JAMANI KWANI LAZIMA?-34
ILIPOISHIA
"Beby mimi wala sina kinyongo kwa hilo niko sawa, na hiki kiumbe?"
"Hiyo ni mali yangu na tutamlea wote pamoja na Paulina, kuanzia sasa wewe si mfanyakazi bali mke wa pili kama nilivyoandika hapa!"
JIACHIE SASA...
Paulina alifuatilia mazungumzo hayo kwa akili ya kujiongeza, hakupata jawabu la haraka zaidi ya kukubaliana na maamuzi ya mumewe, Mozie...
"Basi kama tumemalizana kwa amani kiasi hiki, mimi nakuahidi jirani sitarudia tena na kuanzia sasa nitakuonesha mabadiliko makubwa. Paulina heshimu ndoa yako, lolote mshirikishe mumeo."
"Sawa, nimekusikia."
"Haya, bwana Mozie mimi naondoka sasa," aliaga baba Riziki...
"Sawa, karibu tena."
***
Maisha ya Paulina mke mkubwa, Stela mke mdogo na Mozie ndiye baba mwenye nyumba yalianzia hapo.
Baada ya baba Riziki kuondoka tu, Mozie alisema...
"Mnatakiwa kutafuta msichana wa kazi wenyewe, mimi nitamlipa mshahara tu."
"Sawa," alidakia Paulina, Stela alikubali kwa kutingisha kichwa...
"Kuhusu kulala, kila mmoja nitakuwa nalala kwake kwa siku tatu tu."
"Sawa," alikubali Stela, Paulina alibaki ametumbua macho.
Lakini Mozie hakuwa amesema ataanza ratiba kwa kulala kwa nani!
***
Usiku uliingia, Paulina ndiye aliyeinjinia kushika usukani wa kupika jikoni kwa kupika chakula ambacho Stela angekula.
Moyoni, Paulina alikiri mwenyewe kwamba, baba Riziki ndiye aliyemvurugia mambo yake yote. Alijua kwa kitendo hicho, mumewe alikuwa amefanya kama silaha ya uhalali wa kuonesha mapenzi yake na Stela...
"Kama siyo baba Riziki, Mozie asingekuwa na ubavu wa kunifanyia hivi kwa Stela, mbona pangechimbika. Yaani mwanaume wangu atembee na msichana wa kazi hivihivi naona, wee," alisema moyoni Paulina huku akiendelea na mapishi.
Kwa upande wake, Stela yeye ilikuwa ni furaha tu kwani mwanamke aliyekuwa akitishia maisha yake sasa amemfikia levo. Kwake ilikuwa sawa na timu ndogo kucheza mpira na timu kubwa na kutoa sare ambapo ni cherekochereko...
"Hapo sawa. Sasa tuone kama anaweza kuniambia ataniua. Si tumeambiwa kwamba tutakuwa tunalala naye kwa zamu, zamu moja kwake, nyingine kwangu, hana lake tena," alisema moyoni Stela.
***
Paulina aliamua kuweka kinyongo pembeni na kusalimu amri kwenye ndoa yake. Alipomaliza kupika alitenga chakula mezani, Stela akiwa sebuleni anaangalia vipindi mbalimbali vya kwenye tivii.
Mozie alikuwa akisoma kitabu cha mapenzi kinaitwa Godoro la Mtumba...
"Chakula tayari," alisema Paulina akiwaalika Mozie na Stela.
Stela ndiye aliyekuwa wa kwanza kuchomoka kwenye sofa kwenda kwenye sehemu ya kulia chakula na kujipakulia, kisha akavuta kiti na kukaa.
Mozie alifuata kwa nyumba akiwa ameongozana na Paulina...
Stela alishika sahani nyingine haraka sana na kumpakulia chakula Mozie huku akisema...
"Niongeze nini darling, pilipili au?"
"Noo! Hapo tosha, labda tupia zaidi hivyo vifinyango vya kuku," alisema Mozie huku uso wake ukionesha uchangamfu zaidi.
Paulina alimwona Stela kama anatupia vifinyango hafifu, akamnyang'anya kijiko Stela na kuibua mapenda makubwa ya kuku zikiwemo filigisi...
"Hizo nitakula mimi," alisema Stela...
"Filigisi ni kwa ajili ya baba mwenye nyumba, we hujafundishwa nini?" alisema Paulina...
"Kweli kabisa," Mozie aliunga mkono hali iliyomfanya Paulina kuhisi unafuu wa amani ndani ya moyo wake kuliko kama angekaa kimya au kumuunga mkono Stela.
Stela hakupendezwa na hali ile ya Paulina, akahisi kama anataka kutumia asili ya ujio wake wa kazi pale kwake kuendelea kumwongoza wakati na yeye ni mke mwenzake hata kama ni mke mdogo.
Chakula kililiwa polepole, ukimya na utulivu ulitawala lakini zaidi sana, umakini ulizingatiwa. Tayari Paulina alihisi katika kuongea eneo hilo lilihitaji akili sana la sivyo ilikuwa rahisi kuharibu. Hilo hata kwa Stela lilikuwa wazo lake kichwani...
"Hivi mnakulaje kama mabubu," alikata ukimya Mozie...
"Nashangaa," alisema Stela...
Paulina alimwangalia Stela kisha akasema...
"Sisi tulifundishwa wakati wa kula hakuna kusema...
"Mbona sasa umesema?" alidakia Stela...
"Kwa sababu nimeulizwa kwa nini sisemi."
"Si ungekaa kimya mpaka tungemaliza kula ndiyo ungesema," Stela hakukubali, alisema tena...
"Wewe Stela una matatizo," alisema Mozie...
"Kivipi?"
"Unaongea sana."
"Basi nanyamaza," alisema Stela na akanyamaza kweli.
Waliendelea kula hadi wakamaliza, Mozie ndiye aliyeanza kutoka mezani na kwenda kukaa kwenye sofa sebuleni.
Akafuatia Stela akanawa, akaenda kukaa jirani na Mozie kwenye sofa moja kubwa.
Paulina alitoa vyombo, akavipeleka jikoni, akatoka kwenda kuoga. Alipomaliza, aliingia chumbani mwake na kubadili mavazi. Alivaa gauni la kulalia, tuliite ‘night dress.'
Alijipulizia pafyumu nzuri sana, akajikwatua sana kama ana mtoko, akaenda kukaa sebuleni. Mozie alikaa kwenye sofa kubwa katikati, Stela alikaa kulia kwake, Paulina akajiweka kushoto huku akimwangalia Mozie kwa macho ya mlegezo hali iliyomfanya mumewe kupatwa na hisia f'lani za kimapenzi hasa kwa vile alivyojipara usiku huo...
"Mwenzetu inaonekana una ahadi na baba Riziki, mbona umejipodoa hivyo?" alihoji Stela huku akiachia tabasamu laini na kumpapasa Mozie kifuani huku Paulina akishuhudia.
ITAENDELEA IJUMAAA.................