Mara ya kwanza ilikua kuhusu mapenzi. Msichana akaniacha kituo cha basi, kama uko Dar pale Sinza Kijiweni ndipo nilipopokea kibuti changu.
Uchungu wa ghafla ukanishika gari likaja sijaangalia la wapi mimi nikapanda, rafiki yangu mmoja akaniwahi akaniambia "Castr hili gari siyo la (akataja ninapoenda)" nikaona aibu kuonekana sikudhamiria nikajibu "Naenda kushuka kwa Mtogole"
Kurudi nyumbani chakula hakipandi binti aliwahi kunipa cheni na zawadi nyingine nyingine nikavikusanya kesho yake naenda kumrudishia. Narudi home lakini bado sina raha nikaanza kusikiliza nyimbo nikawa napendelea hip hop.
Ikaja kuna siku nikashukia kituo kinaitwa Kanisani (Maeneo ya Kinondoni) nikiwa nakatiza vichochoro nikakuta eneo vijana wanajiita Jitambue Arts Group wakiwa wanafanya parody wimbo wa Papa Wemba Machozi, baada ya kuwaangalia nikavutiwa na gita, mimi nikawa naenda kama mdananda tu siyo mwanachama ila naomba kupiga gita.
Ikawa kila siku naenda kupiga gita baada ya wiki kadhaa nadhani binti akaona mbona jamaa yupo kimya akarudi tena, kwa baadhi ya watu ingekua ni ushindi au siyo? Kwangu ikawa kanikasirisha ikanibidi niende tena kupiga gita.