kutuliza hisia mbaya za wafungwa na kuwaweka sawa ili wawe na utayari wa kukubali kubadilika.

Mfano mfungwa yupo gerezani kwa kesi ya kumshambulia mtu ambaye ana kisasi nae, Mtu huyu anapokuwa gerezani sio wa kufanyishwa kazi ngumu tu bali anatakiwa pia kushauriwa na wataalamu ajue kuwa maisha ya visasi yatampelekea kwenye matatizo zaidi. Lakini anapoishia kufanyishwa kazi ngumu pindi atakapomaliza kifungo chake bado hisia za kisasi zipo katika akili yake hivyo ni rahisi kwa mtu huyu kurudia kosa na akaishia kurudi magereza mara ya pili.

Lakini pia kuna wafungwa wamefanya uhalifu kwa sababu ya ulevi uliopindukia wa madawa ya kulevya kama ulaji wa unga na uvutaji bangi, Aina hii ya wafungwa ni lazima wapewe ushauri wa kisaikolojia na wafanyiwe tiba za kuweka akili zao sawa kwani kutokufanya hivyo kutapelekea mfungwa kurudia sababu zilizopelekea kufanya uhalifu na hatimae kujikuta anavunja sheria anaporudi mtaani.

2. Jinsi jamii inapelekea wafungwa kurudia uhalifu pindi wanapomaliza vifungo vyao.

  • Mapokezi mabaya kwa wafungwa waliotoka gerezani
Jamii zetu zimekuwa zikiwanyooshea kidole, kuwasema vibaya na kutowapa ushirikiano wafungwa waliomaliza vifungo vyao, Hali hii inapelekea kujihisi kua jamii imewatenga na kuwanyanyapaa hivyo anaona kimbilio lake ni kurudi gerezani na itambidi yeye kufanya uhalifu wa makusudi ili aweze kurudi gerezani kwani jinsi jamii ilivyo mpokea anajihisi kutengwa na kutokukubalika

Mfano kuna weza kukatokea uhalifu mtaani jamii yote ikamshtumu yeye ndie kufanya hata kama hakuna ushahidi au dalili yoyote inayoonyesha kuwa yeye ndie aliefanya uhalifu huo hali hii inapelea kuhisi kukataliwa na jamii yake na hivyo basi kuona ni bora akafanya uhalifu wa kweli kuliko kila siku kuishi kwa kwa kushutumiwa mambo ambayo hajayafanya.

Nini Kifanyike ili wafungwa wanaporudi mitaani waachane na uhalifu na wawe raia wema?
  • magereza yetu kubadili aina ya uendeshaji wa magereza kutoka kua vituo vya mateso na kuwa taasisi inayoendeshwa kijeshi lakini inayotoa huduma kwa jamii kwa ujumla wenye kujitosheleza kwa kuwa na rekodi nzuri ya wafungwa itakayosaidia kushughilika na tatizo lililopelekea mfungwa kufanya uhalifu na kuliondoa tatizo hilo katika maisha ya mfungwa kwa kumfundisha, Kumshauri na Kumwelekeza kwa kumjenga kuwa mtu mwema hii iwe ni pamoja na kupinga vikali mambo yote yanayochochea ufanywaji wa uhalifu kama uvutaji wa bangi ,unywaji pombe,matusi na vitendo vya uasherati ndani ya magereza kwa kufanya hivi jeshi la magereza litatimiza kikamilifu jukumu lake la kuwafanya wafungwa kuwa raia wema ili wanaporudi katika jamii waweze kuishi kwa kufuata sheria za nchi.

  • Jeshi la magereza kuongeza fani nyingi wanazofundishwa wafungwa magerezani, Magereza yasiishie kufundisha kilimo, Ufugaji, Kushona na Ufundi tu bali iongeze fani nyingi na mafunzo tofauti ya kuwafundisha wafungwa hii itasaidia mfungwa kuwa na machaguzi ya kujifunza na kuwa na ujuzi wa fani anayoipenda mfano matumizi ya komputa, Ufanyaji biashara kwa njia ya kisasa, Uwekezaji na ujasiriamali mdogomdogo .

  • Kutumia viongozi wa dini na kuruhusu sehemu za kufanya ibada kwa wafungwa, Jeshi la magereza lihakikishe kila gereza inakuwa na sehemu za kufanyia ibada kwa watu wa dini mbalimbali lakini pia kuwaomba viongozi wa dini kuja mara kwa mara kuwatembelea na kuwafundisha wafungwa juu ya imani zao, Tukumbuke kuwa hakuna imani inayoruhusu uhalifu na imani zote zinalenga kuilinda jamii dhidi ya machafu hivyo basi kupitia imani ni njia nzuri sana ya kumfanya mtu kuwa mwema na kuishi vizuri na watu kwa kufuata sheria.

  • Jamii ifundishwe na ielekezwe jinsi ya kuishi na raia aliyetoka kutumikia kifungo, Jeshi la polisi, Jeshi la magereza pamoja na serikali za mitaa washirikiane kuandaa semina na mikutano kwa jamii kuwaelekeza jinsi ya kuishi na mtu aliyetoka kutumikia kifungo hii itapunguza kasi ya kunyanyapaliwa na kutengwa kwa wafungwa na hivyo kuwa na mahusiano mazuri kati ya mtu aliyetoka kutumikia kifungo na jamii yake.

Hitimisho

Niseme kuwa jeshi la Magereza na jamii kwa ujumla wanaweza kumbadilisha mfungwa kutoka kuwa mvunjaji wa sheria na kuwa raia mwema hivyo basi ni vizuri kwa jeshi la magereza kupitia sera zake na kuzibadili pale inapobidi ili kuendana na utekelezaji wa majukumu yake lakini pia jamii kuacha kuwa sehemu ya kuongeza matatizo na kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuonyesha kuwajali wafungwa wanapomaliza vifungo vyao.
 
Back
Top Bottom