Kama kweli serikali inawafahamu wamiliki wa Dowans haitoshi tu kusema kuwa JK siyo mmiliki wa Dowans na kwamba Dr. Slaa ni mwongo.
Je kutuambia wamiliki wa Dowans kutaigharimu nini serikali? kuna siri gani katika kuwataja hao wamilki?
Dk. Slaa aishika pabaya Ikulu
Yatumia maneno ya kejeli, mtaani kujibu hoja zake
na Edward Kinabo
KURUGENZI ya Mawasiliano Ikulu imeelezea kukerwa kwake na hatua ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kumtaja rais Jakaya Kikwete kuwa alihusika katika uzembe uliosababisha taifa kutakiwa kuilipa kampuni ya Dowans sh bilioni 185 kama fidia.
Taarifa kali ya Ikulu iliyobeba ujumbe wenye maneno ya kebehi na ya mitaani ya kumwita Dk. Slaa mtu aliyechanganyikiwa na mzabinazabina ilisainiwa na Salvatory Rweyemamu ambaye kabla ya kwenda Ikulu alikuwa mmoja wa wahariri watendaji aliyekuwa akiheshimika kwa kutumia lugha fasaha na ya staha.
Rweyemamu katika taarifa yake hiyo iliyoonyesha waziwazi kuandikwa na mtu mwenye hasira, chuki na dharau ama kwa Dk. Slaa, CHADEMA na Tanzania Daima alikwenda mbele na kumwita kiongozi huyo wa kisiasa kuwa ni mtu hatari.
Sehemu ya maneno makali ya Rweyemamu kwa Dk. Slaa ni kama yale aliyosema, Na kama kweli Dk. Slaa ametoa kauli hii na kusema maneno ya namna hii basi sasa Watanzania wanayo kila sababu na haki ya kuamini kuliko wakati mwingine wowote kuwa mzee huyu (Slaa) sasa amechanganyikiwa na ni mtu wa hatari sana kwa utulivu wa nchi hii.
Rweyemamu aliendelea kueleza, Kama Dk. Slaa anataka kweli kujua wamiliki wa Kampuni ya Dowans, basi atafute ukweli huo na aachane na tabia ya kutapatapa na uzabinazabina yenye lengo la kuwapaka watu watope.
Ikulu ambayo katika mazingira ambayo si rahisi kuyaeleza imekuwa na desturi ya kukanusha kwa nguvu kubwa kila wakati jina la Rais Kikwete linapohusishwa na sakata la kashfa ya Richmond/Dowans.
Hii ni mara ya pili kwa Ikulu kufanya hivyo baada ya mara ya kwanza kuchukua hatua kama hiyo wakati Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alipokanusha hoja zilizokuwa zikijaribu kumhusisha Rais Kikwete na uhusiano wake na mkataba wa Richmond.
Wakati Ikulu ikikanusha mara kwa mara kuhusishwa kwa Kikwete katika sakata la Richmond/Dowans kwa namna yoyote ile, upo ushahidi wa kibunge (rejea ripoti ya Kamati Teule ya Mwakyembe) unaoonyesha kwamba, maamuzi kuhusu mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond ulijadiliwa na Baraza la Mawaziri lililokuwa chini ya uenyekiti wa rais mwenyewe.
Kama hiyo haitoshi, gazeti moja la kila wiki linalomilikiwa na kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambalo Rweyemamu amepata kuwa mmiliki wake, limepata kuchapisha katika ukurasa wake wa mbele barua ikionyesha barua aliyoandika aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kwenda kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu suala la Richmond ambayo nakala yake ilikwenda pia kwa Rais Kikwete.
Uamuzi wa jana wa Rweyemamu kuandika taarifa kali dhidi ya Dk. Slaa unakuja siku chache baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya kibiashara hivi karibuni kuamuru Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) kuilipa Dowans fidia kubwa baada ya kuvunja mkataba nayo kinyume cha taratibu.
Katika mahojiano maalum na gazeti Tanzania Daima Jumapili, la juzi Dk. Slaa alikaririwa akisema chanzo cha suala zima lililopelekea Dowans kutakiwa kulipwa fidia hiyo ni uzembe wa serikali na Rais Kikwete mwenyewe kwani ndio waliohusika katika kuileta kampuni ya Richmond ambayo baada ya kuonekana ya kitapeli iliamua kurithisha kazi zake kwa Dowans.
Ikulu katika taarifa yake hiyo kwa sababu zisizojulikana ilijikuta ikipotoka ama kwa makusudi au kwa kutojua ilipoeleza kuwa gazeti la Tanzania Daima lililonukuu maelezo ya Dk. Slaa, linamilikiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakati taarifa zilizopo kwa msajili wa magazeti zinaeleza bayana kwamba, gazeti hilo ni la watu binafsi.
Ikipinga maelezo ya Dk. Slaa kuhusu uhusiano wa rais Kikwete na Dowans, taarifa hiyo ya Ikulu ilisema, Huu ni uongo wa mchana, ni uzushi wa karne na propaganda ya hatari. Kwa hakika na kwa namna isiyoweza kuelezeka kwa ufasaha, tumeshtushwa sana na kauli hii ya Dk. Slaa
Mheshimiwa Rais Kikwete siyo mmiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans. Hakupata kuwa mmiliki, siyo mmiliki na wala hatakuwa, hata siku moja, mmiliki wa kampuni hii. Ikitumia lugha kali dhidi yake Ikulu iliwataka wananchi wampuuze Dk. Slaa ikidai kuwa ni mzushi na amechanginyikiwa.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Dk.Slaa kuitwa mzushi na vigogo wa serikali kwani mara kwa mara anapoibua maovu amekuwa akipingwa kwa kuitwa jina hilo ingawa anayoibua huthibitika kuwa na ukweli ndani yake.
BARUA YA SALVA KWA VYOMBO VYA HABARI HII HAPA
As long as Kikwete/Ikulu doesn't want to tell the wananch who is the owner of Dowans, Dr. Slaa is right.