SoC01 Je, viboko hujenga au hubomoa?

Stories of Change - 2021 Competition
Jul 29, 2021
81
158
Kama umekua katika familia ya Kiafrika hasa ya kitanzania kupigwa pale unapofanya kosa kumekuwa ni Jambo la kawaida. Mzazi anaweza kutumia fimbo, mikanda, au kukurushia kikombe, sufuria au chochote kilichokuwa karibu yake. Lakini je tulishachukua muda na kujiuliza hivi hivi viboko tunavyowachapa watoto wetu au wanavyochapwa na walimu shuleni je huwasaidia? Je kumchapa mtoto humsaidia abadilike au abadilishe tabia yake mbaya na kuwa nzuri au la?

Taarifa kutoka katika gazeti la Mwananchi la tarehe 29/01/2021 ambapo mwanafunzi wa kidato Cha nne alilazwa katika kituo Cha afya cha Mwagika, baada ya kuchapwa viboko na Mwalimu aliye julikana kwa jina la Sara Obby, aliyemtuhumu kwa kosa la kuchukuana kiazi kimoja katika kimoja katika chakula kilichokuwa kimeandaliwa na Mwalimu huyo.

Na pia kutoka katika gazeti la mwanachi la agosti 28, habari ilitolewa kuwa aliyetambulika kwa jina la Sperius alifariki dunia baada ya kuchapwa viboko na Mwalimu wake kwa kudaiwa kuwa ameiba mkoa wa watu wengine.

Kutoka na gazeti la Jambo Tanzania (Star Tv) mwanafunzi wa shule ya Sekondari Idodi wilayani Iringa amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa baada ya kupigwa viboko 100 na Mwalimu wake baada ya kutuhumiwa kuiba simu na baada ya hapo mwanafunzi huyo alifungiwa bwenini kwa muda wa siku tatu ili kuficha siri hiyo.

Nadhani hiyo mifano hai ambayo nimeitoa hapo juu itakuwa imekupa mwangaza kidogo na kuhusu athari za kuchapa mtoto.

Imekuwa kawaida kuwa mtoto anapokosea tu kidogo anachapwa hata mimi nimepitia huko, lakini athari zake ni kubwa ukija kulinganisha na faida. Viboko humfanya mtoto akuchukie kama mzazi, mlezi au mwalimu wake.

Viboko humuharibu mtoto kisaikolojia, kwasababu inamfanya akuone adui na sio rafiki yake. Pia hutengeneza utengano na kuondoa ukaribu kati ya mtoto na mzazi au mlezi. Kibaya zaidi viboko humfanya mtoto amuogope mzazi wake.

Nasema Ni kibaya kwasababu mtoto hukutana na mambo mbalimbali na hivyo anatakiwa kumjulisha mzazi wake kupata ufumbuzi na usaidizi wa jinsi ya kuvikabili. Sasa kama anamwogopa mzazi wake unategemea ataenda kwa nani? Hapa ndipo watoto wengi huangukia kwenye makundi mabaya na wanaume na tabia zisizo faa kama ulevi, na uzinzi. Na nyakati hizi watoto wengi wapo hatarini kufanyiwa ukatili wa kijinsia na kama wanawaogopa wazazi wao, hawataweza kuongea nao na kuwaambia hivyo huu ukatili utaendelea kwa muda mrefu mpaka mzazi atakapo kuja kugundua na madhara makubwa yatakuwa yameshatokea kwa muda huo.

Wazazi ,walezi na walimu inabidi tutafute njia mbadala ya kumkanya mtoto, ambayo haitamfanya mtoto atuchukie au kutuogopa, wala kuleta utengano kati yetu. Kutoka BBC habari iliyoandikwa na Roberto Schmidt, anasema kuwa, “Utafiti umebaini kuwa njia nzuri ya kumkanya mtoto asirudie kufanya Jambo baya alilolifanya ni kumueleza mtoto kwa upole bila ya kumdhuru au kuharibu mahusiano yenu.

Kutokana na utafiti uliofanyika na chuo kikuu Cha Michigan imegundulika kuwa, katika uhalisi, wazazi ambao wanawaadhibu watoto kwa kuwapiga, watoto wanakuwa watukutu zaidi.

Na utaweza kujiuliza kwanini tunajaribu kuondoa huu mfumo wakati umekuwako kwa muda mrefu Sana? Jibu ni hili, kwa nyakati hizi wazazi walezi na walimu huwa tunakuwa na msongo wa mawazo sana tofauti na ilivyokuwa zamani.

Msongo huo wa mawazo tunaupata kwasababu ya mambo mbalimbali tunayoyapitia kila siku inaweza kuwa ni changamoto kazini, nyumbani, kwenye ndoa zetu, kwenye vyombo vya usafiri na sehemu nyingi sana. Sasa haya matatizo yote tunayoyapitia huwa tunayabeba moyoni na hivyo huwa tunakuwa na hasira sana.

Sasa tunapokea na watoto wetu, wakikosea kidogo tu uanakuta unapandwa na hasira sana na hata hasira hiyo haimuhusu sana mtoto hivyo ukimuadhibu au kumchapa tunaishia kumuumiza Sana kwakuwa tunammalizia zile hasira zote ambazo tunazo, kitu ambacho si sahihi. Mwishowe tunaishia kuwa umiza tu watoto na wengine hupoteza maisha bila ya Sababu ya maana.

Hivyo mtoto wako akikosea mchukulie kama mtu mzima ambaye amekosea kwasababu sisi Ni binadamu na tumeumbiwa kukosea ,hivyo mwite pembeni tena kwa faragha na sio mbele za watu kwa kumdharirisha .

Mwite pembeni mweleze kwa upendo kosa alilolifanya, athari zake na pia mwelekeze njia mbadala ya kufanya kwa wakati mwingine atakapo fika katika hali ile, ili asiweze kurudia lile kwasababu ukimchapa tu utakuwa unamuumiza tu badala ya kutatua tatizo, kwasababu sio watoto wote hiwa wanabadilika kwa kugombezwa au kupewa adhabu Kali na ukimzoesha hivyo mtoto huyo atakuwa mtu asiyeweza kuwa na uwezo wa kufikiria na kufanya vitu mwenyewe mpaka aambiwe na mtu kwa kuwa atakuwa umemtengenezea hofu na kutokujiamini kwasababu ulishamwonesha kuwa yeye siku zote anakosea.
 
Back
Top Bottom