Itungwe sheria wanaume waende kliniki

neema shamuhenya

JF-Expert Member
May 24, 2018
312
216
BAADHI ya wakazi wa kijiji cha Muhalala katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wameiomba serikali kutunga sheria kali itakayowadhibiti wanaume wanaokataa kuambatana na wake zao kwenda kliniki wakati wenzi wao hao wakiwa wajawazito.

Rai hiyo imetolewa na wakazi hao wakati timu ya wataalamu wa afya kutoka World Vision Tanzania walipokuwa wakitoa elimu juu ya uboreshaji wa lishe katika kuimarisha afya ya uzazi kwa mama na mtoto (ENRICH) kijijini hapo, mradi unaofadhiliwa na Global Affairs ya nchini Canada tangu Machi 2016.

Meneja wa Mradi wa Enrich, Mwivano Malimbwi alisema kuwa tangu mradi huo uanze miaka miwili iliyopita kumekuwa na mwamko wa wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitalini, ongezeko la lishe kutoka asilimia 16 hadi 33 na ulimaji viazi lishe kutoka asilimia 0 hadi 10.5.

Alisema kutokana na ukweli kwamba wanaume ndio wenye uamuzi wa mwisho na nguvu ya kiuchumi katika familia, ni muhimu iwapo watafuatana na wake zao kliniki ili waweze kupewa ushauri wa kitaalamu kwa pamoja na endapo kuna tatizo, mwanaume aweze kuchukua hatua stahiki mara moja.

Aidha, alitaja baadhi ya sababu za wanaume kukataa kwenda kliniki na wake zao kuwa ni hofu ya kutakiwa kupima Ukimwi na wengine kuwa na michepuko kutokana na tabia zao za kukosa uaminifu kwenye ndoa.

"Baadhi ya wanaume wanakuwa na nyumba ndogo hivyo huona aibu kuambatana na wake zao kliniki wakihofia kuwakuta wapenzi wao maeneo hayo na kuogopa kushutumiwa kuwajali zaidi wake zao kuliko hiyo michepuko,” alibainisha.

Mwajuma Omari, Hamis Makita na Rehema Joseph licha ya kuunga mkono hoja ya kutungwa sheria hiyo pia walisisitiza umuhimu wa wananchi kuacha kung'ang'ania mila potofu zinazomkandamiza mwanamke na kumnyima nafasi ya ushiriki sawa katika maamuzi mbali mbali ndani ya familia.

Mradi unatekelezwa mkoa wa Shinyanga katika Wilaya za Kahama, Kishapu na Shinyanga Vijijini na mkoani Singida (Ikungi na Manyoni) kwa lengo la kuwafikia jumla ya watu 906, 321 wakiwemo wanawake, wanaume, wasichana na wavulana ifikapo Septemba 2020 kwa gharama ya Sh bilioni 8.36. (Dola za Marekani milioni 3.8).
 
Back
Top Bottom