Kwa hali ilivyosasa naamini ndani ya masaa 72 yajayo yataamua Misri inaelekea wapi. Kuna dalili zote kuwa bila ya Mubarak kuachia ngazi wananchi Misri hawatakoma. Ukishaanza kuua wananchi wako kwa ajili ya kubakia mabadarakani katika mazingira ya kisiasa unachochea wananchi wako kuzidi kukupinga. Hii ni kanuni ambayo bado haijaoneshwa kuwa ya uongo.
Hivyo, naamini kwa kuangalia hali ya kisiasa sidhani kama mabadiliko ya kiuongozi yaliyofanywa na Mubarak yatatosha kuwatuliza wananchi- Hivyo umebakia uamuzi mmoja tu nao ni jeshi kuchukua madaraka na kuandaa muda wa kurejesha utawala wa kiraia.
Hali bado ni tete mno Cairo,Lakini kwa vyovyote itakavyokuwa inabidi Rais Mubarak aachie uongozi wa nchi.Ujanja alioutumia wa kuvunja Baraza zima la mawaziri akidhani kwamba wananchi wa Misri wataridhika haukufanikiwa,bado kuna shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi wa kada zote Waislamu,Wakristo,Vijana,Watu wazima,Wasomi na Watu wa mtaani la kumtaka Rais ajiuzulu pamoja na serikali yake.Kitendo chake cha kumchagua mshirika wake na rafiki yake mkubwa Omar Suleiman kuwa Makamu wa rais kimezidisha hasira ya watu wa Misri kwani kina tafsiri ya kutaka kuendelea na madaraka na hata akiachia kwa namna yoyote Suleiman atakuwa na nafasi ya kuwa Rais na kumlinda Mubarak na familia yake.kabla ya kumchagua Suleiman hakukuwepo na cheo cha Makamu wa Rais.
Cha ajabu na kustaajabisha ni kwamba mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani wanashabikia kuteuliwa kwa Comrade Omar Suleiman,kwa sababu tu ni mtu pekee katika Uongozi wa sasa ukimuacha Mubarak atakayeweza kukaa na kukubaliana na Utawala wa Washington DC.Makamu wa Rais Omar Suleiman anaelezwa kama mtu mtulivu na mjuzi wa mambo ya usalama kwa kiwango cha juu.
Jeshi la Misri linaongozwa na Field Marshal Mohamed Hussein Tantawi (74) Mkuu huyo wa majeshi pia ndiye aliyekuwa Waziri wa Ulinzi,bado Wanajeshi wapo kimya na ukimya wao si rahisi kujua tafsiri yake,lakini pia jeshi la Misri linasifika sana kwa nidhamu na kujiendesha lenyewe kama Taasisi.Jeshi hilo kubwa na la kisasa lina bajeti inayokadiriwa kufikia $ 5.80 Bil kwa mwaka pamoja na nyongeza ya $ 1.3 Bil kutoka Serikali ya Marekani.Kuna uhusiano mkubwa wa kijeshi kati ya Jeshi la USA na Misri.Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Misri Lt.Gen Sami Hafez Anan alikuwa Marekani wakati vuguvugu la maandamano lilipoanza Misri,ilibidi aondoke kwa haraka Ijumaa kurudi nyumbani kukabiliana na hali ya huko.
Misri ina historia ya Makamu wa Rais kuchukua Uongozi wa Nchi. Abdel Nasser Gamal alipofariki mwaka 1970 Makamu wake Anwar Sadat ndio aliuchukua Uongozi wa Nchi,na sadat alipofariki mwaka 1981 Rais Hosni Mubarak alimrithi,sasa kama historia inajirudia ni wazi kuwa Omar Suleiman ana nafasi kubwa ya kuja kuwa Rais wa Nchi.Tishio kubwa kwa siasa za Misri ni chama cha Islamic Brotherhood,lakini pia kuna candidates kama Mohammed Elbaradei,Ayman Nur,Al-Sayed Al-badawi na Mohamed Badie wana nafasi ya kushinda kama kutaitishwa uchaguzi huru.Vyovyote itakavyokuwa tukio hili la Misri litakuwa fundisho kwa Viongozi wengi wa Afrika,na kwamba Nguvu ya Umma haiwezi kunyamazishwa na Mtutu wa Bunduki.