Wanasiasa Tanzania hawaaminiki (From Majira)
*Wamo polisi, wafanyabiashara, mabosi NGOs
*Imani zaidi ni kwa ndugu, kabila, wanadini
*D'Salaam yaongoza kwa watu wasioaminiana
Na Joseph Lugendo
*Wamo polisi, wafanyabiashara, mabosi NGOs
*Imani zaidi ni kwa ndugu, kabila, wanadini
*D'Salaam yaongoza kwa watu wasioaminiana
Na Joseph Lugendo
WAKATI wananchi wakisubiri uchaguzi wa Tarime, unaotarajiwa kufanyika kesho, utafiti wa kundi la watu linaloaminiwa zaidi nchini umebainisha kuwa wanasiasa, wafanyabiashara, viongozi wa asasi zisizo za Serikali na polisi ni watu 'wasioaminika' kwa jamii.
Utafiti huo uliotolewa hivi karibuni Dar es Salaam, umefanywa na mfumo wa usimamizi wa Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA), ulio chini ya iliyokuwa Wizara ya Mipango Uchumi na Uwezeshaji.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa wanasiasa wameshika nafasi ya 11, viongozi wa NGO ya 12 na polisi ya 13 kati ya makundi 18 yanayoaminika katika jamii.
Kwa mujibu wa takwimu zake, asilimia 78 ya wananchi wanaamini kuwa jamii haina uaminifu huku Jiji la Dar es Salaam likiongoza kuwa na kiwango cha juu cha kutoaminiana cha asilimia 85 ikilinganishwa na vijijini, ambako kiwango cha kutoaminiana ni asilimia 75.
"Watu wazima waliosailiwa waliulizwa, je, kwa ujumla unaweza kusema kwamba siku hizi watu wengi wanaaminika au kwamba watu wengi hawaaminiki? Idadi ndogo tu ya watu wazima waliosailiwa (22%), wanaamini kuwa watu wengi ni waaminifu," inaeleza sehemu ya utafiti huo.
Katika takwimu hizo, kundi linalohudumia jamii lililopewa nafasi ya juu za kuaminika katika jamii ni la viongozi wa dini walioshika nafasi ya pili kwa kuaminika katika jamii na kufuatiwa na kundi la walimu lililoshika nafasi ya nne.
Hata hivyo, takwimu hizo zinaonesha kuwa viongozi hao wa dini wanaaminika sana vijijini kuliko mijini na hasa Dar es Salaam.
Zinaonesha kuwa wakati vijijini viongozi wa dini wanaaminika kwa wastani wa asilimia 48, katika miji mingine wanaaminika kwa wastani wa asilimia 37 na Dar es Salaam kwa asilimia 36.
Kundi lingine linaloaminika kuliko wanasiasa ni kundi la wenyeviti wa vijiji na kata, lililoshika nafasi ya nane likifuatiwa na madaktari na wauguzi, ambao wameshika nafasi ya tisa na viongozi wa Serikali za mitaa walioshika nafasi ya 10.
Udugu na ukabila wakolea
Utafiti huo pia umebainisha kuwa Watanzania wengi wanawaamini ndugu zao wa familia moja au wanaotoka kabila moja kuliko mtu baki.
Hali hiyo imetokana na wasailiwa wengi kutaja kuwaamini wanafamilia, watu wa ukoo na watu wa kabila moja, ambao wameingia katika 'tano bora' ya makundi yanayoaminika katika jamii.
Nafasi ya kwanza ya watu ambao wanaaminika zaidi imeshikwa na ndugu wa familia, nafasi ya tatu ndugu wa ukoo na ya tano watu wa kabila moja.
Uzee ni busara
Mbali na viongozi wa dini, walimu na ndugu wa karibu, watu wenye umri mkubwa pia wamekuwa miongoni mwa makundi bora kumi yanayoaminika katika jamii.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, wanawake wazee wameshika nafasi ya sita na kufuatiwa kwa karibu na wanaume wazee. Hata hivyo, Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kutoamini wazee ikilinganishwa na miji mingine na vijijini.
Vijana ni balaa
Takwimu hizo zimeonesha kuwa vijana wa kike wameshika nafasi ya 16 ya kundi linaloaminiwa katika jamii wakifuatiwa kwa karibu na vijana wa kiume, walioshika nafasi ya 17 huku kundi la wageni wasio Watanzania likishika nafasi ya mwisho ambayo ni ya 18 kwa kuaminika katika jamii. Nafasi ya 15 ilishikwa na wageni Watanzania.