ILIPOISHIA IJUMAA:
Aliuliza Paulina macho yakimtoka pima na mapigo ya moyo yakimwenda kwa kasi, akisubiri jibu ambalo kama angeambiwa achague yeye lazima angeachagua jibu lenye kumpendeza akilini mwake…
"Haswaa! Na hata mimba aliyonayo ni ya kwangu mimi. Sasa chagua mambo haya Paulina, wewe uendelee kuwepo hapa mimi na Stela tuondoke au wewe uondoke mimi na Stela tuendelee kubaki hapa."
ENDELEA KIVYAKO…
Paulina alihema kwa kasi, hasira zikampanda tena na tena…
"Mimi hapa siondoki, labda aondoke yeye. Mimi ni kwangu," alisema kwa kufoka…
"Stela," aliita Mozie.
"Abee."
"Hebu kafungashe kila kilicho chako uje hapa sebuleni."
"Sawa."
Stela alikwenda chumbani kwake na matumaini mapya kwani mazungumzo ya Mozie na Paulina yaliashiria hakuna ndoa tena!
"Yes! Leo mama kapewa vipande vyake laivu. Hakuna cha nini wala nini! Kaambiwa haswaa! Na hata mimba aliyonayo ni ya kwangu mimi. Sasa chagua mambo haya Paulina, wewe uendelee kuwepo hapa mimi na Stela tuondoke au wewe uondoke mimi na Stela tuendelee kubaki hapa," alisema moyoni Stela akiyakumbuka maneno ya bosi wake na baba mtarajiwa wa mtoto wake, Mozie…
"Kwa hiyo?" Paulina aliuliza kule sebuleni baada ya ukimya wa muda wa dakika tatu nzima…"
"Kuhusu nini?"
"Si Stela anaondoka?"
"Hata mimi naondoka."
"Sasa mume wangu we ukiondoka ndiyo kusema..?"
"Ndiyo kusema nini? Mimi naondoka…we ni uamuzi wako unaweza kumwita hata baba Riziki akaendelea kuishi hapa kwa usalama zaidi."
Paulina alishtuka sana, jambo hilo hakulitegemea hata siku moja katika maisha yake. Alianza kuhisi makosa makubwa aliyoyafanya ya kutembea na baba Riziki na ugumu wa malipo yake katika ndoa…
"Kwani mume wangu, haiwezekani tuka…"
Stela alitokea akiwa amebeba mabegi mawili…
"Mimi vitu vyangu ndani ya nyumba hii ni haya mabegi mawili tu," alisema Stela huku akiyaweka chini mabegi hayo na kutaka kufungua zipu akisema…
"Mama ungeangalia usijesema nimeondoka na vitu vyako."
"Mimi sijasema hivyo Stela, labda kama unajishtukia."
"Sijishtukii ila najua wanadamu walivyo mama."
Mozie alisimama kuelekea chumbani, Paulina akajua anakwenda kufungasha vyake ili aondoke na Stela…
"Stela," aliita Paulina…
"Abee."
"Hebu kaa hapo kwanza."
Stela alikaa…
"Nakusikiliza."
"Hivi Mozie amewahi kukwambia ni kwa nini anatembea na wewe mpaka kukupa mimba?"
"Ni kwa sababu wewe umetembea na baba Riziki ili kutafuta mtoto, akasema basi wewe utafute kivyako na yeye atafute kivyake."
"Mh!" Aliguna Paulina, akajikuta nguvu zikizidi kumwishia.
Alipopiga akili sana akapata uamuzi, akamfuata mume wake chumbani ili amwambie wazo lake…
"Mume wangu please usiondoke, nakuomba sana na niko chini ya miguu yako."
"Mimi siwezi, lazima niondoke na Stela, wewe si una wako lakini," alisema kwa hasira Mozie.
"Basi sikia mume wangu, naomba Stela asiondoke, akae hapahapa na mimba yake, we unaonaje?"
"Una maana gani?"
"Nina maana nakubali kuishi na Stela lakini akiendelea kuwa mfanyakazi wetu na mimba yake tutailea mpaka atakapojifungua."
"Akiendelea kuwa kama msichana wa kazi?"
"Ndiyo."
"Haitawezekana. Mimi nataka kama unamkubali Stela mkubali kama mke mwenzako, kinyume cha hapo mimi na yeye tunaondoa we baki tu," alisema Mozie huku akiendelea na zoezi la kukunja nguo…
"Mama," Stela aliita akiwa amesimama mlangoni, Paulina akatoka kumsikiliza…
"Mimi naondoka mama, niko tayari, mwambie na baba."
"Ngoja kwanza Stela, nenda kakae sebuleni."
"Stela kanisubiri nje ya geti mama angu," alisema Mozie.
"Sasa Mozie jamani, mbona tunaendelea kuongea halafu wewe unatoa matamko bila kufikia mwisho?"
"Mwisho upi zaidi ya huu?" Aliuliza kwa ukali Mozie.
Paulina aliinamia chini, moyoni alijua tabu yote ile chanzo ni baba Riziki kama alivyoambiwa na Stela kule sebuleni…
"Kwanza kabisa naomba unisamehe Mozie."
"Kwa lipi?"
"Kuhusu baba Riziki."
"Kuna tatizo gani kati yako na baba Riziki?"
"Najua unajua."
"Mi sijui," alisema Mozie kwa lengo la kumnasa akili mkewe aone kama atasemaje?
"Si yale madai kwamba nilitembea naye."
"Wakati hukutembea naye?"
"Ni kweli nilitembea naye lakini kwa sababu ya kulinda heshima yako kuhusu sisi kupata mtoto."
"Ndiyo maana na mimi nimeamua kulinda heshima yako kwa kumpa mimba msichana wa kazi ili atupatie mtoto."
Paulina aliumia zaidi kuliko alivyoumia Mozie, kwake yeye kitendo cha mumewe kufanya mapenzi na msichana wa kazi hadi mimba kilikuwa cha kumshangaza sana. Alimchukulia msichana wa kazi kama dhaifu, asiyemvutia mwanaume, asiyeweza kumpindulia mume, sasa leo eti ana mimba ya mume wake, ni ajabu…
"Lakini mume wangu mimi kwangu afadhali ungetembea na mwanamke mwingine wa mtaani kuliko msichana wangu wa kazi."
"Mimi kwa upande wangu afadhali ungetembea na msukuma mkokoteni kuliko baba Riziki."